Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kukupongeza kwa uongozi wako na pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi kubwa anayofanya kwa kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa juhudi kubwa anazofanya yeye binafsi katika kuhakikisha Tanzania ya viwanda inafika na hatimaye kuleta matumaini mapya ya kiuchumi kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kuchangia bajeti ya Waziri Mkuu. Ukurasa wa 34 wa Hotuba ya Waziri Mkuu imeelezea hali ya kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji na hifadhi. Lazima kama Taifa tujue idadi ya watu inaongezeka kila siku ilhali eneo la kiuchumi, yaani ardhi haiongezeki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamekuwepo na hali ya wanachi hasa Jimbo langu la Singida Magharibi ambapo wamekuwa wakipoteza mali zao ikiwemo mifugo, fedha, mazao na mambo mengine yanayoathiri maisha yao kwa ujumla. Katika Jimbo langu pekee wafugaji wamepoteza zaidi ya shilingi milioni 140 kwa kulipishwa faini kwa wanyama wao kukutwa katika maeneo yanayosemekana ni ya hifadhi. Hifadhi hii ambayo inafika maeneo ya Muhintiri, Ihanja, Ighombwe, Mwaru, Mtunduru, Minyashe na Makilawa haijawahi kutangazwa kisheria mahali popote kama hifadhi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wetu wanaongezeka, wakulima na wafugaji wanakosa mahali pa kulima na kuchungia mifugo yao kwa sababu ya mipaka ya hifadhi. Ni wakati muafaka sasa kutokana na ongezeko hili la watu, tunaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii sasa kushirikiana na TAMISEMI kuongeza maeneo ya wananchi na kupunguza ukubwa wa hifadhi ili kuondoa migogoro ya muda mrefu isiyokwisha ambayo inagharimu wakati mwingine maisha ya wakulima na wafugaji pamoja na mali zao. Naomba sana wananchi wetu wa kata nilizozitaja watengewe maeneo maalum ya kuchungia mifugo yao badala ya kila eneo lenye malisho kuonekana ni eneo la hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mapendekezo haya, naunga mkono hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ahsante.