Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kushukuru kwa kupata nafasi hii ili na mimi niweze kujibu baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezichangia wakati wa kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba, naunga mkono hoja ya hotuba yote ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu, imeelekeza, imeeleza utekelezaji wa miradi ya maji katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/2018. Hotuba imeeleza kwamba kwa upande wa vijijini tayari huduma ya maji safi na salama imefikia asilimia 60 na kwa upande wa mijini huduma ya maji safi na salama imefikia asilimia 78. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaendelea na utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo tuliianza mwaka 2006/2007. Programu ya kwanza iliisha mwaka 2017, Juni. Katika awamu hii ya kwanza tulilenga kutekeleza miradi 1,810; lakini hadi leo tayari tumeshatekeleza miradi 1,468. Miradi hiyo tumejenga vituo vya kuchotea maji 123,888 lakini katika vituo hivyo ni asilimia
60 tu ya vituo ndio vinavyotoa maji kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo kwamba miradi mingi tuliweka pump za kutumia dizeli, jenerata za kutumia dizeli ambazo Jumuiya za Watumiaji Maji wameshindwa kuziendesha. Hata hivyo yapo maeneo ambayo hizi jumuiya tulizoziunda kwa ajili ya kuendesha miradi ambayo imekamilika wao wenyewe wameshindwa kuziendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo yaliyolengwa kwamba maji yatapatikana kutoka maeneo hayo lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi maeneo hayo yamekauka maji. Hivyo, Katiba bajeti inayokuja tunataka tuhakikishe kwamba vile vituo vyote ambavyo tayari vimeshajengwa na havitoi maji tutaweka fedha, tutatenga bajeti ili kuhakikisha kwamba tunapeleka yale maji na tunaondoa changamoto zote ambazo zimejitokeza zinazofanya vituo vyote hivi visitoe maji kwa sababu kama vituo hivi vyote vingetoa maji sasa hivi tungekuwa tunazungumzia upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya vijijini tungekuwa tumefikia asilimia 85 kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mijini tayari tuko asilimia 78. Miradi mingi imeshatekelezwa katika maeneo ya mijini na maji yapo, kwa mfano katika Jiji la Dar es Salaam. Sasa hivi bajeti inayokuja tutatenga bajeti ili kuendelea kupanua mtandao, ili wananchi wengi waweze kupata maji tuweze kufikia asilimia iliyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba maeneo ya miji tufike asilimia 95. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako tukufu katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Waheshimiwa Wabunge waliielekeza Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuunda Wakala wa Maji Vijijini. Naomba kutoa taarifa kwamba Wizara inaendelea na taratibu za uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini wenye majukumu ya kujenga miradi, kusaidia usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji vijijini. Kwa sasa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekamilisha kazi ya kuandaa nyaraka muhimu ambazo ni strategic plan, business plan na framework document kwa kutumia Sheria ya Uanzishwaji wa Wakala nchini ili kusaidia uanzishwaji wa wakala hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nyaraka hizo zitaenda sambamba na maoni ya wadau na baadae itapelekwa kwenye mamlaka husika kwa idhini ya uanzishaji wa taasisi hiyo. Mategemeo ya Wizara ni kuwa Wakala wa Maji Vijijini, utaanza kufanya kazi kuanzia mwezi Julai kwenye bajeti ya 2018/2019. Kwa hiyo, tupo mahali pazuri katika kuhakikisha kwamba tunaanzisha Wakala wa Maji Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wameligusa sana ni kuhusiana na mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India ambao utatuwezesha kutekeleza miradi 17, kati yake 16 ikiwemo Tanzania Bara na mradi mmoja Tanzania Visiwani. Upatikanaji wa fedha hizi umechelewa kutokana na majadiliano kati ya Serikali ya India na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imechukua muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, majadiliano haya yamechukua muda mrefu kutokana na sababu kwanza Bunge letu tukufu mwezi Septemba lilibadilisha Sheria ya VAT, kwa hiyo, ili kukamilisha taratibu Sheria ya VAT ianze kufanya kazi imechelewesha kuweza kusaini Financial Agreement, lakini kwa sasa tumefikia hatua nzuri na niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba, fedha hizi dola milioni mia tano tunatarajia kuzitumia kwenye bajeti ijayo kwa mwaka wa fedha 2018/2019…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)