Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba hii nzuri ya Bajeti. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli ameonesha dira nzuri sana na imeonesha kwamba ni kwa kiwango gani uchapaji wake kazi umekuwa ukiongezeka. Kwa maana hiyo hata Mheshimiwa Rais nadhani anamsoma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu hotuba yake hii amelenga maeneo yote husika na jinsi ambavyo uchumi wa nchi hii na mustakabali wa nchi hii katika ustawi wake unavyokwenda. Kwa kweli nimefarijika na napenda tu nichangie hotuba hii kwa kukupongeza la kwanza na ninaiunga mkono moja kwa moja hotuba hii ya kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Tano Mheshimiwa Waziri Mkuu imekuwa na changamoto nyingi sana. Kila mmoja anaweza kuiona kwa sura yake na kwa muono wake lakini naomba nikiri kwamba kazi wanayochapa Serikali ya Awamu ya Tano haina mfano. Wamefanya uwekezaji ambao ni world class record. Haijawahi kutokea katika kipindi chote cha miaka yote Tanzania toka kuumbwa kwake kuwa na uwekezaji mkubwa kwa kipindi kifupi. Hii ni dalili njema kwamba tunaumia kwa kipindi kifupi tutanufaika kwa kipindi kirefu kijacho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii imejilenga katika mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji mpaka sasa hivi katika public sector ni zaidi ya trilioni 48.5 lakini deni la Taifa ni trilioni 46. Nasema kwamba umewekeza mtaji mkubwa kuliko deni la Taifa. Bado tuko vizuri na hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumza kwamba sisi bado tunakopesheka. Naomba tukope kwa kuwekeza hata ile miradi ambayo ina tija kwa Watanzania, tusikope kwa miradi ambayo hatuna tija nayo. Naona kwa hili mmejielekeza vizuri sana nakupongeza sana wewe pamoja na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote haya ningependa kuzungumzia suala moja ambalo ni tatizo sasa linaanza kujitokeza. Kuna suala la mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Simiyu wilaya mbalimbali za Mkoa wa Simiyu. Mheshimiwa Rais mwaka jana mwezi wa kwanza alikuja na akatoa maelekezo kwamba mradi ule uanze mara moja kwa sababu mahitaji ya maji ni ya msingi sana kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mwekezaji kwenye mlima wa Ngasamo, Mheshimiwa Rais akasema kwamba yule mwekezaji kwa vile haendelei na uwekezaji basi leseni yake ifutwe. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mwaka mzima sasa umepita toka Rais atoe maelekezo lakini hakuna kinachoendelea. Tumeongea na Waziri wa Maji anasema kuna mambo ya madini, Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kubwa hapa ni kwamba hakujakuwa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu hebu tuone mamlaka inayohusika ateuliwe huyu Mwenyekiti wa Tume ya Madini ili kusudi leseni iweze kufutwa na mradi uweze kutekelezeka. Bila kufanya vile hatutaweza kusonga mbele, kwa sababu pesa hii inatoka kwa wahisani na moja kati ya sharti lao ni kwamba lazima kuwe hakuna encumbrance yoyote kwenye uwekezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alibebe hili aongee na Mheshimiwa Rais kama inawezekana huyu Mwenyekiti wa Madini basi ateuliwe mara moja ili kazi ifanyike kwa sababu kazi haziendi kama ambavyo tulikuwa tunatarajia na wananchi wa Mkoa wa Simiyu wanasubiri kwa hamu sana mradi huu ambao ni wa kihistoria. Naomba tuendelee kuiunga mkono miradi kama hii, najua kuna maeneo mengi wana miradi kama hii inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wilaya mpya bado ni changamoto. Wilaya ya Busega ni moja ya wilaya mpya ambazo hazijakomaa. Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka juzi alikuja yeye mwenyewe akatembelea Wilaya ya Busega, akaona jinsi tulivyo hatuna jengo. Tunajenga jengo la halmashauri halijakamilika huu ni mwaka wa tatu, hatuna hospitali ya wilaya na miundombinu, hata Mkuu wa Wilaya hana ofisi anatumia Ofisi ya Mbunge kama ofisi yake. Sasa vitu kama hivi ningeomba tuweke kipaumbele kwa sababu palikuwa na miradi mingi mingi midogo midogo bila kukamilisha ambayo imeshaanza tayari. Ningeomba kupitia bajeti hii wilaya ambazo bado zinahitaji kuimarishwa basi zikamilishwe ili tuweze kusonga mbele tumalize moja twende na lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa suala la wilaya hizi mpya hususani Busega na Itilima kwa Mkoa wa Simiyu na wilaya zingine katika nchi hii ziangaliwe kwa kuwekewa miundombinu ambayo ni muhimu sana stahiki ili ziweze kufanya kazi na kutoa huduma kwa Watanzania kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya bado kuna suala la uwekezaji katika viwanja vya ndege. Kiwanja cha Ndege cha Songwe kimeshajengwa lakini kimebaki kukamilika kidogo tu lakini pale hakuna taa za kuongozea ndege kutua pale. Ni uwekezaji mdogo kama bilioni nne hivi. Tunaomba sana Serikali miradi kama hii iweze kukamilishwa kwa sababu leo hii kwa Tanzania tuna viwanja vinne vikubwa. Kiwanja cha Dar es Salaam Julius Nyerere International Airport, kiwanja cha Mwanza, Kiwanja cha Songwe na kiwanja cha Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda hata Mwanza, tunalilia kwamba uwanja wa Mwanza uweze kujengwa jengo la kushukia abiria. Mpaka leo ni miaka nenda rudi bado hatujatekeleza. Ningeomba tuangalie priority ya kiuchumi, ukiweza kuimarisha Songwe ikaweza kufanya kazi vizuri, ukaimarisha Mwanza ikafanya kazi vizuri, ukaenda na Mtwara ukaimarisha tayari tutakuwa na viwanja ambavyo vitaongeza mapato makubwa kwa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kama Serikali mjaribu kuangalia vipaumbele ni vipi ambavyo tuweze kuvifanya vitakavyoongeza tija zaidi halafu tu-service viwanja vingine vidogo vidogo kadri ya fedha inavyopatikana, tusisubiri sana fedha ya wahisani ikiwezekana pesa zetu za ndani zitumike kuweza kukamilisha miundombinu ya namna hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo tunalo na ni tatizo kubwa kidogo na hasa sisi wenyeji wa kanda ya ziwa. Mwananchi wa kanda ya ziwa anategemea uchumi wake kwenye kilimo, uvuvi na ufugaji. Leo hii suala la wavuvi haramu hakuna anayeunga mkono suala la uvuvi haramu lakini bado kitendo kinachofanyika kuhusu kuwanyang’anya vifaa vyao tunaamini wavuvi wao wananunua nyavu kutoka kwenye viwanda na maduka husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya maduka ilikuwa ndio chanzo cha kuweza kuyawajibisha zaidi kuliko mnazuia haramu. Maana yake mvuvi yeye anavua apate riziki yake apate kipato chake lakini anatozwa faini ambazo ziko nje ya utaratibu, ananyanyaswa, jamani nadhani kama CCM sisi tunasema kwamba hatutii watu umaskini tumekuwa tunatia watu utajiri. Ningeomba sana sana Mheshimiwa Waziri Mkuu suala hili tuliangalie kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazao kwa mfano pamba mwaka huu kuna uzalishaji mkubwa sana wa pamba katika mikoa inayolima pamba. Tunaomba kuwe na utaratibu mzuri ili zao hili sasa mkulima anufaike nalo, bila kuwa na utaratibu mzuri tutazidi kuwakatisha tamaa wananchi ambao siku zote wamekuwa wakijitoa muhanga kulima pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wafugaji, migogoro ya wafugaji na hifadhi za Taifa bado ni tatizo kubwa sana. Hata jana hapa kulikuwa na mjadala kuhusu tembo, suala sio dogo Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wananchi wanalia kwa sababu wanyama waharibifu kama tembo, viboko wanavamia makazi ya wananchi na kuharibu