Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuhakikisha kwamba anaisimamia Serikali yetu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa mambo mengi, mazuri, makubwa yaliyofanywa ndani ya miaka miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufufua Shirika la ndege la Tanzania, lakini vile vile naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweza kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ndani ya nchi yetu. Tumeona bajeti ya dawa imeongezeka kutoka shilingi bilioni 252 hadi shilingi bilioni 269. Jamani hili siyo jambo dogo. (Makofi)


Mheshimiwa mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imeanza ujenzi wa reli ya kisasa ya Kimataifa (standard gauge), naipongeza pia. Tumeona barabara za juu zikitengenezwa (flyovers). Vilevile Serikali hii ya Awamu ya Tano imeweza kuimarisha ulinzi wa rasilimali zetu zikiwemo madini pamoja na maliasili. Hivi kesho Mheshimiwa Rais anakwenda kuzindua ukuta ambao utakwenda kulinda Tanzanite yetu ili isiendelee kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwamba kuna elimu bure, tunaona takriban shilingi bilioni 20.8 kila mwezi zinakwenda kuhudumia Shule za Msingi na za Sekondari. Naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya yote mazuri yanafanywa kwa sababu ya amani na utulivu tuliokuwa nao ndani ya Tanzania. Mambo haya yasingeweza kufanyika kama kuna vurugu na fujo na kama kunakuwa hakuna amani. Naamini amani ipo na utulivu na ndiyo maana mambo haya makubwa namazuri yanaweza kufanyika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha kwamba anasimamia amani ya nchi yetu; na yeyote anayethubutu kutaka kuharibu amani ya nchi hii ni lazima ata-deal naye perpendicularly. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mazuri na upungufu pia upo. Nataka nizungumzie sasa changamoto ambazo ziko ndani ya Mkoa wetu wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la elimu sisi tuna changamoto ya madarasa. Madarasa mengi bado ni chakavu, lakini vilevile tuna uhaba wa Walimu wa Sayansi kwa Wilaya zote; Wanging’ombe, Makete, Njombe na Ludewa. Tunaomba Serikali itusaidie tuweze kupata Walimu wa sayansi kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika Wilaya ya Ludewa tuna changamoto ya Walimu wa Shule za Msingi. Tunahitaji Walimu 521 ili kuweza kukidhi idadi ya Walimu katika Wilaya yetu ya Ludewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie suala la Afya. Nakiri kwamba Mkoa wetu wa Njombe tunapokea pesa za dawa zaidi ya asilimia 90, tunaishukuru Serikali, lakini kwenye ile hospitali yetu ya Makambako mnaichukulia kama Kituo cha Afya. Labda niikumbushe Serikali; hospitali yetu ya Makambako ilipandishwa hadhi kuwa hospitali tangu mwaka 2013, hivyo basi, tunaiomba Serikali irekebishe ili tuweze kuletewa dawa kwa kiwango cha hospitali na siyo Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunatambua kwamba Mkoa wa Njombe ni Mkoa mpya, Serikali sasa ione umuhimu wa kujenga Hospitali ya Wilaya katika Wilaya yetu ya Wanging’ombe, lakini vile vile tunaomba Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Njombe Vijijini Jimbo la Lupembe. Ile Hospitali ya Kibena ambayo sasa hivi inatumika kama Hospitali ya Mkoa, tunaomba ipatiwe ukarabati tujengewe fence kwa sababu mbwa wanasumbua sana wagonjwa nyakari za usiku na Wauguzi. Kule kwetu mbwa ni wengi, kwa hiyo, tunaomba mtusaidie katika ukarabati wa fence hiyo ya hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la kilimo. Kwa sasa Mkoa wetu wa Njombe nafikiri na Mikoa mingine ya Tanzania bado kuna changamoto kubwa sana za pembejeo za kilimo. Pembejeo za kilimo zimekuwa ghali na ilhali mazao bei imeshuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itazame suala hili la pembejeo za kilimo, wakulima wetu wapate pembejeo za kilimo kwa bei nafuu ili kuweza kuuza mazao yetu kwa bei nzuri, kwa sababu kama pembejeo za kilimo ziko juu, moja kwa moja itaathiri uzalishaji, lakini vilevile na bei za mazao zitaendelea kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 na 2016 kuna Mawakala wetu wa pembejeo za kilimo kutoka Mkoa wa Njombe bado hawajalipwa pesa zao. Naiomba Serikali itoe tamko ni lini Mawakala hawa watalipwa pesa zao hizo za pembejeo za kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kwenda kuzungumzia suala la maji. Suala la maji bado ni sugu Makambako Mjini, Njombe Mjini; baadhi ya maeneo kama Makete na kule Lupembe zaidi ya vijiji asilimia 50 havina maji. Pale Makambako na Njombe kuna tatizo kubwa kipindi cha kiangazi, maji hayapatikani kabisa, ukizingatia kwamba Makambako Mjini na Njombe ni Miji ambayo inaendelea kukua na mahitaji ya maji yanazidi kuwa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaomba, kuna ule mradi wa fedha za India ambao uko kwenye bajeti, tunaomba sasa zile pesa zitoke ziende zikatumike ili kuweza kuimarisha huduma ya maji katika miradi ile ya maji. Kwa mfano, kama mradi wa Mbukwa wa maji kule Wanging’ombe ili wananchi wetu waweze kuondokana na tatizo hilo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuzungumza suala zima la barabara za Mkoa wa Njombe, nimekuwa nikisimama mara kwa mara ndani ya Bunge hili Tukufu nikiomba barabara za Mkoa wa Njombe. Kama nilivyosema kwamba Mkoa wa Njombe ni mpya, sisi lami yetu tunayo moja tu ambayo inatoka pale Makambako kupita inakwenda Songea. Kwa hiyo, kwa uhalisia, Mkoa wa Njombe bado hatuna barabara kabisa ambazo ziko kwenye kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, basi naiomba Serikali iweze kutujengea barabara zifuatazo: Barabara ya lami kutoka Kibena - Lupembe kutokea Makete ambayo inakwenda kuunganika na Mkoa wa Morogoro. Vilevile kuna barabara ya Njombe – Makete - Kitulo kwenda kutokea Mkoa wa Njombe. Pia kuna barabara ya Njombe - Iyai kwenda kutokea Mkoa wa Njombe; na tuna barabara nyingine ya Njombe – Itoni - Ludewa kwenda Manda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtujengee kwa viwango vya lami ili kuweza kufungua milango ya biashara. Sisi watu wa Njombe tunalima sana, kule Makete kuna mazao ya mbao na viazi. Viazi vyote vinavyoliwa Mjini Dar es Salaam huko vinatoka Njombe. Tunaomba sana Serikali ione umuhimu wa kutengeneza barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.