Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya Benki ya Dunia katika uzinduzi wa Ripoti ya Kumi ya Mwenendo wa Uchumi Tanzania imeonesha wazi kwamba katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2017, uchumi umeshuka kutoka 7.7% hadi 6.8% ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana (2016). Ripoti hii inanipa wasiwasi juu ya jinsi mpango huu unaoandaliwa utakavyotekelezwa kama mapato yetu ya ndani yatapungua siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari zetu (TPA) hasa ya Dar es Salaam mizigo imepungua sana kutokana na ongezeko la tozo kwa mizigo iendayo nchi za jirani pamoja na mifumo mibovu ya bandari yetu. TPA imeshindwa kuboresha mifumo na miundombinu yake kutokana na kwamba mapato yake yanapokusanywa na TRA yanapelekwa kwenye Consolidated Fund Account na ama hayarudishwi au yanarudishwa baada ya muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri wakati atakapojibu hoja za Waheshimiwa Wabunge aeleze kama fedha/mapato ya wharfage ya TPA yanarudishwa kwa wakati au Mheshimiwa Waziri anaweka time frame ya mapato hayo kurudishwa TPA. Vinginevyo bila modernization ya TPA, wateja wengi watapitishia mizigo yao Durban, Beira au Maputo na matokeo yake bandari itakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji, napenda kuunga mkono kwamba fedha zitengwe za kutosha katika sekta ya kilimo, hasa kilimo cha umwagiliaji, kilimo cha kutegemea mvua kimeongeza umaskini kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta za mifugo na uvuvi; nchi yetu inajivunia sana kuwa na mifugo wengi, ikiwa ni ya pili Barani Afrika baada ya Ethiopia. Mifugo inaweza kubadilisha sana kiwango cha maisha ya wafugaji kama mkazo utawekwa katika ufugaji wa kisasa. Ufugaji una faida nyingi licha ya nyama na maziwa, ngozi yake inaweza kuliingizia Taifa fedha nyingi. Serikali pia inashauriwa kudhibiti kwa uingizaji wa nyavu ndogo badala ya kuzichoma na hivyo kuongeza kiwango cha umaskini kwa wavuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya Wanawake na Benki ya Kilimo, benki hizi mbili zingeweza kuchochea maendeleo ya wananchi wa kima cha chini. Bahati mbaya Serikali na BOT wameshindwa kuisimamia Benki ya Wanawake na hivyo mtaji wake kushuka chini ya kiwango kinachokubalika kisheria. Serikali pia imeshindwa kutimiza ahadi zake za kuiongezea Benki ya Kilimo mtaji kama ilivyoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, out of Tshs. 800 billion ambazo Serikali ilikuwa iipatie TADB, ni Tshs. 60 billion tu ambazo kati ya hizo, ni Tshs. 10 billion tu za kukopesha tangu mwaka 2015, mpango ulikuwa TADB ipatiwe Tshs. 10 billion kila mwaka. Hii undercapitalization ya benki hii itaifanya isiweze kukopesha wakulima na hivyo kilimo kuzorota.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kati ya hizo Tshs. 10 billion, ni Tshs. 2 billion tu ndiyo wamekopeshwa wakulima. Fedha nyingine zimekopeshwa benki nyingine. Katika kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge, naomba Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge kwamba atahakikishaje TADB inaongezewa mtaji wa Tshs. 10 billion kila mwaka na jinsi Mheshimiwa Waziri anavyoweza kuisimamia benki hii ili fedha ziwafikie wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umeme wa vijijini (REA), viwanda haviwezi kuanzishwa bila kupeleka umeme kwenye vijiji. Pamoja na kuanzishwa kwa Rural Energy Fund, TANESCO wameshindwa kuwasilisha fedha, kiasi cha Tshs. 7.4 billion kwa Mfuko wa REA zitokanazo na levy pamoja na faini ya ucheleweshaji. Ni vyema Mheshimiwa Waziri wa Fedha atueleze kwa nini TANESCO hailipi deni hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirika ambayo Mpango huu katika ukurasa wa 48 unalenga kuyaimarisha na kuyatumia katika kuleta mageuzi ya viwanda nchini, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akayaangalia upya kama watumishi waliopo wanaweza kwenda na kasi ya Sera ya Viwanda. Kwa mfano SIDO, STAMICO, CARMATEC na COSTECH wana rekodi ambazo si nzuri kiutendaji. Mheshimiwa Waziri atuhakikishie kwamba taasisi/mashirika haya yana wafanyakazi wenye ujuzi, waadilifu au uwezo wa kwenda na kasi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, SIDO wameacha kilio kikubwa sana kwa wakulima wa tangawizi Wilayani Same. Tangu mwaka 2012 wametengeneza mashine za kuchakata tangawizi ambayo haijafanya kazi hadi sasa, hivyo kuwatia hasara kubwa sana wakulima. CARMATEC wana maeneo mengi waliyopewa kazi ya kutengeneza mitambo ya biogas na uvunaji wa maji, lakini hawakukamilisha kazi hizo pamoja na kulipwa fedha zote. COSTECH walipewa kazi ya ushauri na NIDA na kazi yao haikutumika hata baada ya kulipwa fedha nyingi; ina maana ushauri wao haukukidhi mahitaji ya NIDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma, katika kipindi kinachoishia Juni, 2016, kati ya mapendekezo 3,898 yaliyotolewa na CAG, ni mapendekezo 1,449 tu (37%) yaliyotekelezwa kikamilifu. Hata zile Wizara zilizobainika kutumia fedha vibaya zilizopitishwa kwenye bajeti, bado Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameendelea kuwaongezea fedha kwenye bajeti. Nimuombe Mheshimiwa Waziri atoe mapendekezo jinsi atakavyoweza kuweka mpango madhubuti wa kuhakikisha mapendekezo ya CAG yanafanyiwa kazi kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusus suala la kutozingatiwa sheria ya manunuzi na mikataba mibovu. Serikali imekuwa inapoteza fedha nyingi kutokana na Wizara na taasisi zao kutozingatia Sheria ya Manunuzi, kuingia mikataba mibovu na kushindwa kuwalipa wakandarasi kwa muda wa makubaliano. Matokeo yake Serikali inapoteza fedha nyingi zikiwemo za kulipa faini. Fedha hizo zingetumika katika kuleta maendeleo. Waziri alihakikishie Bunge jinsi Wizara yake itakavyosimamia jambo hili kuzuia upotevu wa fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo hapo juu, naamini yatasaidia katika kuboresha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/2019.