Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniruhusu kusimama leo tena hapa jioni kuhitimisha hoja ambayo niliiwasilisha tarehe 7 Novemba, 2017 kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/2019.

Aidha, napenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwako wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia vyema mjadala wa hoja. Vilevile niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote 124 waliochangia katika mjadala huu ambapo Wabunge 103 wamechangia kwa kuzungumza ikijumuisha Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao kwa kweli mmenipa raha, lakini pia wapo Waheshimiwa Wabunge 12 ambao wamechangia kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyobainisha katika hoja yangu kuwa lengo lilikuwa ni kuomba maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wakiwa ndiyo sauti za mawazo na matakwa ya wananchi wetu kuhusu maendeleo ya nchi yao, lakini pia mgawanyo wa rasilimali fedha ili yazingatiwe katika hatua ambayo itafuata baada ya kikao hiki cha Bunge ambayo itakuwa ni kazi ya kuandaa Rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha ambavyo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge hili zitawasilishwa kwa Wabunge tarehe 11 Machi, 2018 na kufanyiwa uchambuzi na Kamati ya Bajeti kuwezesha ukamilishwaji wa Mpango na Bajeti ambavyo vitawasilishwa wakati wa Bunge la bajeti. Kwa niaba ya Serikali nakiri kuwa lengo hilo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa na narudia kusema ahsanteni sana. (Makofi)

Mhesimiwa Spika, niruhusu kipekee nitambue mchango wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini. Kamati ilitupatia ushauri wa msingi ambao niliuelezea kwa kifupi wakati natoa hoja, lakini vilevile tulipokea mchango uliotolewa na Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba kwa niaba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara mbalimbali waliotoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa zinazogusa sekta zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa shukrani kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kunisaidia kusikiliza kwa makini maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge kwa siku zote tano na kutolea ufafanuzi kwa umahiri hoja zilizotolewa hapa ndani muda mfupi uliopita. Nitumie pia fursa hii kuwashukuru kwa dhati watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bwana Dotto Mgosha James kwa kuchambua na kutafuta takwimu na taarifa ambazo zilihitajika kwa ajili ya kutolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali. (Makofi)

Katika majadiliano ya hoja niliyowasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu, Serikali imepokea maoni mengi sana. Naomba nitaje baadhi tu kwa kifupi maoni ambayo yalitolewa na Wabunge wengi na hii ni kuthibitisha tu kwamba Serikali inasikia. Maoni hayo ni kama ifuatavyo:-

(i) Mmetushauri kwamba tuweke msukumo pekee kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

(ii) Mmetushauri tujumuishe mkakati mahsusi wa kumaliza kilio kikubwa cha upatikanaji wa huduma za maji nchini kote. (Makofi)

(iii) Mmetuambia kwamba fursa ya uwepo wa rasilimali kubwa ya gesi asilia nchini ni lazima sasa itumike vizuri zaidi. (Makofi)

(iv) Mmetuelekeza tutekeleze kwa dhati utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi yaani PPP. (Makofi)

(v) Mmetuelekeza na kutushauri tuongeze kasi ya kutekeleza miradi ya miundombinu ya kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na ile ya Umeme Vijijini REA III lakini pia barabara muhimu za kuchochea uchumi katika mikoa mbalimbali. (Makofi)

(vi) Mmetushauri tuongeze kasi ya kulipa madeni yaliyohakikiwa.

(vii) Mmetushauri tuhakikishe kuwa Deni la Taifa linaendelea kubakia kuwa himilivu na kuanza kupunguza kasi ya kuongezeka kwa Deni la Taifa.

(viii) Mmetushauri tukabiliane na tatizo la ukosefu wa ajira nchini. (Makofi)

(ix) Mmetushauri kuwekeza na kutumia kikamilifu rasilimali za bahari na maziwa (the blue economy).

