Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na pumzi na kuwa tena katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape pole viongozi wangu wote wanaopitia changamoto za kisiasa, yote ni mitihani, lakini Mwenyezi Mungu atawavusha salama. Pia nimpe pole Mheshimiwa Spika kwa neema na kwa baraka ambayo pia Mwenyezi Mungu amemjalia na kurudi Tanzania akiwa katika hali ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitajielekeza sana kwenye changamoto za Muungano. Nimepitia kitabu cha Waziri Mkuu ukurasa wa 11 bila kukosea, nimeona masuala ya Muungano Mheshimiwa Waziri Mkuu ameorodhesha sehemu chache sana. Ni kitu ambacho hata ukurasa huu ametoka page hii ya 11 ameishia hapa, hata hii page hapa hakufika akaendelea huku kwenye Serikali kuhamia Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar bado kuna changamoto kubwa ya kero za Muungano. Nilikuwa nategemea angalau tunakuja humu kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano na sisi tumetokea upande wa pili na tumechaguliwa kwa ajili ya kuja kuwakilisha Zanzibar, tuambiwe ni kero ngapi za Muungano mpaka sasa hivi zilishapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuambiwe hata angalau ile Akaunti ya Pamoja tunaichangia kwa namna gani; Bara wanachangia shilingi ngapi na Zanzibar wanachangia shilingi ngapi ili wananchi wakapata ufahamu na wakajua sasa sisi huku labda hatuchukuliwi chetu kabisa au huku sisi hatutumiki, yakawekwa yale masuala yakawa wazi kabisa, kama ni kutangaza kwenye redio au magazeti ya Serikali ili wananchi wakajua huu Muungano ni wa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoungana tunatakiwa tuungane kwa maendeleo na kwa changamoto na zile sekta ambazo ni za Muungano zipewe kipaumbele. Leo tunataka tujue ni Wazanzibari wangapi ambao wameajiriwa kwenye sekta za Muungano, ni Wazanzibari wangapi ambao walikuwa wanakaimu zile nafasi na mpaka sasa hivi wamepata nyadhifa zao kamili, bado kunakuwa na kizungumkuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ikija Ofisi ya Makamu wa Rais pia ile bajeti ambayo inawasilishwa na Serikali haipelekwi kwa wakati muafaka. Sasa hizi kero za Muungano zitatatuliwa wakati gani? Leo tukihoji Akaunti ya Pamoja,

Mheshimiwa Mzee Dkt. Mipango akija hapa Zanzibar inasahaulika. Tuseme sisi Wazanzibari ndio hamtutaki au hatuna haki huku kwenye hili Bunge, mtuambie kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna wimbi la vijana, hawa vijana wengi mlikuwa mnasema ni vijana wa Zanzibar wanaenda kufanya kazi nchi za Uarabuni; Oman na sehemu zingine, lakini pia mpaka vijana wa Tanzania Bara wapo ambao wanafanya kazi Uarabuni. Sasa Serikali imejipanga vipi kusaini mkataba wa kimataifa ili kutambua hawa watumishi wanaofanya kazi nje ya nchi, hasa sehemu za Uarabuni, viwandani na majumbani ili hata zile haki zao waweze kuzidai wanapopata matatizo huko nchi ambazo wanafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie Zanzibar kuhusu masuala ya biashara. Tunatumia bandari ya pamoja lakini hii bandari imekuwa kizungumkuti. Zanzibar unakuta mtu anachukua kimzigo kidogo tu analeta Tanzania Bara, kisiwa kile kinategemea biashara, kinategemea utalii, kinategemea uvuvi, sasa anavyoleta vibiashara vyake kiasi ambacho angalau naye apate kujikimu unakuta analipa kodi mara mbili.

T A A R I F A . . .

