Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipatia fursa hii niweze kuchangia hoja hii muhimu. Nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, mwenye dhamana ya Muungano kwa hotuba yake nzuri ambayo naiunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi kwenye masuala machache ya kikatiba. Moja, ni lile linalodaiwa kwamba Tanganyika imejivika koti la Muungano na inafanya ukoloni na unyonyaji Zanzibar.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii si kweli kwa sababu Muungano huu unatokana na ridhaa ya mataifa mawili yaliyoungana mwaka 1964. Kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010, Ibara ya 1 inatamka hivi; “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 2 inasema hivi; “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko haya yalipigiwa kura ya maoni na Wazanzibari wote wakaridhia. Kwa hiyo, si kweli kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano imejivika koti la Muungano na inafanya ukoloni na unyonyaji kule Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Serikali hizi mbili zimegawana majukumu. Ukisoma Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza wazi majukumu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, majukumu ya Serikali ya Zanzibar, majukumu ya Bunge la Jamhuri, majukumu ya Baraza la Wawakilishi, majukumu ya Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na majukumu ya Mahakama ya Zanzibar. Moja ya mambo hayo ni mambo ya ulinzi na usalama na Mheshimiwa Dkt. Mwinyi ameyatolea ufafanuzi. Kwa hiyo, si kweli kabisa kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano imejivika koti la Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni hili ambalo linazungumzwa kwamba Muungano huu ni wa kulazimishwa.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimekwishasema mabadiliko haya ya Katiba ya mwaka 2010 yamepigiwa kura ya maoni na vyama vyote na wananchi wote wa Zanzibar walishirikishwa wakasema Muungano huu wanaukubali. Katiba hii ya Zanzibar yenyewe inasema Zanzibar ni mojawapo ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ambalo ningeomba kulizungumzia ni suala hiari ya mtu kushiriki uchaguzi. Hii iko kwenye Ibara ya 21 ya Katiba ya Zanzibar, naomba kusoma; “(1) Kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia Wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari.
(2) Kila Mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye maisha yake au yanayolihusu Taifa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushiriki ni wa hiari na kule Zanzibar kuna vyama vingi, vyama vingine vilishiriki, chama kingine kikaamua kutoshiriki ni hiari yao. Kwa hiyo, walitumia haki yao ya hiari kuamua ama washiriki au wasishiriki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hii ni haki yao ambayo iko kwenye Katiba kwamba ni hiari huwezi kuwalazimisha watu waende kwenye uchaguzi na wao walioamua kutoshiriki hawawezi kudai kwamba hawakushiriki. If any thing wanaweza kwenda mahakamani kwa Ibara ya 72 ya Katiba ya Zanzibar inayosema kwamba mtu yeyote anayepinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar ataenda mahakamani. Mpaka leo napozunguza hakuna raia yeyote aliyeenda kufungua kesi kwenye Mahakama ya Zanzibar kupinga matokeo ya Baraza la Wawakilishi katika Jimbo lolote lile. Bunge hili haliwezi kutumika tena kupoka mamlaka ya Zanzibar na Katiba ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba kushauri kwamba Waheshimiwa tuna wajibu kwanza wa kudumisha umoja wa Kitaifa. Hivi ndivyo tunavyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri kwenye Ibara ya 28(1) na ndivyo pia tunavyoelekezwa na Katiba ya Zanzibar Ibara ya 23(4). Ni wajibu kabisa wa Kikatiba na Mungu anawapenda sana watu wanaodumisha amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaosoma Biblia imeandikwa sehemu fulani kwamba heri mpatanishi kwa kuwa ataitwa mwana wa Mungu. Kwa hiyo, tunapozungumza mambo ya umoja wa Kitaifa, naomba kushauri kwamba tuwe waaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.