(x) Mmetushauri kubainisha mkakati wa kuongeza idadi ya watalii na mchango wa sekta ya utalii katika uchumi. (Makofi)

(xi) Mmetushauri kuhusu kuimarisha uhifadhi wa ardhi, kupima na kupanga matumizi yake.

(xii) Mmetushauri kuchukua hatua za kupunguza kasi ya ongezeko la idadi ya watu.

Mheshimiwa Spika, hayo ni baadhi tu, ni masuala kumi na mbili muhimu ambayo tumesikia ushauri wenu lakini yako mengi sana tutayafanyia kazi. Kwa niaba ya Serikali naahidi kuwa wakati wa kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 tutazingatia ipasavyo maoni na ushauri uliotolewa na Bunge lako Tukufu lilipokaa kama Kamati ya Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kazi yangu, kazi ya Naibu Waziri na wataalam wetu wa Wizara kwa siku hizi tano ilikuwa ni kupokea maoni na ushauri ambao tunakwenda kutafakari na kufanyia kazi, nitapenda nitoe ufafanuzi kwa baadhi tu ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge mlizitoa. Kwa kweli hoja ni nyingi kama nilivyosema na kwa muda ambao nimepewa si rahisi kujibu zote na naomba niwahakikishie kwamba tutawasilisha majibu na maelezo ya hoja zote kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, lakini kabla sijafanya hivyo, naomba nisisitize tena mambo matatu kwa sababu yanajirudiarudia kila mwaka, ni vizuri tukawa tunaelewana kwa faida ya Taifa letu.

Kwanza, nilichowasilisha Bungeni ile tarehe 7 Novemba, 2017 siyo Mpango ni mapendekezo ya mambo ya msingi na vipaumbele vinavyotakiwa kuzingatiwa katika kuandaa Mpango wenyewe na bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo wa kuandaa bajeti yalipitia katika hatua zote ambazo ni kupata maoni ya wadau wa ndani na nje ya Serikali, Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Kikao cha Makatibu Wakuu (IMTC) na kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri kabla ya kujadiliwa na Kamati ya Bajeti na hatimaye Bunge. Hivyo, mapendekezo ya Mpango siyo mpango wa Dkt. Mpango bali ni Mapendekezo ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la tatu, Mapendekezo haya ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/2017 - 2020/2021 kwa mwaka wa tatu. Kwa hiyo, wale wanaodai ni copy and paste kutoka Mpango wa mwaka jana ni vema wakazingatia hili.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya maelezo haya, naomba nijielekeze kujibu baadhi ya hoja na nitaomba nianze na ile hoja ambayo naiona ni muhimu sana kwamba Serikali iache kupeleka fedha kugharamia miradi mikubwa ya kielelezo kama Standard Gauge Railway, ununuzi wa ndege mpya, uzalishaji wa umeme Stigler’s Gorge, miradi ambayo inaweza kutekelezwa kibiashara na sekta binafsi. Ilisemwa hapa kuwa utaratibu huo unapunguza fedha kwa ajili ya kugharamia huduma za msingi kwa jamii kama maji na afya na utapelekea kuongezeka kwa mzigo wa Deni la Taifa.

