Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu spika, nishukuru kwa kunipa fursa na mimi kuweza kuchangia hoja hii ya Azimio letu la makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya tabianchi. Mheshimiwa Waziri wangu atawatambua wale wote ambao wamechangia kwenye Azimio letu, mimi nigusie baadhi ya maeneo ambayo wachangiaji wameyasema.

Kwanza kabisa chimbuko la azimio hili ni mkutano ambao ulifanyika kule Stockholm na ulikuwa unahusu binadamu na mazingira. Kwa hiyo, utaona ni kwa kiasi gani jinsi umuhimu ulivyo kati ya binadamu na mazingira jinsi wanavyotegemeana. Sheria yetu namba 20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Mazingira imesheheni mambo ambayo Watanzania wakiyafuata bila shuruti tutakwenda kutunza, kuhifadhi na kulinda mazingira ya nchi yetu na tutakuwa ni nchi ya mfano katika ukanda mzima wa Afrika na dunia nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo katika sheria yetu mazingira yametajwa kwamba ni urithi katika msingi wa ile sheria kwamba mazingira ni urithi wa kizazi hiki ambacho tunaishi sasa na vizazi vinavyokuja kwa hiyo, wananchi wakielewa umuhimu huo watakuwa katika fursa nzuri ya kujali katika kutunza vyanzo vya maji katika nchi yetu, watajali katika kutunza miti, watajali kila wakati kupanda na kutunza miti na hivyo urithi huu ndio hoja ambayo Mheshimiwa Saleh alikuwa anazungumzia masuala ya urithi, namna ambavyo baadhi ya ndege wanatoweka, baadhi ya miti inatoweka, theruji kwenye Mlima Kilimanjaro inapungua kwa hiyo tutakapokuwa katika fursa hii ya kujitambua kwamba mazingira tunatakiwa uwe ni urithi kwa sasa na baadaye Watanzani tutakuwa katika mazingira mazuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumzia suala la kufanyika tafiti hasa kuwatumia wataalamu tafiti hii ya mimea, tafiti ya miti sheria yetu ya mazingira inaanzisha mfuko wa Taifa wa dhamana ya mazingira na mojawapo ya matumizi katika mfuko ule ni katika masuala ya tafiti, ni katika masuala pia ya kuwafadhili Watanzania waweze kusoma katika maeneo haya ya mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yetu Ofisi ya Makamu wa Rais kwamba bajeti hii inayokuja tuombe Waheshimiwa Wabunge wapitishe tuweze kuwa na fedha za kutosha katika mfuko wa Taifa wa dhamana ya mazingira ili kupitia mfuko huo tuweze kuhakikisha kwamba tunakuwa na wataalam wanaofanya hizi tafiti ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wananchi katika kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria yetu ya mazingira kifungu cha sita kimetoa wajibu kwa Watanzania wote kuhakikisha kwamba wanatunza na kuhifadhi mazingira, kwa hiyo sio suala tu la Ofisi ya Makamu wa Rais au NEMC kwamba sisi ndio tunawajibika kuhakikisha kwamba wananchi wanatunza mazingira ni wananchi wote.

Niwaombe Waheshimiwa Wabunge nyinyi ndio mko majimboni kule ambako ndiko kuna halmashauri zetu kuanzia Halmashauri za Wilaya, za Miji za Manispaa na Majiji na amezungumzia Mheshimiwa Richard Mbogo masuala ya uelewa kwenye Vitongoji, kwenye Vijiji Waheshimiwa ninyi ndio Madiwani kwenye Halmashauri zenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba kwa kuwa sheria hii kuanzia kifungu cha 36 mpaka 41 kinazungumzia kuwepo kwa Kamati za Mazingira kwenye ngazi za Vitongoji, Vijiji, Mitaa, Kata mpaka Wilaya na kuwepo kwa Maafisa Mazingira hakikisheni kwamba Kamati hizo zipo na zinafanya kazi pale ndipo tutakuwa katika nafasi nzuri ya kulinda na kuhifadhi mazingira kwa sababu mazingira yako kule chini kabisa kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala lililozungumzwa sana la hasa kuanzia Kambi ya Upinzani kwamba kuwabana zile nchi ambazo zinachafua mazingira ili waweze kuleta fedha.

