Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naomba niungane na Wabunge walio wengi walionipa pole katika mkasa ulionipata huko kwetu Wilaya ya Muleba kufiwa na Katibu wa UWT Bi. Paulina Francis aliyekuwa shujaa wa chama tawala na kwa kweli Wabunge wa Kagera tulio wengi humu ametusaidia, kwa hiyo, nasema kwamba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na waliotangulia kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Timu yake, Waziri wa Nchi na Manaibu na Makatibu Wakuu wao kazi wanayofanya inaonekana na kwa kweli ni nzuri inatia moyo na ni kazi ambayo inakwenda kwa ufanisi mkubwa, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nitakayoyasema ni kwa nia na mantiki ya kuboresha kwa sababu kazi ya Bunge ni kutathmini kazi za Serikali, kutoa maoni na kutoa ushauri, kwa hiyo, ieleweke hivyo lakini kazi ni nzuri. Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa muda mfupi ameonesha kwamba mambo yanawezekana. Kama alivyosema Mwalimu Nyerere it can be done, you play your part. Kwa hiyo, sasa sisi hapa kazi yetu tuna-play our part kwa kuonyesha zile changamoto ambazo tungeomba Waziri Mkuu kwa nafasi yake na nyingine ni za kisekta aandamane na wale watendaji wengine kuziboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mantiki hiyo basi naomba kabisa nianze na sekta muhimu sana, mimi ni mwakilishi wa wakulima, wavuvi na wafugaji. Wafugaji bado suala lao la ardhi ni kizungumkuti katika mikoa ya ziwa. Nasimama hapa tusisahau tulipotoka. Sasa hivi baada ya kuondolewa kwenye hifadhi kwa sababu ya kuzilinda, wengi wanahangaika na suala la ardhi ya ufugaji bado halijakamilika, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aweke nguvu yake mwenyewe kuhakikisha kwamba tunahitimisha jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa pia niko hapa kuwakilisha wavuvi, Mheshimiwa Chegeni ambaye amenitangulia kuzungumza hapa amezungumzia sintofahamu na kwa kweli dhahama iliyowakuta wavuvi naomba nipaze sauti kwa kusema kulinda ziwa ni lazima na ni wajibu wa kila mtu, lakini tunavyolinda ziwa nayo ni muhimu kwa sababu tunapigana na umaskini hatupigani na maskini. Wavuvi walio wengi kipato chao ni cha chini, nyavu zao ziliharibiwa kwa fujo na kwa kukomoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kabisa katika suala hili la kukomoana, Watanzania tuna tabia mbaya ya kukomoana. Mtu anapopata madaraka anamkomoa mwenzake hii haitaleta maendeleo. Kwa hiyo, nataka niseme kabisa kwamba wavuvi walikomolewa, sasa katika kukomoa wavuvi unasababisha ajira zikapotea. Kwa hiyo, hii dhana ya ajira kwa vijana, vijana walio wengi mikoa ya ziwa hususani Muleba Kusini wote wako ziwani ndiyo wanapata ajira. Sasa unaharibu zana zao za kazi badala ya kulinda ziwa, yaani mtu anaweza kusema kwamba ni total confusion sasa hapo unataka nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuta kwamba hili suala la watu kupata nafasi na kuzitumia kukomoa wenzao napenda kabisa niseme kwamba linatuharibia pale ambapo tungekwenda vizuri zaidi. Kwa hiyo, waliohusika na ukomoaji huu naomba wachukuliwe hatua stahiki kusudi isije ikajirudia tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala la kahawa, wakulima Mheshimiwa Waziri Mkuu atambue kwamba wakulima wamenituma wako kwenye msiba mkubwa sana wakulima wa kahawa, kwa sababu utaratibu huu wa stakabadhi ghalani ambao ni utaratibu mzuri lakini una mazingira yake. Nikizungumza tu kama mtaalam wa sekta hizi ni kwamba kahawa iko tofauti na korosho. Unapouza kahawa wewe unayeuza kahawa ndiyo unahangaika nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba ni bias market, wale wanaonunua kahawa kuna kahawa nyingi duniani imefurika inabidi uwabembeleze. Unapouza korosho ni sellers market wewe mwenye mzigo ndiyo unatamba. Sasa naunga mkono kabisa nia ya Serikali ya kufufua ushirika. Katika hilo na kwa uelewa wangu naliunga mkono kwa dhati, lakini sasa ushirika tunaufufua vipi hatuwezi kuufufua kwa kukomoa wakulima sasa na kuwaambia kwamba lazima wote wauze kahawa yao kwa ushirika ambao haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake lazima tukiri kwamba ushirika ulishakufa wengine vyama vya msingi vingine vilishafungwa, kuna buibui na popo kule kwenye stoo, sasa hatujajipanga tunasema kwamba wanunuzi binafsi wasinunue. Naungana kabisa na dhana kwamba wanunuzi binafsi hawawezi kuendeleza wakulima wadogo wadogo, hili nalijua, nalijua tu kama economist nalijua kabisa, lakini sasa tutafufuaje ushirika wetu kusudi uwe na tija na uweze kuleta huduma stahiki kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muleba kule kwetu na Kagera kwa ujumla na naamini sehemu nyingine nyingi hata na majirani zangu Kigoma nasikia nao wako hoi. Sasa katika hali hiyo tunataka kusema kwamba suala la kufufua ushirika lisitangazwe kama tukio ni mchakato unaohitaji ulezi wa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala ambalo lisimamiwe na Waziri wa Sekta najua kwamba anafanya kazi yake kwa bidii, lakini anahitaji nguvu za Mheshimiwa Waziri Mkuu, hata na za Mheshimiwa Rais katika kuliongoza suala hili liende vizuri. Hali ilivyo sasa hivi wametangaza shilingi elfu moja kwa kilo wakati watu wanaweza kuuza elfu mbili jamani hata na sisi Wabunge humu posho yetu ikipunguzwa ghafla tutakubali? Kwa hiyo, hii ni dhahama kabisa, hivyo, naomba suala hili lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kabisa kwamba suala la miundombinu ni muhimu, suala la maji limeshaongelewa, nami naona kwamba tuweke mfuko wa maji, tuweke fedha stahiki lakini sina budi pia kumwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aangalie suala la barabara. Barabara hizi baada ya TARURA kuundwa tunaweza kujikuta katika hali ambapo wanaweza wakachukua fedha zote wakaweka kwenye barabara moja au daraja moja nyingine zikasimama kwa sababu hakuna usimamizi wa Halmashauri. Kwa hiyo suala la TARURA kuripoti kwenye Halmashauri limezungumziwa na wengi na naomba niliunge mkono na nilisisitize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu barabara ya kwenda Lubya wameshaitisha tenda mara tatu; mara ya kwanza wakasema kandarasi hakupatikana; mara ya pili kandarasi alipatikana baadaye wakasema mwenzake amejitoa; mara ya tatu mchakato unaendelea. Kwa hiyo, badala ya kupata barabara ambayo Mheshimiwa Rais ameisimamia, ni ahadi yake, sasa tupo kwenye mchezo wa kuchezeana na kukomoana. Nataka nisisitize suala la kukomoana kwamba halitajenga ustawi mzuri wa Taifa hili, litaturudisha nyuma na ndio tatizo ambalo naliona katika sekta nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa niseme kwamba ajira kwa vijana ni muhimu, lakini katika biashara zao lazima wale wa Serikali wawalee wale vijana. TRA hawawezi kuja wanafunga kila duka bila kuuliza wanakuja na minyororo wanafunga biashara. Sasa unapofunga biashara inamaanisha kwamba unaharibu ajira, kodi lazima zilipwe lakini sasa uweke utaratibu, you must go through the pain ya kuweka utaratibu sio kutafuta shortcut kwa kufunga badala ya kulea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwamba vyombo vyote vya Serikali Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye ndiye ana sera na naona kuna Katibu Mkuu wa Sera hapa Profesa Kamuzola, watusaidie kusaidia kwamba regulatory authorities zote hazikomoi bali zinalea/zinajenga. Wazungu wanasema Roma haikujengwa kwa siku moja, mambo mengine ni polepole, kodi lazima zilipwe lakini pia kodi ziwe na mahesabu ambayo yamehakikiwa na auditors. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi za Ulaya kila mtu analipa kodi, lakini kila mtu anaweza audited accounts kwamba kipato changu ni hiki na kodi yangu ni hii, lakini sasa unakuta mtu hajawahi kufanya biashara hata kidogo lakini anaona kwamba kila biashara ina faida, sio kila biashara ina faida. Kuna biashara zingine zina hasara, kazi ya Serikali ni kuzilea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndio mchango wangu lakini naunga mkono hoja na namalizia kwa kumpongeza Waziri Mkuu na kumkaribisha kuja Muleba, Muleba Mheshimiwa Waziri Mkuu nimemkaribisha lakini bado hatujamwona, tunamsubiri kwa hamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.