Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Naomba kuunga mkono taarifa za Kamati zote mbili, iliyosomwa na dada yangu, Mheshimiwa Kemilembe pamoja na mama Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana kwenye ile Sehemu ya Tatu yenye maelezo ya ushauri, maoni na mapendekezo. Kabla ya hapo naomba nikuombe wewe kwa niaba ya Mheshimiwa Spika kwa sababu Mwenyekiti wa Kamati anapomaliza kutoa taarifa yake anasema naomba kutoa hoja na sisi hoja hiyo tunaiunga mkono lakini baada ya hapo tunachangia anakwenda anafanya winding up akishamaliza unatuuliza tunasema ndiyo. Kwa hiyo, unasimama unasema kwamba mapendekezo, maoni na ushauri tunaupeleka Serikalini na Serikali iuchukue. Sasa mimi swali langu, inapochukua ushauri, mapendekezo na maoni haya, hivi Bunge lako Tukufu kwa kila Kamati linapata feedback wapi na wakati gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu upo utaratibu baada ya kumaliza kwa mfano Kamati zote hizi kutoa taarifa zake, siku ya Ijumaa Ofisi ya Bunge inachukua mapendekezo, maoni na ushauri wa kila taarifa ya Kamati inatengeneza kitabu, hiyo ni Ofisi ya Spika, anakabidhiwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu anatawanya yale mapendekezo kwa kila Wizara husika ili baadaye waje walete taarifa Bungeni, sasa sikumbuki mara ya mwisho ni lini ilifanyika hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili sisi Wabunge tujitendee haki ni vizuri kwa yale mapendekezo tunayopendekeza ushauri na maoni yetu, tuwe tunapata feedback. Kama utakuwa ni utaratibu huu wa business as usual, tunatoa mapendekezo, ushauri, halafu hatupati mrejesho, hakuna kitu ambacho tutakuwa tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe tukianza kwa mfano na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, kwenye yale maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wangu wakati anasoma pale ambayo tuliyaridhia, lakini kwa yale maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Mama Mary Nagu, hebu tujipe kwa mfano mwezi Machi, tuwe tunapewa taarifa na Wizara husika kwa yale ambayo tuliyopendekeza kwamba yametekelezwa kwa asilimia ngapi lakini kwa nini hatukuyatekeleza ili tuone namna nzuri zaidi ya kuishauri tena Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu nakumbuka mwaka 2016 tulifanya hivihivi; mwaka 2017 tulifanya hivihivi; 2018 tunafanya hivihivi. Je, ule ushauri wetu, sisi kama Bunge linalotoa mamlaka na sisi kazi zetu kama sikosei kupitia Ibara ya 65 ya Katiba, kazi yetu ni kuishauri Serikali, sasa tunapoishauri, je, tunapata mrejesho kutoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana uielekeze Serikali huu ushauri wetu ikiwezekana tutakaporudi kwenye Bunge la Machi kama siyo maoni, mapendekezo au ushauri wote angalau tupate ili tuweze kuisadia Serikali zaidi. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe sana Serikali kwa sababu kila taarifa iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati humu ndani niliisikiliza. Taarifa nyingi au miradi mingi au utekelezaji wa shughuli nyingi umekwama kwa sababu ya upelekwaji au kutokupelekwa kwa pesa kwenye maeneo husika. Nimwombe sana ndugu yangu Waziri wa Fedha kwa sababu tunataka tutekeleze yale ambayo tunataka yatekelezwe lakini mengine yanashindwa kufanyika kwa sababu hakuna pesa, yale maeneo ambayo yanakulenga wewe moja kwa moja kuhusu upelekwaji wa pesa basi pesa hizo zipelekwe ili kusudi zikatekeleze haya maazimio au mapendekezo ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, kwa sababu mimi ni senior senator si jambo jema kupigiwa kengele ya pili. Nakushukuru lakini kama nilivyoomba tafadhali mapendekezo haya Serikali iwe na utaratibu wa kutupa mrejesho ili tuweze kujua kwamba limetekelezwa kwa kiasi gani. Nakushukuru sana.