Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa muda ni mchache nitakuwa na mambo machache sana ya kuchangia siku ya leo, lakini namshukuru Mungu kwa kuweza kunipa afya njema ili niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu, naomba nianze kwa kuchangia suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi. Katika ukurasa wa 14 wa hotuba ya Waziri Mkuu ameelezea ni namna gani Serikali imejitahidi kutoa mikopo ile ya asilimia 10 ya Halmashauri kwa akinamama, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache sana ya kuongelea juu ya suala hii la hii asilimia 10 ambayo inatolewa katika Halmashauri. Halmashauri nyingi sana hapa nchini hazitoi hii asilimia 10 kwa akinamama, vijana pamoja pamoja na watu wenye ulemavu ipasavyo. Hata hivyo, hatujaona Serikali ikichukua hatua yoyote juu ya Halmashauri zile ambazo hazitoi vizuri au hazitengi hii asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika ukurasa wa 14 wa hotuba ya Waziri Mkuu ameeleza pale kwamba, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.4 kwa vikundi 5,169 katika Halmashauri
153. Swali la kujiuliza hapa katika taarifa hii, tuna Halmashauri takribani 183, Halmashauri ambazo zimetoa mikopo ni 153, je, hizo Halmashauri zingine ambazo hazijatoa mkopo zimechukuliwa hatua gani mpaka kufikia leo hii? Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge hili wamekuwa wakizungumza sana kwamba Halmashauri ambazo hazitoi mikopo zipewe adhabu au kuchukuliwa hatua za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana wakati tunajadili bajeti tuliona Halmashauri ya Ukerewe pamoja na Halmashauri ya Magu katika Mkoa wa Mwanza, kwa masikitiko makubwa sana Halmashauri hizo hazikutenga kabisa fedha, lakini hatujaona hatua yoyote ile ikichukuliwa. Kwa maana hiyo watu hawa wamekuwa wakiona kwamba hizo pesa wana hiari ya kutoa au kutokutoa na inaonekana kwamba ni sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa stahili hii hatuwezi kuona maendeleo yakiwepo katika Mkoa wa Mwanza. Ukiangalia wanawake wa Mkoa wa Mwanza wanajitahidi sana kujishughulisha na shughuli mbalimbali na wanatarajia kabisa kwamba Halmashauri ziweze kuwasaidia kuwapa hii pesa ya mkopo ili waweze kufanya shughuli zao ndogo ndogo, lakini sasa Wakurugenzi wamekuwa wakifanya sijui niseme ni ukaidi au vipi mpaka hawatoi pesa hizo. Hivyo, naitaka Serikali iweze kuwachukua hatua Wakurugenzi wote ambao hawatengi pesa hizi za asilimia kumi kwa vijana, wanawake pamoja na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, naomba nitoe ushauri mdogo. Fedha hizi ambazo zimekuwa zikitolewa zinatolewa kidogo. Unakuta Halmashauri let’s say inatoa shilingi milioni 200 kwa vikundi vingi, unakuta mwisho wa siku vikundi vinapewa shilingi laki mbili mbili, mwisho wa siku hii pesa ambayo wanapewa inakuwa haileti tija katika kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoshauri ni jambo moja. Kwa kuwa sasa hivi Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na sera ya viwanda basi tuiunge mkono kwamba hizi pesa badala ya hawa akinamama kupewa cash in hand wakakopeshwa na mwisho wake wanashindwa kuzilipa waweze kupatiwa kwa style ya kwamba wanapewa labda mashine kwa ajili ya kuweza kutumia kutengeneza vitu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mkoa wangu wa Mwanza akinamama wengi wanajishughulisha na suala la kusindika bidhaa mbalimbali ambazo zinatumika majumbani kama vile viungo vya pilau, karanga, nyanya, tomato paste na pineapple ambayo inakuja kuwa pineapple sauce. Kwa hiyo, kuna vitu vingi sana ambavyo wanajishughulisha navyo. Kwa maana hiyo naomba Serikali iwasaidie akinamama hawa badala ya kuwapa pesa basi waweze kuwasaidia mashine ambazo zinaweza zikasaidia kuweza kuleta tija katika utengenezaji wa bidhaa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala zuri ambalo linaweza likafanyika. Katika Mkoa wa Mwanza akinamama nimebahatika kukaa nao kikao na wanahitaji wao vifungashio ili waweze kufungasha hizi bidhaa ndogo ndogo ambazo wanatengeneza. Kwa hiyo, naishauri Serikali Tanzania nzima na Halmashauri zote, fedha hizi badala ya kuwapatia cash kwa mkopo wawasaidie kwamba hawa akinamama …

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.