Mheshimiwa Spika, hoja hii ni vema tukaitafakari vizuri. Serikali inathamini sana mchango wa sekta binafsi na tunafahamu kuwa huko ndiko kwenye pesa na mitaji mikubwa na hasa ukizingatia size ndogo ya uchumi wa Taifa letu kwa hivi sasa lakini pia mahitaji makubwa ya wananchi wetu. Hata hivyo, ni muhimu mawazo hayo yapimwe kiuhalisia na bila kusahau historia na uzoefu wa nchi nyingine. Wote mtakumbuka kwa tulikuwa na RITES of India hapa, hivi naomba niulize walijenga kilomita ngapi za reli? Tumesahau kwamba treni karibu zote zilisimama, mizigo ikawa inasafirishwa kwa malori mpaka Serikali ilipofanya uamuzi wa kuondokana na RITES of India. Hivi sasa kweli hata tukikaa hapa si nalisikia linapita hapo, hatuoni treni za abiria na mizigo zinatimua vumbi. Tena nasikia zinaimba kadogosa kadogosa kadogosa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri wangu ameeleza vizuri wazo la kuzalisha umeme eneo la Stigler’s Gorge lilikuwepo kwenye makaratasi kwa miaka mingi. Hivi sekta binafsi si ilikuwepo na ilikuwa inasikia kilio cha kutokuwepo kwa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu hapa nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na Kampuni hapa ya City Water kwenye sekta ya maji mbona kilio cha maji Dar es Salaam hakijaisha? Yaliyotokea ATCL na TTCL vivyo hivyo, mbona tunasahau haraka hivi? Hata hivyo, sasa tumefanya mabadiliko na tumeanza kufaidi huduma za Bombardier kuja Dodoma, Songea, Kigoma na kwingineko. Aidha, hivi sasa nasubiri gawio mwaka huu shilingi bilioni moja kutoka TTCL kwa mara ya kwanza. Najiuliza hivi umeme huu utakaozalishwa Stigler’s Gorge hautaimarisha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na maji kwa gharama nafuu zaidi? Nawasihi ndugu zangu hebu tutafakari vizuri, tusisahau historia, we have the experience. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kuwa ni kweli kabisa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi lakini zipo changamoto kiuhalisia. Mzee Kikwete alituambia akili za kuambiwa lazima tuchanganye na za kwetu kabla hatujafika hatua ya kuwa na sekta binafsi yenye nguvu. Kweli natamani sana wawekezaji wa ndani na nje watatupunguzia huu mzigo. Waheshimiwa Wabunge nilieleza mwaka 2016/2017 kujenga Standard Gauge Railway kwa bajeti ya Serikali ni mzigo mkubwa mno, lakini sekta binafsi tuliyonayo bado inahitaji kulelewa ili iweze kubebea jukumu hili na sekta binafsi kutoka nje hawaji wakati tunapowahitaji na hata wakija wana masharti ambayo baadhi ni magumu kwelikweli na mengine hayana maslahi kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miezi michache ilyopita Mheshimiwa Waziri Mkuu aliita makampuni ili watujengee mtambo wa kuchenjua makinikia na alikuwepo mfanyabiashara mmoja kutoka Dubai, kitu cha kwanza alichoanza nacho anasema pesa ninayo lakini sharti la kwanza sovereign guarantee, aah, magumu haya jamani.

