Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa mwenyekiti, nashukuru sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika nchi hii. Kwa kweli utendaji wake umetukuka, kuna haja ya kumsifia na kumfagilia sana sana. Pia nampongeza sana Mheshimiwa wetu Waziri Mkuu. Mheshimiwa Rais tunamwita Bulldozer, sijui yeye tutamwitaje? Maana ni baba zaidi ya Baba. Anapiga kazi kuliko chochote. Yeye tumwongezee tumwite Tingatinga. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu, anastahili pongezi za hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia katika Wizara ya Uvuvi. Hili suala la uvuvi kwa kweli linawaumiza wananchi wengi sana na limewakosesha wananchi wengi sana ajira kwa uonevu ambao uko wazi kabisa na Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi anapaswa akae na Watendaji wake au wale wadau wa uvuvi ili wamweleweshe kwa undani zaidi, inawezekana kuna mambo mengine hayajui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi nilikuwa ni mvuvi. Kwa uvuvi wa dagaa ukisema ile milimita nane, ni milimita nane ile inavua wale furu wadogo wadogo, siyo dagaa. Labda kama sasa tunaambiwa tusile dagaa, dagaa wawe chakula cha samaki. Kwa hiyo, hili suala kwa kweli halikubaliki kabisa kwa kuwaonea hawa wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai kwamba uvuvi haramu ni kweli kabisa haukubaliki, nasi tunahitaji tule samaki wakubwa. Sasa imefikia hatua uonevu umepitiliza, umekithiri, umevuka mipaka. Hawa watendaji wanatakiwa waangaliwe kwa undani zaidi. Naweza kusema nao pia ni Wapinzani kwa sababu siyo kweli kwamba yaani wao wanawaonea tu wananchi wakati wao wanafanya utekelezaji wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye suala la afya. Kwenye suala la afya, nazidi kusisitiza katika bajeti ya Serikali muiangalie sana Hospitali yetu ya Rufaa, Hospitali yetu ya Mkoa wa Mara ili izidi kuboreshwa na iishe kwa haraka zaidi ili kusudi wananchi wa Mkoa wa Mara na majirani zetu wapate huduma nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Hospitali ya Wilaya ya Bunda, Hospitali ya DDH. Kulikuwa kuna malipo ya wafanyakazi ambao baada ya kwenda kuwasikiliza, nilikuta wana madai. Yale madai yalikuwa ni kipindi kile cha uhakiki wa vyeti, bahati nzuri naishukuru sana Serikali yangu sikivu ilisikiliza na wakaanza kulipwa mishahara. Ila walipoanza kulipwa mishahara kulikuwa kuna malimbikizo yao ya miezi kama mitano, minne hivi ambayo hawajalipwa na mpaka leo hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimsikia juzi juzi tu Mheshimiwa Rais akisema ametoa pesa ambazo zinatakiwa zilipe madeni au mabaki ya watu au wafanyakazi wanaodai madeni yao. Hao wafanyakazi wa DDH ni kati ya wale wanaodai hayo madeni. Basi naiomba Serikali iliangalie sana hili, wakalipwe hayo madeni yao wafanyakazi wa DDH hospitalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwenye suala la madini. Bado nampongeza tena na tena Mheshimiwa wetu Waziri Mkuu maana tulizunguka naye kwa kweli kwa vijiji vya Mkoa wa Mara sana, mpaka alikula ugali wa mtama kwenye nyumba ya bibi mmoja hivi wa Mkoa wa Mara, ule ugali wetu mkubwa pamoja na furu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa aliyofanya. Nilifika naye mpaka kule kwenyeJimbo langu la Nyamongo. Nasema Jimbo la Nyamongo kwa sababu mimi ndio Rais wa Wabunge wa Mkoa wa Mara. Kwa hiyo, Majimbo yote yangu. Tulifika naye kule, akaenda kuangalia matatizo ya wale wananchi. Baada ya kuangalia matatizo ya wale wananchi kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu alichukua hatua za haraka kuongea na wale wawekezaji na kufanya mambo mengine ambayo yanatakiwa wale wananchi walipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu, hili suala limetumia muda mrefu sana na ndiyo maana leo nalisisitiza hapa, naamini Serikali yangu ni sikivu, basi wale wawekezaji ambao tunawapenda sana Tanzania kwa sababu wanaongeza kipato cha nchi, lakini sasa wasipitilize wakawa wao wameota mapembe. Kule kwetu tunaita kuota mbhekela yaani kuota mapembe. Kwa hiyo, tunaomba wasiote mapembe kwa