Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kupongeza hotuba ya Waziri Mkuu, napongeza utendaji wake na utendaji unaofanywa na Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika mambo mbalimbali ya kuongoza nchi, tuko nyuma yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa kilimo katika pato la Taifa na katika kutoa ajira nchini ni mkubwa, hauwezi kupuuzwa na mtu yeyote. Hata hivyo, namna kilimo kinavyoendelezwa hapa nchini hakileti matumaini ya kuleta maendeleo ya haraka katika uchumi wa nchi na vilevile kutoa ajira kwa asilimia 75 ya wakazi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kusema hivyo ni kwamba bado pembejeo hazipatikani kwa wakati hasa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na wakati mwingine pembejeo hazipatikani kabisa. Naomba Serikali ijue misimu ya kilimo ya kanda mbalimbali ili kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kipatikane chombo kitakachopewa wajibu wa kuratibu changamoto mbalimbali za wakulima zikiwemo pembejeo, masoko na utafiti ili kuleta tija kwa wakulima badala ya kufunga mipaka ya nchi kuuza mazao nje. Wakulima wa Rukwa wanapata hasara ya uwekezaji wao katika kilimo pale Serikali inapofunga mipaka na kufanya mazao yao kukosa masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wakulima wa mazao ya nafaka wapate hasara kwa hofu ya nchi kupata upungufu wa chakula wakati mazao ya biashara yanayolimwa na mikoa mingine inapata masoko kama kawaida. Ushauri wangu ni kwamba wakulima waendelee kulima na kuruhusiwa kuuza popote mpaka pale utaratibu muafaka utakapowekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni ukosefu wa ardhi kwa wananchi wa Kata wa Nkandasi, Vijiji vya Mihindikwa, Kasu, Kisura na Malongwe ambapo ardhi yao imetwaliwa na Jeshi la JKT. Takribani ni wananchi 4,000 wa vijiji hivi wamekosa ardhi huku ardhi hiyo ikiwa imekaa bila kutumiwa na mashamba yaliyonyang’anywa wanajeshi mmoja mmoja wanalima huku wananchi wamekaa kushangaa na bila kwenda shamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limezungumziwa sana lakini hakuna aliyelisikia. Naomba Serikali ilione kwa macho mawili. Kama Mbunge wananchi wamenituma niwaletee Bungeni na mimi nimetekeleza wajibu hivyo wahusika walifanyie kazi vinginevyo watabeba dhambi ya lawama ya mateso ya ukosefu wa ardhi kwa wananchi waliofukuzwa kwenye ardhi waliopewa kihalali na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yanayowakabili wananchi wa Jimbo la Nkasi ni kama ifuatavyo:-

(i) Maji ni tatizo na miradi inayoendelea bado haijatoa matokeo chanya kwa wananchi;

(ii) Suala la mtandao wa simu za mkononi Kata ya Kala iliyoko mpakani mwa DRC, eneo la Ziwa Tanganyika ni kero kubwa kwa wananchi hao; na

(iii) Barabara ya Kitisi - Wampembe chini ya TARURA zinafunga kupitika kwa kukosa matengenezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, jimbo langu lina takribani vijiji 60 na kila kijiji tumehamasisha wananchi kujenga madarasa matatu. Wote wameitikia kabisa na sasa tuna madarasa 180 hayajaezekwa. Naomba ombi maalum kwa mwitikio mzuri wa wananchi wapewe fedha ya kuezeka madarasa hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya, jimboni kuna kata 11 ambapo kata nne wameanza kujenga vituo vya afya. Kata hizo ni Nkandasi, Kala, Ninde, na Kate, takribani zahanati 12 zimejengwa tunaomba msaada wa Serikali.