Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, na mimi ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania kwa ujumla kukukaribisha hapa Bungeni kwa mara nyingine. Ni faraja kukuona unaongoza tena jahazi lako hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuipongeza Serikali kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kwa nafasi hii tunawapongeza sana wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, watendaji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Tunafahamu kabisa kwamba mjadala huu unajenga mustakabali wa Taifa kwahivyo kwa yale mazuri yanayofanywa ni vema kuyasemea.

Moja, nikukupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa unayoifanya wewe kama msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali. Umefanya ziara nyingi sana mikoani na maelekezo yako yamesaidia sana kuongeza kasi ya utekelezaji na kurekebisha kasoro ambazo zilikuwepo za kiutendaji. Sengerema tutakukumbuka sana kwa ziara uliyofanya ndani ya mwezi mmoja na nusu uliopita.

Mheshimiwa Spika, ushahidi wa kwamba Serikali inawasikiliza Wabunge na jamii kwa ujumla ni taarifa iliyotolewa sasa hivi na Mheshimiwa Mkuchika, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais. Hongereni sana Serikali kwa kusikiliza mawazo ya wawakilishi wa wananchi, wafanyakazi,
watumishi wetu wa darasa la saba wamekuwa na kilio cha muda mrefu na hivi ndivyo ambavyo inatakiwa Taifa tuendelee kulijenga kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimia Spika, heshima ya Serikali ni pamoja na namna ambavyo inatayarisha nyaraka zake na kuzitunza. Hapa nazungumzia Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Mimi nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge lako Tukufu mara kadhaa tumetembelea Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na kwa miaka mingi amekuwa na changamoto nyingi sana, lakini niseme kuanzia mwaka jana Serikali imechukua hatua kubwa na kwa hili kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tunampongeza sana Mheshimiwa Jenista Mhagama kama Waziri mhusika kwa hatua za kurekebisha management pale.

Mheshimiwa Spika, ninachokiomba kwa Serikali ni kukamilisha management pale. Mkurugenzi Mtendaji au CEO wa pale sasa hivi anakaimu, lakini amefanya kazi kubwa sana kwa kipindi ambacho amekuwa akikaimu. Naomba Serikali ikamilishe uteuzi, mpate Mtendaji Mkuu ili shughuli ziendelee vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamezungumzia pia kwa wale ambao tumeguswa na hii programu ya MIVARF. MIVARF ni programu ambayo inaratibiwa na Serikali kuhusu miundombinu ya masoko lakini uongezaji thamani wa mazao na huduma za kifedha vijijini. Kwa wale tunaoguswa ni programu maalum sana na nzuri sana. Tunashukuru sana kwa wale ambao wamekuwa wakiunga mkono na kujua kwamba kuna taasisi mbalimbali za kimataifa, hii kwa kweli ime-compliment juhudi za Serikali.

Mheshimiwa Spika, Sengerema tuna mradi mkubwa wa umwagiliaji wa maji, uliibuliwa miaka mitano iliyopita, gharama yake ni bilioni 2.5, Serikali ilishaleta milioni 700 lakini
1.8 billions hatujapata. Tumeanza kuzungumza na wafadhili wa MIVARF wako tayari kutusaidia na ndiyo maana tunasema hii awamu ya pili ambayo Serikali inaendelea na mazungumzo tunaiomba sana ikamilishwe haraka kwa sababu inakuja kuisaidia Serikali mahali ambapo ina upungufu wa fedha programu hii itasaidia kukamilisha miradi iliyokwama ikiwemo mradi wa Sengerema wa Katunguru Irrigation Scheme.

Mheshimiwa Spika, ukisoma ukurasa wa 45 kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inazungumzia habari ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA). Tumeanzisha Wakala na tumeukabidhi majukumu ya kufanyia matengenezo barabara za mtandao wa vijijini, madaraja yake na makalvati mbalimbali. Kuna barabara tumeipa Wakala huu jukumu la kutengeneza kilometa 108,946.2

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa taarifa iliyotolewa na Mheshimwa Waziri Mkuu ya utekelezaji kwa mwaka huu wa fedha ni kilometa 4,183 tu ndizo ambazo zimetengenezwa ni kwa sababu ndicho kiwango cha fedha tulichokitenga.