Kwa hiyo, katika mazingira haya hivi kweli tutakaa miaka na miaka indefinitely tukisubiri wawekezaji washuke ndiyo tuijenge upya reli ya kati ambayo ina zaidi ya miaka 100. Uamuzi wa Serikali ni kwamba tuanze kujenga kwa vipande yaani lots wakati tunaendelea na jitihada za kuwashawishi wawekezaji na taasisi za fedha ambazo zinaweza kutukopesha kwa masharti ambayo ni ahueni, hatuja-rule out private sector, hapana, lakini hatuwezi kuendelea kusubiri miaka mingine 50 ndiyo tupige hatua ya kujenga reli yetu ya kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ninong’one na Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Rais Magufuli aliposikia huu mjadala alinipigia simu na aliniambia hivi, Waziri mwambie ndugu yako Mheshimiwa Nape na Mheshimiwa Bashe kuwa nawataka sana hao wawekezaji kwenye ujenzi wa Standard Gauge Railway, wawalete hata kesho, niko tayari kuwapa reli ya Kaliua - Mpanda au Isaka - Mwanza au reli ya Mtwara
- Mchuchuma - Liganga wajenge. Hayo ni maneno ya Mheshimiwa Rais. Natumaini Waheshimia husika will raise up to this challenge from His Excellence the President. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikwa na hoja ya Deni la Taifa linakua kwa kasi kubwa wakati uchumi unakua kwa kasi ndogo na kwamba hali hii itafanya ulipaji wa Deni la Taifa kuwa mgumu sana. Deni la Taifa liliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 22,320.76 mwaka 2016 na kufikia dola za Marekani milioni 26,115.2 mwezi Juni, 2017 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 17% na deni hilo ni sawa asilimia 31.2 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na ukomo wa uhimilivu wa asilimia 56. Uhimilivu wa Deni la Taifa hupimwa kwa kuzingatia uwezo wa nchi kulipa deni husika katika muda mfupi, wa kati na muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kulinganisha Deni la Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki ni kama ifuatavyo; Uganda ni asilimia 35.4, Rwanda asilimia 36.6, Burundi asilimia 43.4 na Kenya asilimia 50.4. Hali hii ya nchi za Afrika Mashariki bado ni nzuri ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine kama Zambia ambayo ni asilimia 57.2, United Arab Emirates asilimia 60.3, Marekani asilimia 73.8, Morocco asilimia 77, Uingereza asilimia 92.2, Misri asilimia 92.6, Msumbiji asilimia 100.3, Italia asilimia 132.5 na Ugiriki asilimia 181.6. Kwa takwimu hizi sisi bado tuna nafasi kubwa ya kuendelea kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, tutaendelea kukopa kwa sababu kuu moja tu, ni kukuza uwezo wetu wa baadaye wa kumudu uendeshaji wa nchi yetu na kulinda uhuru na heshima ya nchi yetu. Napenda nisisitize hakuna dhambi ya nchi kukopa ili mradi nchi husika itumie fedha hizo za mkopo kukuza uwezo wa uchumi, kuzalisha na kurejesha hiyo mikopo, ni lazima iwe prudential borrowing. Kama Mheshimiwa Rais alivyosema alipokuwa ziarani kule Kagera kwa kweli tutaendelea kukopa mpaka kieleweke ili mradi Deni la Taifa tuhakikishe linaendelea kuwa himilivu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda nitoe angalizo kuwa ukokotoaji wa uhimilivu wa Deni la Taifa japokuwa siyo rocket science unahitaji utaalam. Kujua hesabu za kikwetu haitoshi kufahamu namna ya kukokotoa deni in present value terms maana masharti ya mikopo na muda wa kuiva wa madeni haya yanatofautiana sana. Siyo suala la kujumlisha mkopo fulani in nominal terms na kuamua kuwa deni halitakuwa himilivu. Namuomba Mheshimiwa Kishoa na wengine kama wanataka lecture bure kuhusu debt sustainability analysis waje pale Hazina tuko tayari kuwafundisha bila malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliombwa hapa tutoe ufafanuzi kwa nini takwimu za Deni la Taifa katika vitabu vya Mpango vya mwaka 2016/2017, 2017/2018 na 2018/2019 zinatofautiana. Katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2017/2018 takwimu zinaonyesha kuwa Deni la Taifa hadi kufikia Juni, 2016 ni dola za Marekani milioni 18,614.93 wakati katika Mwongozo wa Maandalizi wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/2019 takwimu zinaonyesha Deni la Taifa hadi Juni, 2016 ni dola za Marekani milioni 22,320.76. Deni la Taifa linajumuisha deni la Serikali la ndani na nje pamoja na deni la nje kwa sekta binafsi. Deni la Serikali la nje linajumuisha mikopo kutoka nchi wahisani, mashirika ya fedha ya Kimataifa pamoja na mabenki ya kibiashara ya kimataifa. Wakati deni la ndani la Serikali linajumuisha dhamana za Serikali za muda mfupi na hati fungani za Serikali pamoja na madeni mengineyo.

Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/ 2018 za dola za Marekani 18,614.93 ni deni la Serikali na siyo Deni la Taifa kwa kuwa halikujumuisha deni la sekta binafsi. Aidha, mtoa hoja angepitia kifungu hicho hadi mwisho angeona Deni la Taifa hadi Juni, 2016 ni dola za Marekani milioni 23,093.3 na kiasi hiki ni tofauti na kile kilichoripotiwa katika Mwongozo wa Maandalizi na Mpango wa Bajeti wa mwaka 2018/2019 ambapo Deni la Taifa kwa kipindi hicho ni dola za Marekani 22,320.76. Tofauti hii ya dola za Marekani 772 inatokana na kubadilika kwa deni la sekta binafsi na kupungua kwa deni la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufuatia kukamilika kwa uhakiki wa madeni hayo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya taarifa za benki za biashara nchini zinaonyesha kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa mikopo binafsi, mikopo ya biashara na mikopo kwa sekta za uzalishaji. Hali ya kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mikopo imetokea katika nchi kadhaa ikiwemo Tanzania kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja na nusu sasa. Katika miezi kumi na mbili iliyoishia Septemba, 2017 wastani wa ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi nchini Kenya ilikuwa asilimia 3.8, Tanzania asilimia 5.0, Uganda asilimia 5.2 na Rwanda asilimia 10.3. Katika nchi zote hizi ukuaji wa mikopo katika kipindi kilichotajwa ulikuwa chini ya nusu ya ukuaji katika kipindi kama hicho kilichotangulia.

Mheshimiwa Spika, kushuka huku kuna sababu mbalimbali ikiwemo kupungua kwa utashi duniani yaani kwa kiingereza general decline and global demand ambako kunajidhihirisha kwa bei za bidhaa duniani kuwa chini kiujumla. Hii inaathiri mapato ya sekta binafsi yaani cash flows na kufanya zisichikue mikopo kwa kasi ile ile.

Pili, mabenki kuongeza tahadhari katika shughuli zao kutokana na hali ya wasiwasi duniani yaani global uncertainty. Matokeo ya kuongezeka kwa hali ya wasiwasi ni pamoja na benki kadhaa kupoteza mahusiano na benki za kimataifa yaani correspondent banks katika kile kinachoitwa de-risking.

