Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, na mimi naungana na Waheshimiwa Wabunge wote, ambao wamemshukuru Mungu kwa ajili ya afya yako tunaendelea kukuombea. Inawezekana hata sisi wenyewe tuna matatizo lakini bado hatujapimwa sawasawa. Kwa hiyo, kwa kweli tunakuombea Mheshimiwa Spika uendelee kuimarika ili uweze kuwatumikia wananchi wako wa Jimbo la Kongwa lakini na sisi Wabunge wenzako.

Mheshimiwa Spika, pongezi zangu za pili zinakwenda kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wanaomsaidia kazi. Hotuba ni nzuri, wameiwasilisha vizuri lakini imegusa maeneo mengi muhimu. Isipokuwa kuna baadhi ya maeneo Waheshimiwa Wabunge tutawakumbusha ili nanyi muweze kuongeza nguvu kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mungu sana kwa sisi wakazi wa Mkoa wa Dodoma kutupatia mvua za kutosha mwaka huu ingawa baadhi wa maeneo zimeleta majanga makubwa sana, kama uharibifu wa barabara inayotoka Dodoma Mjini kwenda Ilangali. Pale daraja limesombwa kwa hiyo, tuna uhakika kwamba Serikali watafuatilia kulitengeneza haraka ili kuweza kuwanusuru wananchi wa ukanda ule wa Tarafa ile ya Mpwayungu ili mazao yao ya biashara yaweze kufika kwa wakati hapa Dodoma ambapo kwa kweli ndiko kwenye soko kubwa tunalolitegemea.

Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa mengi nami naomba nitoe mchango wangu kidogo katika baadhi ya masuala ambayo yamezunguzwa mahali hapa.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa, kuna mambo ambayo yamefanyika kwa miaka miwili na nusu unaweza kusema ni miujiza. Kwa sababu matukio makubwa na ya kutisha tumeyaona yakifunguliwa na haya yote yakikamilika, reli ikakamilika, umeme wa maji ukakamilika, barabara zetu zimekamilika nina hakika kabisa kwamba yatachagiza maendeleo kwa kiwango kikubwa. Kwa hiyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunamwomba Mungu aendelee kumlinda.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ununuzi wa ndege; nataka niwakumbeshe baadhi ya watu wanaweza kuwa aidha wadogo au wamesahau. Uamuzi wa kulifufua shirika la ndege sio mara ya kwanza, baada ya iliyokuwa Jumuiya ya East Africa kufa na ndege nyingi kubakishwa nchini Kenya na sisi tukapata moja. Mwalimu Nyerere mwaka 1977 alifufua shirika lile kwa kununua ndege zinazokadiriwa kufikia kama nne au tano kwa wale watu wazima kama mimi mnaweza kukumbuka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Rais anachokifanya sasa anafufua shirika la ndege, ni kama vile una debe moja la mbegu unajiuliza ukaange ule au uende ukapande zizae ili waweze kutumia wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa wengine wamezungumza kwa dharau sana. Mtu anasema eti watu wanaenda kupiga picha kwenye ndege, watu wanashangilia ndege. Hapa wako Wabunge hapa wako humu ndani kwa sababu wameletwa na ndege. Wengine helicopter zilipokuwa zikikusanya watu ndiyo wakachaguliwa kuingia humu ndani ya Bunge wamesahau.

Mheshimiwa Spika, kuna chama hapa hakina ofisi ya mkoa, hakina ofisi ya wilaya, kimepata ruzuku zaidi ya mabilioni ya pesa, lakini huwa wanakodia ndege wakati wa uchaguzi ili Wabunge wao waweze kushinda. Wamesahau wanaingia humu ndani kutukana ndege maskini wa Mungu. Hivi kama kweli isingekuwa helicopter zinawasaidia, si tungeona mmejenga hata ofisi ya Mkoa?

Mheshimiwa Spika, tumeona NCCR Mageuzi mahali pengine wana ofisi, tuwameona CUF wana ofisi ya kueleweka lakini kuna chama kina kaofisi squatter pale Kinondoni wanapiga kelele kila siku hapa.

