Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye taarifa ya Kamati hizi mbili. Niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwanza kupongeza kazi ambazo zimefanywa na Kamati hizi mbili kwa mapendekezo na ushauri ambao wameweza kuutoa kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye Kamati hii ya Kilimo, Mifugo na Maji hasa katika upande wa mazao ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona changamoto ambazo baadhi ya mazao ya biashara ambayo Watanzania ndio tumekuwa tukitegemea kama zao la kahawa, soko limekuwa ni changamoto kwa sababu pia bei imekuwa haipandi na hii ni kutokana na kodi nyingi ambazo zimekuwepo. Pamoja na kwamba Serikali imejitahidi kupunguza, lakini bado kwa kweli mazingira ya uzalishaji wa zao la kahawa na soko na bei bado haijawa nzuri, hususan kwa wakulima wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na zao hilo la kahawa, tumeona maboresho ambayo yamefanyika kwenye zao la korosho na tumeona jinsi ambavyo bei imekuwa ikipanda kwenye korosho. Pamoja na kwamba kumetokea changamoto hiyo ya baadhi ya watu kutokuwa waaminifu na kutaka kuvuruga soko letu, lakini naamini kwamba Serikali itaweza kufuatilia hususani katika uchambuzi huu ambao ulifanyika kwenye mzigo uliokuwa umeuzwa nje na kukuta kwamba kuna uchafu kama mchanga na mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapaswa kujua kwamba kwa kadri tunavyoendelea, yapo mazao mengine ya biashara ambayo yamefanya vizuri duniani na kama ambavyo tunajaribu ku-adapt teknolojia mbalimbali kulingana na mabadiliko ya teknolojia, nafikiri ni wakati muafaka pia kuweza ku-adapt hata katika teknolojia ya kilimo ambayo inaweza ikatusaidia kuweza kuinua kipato cha wananchi walio wengi zaidi asilimia 75, lakini pia ambayo inaweza ikasaidia kuendana na kauli mbiu na sera ya Taifa ya kuwa na uchumi wa kati na uchumi wa viwanda kwa kuanzisha mazao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe wakati wa Bunge la Bajeti lililopita niliwahi kusema kwamba lipo zao linaitwa stevia ambalo linaonekana linafanya vizuri duniani, nikaomba tuanze kufanya utafiti wa zao hili kwa kushirikiana na center ya Utafiti ya Maruku, Mkoa wa Kagera. Naishukuru Wizara ya Kilimo ambao wamekuwa wakinipa ushirikiano kuhakikisha kwamba zoezi hili linafanikiwa, pamoja na kwamba changamoto bado yako kwenye bajeti, lakini naiomba sasa kama ambavyo tulifanya wasilisho la utafiti wa zao hili Wizara ya Kilimo mapema mwaka 2017, basi waweze kupeleka fedha katika Kituo cha Maruku kwa ajili ya kuhakikisha kwamba utafiti huu unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mazao kadha wa kadha. Leo kuna zao kama chia seeds, wengine wanaita super food, ni zao ambalo linafanya vizuri duniani na ambalo katika hali ya kawaida linaweza likabadilisha uchumi wa wananchi wa kawaida, kwa sababu ni zao la muda mfupi, lakini ni zao ambalo linahitajika, pia ni medicinal kwa maana ya kwamba linaweza likaboresha afya ya Watanzania, lakini pia likaboresha uchumi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Kilimo kwamba tayari wanaendelea kunipa ushirikiano na muda siyo mrefu tunaamini kwamba tutapata kibali kwa ajili ya kuingiza mbegu kwa ajili ya kufanya na utafiti wa zao hili ili kuinua uchumi wa wananchi wa Ngara, lakini na wananchi wa Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna namna tunavyoweza kufanya miujiza kubadilisha maisha ya wakulima wa kawaida tusipowekeza kwenye suala la kilimo na kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kwa sababu kumekuwepo na mabadiliko ya tabia nchi, mara kwa mara tunajikuta tunaenda tofauti na matarajio katika misimu yetu ya kilimo.

Kwa hiyo, naomba tuwekeze zaidi katika kilimo cha umwagiliaji. Hatujafanya vizuri, ukiangalia ni kwamba, ni asilimia 1.6 tu ambayo tumefanya kwenye sekta hii ya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuwekeze katika miradi ambayo tayari imeanzishwa, kama mradi wa Bigombo kwenye Wilaya yetu ya Ngara ambayo takribani sasa miaka mitatu iliyopita ulitakiwa uwe umekamilika, lakini haujakamilika mpaka sasa hivi na tumeshatumia fedha nyingi zaidi ya shilingi milioni 715 na miundombinu inaanza kuchakaa wakati haijaanza kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tujikite katika kilimo cha umwagiliaji ili kuboresha maisha ya Watanzania, lakini pia kuandaa mazingira ya kupata malighafi kwa ajili ya kulisha viwanda vyetu ambavyo tunakazana navyo kwa ajili ya kuvianzisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii iko migogoro ambayo imekuwa ikiendelea katika sekta hii, migogoro ya ardhi ni pamoja na mipaka; mipaka kati ya wilaya na wilaya, kijiji na Kijiji, mipaka kati ya maeneo ya ufugaji na kilimo.

Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati.