Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na namshukuru Mungu kwa uhai na afya na ninaendelea kuwashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kunipa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ujumla wake, lakini kuna maeneo ambayo inabidi tuseme. Biharamulo hivi tunavyoongea sasa hivi, kuna kilio kikubwa sana cha wakulima wa pamba. Wakulima wa pamba wameingia kwenye dimbwi ambalo hawajui na hatujui tunatoka vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dawa kwa ajili ya kupambana na wadudu, tunaambiwa wanaletewa dawa aina ya Duduall, Duduba na Bamethrin. Dawa hizi hazifanyi kazi, kabisa na kuna maoni mara tatu. Wataalam wetu wa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya pale wanasema tatizo la kwanza ambalo wanadhani ndiyo linasababisha hili inawezekana ni kukosekana kwa mwendelezo wa upatikanaji wa dawa kwa sababu mkulima anapotakiwa kuweka dawa kwenye pamba wiki ya mbili, lakini labda anatakiwa wiki ya nne apate dawa nyingine isipokuja kwa wakati hao wadudu wanajenga usugu.

Lakini kuna malalamiko kutoka kwa wakulima hao, wakulima wanasema wanapokwenda kwenye maduka binafsi wakachukua dawa kwenye maduka binafsi mbali na hii dawa inayoletwa na Bodi ya Pamba dawa hii inafanya kazi. Hiyo ni hypothesis inayoonesha kwamba inawezekana kwenye dawa inayopita kwenye Bodi ya Pamba kuna uchakachuaji na wamefikia hatua ya mbali wakulima wakafanya utafiti wao wenyewe (wakulima wa Biharamulo wana akili sana) kuna tuhuma kwamba wakulima hawa hawatumii vizuri dawa ndiyo maana haifanyi kazi. Wakamtafuta Afisa Ugani wakampeleka kijijini, pale Kijiji cha Kagondo, Kata ya Kabindi wakamwambia chupa ya dawa hii hapa changanya mwenyewe weka kwenye shamba mwenyewe. Akafanya hivyo mtaalam wakaenda siku inayofuata wakakuta wadudu sio tu wapo, inawezekana wameanza kuota na macho wanatazama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakasubiri wiki moja wakaenda wakatazama. Wadudu wapo! Wakasubiri wiki tatu, wakamuita na Afisa Ushirika akaja kutazama, wadudu wapo! Kwa hiyo, kuna tatizo. Inawezekana kuna uchakachuaji wa dawa kwenye Bodi ya Pamba kwa sababu wakulima hawa wakienda kuchukua dawa kwenye maduka binafsi inaonekana dawa ile inafanya kazi. Sasa tuna maswali mawili.

Swali la kwanza, tunatatuaje tatizo kwa msimu unaofuata? Lakini swali la pili, tunawafidia vipi wananchi hawa kwa sababu Bodi ya Pamba ambayo ni taasisi ya umma ndiyo imewaletea dawa na tuna sababu kwanini tunataka kudai fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa pamba kwenye msimu juzi ulikuwa hekta 500 kwa Wilaya nzima, msimu jana heka 900 na msimu huu heka 2,800 na mwaka jana msimu uliopita wameuza wamepata jumla ya kilo milioni sita. Kwa hiyo, uzalishaji umepanda sana kwa sababu ya uhamasishaji na wananchi walikuwa na matumaini sasa ya kuondoka kwenye umaskini. Msisahau Biharamulo ndiyo Wilaya ya pili kwa umaskini nchi hii kwa kipato cha ngazi ya kaya, mnafahamu. Sasa kama kupitia kilimo ndilo eneo ambalo wananchi wanaweza kujiinua lakini Serikali na vyombo vyake havitimizi wajibu wao ina maana tunakaa kwenye mzunguko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama ukurasa wa 29 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna ushahidi kabisa wa kitu kinaitwa The know-do gap. Tunachojua ni moja lakini tunapokwenda kwenye field hatufanyi hiyo moja, tunafanya mbili. Anasema kabisa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba moja ya matatizo yanayosababisha kilimo kisiwe moja ya nyanja zetu ambazo zinatuinua kiuchumi ni, kuna habari ya ukosefu wa utafiti, ukosefu wa pembejeo, ametamka Waziri Mkuu, tunafahamu lakini hatufanyi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza wananchi wangu wakulima wamenipigia simu wameniambia chupa mbili za hii dawa ya Duduall ambayo imekuwa inatumika kama ushahidi. Tunaiomba Serikali iende ikafanya tathmini ya hiyo dawa tuone kama je ni kweli kuna uchakachujai ama ni tatizo lile lile la ucheleweshaji wa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri Mkuu tufanye tunachoamini ambacho tumeandika kwamba tunavyoshindwa kufanya huduma ya ugani kwa wakulima ni moja ya sababu kubwa ya kilimo kinakuwa hakina tija kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 27, Mheshimiwa Waziri Mkuu anataja kabisa kwamba tutaweka mkazo kwenye mazao matano yakiwemo pamba lakini ukurasa wa 32 anasema; “tumeamua kwa dhati kusimamia sekta ya kilimo.”