Mheshimiwa Spika, unashindwa kuwaelewa kabisa kwa nini msioneshe hayo maendeleo kwenye chama chenu kwa ruzuku mlizopewa? Mbona mnakodia helicopter hizo hizo? Kwa hiyo, kununua ndege Mheshimiwa Rais mimi naona ni jambo jema kwa sababu tutapanda sisi, watapanda Watanzania na lile shirika litaleta maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dharau kwenye viwanda vidogo si njema. Tunadharau mafundi cherehani, hivi hapa Waheshimiwa Wabunge bila mafundi cherehani si tungekuwa uchi tu hapa. Wengi tunashona tunashona nguo huko. Leo nataka niwaambie kiko kiwanda ambacho kinatusaidia sana juzi tu ndiyo nimekiona. Kiwanda cha Saloon jamani kumbe Wabunge tunalindwa sana na saloon. Kuna Mbunge mmoja amekosa kwenda Saloon siku tatu, sura yake imebadilika kabisa, wala siyo yeye.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunataka tuwashukuru sana hata watu wa saloon; akinadada wa saloon, akinababa wa saloon kumbe mnatuweka vizuri mpaka tunaonekana watu wa maana mbele za watu. Kwa hiyo hivi ni viwanda vidogo ambavyo Watanzania vinatuletea maendeleo lakini na sisi vinatuletea heshima fulani. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nataka nikubaliane, Waheshimiwa Wabunge wameongea vizuri sana hapa kuhusu gharama za uchaguzi, hili nataka niwaunge mkono. Kuna gharama kubwa sana kurudia chaguzi ndogo, lakini ambao wanaweza kutusaidia kwa kweli wanaweza kutusaidia Wapinzani, kwa sababu Serikali imeshaundwa Wabunge wengi wa CCM una uhakika Mbunge wa Upinzani hata akishinda haendi kubadili Serikali. Kwa nini mnaweka wagombea msiweke ili kunusuru mapesa hayo yaende kwenye maendeleo. Hakuna sababu maana hata ukishinda kiti kimoja, kilo moja ya sukari haiwezi kwenda kukolea kwenye pipa la maji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hakuna sababu ya vyama vya upinzani kuweka wagombea kwenye uchaguzi mdogo, maana tayari umeshafahamika aliyeshinda kafahamika kuna sababu gani za kuweka mgombea kwenda kupoteza hela za nchi. Kwa hiyo ni vema wakatuunga mkono, kuanzia sasa hivi kukitokea uchaguzi mdogo hakuna sababu ya wao kuweka mgombea na sisi tutapita bila kupingwa, hakutakuwa na gharama pesa zote zitaenda kwenye maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge wamezungumza sana leo hapa, wamezungumza kwa uchungu mkubwa sana. Mbunge mmoja wa CHADEMA amezungumza sana kuhusu Rais kutoka Kanda ya Ziwa na kwamba ni aibu sana Kanda ya Ziwa kukosa maji. Akasimama ndugu yangu Nape akasema Waziri Mkuu anatoka Kusini ni aibu kukosa maendeleo. Sasa najiuliza tuna Waziri Mkuu wa Kusini, tuna Rais wa Kanda ya Ziwa? Tuna Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jamani. Hatuna Rais wa Kanda, tuna Waziri Mkuu wa Jamhuri Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tusiwafanye viongozi wetu wakawa viongozi wa Kanda haiwezekani na mtakuwa hamtutendei haki. Hivi na sisi ambao Spika unatoka Dodoma mbona unawaruhusu wao kusema, kwa nini usituruhusu sisi wa Dodoma tuseme sana ili shida zetu zisikilizwe. Haitawezekana!

Mheshimiwa Spika, hili jambo lazima tujue Viongozi wakishakuwa wa Kitaifa, wanaongoza Taifa la Tanzania na sio sehemu walikotoka. Kwa hiyo kama Rais anahakikisha kwamba kwao hakuna maji lakini wengine wamepata huyo ndio Rais bora analitazama Taifa, hatazami upande wake. Kama Mheshimiwa Waziri Mkuu anaelekea sehemu zingine za Tanzania anazunguka kuhakikisha maendeleo yanapatikana huyo ndio Waziri Mkuu bora.

Mheshimiwa Spika, sikutegemea kwamba tuanze kuwagawa viongozi wetu kwa namna ya wanakotoka haiwezekani. Tusimame katikati tuishauri Serikali mambo ya msingi yafanyike ili nchi nzima ipate maendeleo. Nchi hii ni kubwa ndugu zangu, nchi hii changanya Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi ndipo unaweza ukaikaribia ukubwa wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, huwezi ukapeleka maendeleo kwa haraka na maeneo yote yakaridhika ndugu zangu, twendeni taratibu. Twendeni taratibu, twendeni awamu kwa awamu. Sehemu zingine ukipeleka sehemu zingine wanasubiria, sehemu zingine ukipeleka sehemu zingine wanasubiria, tutafika tu mahali na nchi nzima itapata maendeleo. Kwa hiyo nawaombeni sana Waheshimiwa Wabunge tuvute subira, viongozi wanahitaji kuungwa mkono.

