Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa nami niweze kuchangia taarifa ya Kamati ya Nishati. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kibali chake na kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge lako. Pia naishukuru sana Kamati yetu ya Nishati na Madini kwa taarifa yake nzuri ambayo iliwasilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri hasa katika Sekta yetu ya Nishati kwa kuwa natambua kabisa na wao wana tambua kwamba sekta yetu ni mtambuka na wezeshi kwa sekta nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zimejitokeza hoja nyingi, lakini naomba nijielekeze kwenye hoja ya umeme vijijini; na hapa naomba nijieleke kwenye miradi kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamesema, kwamba miradi kuna miradi ya REA II ambayo pengine haikukamilika kwa namna moja ama nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeshughulikia na ninavyosema sasa, Wakandarasi mbalimbali wameteuliwa kwa ajili ya kutekeleza miradi REA II ambayo ilikwama. Hapa nasemea kwa Mkoa wa Kilimanjaro na Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, Mama Anne Kilango Malecela na nimtaarifu katika Jimbo la Siha, Jimbo la Siha peke yake lilibakiwa na vijiji vitano tu ambapo REA II sasa ndiyo vinakamilisha. Ndiyo maana naamini Mbunge yule alishawishika baada ya kuona Jimbo zima umeme upo kasoro vijiji vitano, ambapo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, Mama Anne Kilango Malecela, Mkandarasi Njalita yupo site na anaendelea na kazi ya kukamilisha upungufu uliojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, mikoa mbalimbali yote ambayo ina upungufu kwenye REA II, naomba nitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wakandarasi wale walikuwa hawajamaliza kazi katika kipindi cha uangalizi. Kwa hiyo, nawathibitishia, katika kipindi cha uangalizi ni kwamba Wakandarasi watamaliza upungufu uliojitokeza; na kwenye REA III tunawaahidi kwamba upungufu hautajitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwenye suala la nishati vijijini imejipanga vizuri. Ndiyo maana sasa tumeanza safari ya vijiji vilivyosalia 7,873 na Wakandarasi. Ni kweli kipindi cha miezi sita walikuwa na survey, lakini sambamba na hilo Wakandarasi katika kipindi hicho chote walikuwa wameagiza vifaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana nami kwamba Mikoa mbalimbali ambayo tumefanya ziara Wakandarasi wameanza kazi. Ninaposimama leo kusema ndani ya Bunge lako Tukufu, yapo maeneo vijiji vimeshawasha umeme. Kwa mfano, Mkoa wa Geita, Rukwa, Tanga, Pwani na mikoa mingine, Wakandarasi wapo site na wanaendelea na kazi. Ndiyo maana tarehe 13 tulikutana nao tukawapa maelekezo mbalimbali ya namna ya kuanza miradi hii kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nalithibitishia Bunge Tukufu kwamba tumepokea changamoto ambazo zimeelezwa. Tuwataarifu tu kwamba Wizara hii chini ya Waziri wangu tumejipanga vizuri katika usimamizi. Ndiyo maana kwa sasa ngazi ya Mkoa yupo Engineer pekee kwa ajili ya miradi ya REA; ngazi ya Wilaya yupo Technician kwa ajili ya miradi ya REA; na ngazi ya Kikanda yupo mtu wa REA kwa ajili ya kusimamia miradi hii tu. Kwa hiyo, hii yote imefanywa ili kuboresha usimamizi na kuona changamoto ambazo lizijitokeza REA Awamu ya Pili hazijitokezi tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilithibitishie Bunge lako kwamba kwa sasa hata miradi ya Densfication ambayo lengo lake ni kuvifikia vijiji 305 inaendelea vizuri katika maeneo mbalimbali. Sambamba na hilo, hata mradi huu ambao unaendana sambamba na REA III, huu wa Msongo wa KV 400 wa Mikoa ya Iringa, Dodoma, Shinyanga na Tabora nao unaendelea vizuri ambapo vijiji 121 vitafikiwa na miundombinu ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kama ambavyo Mheshimiwa Mama Anne Kilango amesema, ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, imeongeza usambazaji umeme kwa asilimia 28 miaka miwili; naamini na ninawathibitishia, kwa miaka ambayo tumejipanga 2018/2019, 2019/2020 vijiji vyote vilivyosalia 7,873 vitapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie; tulitoa maelekezo kwamba kisirukwe Kijiji chochote, Kitongoji chochote, Taasisi ya Umma yoyote, iwe Sekondari, iwe Shule ya Msingi, iwe Zahanati. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wamesema hilo na sisi ndiyo mwongozo ambao tumetoa na nawaomba Wakandarasi wafanye kama ambavyo Serikali imewaelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote na tunawaahidi Utumishi uliotukuka. Ahsanteni sana.