Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla sijaanza naomba nitoe shukrani zangu za dhati kabisa na pongezi za kutosha kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Awamu ya Tano kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya hususan katika Mkoa wetu wa Manyara. Napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Rais, alikuja mwaka jana mwezi Julai kuzindua barabara ya lami ambapo kwa mara ya kwanza ndiyo tunaiona lami Mkoa wa Manyara, hususani eneo la Simanjiro Mererani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kutokana na swali langu nililoliuliza hapa Bungeni tarehe 31, Januari kwamba ni lini Mkoa wa Manyara hususan Kituo cha Afya cha Mererani kitapatiwa ambulance na nikajibiwa hapa na Mheshimiwa Jafo ya kwamba atalifanyia jambo hilo kazi.

Kwa kuwa Rais ni Waziri wa TAMISEMI pia, alichukua hoja hiyo na juzi alipokuja kufungua ukuta pale Mererani alikuja na ambulance hiyo, kwa hiyo namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kile alichowatendea watu wa Manyara, hususani eneo la Mererani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimekuwa nikiuliza mara kadhaa hapa Bungeni jinsi gani yale madini ya Tanzanite yanayochimbwa pale Mererani yanaweza kuwafaidisha wakazi wa Manyara maana yanachimbwa pale na yanauzwa Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, namshukuru Mungu kwamba tayari sasa tunaelekea kwenda kufaidika na madini haya ya Tanzanite kutokana na kwamba tayari ukuta umejengwa wa kuzuia upoteaji wa madini haya ambayo mara nyingi yamekuwa yakifaidisha mataifa ya nje zaidi kuliko wakazi wa Tanzania na hususani watu wa Simanjiro na Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Tanzania ya kuweza kuzuia upotevu wa madini haya ya tanzanite na madini mengine ya dhahabu na kadhalika. Kila mtu ni shahidi hapa ni nini ambacho Rais amekifanya karibuni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba yale yote yanayofanyika katika nchi yetu ni kwa manufaa ya wananchi wenyewe.

TAARIFA . . .