Mheshimiwa Spika, watu wanazungumzia habari ya usalama…

T A A R I F A . . .

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yako Mheshimiwa Musukuma. Bahati mbaya tu mwenyewe hayupo maana na mimi nilitaka asikie lakini atakusikia. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba sana sisi kama Taifa kama nchi, viongozi wetu wagawanye rasilimali za nchi kwa usawa maeneo yote. Hata yale ambayo haya vivutio vikubwa vinavyokusanya hela nayo wayatazame. Kwa mfano tunaelewa sisi Dodoma hapa tuna zao la zabibu. Zao la zabibu hili likifunguliwa viwanda vya kutosha tutanufaika, watu wetu watapata pesa, watalima, watauza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mifugo, sisi tumepata kiwanda kizuri kabisa cha kuandaa ngozi pale katika Kijiji cha Idipu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu umeme upelekwe kwenye kile kiwanda. Kile kiwanda hakiishi kwa wakati kwa sababu umeme wenye nguvu kubwa haujafika pale kiwandani.

Mheshimiwa Spika, umeme ukiweza kufika na sisi ni wafugaji, tuna ng’ombe wengi wanachinjwa kwenye minada, ngozi nyingi zinapelekwa pale, wananchi wa jimbo la Mtera nao watapata maendeleo makubwa. Tutanufaika na hii hoja ya uanzishwaji wa viwanda maana kiwanda tayari kinajengwa.

Mheshimiwa Spika, naomba tuitazame Tanzania katika yale maeneo ambayo yamesahaulika kwa muda mrefu tuyatupie macho. Maana kuna mwingine ana maji ana barabara nzuri akija hapa kupiga porojo ni sawa, lakini kuna wengine vitu vyote vitatu hawana, tuangalie kimoja wapate. Watu ambao wanaishi kijijini; tunapoteza akinamama wengi sana wakati wa kujifungua, kwa sababu unaweza kukuta wakati wa kujifungua njia imefunga, maji yamekata barabara, gari haliwezi kufika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kupata ambulance, lakini kuna mahali ambulance hazipiti kwa sababu barabara ni mbovu. Tumeondoa barabara kutoka Halmashauri tumezipeleka TARURA, lakini ukitazama uwezo wa TARURA na bajeti yao bado ndogo bado hai-reflect maendeleo ya barabara za vijiji. Kwa hiyo, tunaomba waongezewe pesa, ziwe nyingi ili waweze kutengeneza zile barabara kwa kiwango kinachotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwatazame sana! Watu tumejenga sekondari za Kata, tumejenga mashule vijijini, lakini bado namna ya kuwachagiza wananchi wa vijijini ni umeme ufike kwa wakati. Kuna baadhi ya maeneo hayana umeme Tarafa nzima ya Mkwayungu haina umeme. Tukiwapelekea umeme watu wa Mkwayungu baadhi ya mambo yao mengi watafanyia kule, watakamua alizeti zao kule, hawana haja ya kuzileta Dodoma Mjini. Dodoma Mjini wataleta mafuta. Kwa hiyo viwanda vidogo vitaanzishwa Mkwayungu.

Mheshimiwa Spika, nakuomba sana tunaposimama hapa na sisi lengo letu ni kuwaunga mkono na kuwatia moyo Waheshimiwa Mawaziri. Ukilitazama Baraza hili ni dogo kuliko lililopita, lakini Mawaziri wake wanafika kila kona ya Tanzania, lazima tuwapongeze na kuwatia moyo. Hawa ni binadamu usiku kucha wanasafiri wanafika kwenye majimbo yetu wanaongea na wananchi, lazima na sisi tuwaunge mkono.

Kwamba Waheshimiwa Mawaziri tunatambua kazi kubwa mnayoifanya sisi kama Wabunge wenzenu tunawaungeni mkono, endeleeni kuchapa kazi ili Taifa hili liweze kusogea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wamezungumza hapa kuhusu amani. Amani na utulivu ipo lakini ipo kwa sababu na wahalifu nao wapo. Tuwaombe Serikali waendelee kuwasaka wahalifu kwenye kila nyanja ya uhalifu unavyotokea. Tusiichafue Serikali kwa sababu ya kosa moja.

Mheshimiwa Spika, ikitokea kiongozi mmoja wa dini amekengeuka pengine amezini Mungu aepushe mbali hatuwezi kulaumu dini nzima, haiwezekani. Tunamlaumu huyo huyo kwa kufanya hilo kosa. Kwa hiyo lazima tukubaliane, kwamba uhalifu upo lakini tuitake Serikali kupambana na uhalifu kama inavyofanya siku zote.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.