Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuzipongeza Kamati zote kwa hoja iliyowasilishwa leo Bungeni hapa na ninaomba nikiri wazi hapa kwamba sisi hapa jukumu letu kubwa ni kupokea michango ya Wabunge kwa maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha Wizara yetu au Serikali kwa ujumla wake tuweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Kamati ya TAMISEMI na Kamati ya Sheria Ndogo. Mheshimiwa Mwenyekiti ninafahamu fika wewe ndiye mwenye dhamana ya Kamati ya Sheria Ndogo na maelekezo yako ya aina mbalimbali yameweza kutusasidia katika utekelezaji wa majukumu yetu. Hata hivyo tutaendelea kuboresha yale ambayo yamebainishwa hapa na Waheshimiwa Wabunge hasa katika suala zima la zoezi la kusaini sheria ndogo. Wataalam wanazipitia ili kuondoa makosa ambayo yamebainika na hatimaye tufanye maamuzi kwa ajili ya kuzisaini tupate sheria ndogo zenye kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni mbalimbali yametolewa hasa katika suala la ujenzi wa Strategic City Project. Kuhusiana na mradi huu niishukuru sana Kamati ya TAMISEMI, imefanya kazi kubwa sana katika maeneo mbalimbali. Wamekwenda maeneo Jiji la Tanga, wametembelea hapa Dodoma kwa ufupi, lakini na maeneo mengine na tumepata mchango wao kwa kadri iwezekavyo, kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachukua ushauri kuhusu ujenzi wa mifereji. Tukumbuke mradi huu sawa sawa na ile miradi mingine mitatu mikubwa tuliyo nayo. Mradi wa karibuni shilingi bilioni 840, ambapo tunajenga katika miji yetu hii. Tuna Mradi wa DMDP wa milioni 660 na Mradi wa UGSLP karibuni milioni 800 vilevile ambapo katika sehemu hii tunachukua maoni ya Kamati, kwamba kipaumbele kikubwa ni lazima tuhakikishe kwamba tunatengeneza mifereji katika maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie kwamba katika mradi huu jambo hili tunalichukulia kwa nguvu zote licha ya mifereji pia tunaweka taa za barabarani kwa ajili ya wakati wa usiku. Hali kadhalika katika maeneo mbalimbali tunajenga na madampo ya kisasa ili kuiwezesha miji yetu iwe miji rafiki sambamba na ununuaji wa mitambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja inayohusu huduma ya afya, naomba nishukuru sana na nishukuru Kamati kwa kiwango kikubwa. Katika mpango wetu wa kuboresha vituo vya afya 205 hivi sasa zoezi lile linaenda vizuri. Hata hivyo nafahamu kwamba changamoto ya afya hatuwezi kuimaliza kwa siku moja, lakini Serikali imeweka uwekezaji mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru mama yangu mama Kahigi aliipongeza Wizara hii kwa nguvu zote na kutoa changamoto katika Hospitali ya Bukoba Vijijini. Mchango wako mama Kahiji sambamba na Mzee wetu Mbunge wa Bukoba Vijijini; ndiyo maana kwa sababu mlikuwa hamna Hospitali ya Wilaya tumepeleka ujenzi vituo vya afya pale Katoro na Kashanje kwa lengo la kwamba huduma za upasuaji ziweze kufanyika katika eneo lile. Hata hivyo Halmashauri ya Bukoba Vijijini tumeiweka katika mpango wa ujenzi wa zile hospitali 64 katika Wilaya ambazo hazina hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hili sasa hivi lipo katika kipaumbele chetu; eneo hilo tutalipatia huduma ya afya kama tunavyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi kama nilivyosema kwamba Kamati ya TAMISEMI imefanya kazi kubwa sana hasa ushauri wa meneo mbalimbali; si wa Bunge tu lakini hata nje ya Bunge tukiwa katika vikao vya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri wazi kwamba walivyotembelea kule Kilolo waliona hospitali ya mfano ya Wilaya ya Kilolo, na mimi tu niseme kwamba nimetoa maelekezo na tutaendelea kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi nini afanye ili hospitali ile ya mfano iweze kukamilika ili sisi sote tujivunie tumefanya jambo kubwa la mfano katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja iliyohusu mabasi ya mwendo kasi, kwamba ratiba imebadilika. Naomba niwahakikishie kwamba ofisi yetu inafanya kazi kubwa sana; kwa sababu mradi huu leo hii katika Bara la Afrika ndani ya miaka 13 baada ya utoaji wa tuzo maalum Afrika sisi Watanzania tumekuwa watu wa kwanza katika miaka 13 tumeweza kushinda mwaka huu. Tarehe 9 JAnuari wa kwanza Tanzania imetunukiwa tuzo hii maalum kwa mradi wa mwendo kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mradi huu una changamoto yake kubwa kama mama Ruth Mollel alivyosema na ndiyo maana kila siku tunaendeleza uboreshaji na ndiyo maana sasa hivi kuna tender imetangazwa lengo kubwa ni kwamba tuweze ku-meet zile specification za World Bank ambazo katika agreement yatu tumekubaliana kwamba tuwe na service provider ambao mkataba wao tunadhani ndani ya mwezi wa tano inawezekana tukaenda mahala pazuri zaidi kuhakikisha kwamba tunapata service provider. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu hii ni awamu ya kwanza lakini tunajumuisha awamu zote sita; tutakuwa na watoa huduma vizuri zaidi kuondoa shida kubwa ya mabasi yaendayo kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la karakana pale Jangwani ni kweli na Wajumbe wa Kamati wanafahamu, mmelitembelea pale, changamoto ile ni kubwa. Ndiyo maana katika mpango wa muda mfupi kupitia Mradi wa DMDP tumepeleka fedha kwa ajili ya survey, na sasa hivi wataalam wanafanya survey kuondoa lile tope na bonde lote ili kulibadilisha Bonde la Msimbazi ili mvua inaponyesha maji yote yaelekee kwenda baharini.

