Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba hii kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Mheshimiwa Waziri Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye anatulinda, ambaye yeye si binadamu, yeye anatupenda hata kama wengine wanatuchukia na Mwenyezi Mungu ameokoa maisha ya Tundu Lissu napenda sana kumshukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka yangu miwili ambayo nimekaa hapa Bungeni kumekuwa na Mpango wa mwaka 2016/2017 na bajeti yake, kukawepo na Mpango wa mwaka 2017/2018 na sasa Mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2018/2019 na bajeti zinakuwa zinapitishwa. Pia mojawapo ya kazi ambazo Bunge hili limekuwa likifanya ni kutunga sheria na mambo mengine yote ambayo yapo kwa mujibu wa vitabu na katiba ya nchi hii na sheria zetu kwa ajili ya kufanywa na Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini najiuliza na kila Mbunge hapa aende ajiulize kama kuna sababu yoyote ya kuendelea kuwa tunaleta hiki kinachoitwa mpango, hiki kinachoitwa bajeti na sheria tunatunga humu tunatumia pesa za walipa kodi maskini wakati Serikali na Rais mwenyewe hafuati hiki kinachoitwa mpango, hafuati sheria na hafuati bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mambo ya mwanzo mawili. La kwanza Mheshimiwa Mpango kila kitu mnachopanga kwa ajili ya wananchi mwisho wake kinaishia kwenye vijiji au vitongoji au mitaa. Bahati mbaya hao Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji na Mitaa wanachaguliwa na wananchi, wanapigiwa kura kama sisi Wabunge kama Madiwani na kwa kampeni.

Kwanza jambo la kwanza hawana security of tenure, anakwenda tu Mkuu wa Wilaya anaweza akamfukuza Mwenyekiti wa Kijiji aliyechaguliwa na wananchi kwa kumsimamisha. Anamfukuza kazi wakati Mkuu wa Wilaya huyo hajateuliwa, hajui hata kura aliyogombea pengine kura za maoni akapigwa, anamfukuza Mwenyekiti wa Kijiji bila kufuata utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili mmekuwa mkiwaaidi kwenye mipango yote, na mnategemea hawa watu ndio wasimamie kazi zile za kuendeleza maendeleo ili mpande kwenye majukwaa mjisifie. Unamlipa Mtendaji wa Kijiji, unamlipa Mtendaji wa Kata lakini haumlipi Mwenyekiti wa Kijiji ambaye ndiye bosi wa Mtendaji. Kwa hiyo, mimi nataka niwaambiwe Wenyeviti wote wa Vijiji wa CHADEMA na wa CCM; hapa ni issue ya maslahi yao, wajue Serikali hii ya CCM haitaki kulipa maslahi yao na inawadharau. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni aibu wakati mwingine Serikali inakuja inazungumza hapa na inasema uongo na wananchi kule chini wapo wanaona hivi vitu.