mazao ya wananchi, lakini wananchi wamekuwa ni waaminifu kulinda rasilimali hizi. Tunaomba na Serikali iweze kuwasaidia angalau kuweza kuona kwamba wanalindwa na wao. Tembo wanaua watu, tembo wanaharibu mali ya watu lakini bado Serikali haiwajibiki kikamilifu, haiwezi kuwasaidia wananchi kwa uharaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata tembo anapotokea kuvamia maeneo ya wananchi, unapoomba msaada wa vikosi vya kuweza kuzuia, inachukua muda mrefu sana. Niombe Wizara husika wajaribu kuongea na watu hawa wahusika wote na tuweze kuwa na mustakabali mzuri wa utumiaji na ulindaji wa rasilimali za Taifa. Wakulima na wananchi wanapenda tulinde rasilimali zetu hizi lakini naomba na Serikali iwajibike kwa kiwango kikubwa sana kuona thamani ya mwanadamu katika suala hili lote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la barabara, wilaya mpya zinapoanzishwa zinakuwa hazina miundombinu ya barabara. Tunaomba ile kilomita tano kwa kila halmashauri mpya itekelezwe na tungeenda angalau kwa kwenda kwa mpangilio kwamba mwaka huu labda halmashauri kama ni kumi, kumi na tano zikamilike, mwaka ujao hizi zikamilike, lakini naona unakuta muda mrefu unakwenda hakuna ambacho kinachofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana na Mheshimiwa Waziri Mkuu yuko hapa na bahati nzuri anaijua vizuri sana Busega kwa sababu alikuja Busega na wananchi wa Busega wakamkarimu vizuri na wakampa jina la Chifu Masanja, maana yake Masanja ni mtu ambaye anayekusanya watu, ni mtu wa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarimu wa watu wa Busega, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, basi awafikirie kidogo ili mambo yao yawanyookee. Alipokuwa pale mzee alitoa kauli nzito nzito, yeye sio mtu wa kubabaisha, ni mtu wa kauli nzito na vitendo kama alivyo Rais wake. Hebu aende kwa vitendo ili wananchi wa Busega wapate kumbukumbu nzuri ya maneno yake na uchapakazi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija suala zima la UKIMWI, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukimwi, Mheshimiwa Mukasa ameniomba nizungumze kidogo. Kwa vile suala hili liko katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, hawa watu ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI naomba wapewe msaada mkubwa, Serikali iwasaidie. Najua kuna baadhi ya halmashauri zimeshaainisha namna ya kuweza kuwasaidia na kushughulika nao, lakini naomba kama jitihada za kiserikali ziongezwe zaidi. Hawa watu wanahitaji msaada mkubwa zaidi na naomba Serikali iweze kuliangalia kwa nafasi ya pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa viwanda ni wa kuondoa umaskini kwa Mtanzania. Ni watu wachache ambao wanaweza kufikiri vinginevyo, lakini naamini kabisa kwamba tukiweza kuunga mkono jitihada ya Serikali ya Awamu ya Tano haya yanayotokea mengine ni mihemko tu na sidhani kama mtu anatoka Zanzibar anasema kwamba sukari haiwezi kuja Bara wakati anazalisha tani elfu nane peke yake na mahitaji ni zaidi ya tani elfu kumi na saba mpaka tani elfu ishirini. Sasa mambo mengine haya tunayaibua bila kuwa na sababu yoyote ya msingi na wanasema kama huna takwimu usiseme kitu, unaibua kitu ambacho hakina maana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini sisi Watanzania wote kwa umoja wetu, mali iliyoko Bara ni kama iliyoko Zanzibar, iliyoko Zanzibar ni kama iliyoko Bara na ndiyo Muungano wetu uliposimama katika misingi hiyo. Tunapoanza kusema unajua mali ya Zanzibar haiwezi kuja huku wakati takwimu yako siyo sahihi, naomba Waheshimiwa Wabunge tujaribu kuliangalia hili na tujaribu kuwa makini zaidi, tusichanganye wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.