Tatu, ni kupungua kwa fedha za bajeti za Serikali kutoka nje ya nchi ambako kumepunguza ukwasi uliokuwa ukisababishwa na matumizi ya fedha hizo na hivyo kuathiri utashi ndani ya nchi kiujumla yaani domestic demand. Mfano, fedha za bajeti kutoka nje zilizotumika zilipungua kutoka shilingi bilioni 2,711 mwaka 2013/2014 hadi kufikia shilingi bilioni 1,774 mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua za kuongeza ukwasi na zinafahamika, Benki Kuu imeshusha riba yake yaani discount rate kutoka asilimia 16 Machi, 2017 hadi asilimia 9 Agosti, 2017. Pia kupunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara (Statutory Minimum Reserve Requirement - SMRR) kutoa asilimia 10 mpaka 8 Aprili, 2017. Benki Kuu pia imeendelea kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua hizi, hali ya ukwasi katika mabenki imekuwa ni ya kuridhisha kuanzia kipindi cha nusu ya pili ya mwaka 2016/2017 na hii inadhihirika katika kupungua kwa riba ya mabenki yaani interbank market rate kutoka wastani wa asilimia 13.49 Disemba, 2016 hadi asilimia 3.72 Oktoba, 2017. Kupungua huku kwa riba katika soko la mabenki kumedhihirika pia katika soko la dhamana za Serikali ambako wastani wa riba umeshuka kutoka asilimia 15.12 - Disemba, 2016 hadi asilimia 9.45 - Oktoba, 2017. Matumaini ya Serikali ni kuwa hatimaye matokeo ya hatua hizi yatajionesha katika ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwa nini Benki Kuu imeacha kutoa takwimu za uuzaji na uingizaji wa bidhaa nje (import and export data). Ripoti za uchumi za Benki Kuu za kila mwezi (Monthly Economic Reviews) za Julai, Agosti na Septemba ni kweli hazikuonesha takwimu za biashara ya bidhaa nje ya nchi (trade statistics) na sababu yake ni changamoto za data (harmonization) ambazo zilijitokeza katika kukamilisha takwimu hizo baada ya kuanza kutekelezwa mpango wa Himaya Moja ya Forodha ya Afrika Mashariki yaani EAC-Single Customs Territory. Changamoto hizi zinashughulikiwa na mara zitakapokuwa zimetatuliwa takwimu hizi zitaendelea kutolewa, Serikali haina sababu ya kuficha chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, palikuwa na hoja kwamba mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa hayakugusa Zanzibar. Niseme tu kwamba tumesikia hoja hii na tutajadiliana na wenzetu upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar namna bora ya kulishughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Mheshimiwa aliyetoa hoja anafahamu kuwa ilivyo sasa Zanzibar ina Tume ya Mipango Huru lakini pia ina Ofisi ya Takwimu ambavyo sio vya Muungano. Aidha, Zanzibar ina Dira yake ya Maendeleo 2020 na ina Mkakati wa Kupunguza Umaskini (MKUZA) na Maandalizi ya Mipango ya Maendeleo ya Zanzibar inaongozwa na nyaraka hizo na taasisi nilizozitaja, of course, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtakumbuka kuwa yalikuwepo mawazo katika Katiba Pendekezwa kwamba Taifa lifikirie kuwa na Tume moja tu ya Taifa ya Mipango lakini mchakato haukufika mwisho. Aidha, kuna vikao vya pamoja vya Kiwizara na Kitaifa vinavyoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kujadili changamoto mbalimbali za Muungano wetu zikiwemo zile zinazohusu masuala ya kodi ambazo Waheshimiwa Wabunge walizisema, biashara na kadhalika na Wizara ninayoiongoza tunashiriki kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, kikao kijacho kimepangwa kufanywa tarehe 17 na 18 Novemba, 2017 Dar es Salaam na nishauri tu kwamba baadhi ya mambo na hoja ambazo zilisemwa ziwasilishwe kwenye jukwaa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano kwenda Zanzibar napenda sana na nimekwishakwenda mara mbili na napanga kwenda huko mara baada ya kikao hiki cha Bunge. Namuomba sana Mheshimiwa Saada aniandalie urojo tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, aidha, tumefanya vikao na wenzetu wa Zanzibar si chini ya mara nne ndani ya miaka miwili hii ikiwa ni pamoja kikao ambacho aliongoza Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, nyumbani kwake Oysterbay mwezi uliopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, palikuwa na hoja muhimu ambayo mimi nasema ni ya msingi sana kwamba sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi vipewe kipaumbele katika Mpango na Bajeti kwa kuwa mchango wake ni muhimu sana katika kuwezesha harakati za kufikia uchumi wa viwanda na kupunguza umaskini. Serikali inakubaliana kabisa na hoja hii na tutaizingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba toka mwanzo na pia katika wasilisho langu wakati natoa hoja, sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda. Kwa msingi huo, eneo hili litafafanuliwa katika Mpango wa mwaka ujao na litahusisha maeneo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge waliyasisitiza ikiwemo upatikanaji wa uhakika wa chakula, malighafi za viwanda, miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo, utafiti wa kilimo na mbegu bora na pia kuboresha huduma za ugani, usindikaji wa mazao, miundombinu, hifadhi ya masoko pia kuboresha miundombinu ya uzalishaji wa mifugo na kuongeza bidhaa za mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, hoja ni nyingi na ningependa tungepata muda zaidi wa kuzifafanua lakini tutazifafanua kwa maandishi.