Hata hivyo katika backup strategy nimetoa maelekezo kwa wenzetu wa DART kwamba mabasi yale yote yaache kulala pale eneo la Jangwani yaende kulala eneo la Gerezani ambako kuna eneo limetengwa ili kuepusha gharama nyingine ambazo zinaweza kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu jambo jipya lolote lazima lina changamoto yake kubwa, lakini changamoto hii tunaendelea kujifunza na kufanya marekebisho makubwa hatimaye tuweze kupata fursa kubwa sana kuhakikisha nchi yetu inaenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Kamati ya TAMISEMI na ushauri wenu mmetoa mlipotembelea ukarabati mkubwa wa shule kongwe Tanzania, tunachofanya ni ukarabati wa kwanza kihistoria. Tunakarabati shule 89 tunatumia takribani shilingi bilioni 89 na kazi hii kubwa inafanyika na Kamati imeendelea kushauri japokuwa kuna baadhi ya wakandarasi walitukwamisha especially TBA.

Hata hivyo tumetoa maelekezo ili kwamba miradi hii yote ipate mafanikio makubwa na shule zetu kongwe zirudi katika ubora wake ule tunaokusudia. Hatimaye tupeleke elimu bora kwa vijana wetu na sisi kama Watanzania tujivunie kwamba katika mamlaka zetu za Serikali sasa shule zetu za Serikali zinatoa huduma bora kwa vile vijana wana mazingira rafiki ya kujifunzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna inayohusu TARURA. Nishukuru Kamati imetufundisha mambo mengi sana. TARURA ni chombo kipya na hivyo tunapaswa kukilea kuanzia sasa. Sasa hivi ndiyo kwanza kama mtoto anaanza kukaa chini, ana miezi sita. Wabunge mnafahamu eneo hili sasa ninyi mna ownership kubwa sana katika TARURA. Leo hii ukiwa Mbunge wewe ndiye msemaji mkubwa sana wa TARURA katika Wilaya yako. Yaani ndiyo maana ninasema kwa Wabunge kwamba kuanzishwa kwa TARURA inakuwa kama kipa katoka wewe Mbunge unadhamana kubwa ya kukielekeza chombo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba niseme, na ninyi mmeona changamoto kubwa ya kifedha, kwamba mgawanyo ni wa asilimia 30 naomba hili kwa sababu ni suala la Wabunge wote tutalijadili hapo baadae kwamba nini kifanyike ili kuufanya wakala huu uweze kusimama vizuri. Hata hivyo jukumu letu kubwa kupitia TARURA sasa tunataka tuhakikishe kwamba tunaimarisha miundombinu yetu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa kujali value for money na ubora wa kazi.

Mheshi,wa Mwenyekiti, ni imani yangu kubwa kwamba tutashirikiana kwa pamoja, wakala huu utaweza kutimiza wajibu wake kwa sababu mwisho wa siku jambo hili litaleta faraja kubwa kwa Watanzania. Hii ni kwa sababu huko chini ndiko mazao yanakozalishwa wananchi maskini wako huko. Nina imani miundombinu hii tutaiimarisha, na tutahakikisha kwamba katika maeneo mbalimbali wananchi wanapata huduma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepewa dakika tisa, japokuwa nina hoja nyingi sana za kujadili, niseme kwa ujumla na nikuhakikishie kwamba sisi ambao tuna jukumu kubwa sana la kuhakikisha katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tunafanya kazi kubwa ya kutosha tumejipanga. Kamati nawaombea sana ili Mungu asaidie muendelee kutushauri. Lengo kubwa ni kwamba Wizara hii iweze kufanya vizuri na wananchi wapate huduma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana ninaomba kuwasilisha, lakini naunga mkono hoja zote zilizowasilishwa hapa.