Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja hizi za Kamati zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kuunga mkono hoja za Kamati lakini nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-Wataala na kwa namna ya kipekee kabisa niweze kukushukuru wewe kwa kuweza kunipa hii nafasi kwa wakati huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa ya kuweza kuchangia kwenye Kamati hizi zote mbili. Jambo la kwanza Mtume Muhammad Swalallah-Alay-Wasallama karne ya sita (AD) alisema kullil-hakka laukana murra kwamba sema ukweli japokuwa unauma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitakuwa mkweli sana katika maelezo yangu haya machache. La kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri mpya wa Wizara hii ya Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Kigwangalla kwa maamuzi yake magumu anayochukua usiku na mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa wakweli, sisi kama Wabunge ni mapema sana leo hii kuanza kum-judge Mheshimiwa Kigwangalla kwamba eti anaipotosha Wizara, Wizara haiendi sawa, atakaa kwa muda mfupi. Naomba nizungumze jambo moja tu ambalo kimsingi namuomba Mheshimiwa Waziri Kigwangalla achukue maamuzi magumu, kwa sababu nilishawahi kusema ndani ya Bunge hili kwamba kama nchi haichukui maamuzi magumu, tutarudi kule tulikotoka. Ni lazima tutoke tulipo, tuelekee mbele ili tuweze kuwa na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapitia taarifa ya AICC mwaka 2017 tukiwa kwenye Kamati yetu pale Arusha, kwamba wale mkakati wao na strategic plan zao zote wamepewa tangu mwaka 1978 waendeleze utalii Tanzania na siyo kung’ang’ania pale Arusha kwenye yale majengo. Tukawa tumewaeleza, kwa nini mpaka leo hii Tanzania ina ardhi kubwa sana, hamjajitanua? Wakawa hawana majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukiwa tunapitia taarifa za AICC tuliweza kugundua ukarabati wa Jengo la Simba, ule ukumbi wa Simba hawa AICC, wamekarabati kwa shilingi bilioni 3.5. Tukiangalia nyumba walizojenga, wamejenga nyumba zaidi ya sita pale zenye ghorofa zaidi ya sita kila moja na zile nyumba zimegharimu shilingi bilioni 1.8. Kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha unaofanyika na Idara hizi za Utalii Tanzania na lazima Mheshimiwa Waziri asimame imara kufufua makaburi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine taarifa ya Kamati imezungumza suala la Olduvai Gorge kwamba ni sehemu ambayo binadamu wa mwanzo Tanzania kwa taarifa za kihistoria amegundulika Olduvai Gorge. Taarifa za mapato ya Serikali kuanzia mwaka 2012/2013 Olduvai Gorge kwa mwaka ilikuwa inaliingizia Taifa hili shilingi bilioni 1.7. Baadae akatokea kidudu mtu pale, Wizarani Idara ile ya Olduvai Gorge ikaondolewa kwenye Idara ya Mambo Kale na ikapelekwa kwenye Shirika la Umma la Ngorongoro na hivi sasa Olduvai Gorge kwa mwaka inakusanya shilingi milioni 700 pekee badala ya shilingi bilioni 1.7. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ufisadi watu wame- under estimate pale. Serikali lazima ifanye upembuzi yakinifu, ihakikishe ya kwamba Mheshimiwa Waziri anaunda Tume Maalum, anafukua makaburi ili tuweze kutoka hapa tulipo na nchi yetu iweze kupata mapato. Kwa hiyo, kusema kwamba eti Mheshimiwa Waziri anafanya maamuzi haraka haraka, hili siyo kweli na mimi siungi mkono hoja. Nampongeza na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kufufua makaburi ili sekta hii ya utalii iweze kuingiza pato kubwa kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine mizungumzie kidogo, kuna pesa ambazo Serikali imekopa, pesa za REGRO ni pesa zilizokopwa Benki ya Dunia, dola milioni moja sawa sawa na shilingi 1,800,000,000 hivi za Kitanzania hivi sasa, ambazo zimepangwa kuendeleza utalii Southern Circuit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa za TTB, zile pesa zimepangwa kuendeleza Southern Circuit, wanazungumzia Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza Kusini, tunazungumza Mtwara na Lindi, Morogoro siyo Kusini, Kusini ni Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, naomba sana zile shilingi bilioni mbili kasoro ambazo zimepangwa kwa ajili ya kuendeleza utalii Kusini ziletwe Mtwara na Lindi watangaze vivutio vilivyopo Mikindani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikindani kuna vivutio vingi sana, tuna soko la watumwa pale, tuna custom pale ya zamani, tuna majengo ya karne ya saba mpaka leo yapo Mikindani, kuna maeneo ambayo Vasco Da Gama alipita akaweka mahema na ndala pale Mikindani, lakini yameachwa. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, Idara hii ya mambo ya kale ipewe pesa na hasa Mtwara Mikindani kule Kilwa Masoko, Kilwa Kisiwani, kuna mambo mengi ya kitalii ambayo Serikali hii inatakiwa iyaone na hasa kupitia idara hii ya mambo ya kale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba Serikali imekuwa ikiangalia sana Northen Circuit, yaani unavyozungumzia utalii, tunazungumzia sana Arusha, Ngorongoro na maeneo mengine kule, lakini huku Kusini kumesahaulika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naitaka Serikali kwamba bajeti inayokuja hizi shilingi bilioni mbili ambazo zimetengwa, basi ziletwe kule Kusini zitangaze vivutio hivi vya utalii kule Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.