Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata nafasi kwa siku ya leo kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kuweza kusimama kwa mara ya kwanza leo kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Mimi sitaki nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri nataka nikupe pole, mzigo huu ni mkubwa na nadhani Serikali ya Chama cha Mapinduzi hamjajipanga katika kutekeleza na kuwatumikia Watanzania ipasavyo katika suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo, mifugo na uvuvi imebeba sehemu kubwa kama siyo yote ya maisha ya Watanzania. Watanzania wote utawakuta asilimia kubwa wanaogelea katika taasisi hizi tatu. Kwa hiyo, sidhani kama mmejipanga vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali nzima kutokuwa na vision tunakwenda wapi ndiyo tatizo ambalo linapelekea kilimo chetu na masuala yetu yote ndani ya nchi hii hatufikii pale ambapo tunakusudia na inakuwa ni ubabaishaji tu. Hatuna vision tunataka kulima nini, tulime wapi, tupeleke wapi na kwa namna ipi, hakuna!
Kwa hiyo, unakuta Rais anayekuja ana mipango yake katika kichwa, Waziri anayemweka ana mipango yake katika kichwa, hatuna vision ambayo kama nchi tumepanga kwamba tunataka kulima kitu hiki ili tukipeleke kwenye kiwanda hiki au tusafirishe, hakuna hiyo vision. Ni kila anayekuja, anakuja na mawazo yake na fikra yake ndio maana ndugu ni kawapa pole.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hatuna vision, tunataka kulima nini, tulime wapi, tuelekee wapi, hatuwezi kupata maendeleo ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mipango ya Serikali si mipango ya kifamilia, si mipango ya mtu binafsi, lazima tuwe na vision, tuwe na mpango ambao tumejipanga. Hatuwezi kupata mafanikio ya Kitaifa kwa miaka miwili au mitatu yakaweza kuonekana, hii siyo sunsumia bwana. Kuendesha Serikali ni lazima watu wajipange, wawe na vision ili mafanikio yale yataonekana baada ya miaka 10, 15 lakini kwa mfumo huu hatuwezi kwenda na itakuwa kila siku tunacheza chakacha tu hapa. Ni lazima tuwe na vision ambayo itakuwa inatuonesha tunataka kwenda wapi, kila Rais na Waziri ajaye awe anaelekeza nguvu zetu hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013/2014 nchi hii imevuna mahindi mengi sana. Natoa mfano wa kuthibitisha kwamba Serikali haina vision. Kila ukipita humo mikoani unakuta rumbesa za mahidi yamefunikwa maturubai kwa sababu Serikali haikuwa na mpango, haikujipanga mvua ikanyesha mahindi yale yakaharibika yote. Mwaka jana tayari nchi hii unasikia baadhi ya mikoa ina njaa, kwa nini ni kwa sababu hatukujipanga. Hebu kama Serikali kaeni mjipange tunataka kulima nini, kwa wakati gani, tupeleke wapi, tuuze wapi? Tukifanya hivyo tutakuwa tumefanikiwa na haya maendeleo tunayoyazungumza leo kutoka hapa kwenda kwenye uchumi wa kati yataonekana vinginevyo itakuwa tunakata viuno tu hapa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee suala la pili la mifugo. Nchi ya Tanzania imebahatika kuwa na mifugo mingi zaidi ya wananchi wake, lakini tukijiuliza hii mifugo imetusaidia nini, imetupeleka wapi, imesaidia nini katika Pato la Taifa? Matokeo yake badala ya kutupa mafaniko chanya inatupa mafanikio hasi. Leo wananchi kwa wananchi wenyewe kwa wenyewe Watanzania wanapigana kwa sababu ya mifugo yao, kwa sababu ya kilimo chao. Leo wafugaji wanaonekana kama ni maadui ndani ya nchi hii, leo