Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Bunge lililopita nilisimama hapa na Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(2) juu ya kazi za Mbunge, kazi ikiwa ni kuisimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana nishauri Waheshimiwa Wabunge tutimize majukumu yetu ya kikatiba. Hii habari ya kusimama Bungeni na kusifia sifia wakati mambo yanaharibika haitatusaidia kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unashangaa mtu anaunga mkono anasema asilimia mia moja halafu anaweka neno lakini sasa mimi kama mwalimu haiingii akilini; kama una mambo yameharibika ueleze yalivyoharibika tu usianze kutafuta mambo mazuri wakati hayo mazuri hayapo. Kama unaona hayapo hili Taifa ni letu wote; tuisimamie Serikali na kuishauri, ndivyo ambavyo Katiba imetuambia, hii hapa ibara ya Ibara ya 63. Sasa kuna watu humu wanaremba remba wanapamba mambo ambayo hayapo, wanaogopa kuishauri na kuisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninyi Wabunge wa CCM mlikuwa na nafasi nzuri sana ya kuisimamia Serikali yenu inayoongoza ya Chama cha Mapinduzi, maana sisi tukitoa ushauri huku bahati mbaya tunaonekana kama ushauri wetu bado hamuukubali, lakini hatutachoka kusema, tutaendelea kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati zote zimekwenda kwenye ukaguzi wa miradi, lakini fedha za miradi ya maendeleo hazikwenda/hazijapelekwa. Ilikuwa ni aibu wakati fulani mnakwenda kwenye mradi hata shilingi moja haijapelekwa, mnakwenda kukagua fedha za wafadhili wengine tu waliojitolea kuleta fedha, ninyi za kwenu nchini hazijapelekwa. Hili nalo tukishauri mnatuona wabaya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa tulisimama tukashangilia bajeti hii ya mwaka, ya karne, haijawahi kupatikana, haya ndio madhara yake sasa sisi tuliona haikubaliki ndiyo maana tulikataa kuiunga mkono. Tulikataa kuunga mkono kwa sababu tulijua ni bajeti ya mbwembwe ya maandishi mazuri kwenye karatasi utekelezaji wake haupo, tunafanyaje hii kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia miradi inatekelezwa, fedha za maendeleo kwenye wizara zinapelekwa asilimia 11, asilimia 33, kilimo wamepeleka asilimia 11, hiki kilimo tunakipeleka wapi kama kinapelekwa kwa asilimia 11 tu ya maendeleo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na bahati nzuri kuna mtu mmoja wa Hazina alikuja akatuambia akasema kwa kweli Serikali ina majukumu mengi, fedha iliyokusanywa ni kidogo na haiwezi kukidhi, hata wafadhili wenyewe waliokuwa wakituletea fedha hawaleti vizuri. Mimi nikahoji tuna mahusiano mabaya na mataifa ya nje? Kama yapo mtuambie uhusiano wetu wa kidiplomasia umekuwaje mpaka wafadhili walioahidi kuleta fedha hawaleti fedha nchi hii? Kwa hiyo, hili lazima tulione. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote ni Wabunge humu, tusione tu Serikali ni kuisifia, tuishauri, wapo watu hapa, mimi napongeza naliona jambo zuri la ununuaji wa ndege, lakini sio kununua ndege kwa cash. Mataifa yote hayanunui ndege kwa cash, hii cash ingeweza kufanya shughuli zingine za maendeleo tukanunua ndege kwa mkopo ndege ikawa inalipa deni la ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndege ya mwisho iliyokuja tuliwahi sisi wapinzani kusema nje kwamba kuna ndege imeshikiliwa, lakini waliosema ndege imeshikiliwa walipata misukosuko, juzi Serikali imekiri ndege iliyokuwa imeshikiliwa Canada sasa imeletwa. Mimi napata wakati mgumu, tulipowaambia imeshikiliwa tulipata msukosko, imerudi mkakiri wenyewe iliyoshikiliwa imerudi sasa… (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndege hii imekuja kama ndege moja tumenunua ndege tatu, kuna ndege moja ya bilioni 31 ambayo ndio hii iliyokuja ikaonekana baada ya kushikiliwa muda mrefu, lakini ili itoke tumelipa bilioni 78 sawa na fedha za Kitanzania bilioni 140 na kidogo ili hiyo ndege moja ipatikane. Sasa watu tunaposhangilia ni lazima tujiulize tumeumia kwa kiasi gani? Unanunua ndege moja kwa bilioni karibu mia moja na hamsini halafu tunalishangilia hilo, hapa watu tuna matatizo ya maji na kiafya hatulioni hilo wala hatuishauri…