Unajua wakati mwingine kuna vitu mnaweza mkasema tumefanya, ukasema tumenunua ndege kwa pesa zetu wenyewe kumbe umekopa, hiyo wananchi wa kawaida hawatakuewa. Lakini ukija ukasema kuna madawa hospitali na siku hizi bahati nzuri tv zipo, wananchi wakiwa hospitali wanaona na wakati hakuna madawa, hivi wewe Mheshimiwa Waziri unavyojibu hapa wale wananchi waliopo kule hospitali wanakuelewaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 13 dereva wangu alikatwa panga saa nne usiku, na mimi nilimpeleka kwenye Hospitali ya Wilaya ya Tarime, hakuna gloves, hakuna gozi, hakuna hata sindano ya dawa ya ganzi. Sasa mimi namshangaa Mheshimiwa Waziri wa Afya anakuja hapa anasema madawa yamejaa tele. Sasa labda mtuambie kuna maeneo mnapeleka na maeneo mengine mnayabagua, lakini kama sivyo si vyema mkaja hapa mkazungumza mambo ambayo mnajua Serikali yenu hii imeshindwa na hivyo vitu haviko kule vijijini. Haviko kwenye vituo vya afya, haviko kwenye Hospitali za Wilaya, haviko wala kwenye zahanati na hizi zahanati wanajenga wananchi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Mpango ni mchumi. Huwezi kufanya maendeleo kwa kuharibu maendeleo yaliyokwishafikiwa, yaani huwezi leo ukakuta mtu amejenga nyumba yake, ukabomoa nyumba yake halafu akawa analala barabarani kama watu wa Kimara walivyo sasa hivi na maeneo mengine ya nchi hii, halafu ukasema umefanya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kurudisha watu nyuma. Na unawaambia kwa kiburi kabisa kwamba hakuna fidia yoyote watakayoipata, watu wameishi tangu mwaka 1974, tangu miaka 1980 leo unakuja unapomoa nyumba zao, watoto wa watu wanalala nje. Hebu jiulizeni miongoni mwenu kama ni wewe Mpango kama mtu mwingine yeyote, hebu jaribu kujiweka kwenye hiyo picha, umeangaika umejenga na ndiyo maisha yako yote kesho unajikuta umelala barabarani, jaribu kujiweka hapo kwa sababu sisi pia ni binadamu kama wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekit, miji ya watu inachomwa huko vijijini kwa kisingizio kwamba mnahamisha watu kutoka kwenye mapori. Mnachoma nyumba za watu moto. Watu maskini wamejenga nyumba za miti na majani ma-DC wanakwenda wana-set fire kwenye miji ya watu, watoto wanabaki wanabaki nje unga unaungua madaso, vitaa na vitanda kama anakagodoro kanaungua anarudi kuwa maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo ya watu ya watu maskini, alizungumza jana Mheshimiwa Ryoba hapa, wanakamata mifugo, Serikali hii ya CCM inakamata mifugo ya watu. Sisi Wakurya kwa mfano unakuwa na ng’ombe ndiyo unatumia ng’ombe hao kwa kufanyia kazi ya kulima. Unalima chakula, unakuwa nacho kwenye ghala ng’ombe ndiyo wanatoa maziwa unatumia kama mboga. Leo unakamata ng’ombe wa mtu wote unauza, tena kwa shilingi 70,000 na unamshitaki huyo mtu unamfunga na haya yamefanyika mpaka kule Chato mpaka maeneo mengine ya kwa kina Mheshimiwa Doto kule Bukombe wanajua hili ninalolizungumza. Mnarudisha watu kwenye umaskini, ufukara, mnawaambiwa watu mnawaendeleza subiri hasira yake mtaiona mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala haya yakuwa yanafanyika bila kufuata mpango wa Serikali wala bila kufuata utaratibu. Ukichukua kitabu cha mwaka 2016/2017 zilitengwa pesa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa uwanja wa ndege wa Chato. Juzi nikaona kwenye tv kwamba zimeshatolewa shilingi bilioni 39 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na uwanja umejengwa umefikia kiwango cha asilimia 63; running way yake ina ukubwa wa kilometa tatu wakati uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salamu una running way ya kilometa 3.3; uwanja huu unazidi uwanja wa ndege wa Mkoa wa Kagera, unazidi uwanja wa Dodoma, unazidi uwanja wa Mwanza.

Sasa nataka Mheshimiwa Mpango aje awajibu Watanzania, kama tuna haja ya kuwa na Bunge hili ambalo halijapanga mipango, lakini Serikali ya CCM na Rais wanatekeleza. Ni lini tender ya uwanja ule ilikuwa floated na ni nani na nani walishindana kwenye hiyo tender ili wapate huo uwanja? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi pesa shilingi bilioni 39 zimetoka kwenye bajeti gani ya Serikali ambayo haikupitiwa na Bunge hili? Hizi shilingi bilioni 39 zimetoka kwenye chanzo gani? Tunataka Mheshimiwa Mpango atujibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi sina chuki yoyote na uwanja kwenda Geita sina chuki hiyo, wala Chato lakini uwanja huu ungewekwa walau Geita kwenye maeneo ya Geita au…

T A A R I F A . . . .

MHE. JOHN W. HECHE Mheshimiwa Mwenyekiti, sihitaji hata kupokea hiyo taarifa kwa sababu haelewi kwamba uwanja wa Musoma uko Makao Makuu ya Mkoa kama Geita ambapo kama ungewekwa Geita ungekuwa Makao Makuu ya Mkoa ambako ndiko kwenye economic activites kubwa zaidi kuliko Chato Wilayani, ambako kwanza labda haelewi, kutoka Mwanza Mjini kwenda Geita ni kilometa 105, ambako kuna uwanja mkubwa. Kutoka Chato kwenda Geita ni kilometa 185. Nini maana ya uwanja huu kupelekwa kule? Wanakwenda kubeba nini? (Makofi)

Mnakwenda kubeba ng’ombe mle ndani ndiyo maana mmeweka taa za kuongozea gari barabarani wakati hakuna gari hata tatu zinazopita kwenye ile barabara? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoangalia huu uwanja unatengewa pesa nyingi za watanzania mabilioni nikiwemo mimi. Lazima values for money ionekane, lazima uwanja huu uonekane utabeba nini na utazalisha nini, siyo tuchukue uwanja tupeleke kama Mobutu alivyo…

T A A R I F A

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilindie muda wangu kidogo tafadhali. Huyu ni Naibu Waziri ambaye hajui kwamba KIA ni uwanja wa ndege wa Kilimanjaro na uwanja wa Arusha ni wa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninachojaribu kuzungumza, wala sina chuki na watu wa Geita, ninachozungumza ni kwamba uwanja huu uweze kufungamanishwa na uchumi, unategemea makao Makuu ya Mkoa ndiko kwenye economic activities nyingi; na kama kuna uwanja wa karibu mtu ata-opt kushukia Mwanza badala ya kwenda kushukia Chato ambako ni kilometa 180.