wafugaji mifugo yao haijawasaidia chochote, haijawanufaisha chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Serikali basi ituambie ni mkakati gani wa muda mrefu ambao imepanga ili kuweza kuona kwamba mifugo hii, tena hapa ametaja vizuri tu katika ukurasa wa kumi idadi ya mifugo ile ambayo inamilikiwa na watu tu inazidi idadi ya Watanzania mbali ya hiyo ambayo ipo katika mapori. Sasa itatusaidiaje au sisi tunalewa sifa tu kwamba Tanzania ni nchi ya tatu katika Bara la Afrika kuwa na mifugo mingi lakini inatusaidia nini, tumejipanga vipi? Kwa hiyo, sisi ni sifa tu Watanzania tupo hivi na hivi. Akili za kupanga mapinduzi ya kupindua Serikali ya Zanzibar ya wananchi mnayo lakini akili ya kukaa mkapanga sasa namna gani tutumie rasilimali hii Mwenyezi Mungu aliyotupa ili tuwaletee wananchi wetu maendeleo hiyo hakuna, ni ubabaishaji tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii ambayo unatupa mwaka huu na mwakani kipindi kijacho cha bajeti utakuja kutupa taarifa hii. Hata hivyo, tuseme ukweli kama bajeti iliyotengwa kwa Wizara ya Kilimo wanapewa asilimia 38 tunategemea nini? Tusitegemee kitu chochote kwa sababu asilimia 38 hawawezi hawa kutekeleza majukumu yao, kwa hiyo, atakuja hapa iwe sababu yake sikuwa na bajeti na kweli tutamlaumu nini? Hebu tuacheni kuongeza kimo kwa kinu tupange bajeti kulingana na ule uwezo ambao tunao halafu tumkamate Waziri tumekupa kiasi hiki na hukuweza kufikia yale malengo. Leo unampa asilimia 38, kwa hiyo, badala ya kufanya kazi unampa mzigo sasa wa kufikiri atumie vipi kiwango kile kidogo cha pesa uliyompa kwa ajili ya kufanikisha majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa sekta ya uvuvi, hapa ndipo kwenye mtihani mkubwa. Waziri hapa katika hotuba yake amesema nchi ambayo inatarajiwa angalau tuwe na wavuvi milioni mbili tuna wavuvi laki moja, hatujaitumia hata kidogo sekta ya uvuvi, bahari kuu hatujaitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya 2013/2014, Waziri alisema kwamba wamezalisha vifaranga vya samaki milioni 20 na hivyo ndivyo vitagawanywa kwa wakulima ili iwe ni kichocheo cha kuongeza samaki. Vifaranga milioni 20 Tanzania, haitoshi hata mboga ya siku moja, kweli Serikali mpo serious kwamba mnataka kuongeza samaki? Mwaka uliofuata mwaka jana hajatuambia hivyo vifaranga milioni ishirini vingapi vimepona, vingapi vimekufa na imepatikana faida gani. Kwa hiyo, hakuna kitu chochote ni usanii tu ambao unapita hapa tunapigana usanii, tunakuja hapa tunajidanganya, tunawadanganya na Watanzania kuona kwamba tuna bajeti ya trillions of money lakini mwisho wa mwaka faida hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia kwamba kuna uvuvi haramu, tumefanya nini sasa kukomesha uvuvi haramu, unapiga nyavu moto. Hawa wavuvi umewasaidiaje, umewapa elimu gani na umewapa mbadala gani? Je, ni nani kaingiza hizo bidhaa, zimepita wapi, zimelipiwa kodi au hazikulipiwa? Tumlaumu nani, are you serious Serikali ya CCM? Hamjawa serious jamani, hebu kuweni serious halafu tuone baada ya miaka mitano, kumi tutayazungumza haya? Sasa wapinzani tunaposema tunasema kwa sababu tuna uchungu, tunaumia na ndiyo maana tunasema hebu kaeni pembeni tuwaonyeshe namna gani Serikali inaendeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa vifaa, huwezi kwenda kuvua katika bahari kuu na kidau, lazima…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)