Sisi huko kwetu Kagera kuna msemo unasema wakati mnakula chakula cha mchana au usiku pale, mtoto ambaye ni mroho ama mlafi unamuona wakati wa kunawa. Kwa hiyo, kama Waziri Mkuu anatuhakikishia sasa anaweka kwa dhati tunaomba aanze na Biharamulo, twende tukatazame hizo dawa ambazo tumetunza sample, twende tutazame tuone tatizo liko wapi, tatizo liko kwenye uchakachuaji, kukosa consistency ya kuleta dawa ama tatizo liko wapi? Hiyo ndiyo itakuwa alama sahihi kwamba huyu mtoto anayenawa sasa hivi vizuri hatakula kwa ulafi. Nakushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee habari ya Waziri Mkuu amesema ukurasa wa 38 na 39 habari ya madini. Tunatambua Mheshimiwa Rais anaendelea na utaratibu wa kuunda ile Kamisheni. Tunaomba twende kwa kasi kwa sababu wananchi wa Biharamulo tumepata maeneo ya uchimbaji wa madini pale, tunahitaji kupata leseni, tumeshajipanga. Huu muda unavyokwenda tunaendelea kupoteza ile momentum na tutakosa fursa ya kufanya kazi yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo viwanda. Mheshimiwa Mwijage yuko hapa. Nimeona kwenye ukurasa wa 35 wa hotuba ya Waziri Mkuu tunasema viwanda 3,000. Naomba tusiiweke too general tuzungumze kwenye hivyo 3,000 vingapi ni vikubwa, vingapi ni vya kati na vingapi ni vidogo, lakini pia twende mbali zaidi, tutafute utaratibu wa incentive, namna gani mtu unamvutia. Unajua kuwekeza kiwanda Dar es Salaam kwa sababu ya baadhi ya miundombinu na kuwekeza kiwanda Biharamulo kuna tofauti! Tukiwawekea hawa private sector incentive kwamba akiwekeza Biharamulo kuna zawadi fulani ambayo anaipata kikodi ili apunguze maumivu kwa sababu ya habari nyingine za miundombinu ya aina mbalimbali itamfanya aende kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ikitokea na mimi Mbunge au Mkuu wa Wilaya, mtu yeyote kutoka Biharamulo akawezesha kupata wadau ambao wataweka kiwanda pale Halmashauri nayo ipate incentive namna gani Halmashauri itapata incentive kikodi badala ya ushuru kwa sababu tunajua vyanzo vingi vimehamishwa kutoka kwenye Halmashauri kwenda Serikali Kuu. Tukienda namna hiyo tutapata namna sahihi ya kuwezesha hata kule ambako kimiundombinu ni vigumu watu kwenda, lakini ukiwawekea uvutiaji watakwenda na mambo yatakaa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo niongelee uwezeshaji wa makundi maalum. Naomba tuwakumbuke Watanzania wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Ni kundi maalum ambalo linashiriki kwa kiwango kikubwa kwenye ile habari ya 90-90-90. Asilimia 90 ya watu wanaodhaniwa kuwa na virusi vya UKIMWI wapime, asilimia 90 ya waliopima watumie dawa na asilimia 90 ya wanaotumia dawa watumie vizuri ili ifubae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakitumia dawa vizuri siyo faida ya kwao peke yao ni faida ya umma mzima. Anapokuwa ametumia dawa kwanza anaondoa utegemezi wa kiuchumi kutoka kwa umma mzima kwa sababu ana uwezo wa kufanya kazi, lakini kama unampa uwezeshaji anaweza akapata Bima ya Afya yeye na familia yake wasiwe na utegemezi. Pia hiyo ni namna moja ya kufanya prevention kwa sababu mnajua prevention is better than cure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo hili la walimu wa sekondari kutolewa sekondari kwenda shule ya msingi, najua ni dharura na Mheshimiwa Ndalichako naamini ananisikia na nilimwambia kidogo kule kwenye Kamati, naomba nisisitize. Nafahamu ni dharura, lakini ni kwa kiwango gani hili tunalifanya kwa muda mfupi lisiwe endelevu? Kwa sababu likiwa endelevu hili halina tofauti na ile habari ambayo nakumbuka nimewahi kumwambia Waziri, jamaa mmoja alienda kwa fundi wa kitanda akamwambia nitengenezee kitanda cha nne kwa sita, fundi akakosea akatengeneza nne kwa tano. Jamaa alivyokwenda kupima pale akakuta miguu inazidi anamuuliza fundi, tufanyaje? Fundi anasema hapa njia rahisi kabisa ya mkato ni kukata miguu ili kitanda kitoshe. Tukienda namna hiyo kwa muda mrefu, kwamba kazi yetu itakuwa ni kurudisha walimu wa sekondari shule ya msingi kuna mzunguko ambao tutaingia, walimu wa sayansi haitatokea siku watoshe.

Moja; sample chupa mbili za nusu lita ziko Biharamulo; moja anayo Extension Officer wa Kata ya Kabindi, moja anayo Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika.

Mbili; naamini na ninadhani, utaniongoza ni kazi ya mnyororo wa Serikali kuhakikisha zinatoka huko zinakuja huku kwa sababu ziko mikononi (hasa hiyo moja iko kwa Afisa wa Kilimo), lakini jambo la tatu narudia na utatazama Hansard. Nimesema hypothesis ni tatu, moja; kukosa consistency ya kupeleka dawa ndiyo kunasababisha wadudu wasiwe, mbili, dawa inayoletwa na Bodi ya Pamba haiui kwa sababu wananchi wanasema ukienda kwenye maduka binafsi wanayopata inaua. Tatu, kuna hypothesis kwamba wakulima hawatumii vizuri ndiyo maana walimleta Afisa Ugani wakamthibitishia na yeye yupo aletwe pamoja na sample. Maana ya hypothesis ni kwamba hujajibu mnatakiwa kufanya kazi mjibu kipi ndiyo kinasababisha. Ahsante.