T A A R I F A . . .

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, umri wangu na aliyetoa taarifa haulingani, kwa hiyo, naachana nae kwa sababu ya umri nilionao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa ushauri mzuri tu ambao unaweza ukatusaidia kwa baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwenye upande wa Wizara ya Elimu. Tunalo tatizo la uhaba wa walimu, hali ya uhaba wa walimu ni kubwa sana, tuna tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi, walimu shule za msingi hawatoshi, tuna upungufu karibu wa walimu 95,000.

Vilevile bado tuna tatizo la walimu wa sayansi, walimu wa sayansi karibu 15 na point hawatoshi. Hivi viwanda tunavyohubiri katika nchi yetu bila walimu wa sayansi ni viwanda gani? Kwa sababu tunaweza kutafikia hatua; mimi sijui kama kuna kiwanda kinaendeshwa na mtu aliyesoma history na geography aka-run mitambo ya viwanda na hivyo viwanda vikawa salama na mwenyewe anayekiendesha akawa salama. (Makofi)

Tuchukue hatua za makusudi kunusuru taifa hili upande wa elimu. Walimu wamekata tamaa morali ya kufundisha imeshuka. Taarifa ya Haki Elimu inasema walimu waliobaki na morali ya kufundisha ni asilimia 37, hawa 60 na kidogo wote wamepoteza morali wa kufundisha kwa sababu tu ya kukosa motisha. Wana madai mengi hawalipwi, wamebaki kulipa wanadokoa dokoa. Mwezi wa pili tulidhani walimu watalipwa wote, walidokoa dokoa wakalipa baadhi ya walimu, hivi hii hali tunaipeleka wapi Taifa hili? Kama hatutakuwa na elimu nchini hakuna sekta ambayo itakwenda vizuri, sekta zote zinategemea elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufaulu sasa hivi division four na division zero ni asilimia 60 na point, yaani mimi hata sielewi ni ufaulu kwa sababu zero si ufaulu hata four yenyewe si ufaulu yaani waliopata four na zero ni asilimia 60 yaani tunatarajia nchi iendeshwe na asilimia 30 ndio uwezo kidogo waliofanikiwa darasani division one, two na three, where are we heading to? Halafu tunakaa humu tunasifia, tunapongeza, tupongeze lakini tuisimamie Serikali, tuinue ubora wa elimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati yetu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii tuliwahi kufikia hatua jamani tuwe na mkutano wa kitaifa wa elimu na bahati nzuri juzi alizungumza Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin Mkapa akasema hali ya elimu ni mbaya tuwe na mkutano wa kitaifa kuliangalia hili.
Naomba hili tuliangalie kwa pamoja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumzia suala la utawala bora. Kwenye suala la utawala bora tuzungumzie habari ya Tume Huru ya Uchaguzi, kama hatutakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi hatutakuwa na utawala bora hapa nchini, na hili ndilo limetufikisha hapa. Nafurahia maoni ya Kamati yaliyosema Tume Huru ya Uchaguzi iangalie wale wasimamizi wa uchaguzi waendeshe uchaguzi kwa uadilifu. Ile habari ya kila chaguzi ndogo zinazofanyika ni mauaji, ni fujo, vurugu na uporaji wa kura na matokeo mnaambiwa nendeni mahakamani, hatutaki; uchaguzi ufanyike ulio huru tuepukane na mahakama.