Mheshimiwa Spika, ninachoomba kulishauri Bunge lako tukufu ni kwamba kwa hatua tuliyonayo hii, tukienda kwa speed hiyo kwa huo mtandao wa kilometa zaidi ya 100,000 itatuchukua miaka 26 kuweza kurekebisha barabara zetu za vijijini, leo tunafahamu kwamba zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania na hasa uchumi wao unategemea vijijini. Ushauri kwa Bunge lako tukufu na kwa Serikali ni kwamba, ule mgawanyo wa fedha za Serikali kutoka kwenye Mfuko wa Barabara ambao sasa hivi unasimamia kwa asilimia 70 barabara kuu na za mikoa na asilimia 30 kwa barabara za vijijini, tuurekebishe ili tuuwezeshe Wakala huu ufanyekazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba twende 50 kwa 50 na ninasema hilo nikitambua kwamba tuna umuhimu wa kutengeneza barabara za vijijini na mijini, lakini ukilinganisha uwiano wa uwezekano wa kupata mikopo na Serikali imethibitisha hivi karibuni kwamba tunakopesheka. Kwa wale wanaoweza kutukopesha kwa masharti nafuu wataweza kutukopesha kirahisi kwa barabara za mijini ama zinazounganisha mikoa ama barabara kuu, lakini siyo rahisi sana kupata mkopo kwa barabara za vijijini. Tufanye kama tulivyofanya kwenye Umeme Vijijini (REA) tumetumia fedha ya ndani na leo tunajisifu kwa sababu ya hatua tuliyofikia ya kutenga bajeti mahsusi kutoka kwenye vyanzo vyetu. Ninaomba tuurekebishe mgawanyo uwe fifty/fifty vinginevyo uwe 45 kwa 55 ili tupate fedha nyingi za kurekebisha barabara zetu za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine sambamba na hilo ambalo wenzangu wamelizungumza, Wakala huu bado unaeleaelea uwajibike sasa, taratibu na kanuni zirekebishwe, uwajibike kwenye Halmashauri husika na hasa za kule kwenye Wilaya zetu kwa sababu hao ndiyo watakaoshirikiana nao kubaini barabara zipi mbovu na hata mipango wanayoipanga ya kwenda kutekeleza hizo barabara, tukifanya hivyo tutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 56 unazungumzia afya, nizungumzie eneo moja tu la huduma za tiba za kibingwa. Taarifa za Serikali kama kumbukumbu yangu iko sahihi na Waheshimiwa Wabunge wengine ni kwamba ugonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road tumekuwa tukitaarifiwa zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaofikishwa pale kwa matibabu wanatoka Kanda ya Ziwa. Ombi langu ni moja tu, Kanda ya Ziwa tuna Hospitali ya Rufaa Bugando tunaomba ipewe kipaumbele, washirikiane na Bugando Hospital.

Mheshimiwa Spika, najua Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu yupo hapa wamekuwa wakishirikiana vizuri sana, tunaomba waongeze kuna kifaa ambacho kinahitajika ili watekeleze vizuri utaratibu wa kuwasaidia Watanzania wenye magonjwa ya saratani na kwa sababu ni eneo ambalo linahusu wagonjwa wengi, nadhani mkiwasaidia tutafika mbali zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Nape amezungumzia uwekezaji katika sekta ya gesi, nalizungumza suala hili ikiwa ni eneo ambalo ninalifahamu kidogo. Nimekuwa nikiskia Serikali inasema mkakati uliopo ni kwamba inapofika mwaka 2020 tuwe tumeshafikisha megawati 5000 na mwaka 2025 tufikishe megawati 10,000. Kiufupi tu ni kwamba kwa vyanzo vilivyopo ikiwemo cha maji cha Stieglers Gorge havizidi megawati 5000 sasa nataka kujiuliza tunatokaje kuanzia hapo mwaka 2021 kwenda kwenye mwaka 2025 kama hatufanyi mipango ya kuendeleza gesi sasa hivi ikiwemo na huu mradi mkubwa wa kuchakata gesi wa LNG ambao amezungumza Mheshimiwa Nape. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania kama walivyo binadamu wengine wanahitaji kuishi kwa matumaini kwa kupewa mipango ya Serikali. Tunapowataarifu Watanzania kwamba mipango imefikia lengo fulani, tunawajenga kisaikolojia lakini tunawandaa pia kupokea fursa zinazokuja na uwekezaji wa namna hiyo. Kwa hivyo, ninachosisitiza ni kwamba, kwa sababu bomba la gesi tulilo nalo sasa hivi linatumika kwa asilimia sita tu kwa taarifa ambazo zimekuwa zikisikika, asilimia 94 haijatumika, tuendeleze miradi hii, tuhakikishe kwamba gesi pia tusiiache pembeni, kwa sababu mipango yake ya uwekezaji katika gesi inachukua muda mrefu sana siyo suala la miaka miwili/mitatu; kwa hiyo, tusipoanza mapema maana yake ni kwamba tunajiweka katika mazingira magumu mno kufikia lengo ambalo tumelikusudia megawatts 10,000 za umeme mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali izingatie suala hili, tulifanyie kazi, wafunguke pia kwenye upande wa sekta ya gesi. Lakini tunafikaje huko?

Mheshimiwa Spika, sisi wenyewe hatuwezi kuifadhili miradi hii, njia pekee iliyopo na juzi Mheshimiwa Rais amefungua ukurasa mpya wa mahusiano na sekta binafsi, tuipe kipaumbele sekta binafsi itusaidie, isaidiane na Serikali katika kuendeleza miradi hii, vinginevyo kama tulivyo kwa fedha zetu, tunajenga SGR, tunanunua ndege zetu wenyewe, tunajenga Stieglers Gorge kwa fedha zetu, hatujakamilisha miundombinu ya elimu, bado tuna changamoto katika afya, tunataka fedha nyingi kwa ajili ya TARURA, tunahitaji kuboresha huduma za maji, sisi wenyewe kama tulivyo, kama Serikali hatuwezi kufanya hivi na ni nchi chache sana duniani zilizofanikiwa kwa kutegemea vyanzo vyake vyenyewe bila kuishirikisha sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba tuipe sekta binafsi kadri itakavyowezekana ushirikiano mkubwa ili waweze kutusaidia kutufikisha kwenye malengo ambayo tunakusudia.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni kwenye maji. Mwaka jana tuliongeza shilingi 50 kutoka kwenye lita ya mafuta, naomba tena mwaka huu tuongeze shilingi 50 nyingine ili tuongeze kasi ya kufikisha huduma za maji katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa na fursa hii, nawatakia kila la kheri. Naunga mkono hoja.