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikatae taarifa hiyo. Unajua mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Mtoto hazaliwi akakimbia siku hiyohiyo. Kazi inayoendelea kufanyika na imekwishafanyika ya jinsi gani ya kuhakikisha madini haya yananufaisha Watanzania hakuna ambaye hajui. Kwa hiyo, wenzetu wanashindwa tu ku- appreciate juhudi zinazofanywa na Rais pamoja na Serikali kwa ujumla. Naomba niendelee na mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inajulikana kabisa kwenye ule ukuta unakwenda kuwekwa CCTV cameras, unakwenda kuwekwa electrical fence juu yake, kwa hiyo kwa namna moja ama nyingine haya madini hayataendelea kupotea, sambamba na kuhakikisha kwamba mikataba hiyo inaendelea kutazamwa kwa ajili ya kuhakikisha madini haya yanaendelea kutunufaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia pia kwa Waziri, Mheshimiwa Jafo pamoja na timu yake ya Naibu Mawaziri kwa yale ambayo wametufanyia watu wa Mkoa wa Manyara. Tayari Mkoa wa Manyara tumepokea fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda pale Mbulu tumepokea fedha kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Daudi, Kituo cha Afya cha Dahwi na Dongobesh pia. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia Ofisi ya TAMISEMI kwa kuona changamoto hii na kuifanyia kazi. Natoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Mbulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo ukisogea pale Babati tayari tumepata fedha kwa ajili ya Kituo cha Nkaiti nacho tayari kimejengwa lakini pia tumepata ambulance kwa ajili ya kituo hicho. Hizi juhudi sio za kubezwa, Serikali inafanya kazi na tunaona kwa macho ya nyama na tunaendelea kushuhudia. Hanang tumepata kwa ajili ya Kituo cha Simbai pamoja na ambulance, kwa hiyo, niseme tu naishukuru sana Serikali hii kwa ajili ya kile ambacho inaendelea kutenda kwa ajili ya watu wetu wa Manyara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisogea kwenye suala zima la elimu, tumepata pia fedha, milioni 215 kwa ajili ya ukarabati wa shule mbalimbali, Shule ya pale Kiteto, tumepata fedha Mbulu, tumepata fedha Hanang, tumepata fedha maeneo mbalimbali kwenye Mkoa wetu wa Manyara kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule ikiwemo hostels, yakiwemo madarasa na ofisi za Walimu na matundu ya vyoo; kwa hiyo, niishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisemee kidogo mfuko wa asilimia tano za akinamama na asilimia tano za vijana. Nimesoma kwenye hotuba ya Waziri wa TAMISEMI jinsi gani ofisi yake ina mkakati wa kuhakikisha fedha hizi zinatengenezewa mwongozo mzuri wa namna gani ziwafikie walengwa hawa ili kuendelea kupunguza na kuondoa umaskini kwa vijana na akinamama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Jafo, amesema wana mpango wa kuondoa riba katika mikopo wanayopewa akinamama na vijana, hili jambo ni jema sana na naitakia kila la heri ofisi ya Waziri, Mheshimiwa Jafo hili jambo likapate kufanikiwa ili watu wengi wakapate kukopeshwa fedha hizi na hatimaye tuendelee kuondoa umaskini kwa ajili ya watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pia kwa ajili ya suala zima la miundombinu ya maji katika Mkoa wa Manyara, inaenda ikiimarika. Hata hivyo, nina ombi moja, kuna mradi wa maji mkubwa unaoendelea katika Wilaya ya Mwanga karibu na Bwawa la Nyumba ya Mungu, mradi huo unapakana sana na Vijiji vya Ngorika katika Wilaya ya Simanjiro na wale watu wa Ngorika hawana maji kabisa na mradi huo unaondoka kutoka kwenye eneo hilo la Ngorika ama karibu na Bwawa la Nyumba ya Mungu kuelekea Mwanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lao ni moja tu kupitia Wizara hii ya TAMISEMI, kwamba ikiwezekana na wao waweze kupata connection ya maji hayo kwa sababu wako jirani sana, ili kwamba na wenyewe waendelee kufaidi matunda ya Serikali hii ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio yote niliyoyasema changamoto hazikosekani, naomba tu niseme bado tuna changamoto ya miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Manyara hususani maeneo ya Kiteto. Kipindi hiki Kiteto wamekuwa kama kisiwa, hawafikiki kwa sababu ya barabara kuvunjika sana kipindi hiki cha mvua. Niombe tu TARURA, najua wanafanya kazi kubwa na wanafanya kazi nzuri, kila mtu ameona hapa ya kwamba TARURA wanafanya kazi kubwa na barabara zao ni nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ikiwezekana wapate hata asilimia 50 kwa 50, TANROADS 50, TARURA 50, ili kwamba barabara nyingi zinazotumiwa na wananchi wengi maskini ziweze kutengenezwa na ziweze kupitika, waweze kuuza mazao yao, waweze kufanya biashara zao na hatimaye waondokane na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kila mtu ni shahidi, mvua zimekuwa zikiendelea kunyesha kipindi hiki, barabara nyingi zimevunjika katika maeneo mbalimbali ya nchi hii, kwa hiyo, naomba ile dharura waliyoiomba TARURA wapatiwe ili waweze kuboresha baadhi ya maeneo korofi sana na wananchi waweze kuendelea na shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisichukue muda mrefu sana lakini niseme tu kwamba, tunaendelea kuona upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo katika shule zetu na hali hi imekuwa ikileta shida kwa wanafunzi wetu especially watoto wa kike. Naomba Ofisi ya Rais,TAMISEMI atakapokuja hapa Mheshimiwa Jafo hapa atuambie ni mkakati na mpango gani Ofisi hii imeandaa wa haraka sana yaani kama crash program ya kuhakikisha mwaka kesho hatuji hapa kuzungumzia suala la upungufu wa matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tuna zaidi ya upungufu wa matundu ya vyoo 270,000. Ni aibu kuendelea kuzungumza suala la upungufu wa vyoo katika karne hii naomba, Mheshimiwa Jafo atakapokuja nina hakika yeye ni mchapakazi pamoja na Naibu Mawaziri na watu wa kwenye Ofisi yake watuambie ni mkakati gani mahsusi ulioandaliwa kuondoa tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nisisahau suala zima la watoto wakike ambao wanabebeshwa mimba wangali bado wako shuleni. Hili suala si suala la kuchukulia mzaha mzaha, hawa watoto wanakatishwa masomo yao bila ridhaa yao, lakini ninaona bado hata ule mfumo uliyowekwa si rasmi wa wao kurudi hatuwatendei haki...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa mzungumzaji)

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.