Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuweza kunipatia nafasi kidogo nami niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijatoa mawazo yangu napenda nichukue nafasi hii kwanza kuunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani, pia napenda tu kuwashukuru Viongozi wetu wa kambi, Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa Riziki S. Mngwali pamoja na James Francis Mbatia kwa kazi nzuri wanayoifanya na niwaambie kwamba kufanya kazi ya upinzani katika nchi zetu za Kiafrika inataka moyo. Kwa hiyo, tuendelee tu kupambana na matokeo ya kazi yetu yanaendelea kuonekana na kuleta mabadiliko katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza maji katika bajeti hii, nikiamini kabisa kwamba tumekaa hapa takribani miezi miwili, tukifanya mipango na kutafsiri mipango hii katika pesa ndiyo maana ya bajeti, tunapanga halafu tuna tafsiri mipango katika pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunahitaji kuona mafungu tunayoyagawa yanaleta matokeo mazuri, kwa vikundi vya wananchi na mwananchi mmoja mmoja na tunapima matokeo haya tunaona bajeti yetu tuliyoipanga imeleta matokeo yapi, imeweza kuleta maendeleo ya nchi na watu wake imeweza kupeleka mbele maendeleo ya mtu mmoja mmoja katika makundi yao na baadaye tunarudi mwaka kesho tunakuja kushangilia na kupiga makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiria kwamba hii bajeti inapaswa kujibu matatizo ya maji, kwa sababu tulikaa hapa na hasa wanawake, tulipanga mkakati mzuri na tukafanya lobbying, Wanaume wakatusaidia tukasema Serikali iongeze tozo ya Sh.50/= kwenye mafuta iende kwenye maji ili tuweze kuwatua wanawake ndoo, lakini cha kushangaza Serikali imekataa maombi yetu. Kwa lugha nyingine Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi isitudanganye haipo tayari kuwatua wanawake ndoo, badala yake mmetuletea sasa hoja nyingine ya Sh.40/= ambazo wanasema zitaongezwa kwenye mafuta baada ya kufuta road license. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejiuliza Mheshimiwa katika kitabu cha bajeti cha Waziri mbona hajatuonesha hii Sh.40/= kama inakwenda kwenye maji? Hii Serikali inaelewa vizuri mafuta yanayoingia nchini kwa sababu wanaagiza mafuta kwa bulk procurement, kama wanafanya hivyo wanajua ni lita ngapi, kwa hiyo mngeweza kukokotoa kutueleza ni fedha kiasi gani zitapatikana, hakuna jambo kama hilo katika vitabu vyao. Sasa tunakaa hapa tunaanza kupigwa wananchi kiini macho kwamba unajua hiyo Sh.40/= itakwenda kwenye maji, wapi na wapi watuoneshe mahali ambapo mmeandikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atuonyeshe ni shilingi ngapi ambazo zitatokana na mafuta hayo. Wanajua kwa nini wameshindwa kufanya calculation ni kwa sababu walikuwa hawakuipanga kwenye bajeti hata kidogo ni wazo limeletwaletwa tu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikubaliani kwamba hii Sh.40/= haziwezi kupandisha maisha ya watu. Nilikuwa nafanya simple calculation, kwa basi ambalo linatoka Dodoma kwenda Mwanza, mtu tu ambaye anaweza kutumia lita 200 analipa road license zaidi milioni mbili, kwa hiyo na wao watufanyie mahesabu tuone haya mafuta ambayo wanaagiza kwa bulk procurement yanaleta pesa kiasi gani ambazo wanasema zitakwenda kwenye mafuta, otherwise wanachofanya wanajaribu kutetea hii hoja, wakijua wanafanya siasa, sawa tunafanya siasa hapa, lakini wasifanye siasa za kwenda kudanganya au kuwaweka sawa au kuwaweka vibaya wananchi wa chini na hasa akinamama wanaotumia vibatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa kwenye Halmashauri, siwezi kuchangia bila kugusa Halmashauri. Bajeti ijibu matatizo ya wananchi, tukienda kwenye Halmashauri tunatazama pesa za barabara ambazo zinatolewa na Serikali Kuu katika Mfuko wa Barabara, ukienda kwenye kitabu cha ujenzi ukurasa wa 172 kinaonesha kwamba wao mwaka huu watakusanya bilioni 832.4. TAMISEMI wanapewa pesa bilioni 249.7, pesa hizo siyo kwamba zinakwenda zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona bajeti ya mwaka huu Serikali imeweza kutoa fedha za maendeleo asilimia 38, kwa hiyo tunaona ni namna gani Serikali ilivyoshindwa kabisa hata kufika asilimia 50. Kama pesa hizi zinakuwa ndogo