Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu; Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa na Baraza lote la Mawarizi kwa namna wanavyofanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania na Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo endelevu ni maendeleo ya watu na siyo vitu. Maendeleo ya watu huonekana katika viashiria kama vile pato la mtu mmoja mmoja, fursa ya kupata huduma muhimu kama elimu, afya, mavazi, maji safi, umeme na huduma za usafiri. Naipongeza sana Serikali kwa kuhakikisha kwamba maendeleo ya watu yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yote makubwa yanayofanyika nchini yamelenga kuboresha maisha ya Watanzania. Mfano, elimu bure, maboresho mbalimbali katika Sekta ya Afya, miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege na mengine mengi yanaendelea kufanyika na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi maridadi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya ahadi za viongozi wa Kitaifa hususan Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, mpaka sasa hazijatekelezwa. Kwa namna moja au nyingine zinakatisha tamaa wananchi kwa kuona baadhi ya ahadi hazitekelezwi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu hususan barabara, katika Jimbo la Lupembe Halmashauri ya Njombe DC kuna barabara ya Lupembe, yaani Kibene – Lupembe – Madeke (kilometa 126) iliahidiwa na Mheshimiwa Jakaya Kikwete mwaka 2010 na kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 iliahidiwa kuwa barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Mwaka 2016/2017 na mwaka 2017/2018 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliipangia bajeti barabara hii kwa ajili ya kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami kilometa 50, lakini mpaka leo hii tukiwa tunamaliza mwaka wa fedha, barabara hii haijaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana kwani ndiyo barabara pekee inayounganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro kupitia Mlimba. Pia kiuchumi barabara hii ndiyo inayoongoza kwa kuwa na magari mengi yanayosafirisha mazao mbalimbali katika Mkoa wa Njombe. Mazao yanayosafirishwa na barabara hii ni mbao, chai, mahindi, maharage, matunda mbalimbali na viazi. Hivyo tunaomba barabara hii itengenezwe kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru Serikali kwa kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana katika hospitali zote. Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni miongoni mwa Halmashauri ambazo hazina Hospitali za Wilaya. Halmashauri hii ina Vituo vya Afya vinne; Kituo cha Lupambwe, Kichiwa, Matembwe na Sovi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa ukarabati wa Vituo vya Afya, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilikuwa ni miongoni mwa Halmashauri ambazo ziliahidiwa kupewa shilingi milioni 500. Nami kama Mbunge wa Jimbo, nilipewa taarifa na kuoneshwa orodha ya Halmashauri zilizopata shilingi milioni 500. Cha kushangaza, fedha zilipotoka hazikuletwa kwenye Halmashauri yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kufuatilia sana, nikaambiwa tutaingiziwa kwenye mpango wa shilingi milioni
400. Fedha zilipotoka, bado Halmashauri yangu haijapata fedha hizo wakati kuna Halmashauri zimepata fedha za ukarabati kwa Vituo vya Afya viwili, nyingine vitatu. Juzi juzi tumeona baadhi ya Halmashauri zimepata vituo mpaka vitano. Halmashauri hii licha ya kuwa ina changamoto ya usafiri, vituo vyote havina hata gari la wagonjwa, lakini pia kwenye mgao wa magari tumekosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba resources tulizonazo hazitoshi kusambaza kwenye Halmashauri zote, lakini angalau basi wale wenye matatizo makubwa zaidi angalau wawe wanafikiriwa. Fedha ni kidogo lakini kilichopo angalau tugawane wote. Wananchi wa Jimbo langu wanavyopata taarifa zinazoonesha Halmashauri nyingine zimepata fedha za ukarabati na miradi mingine ambayo viongozi wetu wameahidi na wao hawapelekewi hizi fedha, wanajisikia vibaya na kuona kama wanatengwa. Hivyo naiomba Serikali angalau itusaidie fedha hizi za ukarabati wa Vituo vya Afya vya Lupembe, Kichiwa na Sovi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Napongeza jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba vijijini na mijini kunakuwa na umeme. Hii itasaidia sana maendeleo ya viwanda nchini. Katika Jimbo langu kuna maeneo tayari wananchi wameitikia kaulimbiu ya Tanzania ya viwanda kwa kununua viwanda. Mfano Kijiji cha Ninga wamenunua Kiwanda cha Sembe chenye uwezo wa kuchakata tani 12 mpaka 20 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba kijiji hiki hakina umeme pamoja na ahadi za muda mrefu kwamba wataletewa umeme. Pia tuna Kijiji cha Madeke walinunua Kiwanda cha Kusindika Matunda lakini hakuna umeme. Pamoja na jitihada za Serikali kupitia mpango wa REA, lakini kasi yake bado ni ndogo. Hivyo tunaomba maeneo haya yapelekewe umeme haraka ili viwanda hivi vianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naipongeza Serikali hasa Waziri Mkuu kwa kufika Lupembe na kutatua baadhi ya changamoto mwaka 2017. Naomba Mwenyezi Mungu amjalie afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja iliyopo mezani.