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napokea taarifa ya kaka yangu na Wazanzibari tutasimama pale ambapo tunasimama tunakuwa kitu kimoja tunaitetea Zanzibar, Zanzibar ina Serikali yake, Zanzibar ina Baraza la Mawaziri, Zanzibar ina Baraza la Wawakilishi na sisi tumetumwa na wananchi kuja kutetea Zanzibar ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, haki za Wazanzibari tunataka zipelekwe kwa wakati muafaka. Ahsante kwa kunipa taarifa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe na niiombe Serikali ya Muungano iangalie wafanyabiashara wa Zanzibar isiwe inawatoza kodi mara mbilimbili. Kama kodi ilishalipwa nao kama wanakuja huku wapate haki sawa kama wanavyopata haki sawa huku Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie kwenye taasisi kama hii miradi ya TASAF ambayo inatolewa Zanzibar, ni kaya ngapi maskini ambazo zimenufaika au hizi pesa zinaishia tu kwenye mifuko ya watu wachache ambao wana uwezo. Hiyo pia tunatakiwa tupate taarifa ya kina na wale wananchi nao wapate taarifa ya kina kama zile fedha kweli zinawafikia walengwa au ndio zinaishia kwenye mikono ya watu wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Marais waliopita walithubutu kuiweka Zanzibar vizuri kulikuwa na zile kero wakazipelekapeleka mambo yakaenda. Nimshauri Mheshimiwa Rais na tumwombe naye afuate nyayo za Marais waliopita, aangalie Zanzibar. Kwa sababu hata kama mkikopa nje ni lazima mnaishirikisha Zanzibar, sasa Zanzibar nayo inanufaika vipi na hii mikopo ambayo inakopwa nje? Tuangalie kabisa masuala haya, ambalo ni fungu la Zanzibar lirudi Zanzibar, ambalo ni fungu la Tanzania Bara lirudi Tanzania Bara, hapo tutakwenda sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ajira kwa vijana. Vijana wengi wameingia kwenye matatizo, sasa hivi vijana wanasoma hawana ajira. Serikali imejipanga vipi kuwasomesha vijana ili waweze kujiajiri wenyewe? Kwa sababu tunaona vijana wengi wanaranda na vyeti mpaka vinapauka kwenye mifuko lakini suala la ajira hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kujua Serikali ina mpango gani hasa kwenye sekta ya kilimo vijana wanapata namna ya kujiajiri, wanapata elimu na mitaji. Tumesikia kuna pesa ambazo zilikuwa zinatakiwa zitolewe, shilingi milioni 50; hizi shilingi milioni 50 vijana wa Kitanzania ambao hawana ajira watanufaika vipi na hizi pesa angalau wajiajiri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wana vipaji, Serikali inatumia vipi hivi vipaji vya hawa vijana ili wapate kujiajiri? Tumesikia Tanzania ya Viwanda, kama huyu kijana hujamuandaa bado tutakuwa na vijana wengi maskani na wengi wataishia kwenye mambo ya uhalifu. Tuangalie ni namna gani ya kuwaandaa hawa vijana waende kwenye Tanzania ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye suala la vyama vya siasa. Siasa si ugomvi, siasa siyo uhasama, sisi sote ni wanasiasa na sisi wanasiasa wote ni ndugu. Leo mimi niko CHADEMA, kuna mwingine yuko CUF, kuna mwingine yuko CCM, lakini vyama vya siasa visitutenganishe. Tuangalie ni namna gani kila mwanasiasa anapata fursa sawa katika Serikali hii, hasa kwenye suala la mikutano na kutangaza vyama vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama chama cha siasa mitaji yetu ipo kwa wananchi, hawa wananchi tutawatumia vipi kama sisi sera za vyama tumekatazwa kuzitangaza. Hawa wapigakura wetu wataelewa vipi kama sisi chama fulani sera yetu ni hii na sera ya chama hiki ni hii. Kwa hiyo, vyama vyote vitendewe haki, viruhusiwe kufanya mikutano bila kubagua chama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Watendaji wa Serikali maana baadhi yao wanashindwa kufanya kazi zao wanamsingizia Mheshimiwa Rais…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)