na mara nyingi tumekuwa tukiwaambia kwamba waongeze pesa katika Halmashauri ili Halmashauri ziweze kutengeneza barabara na barabara hizi zikipitika ni njia ya kusaidia wananchi kuweza kusafirisha mazao yao lakini pia kusaidia wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemwona Mheshimiwa Waziri Ummy hapa anahangaika kutafuta ambulance, hizo ambulance zinakwenda kupita barabara gani, kama Halmashauri barabara zake hazitengenezwi? Kuna mtu ameuliza hapa kwamba inawezekana Serikali Kuu wana mpango wa kutoa huduma wenyewe badala ya Halmashauri ndiyo maana wanachukua vyanzo vyote. Wanachukua vyanzo vyote vya Halmashauri Je, ninyi wana mpango ngani mbadala wa kutoa huduma kwa Halmashauri hizi. Nina wasiwasi mkubwa haya mambo yote tunayoyapanga yatakwenda kushindwa kutoa majibu sahihi na kusaidia wananchi ili waweze kuinua maisha yao kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama barabara hazitengenezwi za Halmashauri, Serikali Kuu watakwenda kuona mashimo yaliyomo kwenye mitaa? Wanaweza wao wenyewe kukaa Dar es Salaam pale au kukaa Dodoma hapa wakajua mimi kwetu kule Kamachumu Makongola Kijijini kwangu nilikozaliwa kwamba kuna barabara mbaya, hamna barabara ni mbaya za Halmashauri hazitengenezeki, hakuna mahali pa kupitisha mazao, wananchi wanahangaika lakini bado Serikali inatoa pesa kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kutamka kuhusu percentage ya pesa ambazo zinakwenda Halmashauri kwenye Mfuko wa Barabara, Serikali inakaa kimya Mawaziri wanakaa kimya, ni kwa nini hawaleti sheria, wasilete Sheria za Madini tu na hizi wazilete tuzibadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo niongelee kuhusu madini na mikataba, watu wengi wanasema mchawi mpe sifa yake, mimi namshukuru sana Mheshimiwa Bashe amesema mtu akifanya kitu kizuri asifiwe wakati mwingine kwa kitu kizuri, kama wanavyosema tumuunge mkono Rais wetu, mimi nafikiri wazo siyo baya, pia hata Mheshimiwa Lissu amefanya kazi kubwa sana kuhusu mambo haya ya mikataba, amesimamia kesi mbalimbali. Kwa hiyo siamini kama kuna mtu ambaye anaweza kushindwa kutambua kazi ya Mheshimiwa Lissu ambayo ameifanya tangu mwaka 2004 mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema walete sheria na wakubali tumewaambia kwamba hakuna sababu ya kupigiana makofi, kufanya kosa kitu kibaya ni kulirudia, kama CCM walitufikisha hapa kwa miaka 50, basi wawaombe radhi Watanzania na wakubali tusahihishane humu ndani. Waende walete sheria maana yake hata Ndugu Ludovick Uttoh, aliyekuwa CAG amewaambia kwamba nchi iliingia kwenye mikataba ya kipumbavu, siyo maneno yangu yako kwenye magazeti, alisema tulipitisha sheria ambazo zinaruhusu madini na kila kitu kiende. Kwa hiyo, waende walete sheria, hata tukiongea maneno ya namna gani hapa, kama hakuna sheria wale jamaa wataendelea kubeba mabonge ya dhahabu kwa asilimia 95.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani Waziri ambaye anaweza kwenda kwenye uwanja wa ndege hapa? Nenda kwenye machimbo, kwenye uwanja wa ndege hakuna anayekanyaga pale hata Waziri wa Fedha hakanyagi, hata wewe Mwenyekiti wa Bunge leo hukanyagi mle, ni sheria tulizoziunda zinatupeleka. Walete sheria hapa tubadili ili tuweze kwenda na jambo hili vizuri kwa sababu ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba ni kwamba tuhakikishe bajeti hii inajibu matatizo ya Watanzania, inaangalia kilimo kwa mfano, hebu tuangalie kilimo kwa undani, wameanzisha mashamba darasa hayafanyi kazi, mimi ninapoishi nyumbani kwangu kijijini natazamana hivi na shamba darasa hamna kitu, kwa sababu hakuna Extention Officers hawatuoneshi katika bajeti kwamba wanaenda kuajiri Extention Officers hawatuambii wanakwenda kufanya mikakati ipi kwa ajili ya kilimo ili wananchi waweze kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wangekubali issue yetu ile ya Sh.50/= wangeweza kutuambia tutapata pesa kiasi gani, tutajenga malambo, tutajenga mabwawa, tutafanya umwagiliaji and then wananchi watalima, tutapata chakula lakini hata lishe, hatuwezi kuongea ya lishe wakati watu hawashibi, watu hawana chakula na utegemee watu wafanye kazi wakati watu wana njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)