maana ya kwamba wasifanye uonevu sana kwa wananchi, basi wawalipe fidia yao wale wananchi wa Nyamongo kule mgodini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwenye suala la maji. Naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi iangalie sana Mkoa wetu wa Mara na hasa katika Wilaya yangu ya Serengeti, Bunda, Tarime, Musoma Vijijini, Rorya na kwingineko kwa maana ya kwamba suala la maji limekuwa ni muhtasari ambao unaandikwa na mtoto wa darasa la kwanza. Kwa maana ya kwamba sisi tuna Ziwa la Victoria ambalo linatuzunguka lakini maji yanatoka pale kwetu Musoma, yanatoka pale kwetu Ziwa Victoria yanapelekwa wilaya nyingine au mkoa mwingine, wakati sisi pale pale ndiyo wenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, wewe ndio mke wa kwanza, lakini mke wa pili anapewa nyumba ya urithi wakati wewe mke wa kwanza ndio unapaswa kupata urithi wote. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu ingalie sana hili suala la maji kwa kweli kwani Mkoa wa Mara tuna haki kabisa kwanza ya kuenziwa kutokana na kwamba sisi ndio tulikuwa na Mwasisi wa Taifa hili au Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa hiyo, tunapaswa kuenziwa kwa kutokosa umeme wa REA, ukipita tunatakiwa tupate, maji tunatakiwa tupate, basi hata ikiwezekana Mkoa wetu wa Mara uwe Mkoa wa maonyesho kwamba huu ndiyo Mkoa aliotoka Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni kuhusu Serikali kuangalia Watendaji wa Vijiji na Kata wa darasa la saba waliotolewa kazini. Naomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi; Mheshimiwa Waziri Mkuu amfikishie Mheshimiwa Rais haya maombi yetu kwamba hawa Watendaji wa darasa la saba ni tumetoka nao mbali sana. Wengi wao wanakaribia kumaliza muda wao na wengine wanakaribia kustaafu. Kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, warudishwe kazini hao Watendaji wa Darasa la VII kwa sababu sasa watakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametutoa mbali, kwa sababu hawa Watendaji ndio waliotusababisha kujenga Shule za Kata, kujenga hospitali zetu na vituo vyetu vya afya. Kwa hiyo, tunapowaacha njiani namna hii, ni kama vile tumewatia jiti wakati wamesimama, tena jiti lenyewe la machoni. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu hili suala tunapaswa kuliangalia kwa undani zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuangalia sana kwa undani hili suala la watu wanaoishi na VVU. Kwa kweli mmetoa msaada mkubwa sana, Wizara ya Afya imewapa kipaumbele hawa wagonjwa wa VVU, lakini kipekee kama inawezekana kwa sababu sasa hivi ni watu ambao wanajitambua sasa; katika mikoa yote na wilaya zote ukiwemo Mkoa wangu wa Mara wana vikundi vyao vya ujasiriamali mdogo mdogo. Basi zile asilimia kumi ambazo zinakwenda kwenye Halmashauri, waangaliwe angalau nao wawe wanakopeshwa. Wanafanya biashara zao au shughuli zao ndogo ndogo ili kusudi waweze kujiwezesha kwa vitu vya dharura ambavyo vinatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, nawashukuru sana ndugu zangu wa Upinzani kwa sababu kwa kweli wameongea kitu kizuri sana hata mimi kimenigusa. Sasa kutokana na kwamba na wao ni kati ya watu wanaohamasisha, tusitumie vibaya pesa za Serikali, kuliko kusema tena tuanze huu mchakato wa Katiba kwa sababu ni mchakato ambao sisi Wabunge tutakaa chini na watu wengine kuongelea habari za Katiba, tutakuwa tunalipwa hapa chini. Nafikiri wazo aliloongea pale Mheshimiwa Cecilia Paresso, kwa kweli ni zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi nawashauri na kuwaomba kwamba sasa wao wahame tu kwenye hicho Chama chao, wahamie CCM haya mambo yaishe, ionekane moja kwamba CCM ni chama kimoja, kwa sababu inaonekana hata wao wameshakubali kwamba CCM ndiyo chama kimoja, kuliko tukaanza malumbano huku ndani, mara tuandike sijui barua, mara vitu gani, au mmoja kati yao ajitolee basi aandike pale barua aitume kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, akishaituma pale kwa Msajili wa Vyama vya siasa, basi itakuwa imeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)