Kabla ya kuhitimisha hoja yangu, napenda kwa mara nyingine tena kutoa shukrani za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/2019. Nasema hivi kwa dhati ya moyo wangu. Aidha, naomba sana Mbunge yeyote asisite kunikosoa katika utendaji wangu wa kazi kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia tena, naomba sana Mbunge yeyote asisite kunikosoa katika utendaji wangu wa kazi kwa maslahi ya Taifa letu. Hata hivyo, nawasihi mnikosoe au kunipongeza kwa haki na hofu ya Mungu. Namuomba sana Mungu, napata kigugumizi kusema maneno haya lakini nitasema tu. Namuomba Mungu anipe moyo wa kuyapokea yale yote yaliyonenwa juu yangu pasipo kweli, japokuwa kama binadamu yalinisononesha, napenda nilihakikishie Bunge hili na Watanzania kwa ujumla kwamba mwenendo wa mjadala wa hoja hii umeniimarisha zaidi kuendelea kutimiza wajibu wangu kwa Taifa na naamini Mungu atanisaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kumsihi Mungu awabariki Waheshimiwa Wabunge wote bila kuwabagua wale walionivika joho la ujeuri yaani arrogance na uziwi. Hii imenifanya nikumbuke kuwa watoza ushuru walichukiwa hata kabla ya wakati wa Yesu na hivyo mimi nikiwa msimamizi wa watoza kodi inabidi tu niyapokee. Bahati nzuri ni kuwa wananchi wenu ambao fedha hizi za kodi tunazielekeza kwenye maendeleo yao ikiwemo kununua dawa na vifaatiba, elimu msingi bure, umeme vijijini, kuboresha huduma za maji na kadhalika wamewasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo awali, Serikali itazingatia maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge katika kukamilisha maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019. Kuthibitisha hili, napenda nirudie kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Mpango ujao utazingatia kwa kadri inavyowezekana ushauri uliotolewa na Kamati ya Bajeti na Bunge zima likikaa kama Kamati ya Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi kuhitimisha hoja hii bila kumshukuru kwa dhati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake wa karne, ni chuma kweli kweli. Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliposema hayo hakukosea kabisa. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunitia moyo niendelee kutekeleza majukumu yangu ya msingi ya kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kudhibiti matumizi ya fedha za umma bila uoga kwa faida ya wananchi wanyonge hata pale wachache wanaponidhihaki binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kadhalika namshukuru sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa Ruangwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimejifunza katika miaka hii miwili kwamba kweli Waziri Mkuu wetu ni kocha na kapteni mahiri wa utendaji Serikalini kama alivyo kwenye medani za mpira wa miguu. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuendelea kunipa confidence katika utumishi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wito wangu ni kwa Waheshimiwa Wabunge wote kuendelea kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli katika dhamira yake ya kujenga Tanzania mpya ambapo wananchi wote watanufaika na rasilimali za Taifa ili kuwaondoa kwenye lindi la umaskini. Pamoja na mambo mengine, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, kuendelea kuwahimiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao na Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rai yangu kwa Watanzania wote ni kuwa tuungane kwa pamoja na kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na uadilifu mkubwa kwa nchi yetu. Mageuzi makubwa anayoyaongoza Rais wetu ni magumu tena magumu sana lakini ndiyo njia sahihi kuelekea Tanzania mpya. Kwa mfano, uamuzi wa kuhakikisha fedha za Serikali zinarejeshwa Serikalini ili zitumike kuwahudumia wananchi haukupokelewa vizuri na wahusika lakini ukweli utasimama. Haiwezekani, labda wasubiri nitakapoondolewa kwenye Uwaziri huu, akaunti za Serikali, mfano fedha za polisi zikaendelea kushikiliwa na kampuni binafsi inaitwa Max Malipo kwa ambao hawaijui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaahidi kuwa yale yote yaliyo chini ya mamlaka niliyopewa nitayasimamia bila kutetereka ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa tunapiga hatua kubwa zaidi katika ukusanyaji wa kodi na mapato yote ya Serikali, kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato na kupanua wigo wa kodi sambamba na kusimamia matumizi ya fedha za umma kama Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 inavyotuongoza.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.