Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimefurahi sana kwa kuwa umerudi salama kutoka katika matibabu, tunakuombea Mwenyezi Mungu afya yako izidi kuimarika na Inshallah itaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitazungumzia sana habari za siasa na hususan hali ya kisisasa katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye utangulizi pale, misingi ya Katiba na kwa kuwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, undugu na amani. Kwa hiyo, Katiba yetu inazungumzia uhuru na haki ndiyo jambo la kwanza ili nchi yetu tuwe na mapenzi, kupendana, undugu na amani, lakini kama nchi yetu haitokuwa na uhuru na haki undugu na amani hautokuwepo katika nchi yetu, ndiyo msingi kwa Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nia yetu ni nchi yetu na jamii yetu ijengwe kwa msingi huo, kwa hiyo kwa msingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake huamini Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na Mahakama iliyowakilisha kwa nchi pia yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ukurasa wa saba inasema, nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu ili hali mimi kwa utafiti wangu naona hizi habari siyo za kweli kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina matatizo sana, kama hatukubali kama nchi ina matatizo naomba tutegemee kwamba nchi yetu huko mbele tunakokwenda hali itakuwa mbaya sana. Mimi mwenyewe nilimuandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani, kuna gari Noah ilifika Kilwa tarehe 29 Novemba, ikampigia simu kijana mmoja anaitwa Abdallah Said Ngaranga wakamwambia njoo uchukue mzigo wako hapa Kilwa Masoko, Mheshimiwa Abdallah Ngaranga alifuatana na Mheshimiwa mmoja anaitwa Hamisi Mtori, kufika pale Kilwa Masoko ile gari ya aina ya Noah nyeusi wakamuita yule kijana njoo ndani uchukue mzigo, alipoingia ndani yule kijana, kijana wa pili akawa yuko nje alivyoingia ndani wakamuita na yule wa pili, yule wa pili kaona hata Noah hii nyeusi siielewi akakimbia na askari mmoja akamkimbiza yule kijana akaingia katika makapa akapiga risasi yule askari, lakini jamaa hakusimama, akaondoka akafika Kivinje.

Mheshimiwa Spika, nikaitwa mimi kwamba mtu wetu mmoja katekwa, kwa bahati nzuri nikapiga simu Polisi Masoko nikaambiwa kwamba kweli yule kijana amekamatwa yuko polisi hapa. Usiku huo wakakamatwa vijana tisa, nikaenda polisi siku ya pili nikaambiwa kweli vijana walikamatwa walikuwepo hapa, lakini hatuwezi kuwaandikia kwa sababu walikuwa wamepitia tu. Nikaandika barua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, katika vijana hao 11 wakarudishwa tisa na mpaka sasa hivi wako Kilwa, lakini wawili hawajarudishwa mpaka leo. Mmoja anaitwa Ndugu Ally Mohamed Shali na mwingine anaitwa Ndugu Yussuf Kipuka mpaka leo hawajarudishwa, lakini tuna uhakika walichukuliwa, walikuja kituo cha Polisi Kilwa Masoko mpaka leo hawajarudishwa na wazazi wao hawajulikani wapi walipo.

Mheshimiwa Spika, hii ni ukweli kabisa ninataka leo Waziri atupatie vijana wetu wawili hawa, ushahidi upo tarehe 21 Julai, askari hao hao walikwenda Kijiji kimoja cha Chumo wakaenda msikitini usiku saa saba, wakapiga risasi msikitini mle, wakawachukua watu 10 msikitini. Tumekwenda asubuhi damu zimetapakaa ndani ya msikiti, katika watu hao wakarudi wote 10, katika 10 waliorudi mmoja kafa, mmoja hana jicho, mmoja wakamwambia wewe unafuga ndefu wamemchoma ndevu zake, wamemnyoa ndevu kwa kumchoma moto, watu hawa wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mnatuambia kwamba nchi hii ina amani na utulivu mimi sielewi? Watu hawa wapo na huyo mtu mmoja amekufa tumemzika na majina yao nitakutajia. Samahani kidogo nimeandika aliyefariki anaitwa Ismail Bwela, aliyetoka jicho anaitwa Mbaraka Masaburi, aliyechomwa ndevu anaitwa Muharam Yalife, wapo! Wamepigwa risasi msikitini, mmoja amekufa na Serikali haijasema chochote mpaka leo na wamerudishwa wako Kilwa pale.

Mheshimiwa Spika, unaposema nchi hii ina amani na utulivu sielewi! Ninawaunga mkono waraka uliotolewa na Maaskofu. Nawaunga mkono Maaskofu mlichokisema ni sawasawa na maneno ya Maaskofu ni maneno ya Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii nchi imeharibika leo waislamu lazima wasiseme, tumetengenezewa jambo tunaitwa magaidi, kwa hiyo Mashekhe wote wa kiislam wakitaka kutetea haki zao kuhusu waislam wenzao tunaambiwa aah!Ninyi magaidi mnawatetea magaidi na ndiyo maana waislam hawawezi kusema sasa hivi, watasema vipi wakati wao wanaambiwa ni magaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawapongeza Maaskofu sasa hivi matumaini kwa Watanzania ni sehemu mbili tu Mahakama na Maaskofu, lakini waislamu hatuwezi kusema! Akipigwa muislam akisema unaambiwa unatetea magaidi eeh! Waislam wote tumerudi nyuma, tunaomba sana…..

Mheshimiwa Spika, nitunzie muda wangu.

T A A R I F A . . .

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, taarifa nimeipokea. Wewe tulia nitamjibu mwenyewe huyu.

Katika watu wanaolaani kwamba wale watu wamepigwa kwa makosa wale askari pamoja na mimi, lakini siwezi kuacha kusema watu wengine wakionewa haiwezekani!

Mheshimiwa Spika, polisi wakionewa nitasema, wananchi wakionewa watasema! Nia yetu hapa tunataka amani na utulivu ndiyo hoja, sijasema kwamba waliopigwa risasi polisi sijasema hivyo, nimesema polisi wameiniga msikitini wamewapiga watu risasi sasa mkatae kwamba hamkupiga watu risasi.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Rufiji hiyo ilikuwa watu wanapigwa risasi wanauawa, mkatengeneza mazingira kwamba wale wanaopigwa ni wa CCM na mkahalalisha Viongozi wetu wa CUF wamekamatwa na mpaka sasa hivi hawajulikani walipo, nitawatajia watu sita waliokamatwa katika operation mpaka sasa hatujui walipo, nataka tujue wako wapi.

Mheshimiwa Spika, basi nitakuletea majina ya hao watu sita waliokamatwa tunataka tujue wako wapi, ni wa Rufiji nitakuletea majina. Ahsante sana.