Katika Azimio hili kwenye mkataba imewekwa bayana kabisa namna ambavyo hizi nchi zinawajibika kusaidia fedha na tumetaja Mifuko mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa ambako sisi hupata fedha. Tumewaonesha miradi mbalimbali, mingine ambayo Mheshimiwa Lubeleje amesema itaenda kwenye Wilaya yake na baadhi ya Wilaya za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba sisi tutakapotenga fedha za ndani na tukaendelea kupata fedha hizi kutoka kwa wafadhili, ni imani yetu kwamba tutakwenda kuhifadhi na kutunza mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na wasiwasi Mheshimiwa Mbogo. Anasema kweli, kwenye Ilani yetu ukurasa wa 213 tumezungumzia kwamba kila Halmashauri hapa nchini lazima kila mwaka wawe na miradi ya kupanda miti isiyopungua 1,500,000 na kwamba, ni kweli hiyo miti ipo?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba mimi na Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukizunguka nchi nzima ikiwa ni pamoja na kutumia Sikukuu za Mazingira Duniani, tumekuwa tukizunguka na kuhimiza Halmashauri waweze kupanda hiyo miti na kutuonesha kwa macho. Tunajipanga kama sehemu ya mkakati wa Kitaifa ili kuanzia mwakani, kama ilivyokuwa kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Magufuli, akiwa Waziri wa Uvuvi, alikuwa na uwezo wa kujua idadi ya samaki kwenye bahari na kwenye maziwa na mito; nasi tutakuwa na sensa ya miti ili tujue kwamba hii miti tunayoambiwa kwenye taarifa mbalimbali wamepanda, je, hii kweli hii miti ipo, ili tuwe na uhakika kwamba mazoezi haya yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mita 60 na wamezungumzia kwenye Kambi ya Upinzani vinyungu kule Iringa na Njombe; wamezungumzia kule milimani kule Kilimanjaro. Niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri alishatoa mwongozo kwamba Halmashauri zote nchini walete orodha ya vyanzo vyote vya maji, pamoja na milima na vilima ili wachanganue kwamba vyanzo hivyo vya maji vina changamoto gani ili sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tuweze kutengeneza mkakati wetu wa Kitaifa ambao unaendelea kwenye task force ili tuweze kuwabana hao ambao wanaharibu na kuchafua vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba nchi hii ambayo tumekuwa tukisema Mataifa yanayochafua na kuharibu mazingira, hasa kwenye hewa ya ukaa ambayo inakuja mpaka huku na kuleta athari za mabadiliko ya tabianchi kwamba tuzibane zilete fedha; sisi kwa kutumia Sheria ya Mazingira tunawabana wananchi watumie fedha katika kuhifadhi na kutunza mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawabana wawekezaji na hasa wenye viwanda kuhakikisha kwamba katika uwekezaji wao, nao wasiangalie tu sehemu ya faida, waangalie pia kuweka mifumo rafiki ambayo itahakikisha kwamba wanalinda na kuhifadhi mazingira ili siku ya siku Tanzania ya viwanda ambayo Mheshimiwa Rais ni champion kuhakikisha kwamba Tanzania ya Viwanda inaenda sambamba na kuzingatia sheria za kutunza na kuhifadhi mazingira. Kwa hiyo, tutaendelea sisi Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa wakali sana kusimamia sheria hii ili Watanzania wote wahakikishe kwamba wanatunza na kuhifadhi mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala aliloligusia Mheshimiwa Lubeleje. Mheshimiwa Lubeleje amegusia suala la Mpwapwa. Mheshimiwa Waziri wangu alishaniagiza niende Mpwapwa ambako wananchi wanaendelea kukata miti ovyo kwenye vilima, wanaharibu vyanzo vya maji na kuchoma moto ovyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule moja ya sekondari ambayo inasemekana kuna mwananchi mmoja alienda akakata miti ya shule ambayo wao walikuwa wameipanda kwa ajili ya kuhifadhi mazingira. Kwa hiyo, nitoe wito kwa nchi nzima, siyo Mpwapwa tu kwa Mheshimiwa Lubeleje, kwamba suala la kisingizio cha kwamba tunatumia kuni, tunatumia mkaa, vijijini kule wananchi wengi hawatumii mkaa, mkaa mwingi unaenda mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali imeshajipanga kuhakikisha kwamba kupitia Wizara ya Nishati wanaanza kusambaza gesi katika Mji wa Dar es Salaam ambapo tunaamini sasa tunaenda kuwa na nishati mbadala kwa njia ya gesi ili tuanze kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi nyingi za Serikali yakiwemo Magereza, Hospitali na shule, tumeshawapa mwongozo na maelekezo kwamba waache sasa kutumia kuni na mkaa, waende kwenye nishati mbadala. Wazo zuri alilolitoa hapa Mheshimiwa Mbogo, kuwa shuleni kwenye bio- gas, kuna baadhi ya shule ambazo tayari tumeanza kuzitembelea kwamba wana-recycle, wana bio-gas ili sasa kupitia Bunge lako tutakapopata uwezeshaji wa kibajeti, tuanze kupita kwenye shule na taasisi nyingine ambazo nimezitaja kama majeshi na shule ili waanze kuwa na nishati hii ya bio-gas ili tupunguze ukataji wa miti.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.