Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba (Intergovernmental Agreement – IGA) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamuhuri ya Uganda kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania)

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba (Intergovernmental Agreement – IGA) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamuhuri ya Uganda kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania)

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Sina budi kuanza kwa kusema naunga mkono hoja tena kwa furaha kubwa sana. Ungekuwa unaruhusu kidedea humu tungesema neema, neema, neema imefunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imepata bahati nzuri, bahati kubwa kwamba hayawi hayawi yanakuwa, hatimaye makubaliano haya au mkataba huu ukawa umesainiwa na sasa hivi unaendelea kuwa mkataba unaitwa treaty. Kwa hiyo, naomba kwanza niseme kama Watanzania tujue tofauti ya mkataba huu na ile mikataba ya madini, mikataba ya madini, those are contracts, ile ni mikataba ya makampuni, lakini hii ni treaty maana yake makubaliano kati ya Serikali na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba kabisa kusema tusipotoshe Watanzania kwa sababu tunataka kutoa mawazo mbadala. Katika suala hili tuungane kama Taifa na kama Bunge, kwanza kumpongeza Rais wetu kwamba hapa ameingiza goli, hapa utake usitake goli limeingia na hongera sana, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili mimi nimelifuatilia kwa muda mrefu na najua kwamba ilichukua muda. Haikuwa kitu rahisi kwa mtu kufanya maamuzi kutoa zile concessions kama tulivyoona pale Chongoleani kwa wale tuliokwenda kuwawakilisha. Katika hili nawashukuru sana kwamba na ninyi mlihakikisha kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Kamati mbalimbali tulishiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niungane kabisa na Taarifa ya Kamati kama ilivyotolewa. Niwapongeze sana kwa kufanyia kazi mkataba huu. Nimesikiliza sana mapendekezo na mimi nakubaliana nayo. Sasa nasimama hapa kuongezea tu yale ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, mimi bomba hili linapita katika kata sita za Jimbo langu. Bomba hili linapotoka Ngenge linaingia Burungula, likitoka Burungula linakwenda Mubunda, likitoka Mubunda linapiga kona liko Karambi, likitoka Karambi linaingia Kimwani, likitoka Kimwani linaingia Nyakabango likipinda likitafuta Chato. Kwa hiyo, jamani ni mambo makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa niaba ya wananchi na naungana na Waheshimiwa Wabunge wengine walionitangulia waliosema kwamba sisi kazi yetu ni nini, kazi yetu kwanza ni kuuelewa mkataba huu na kuusifu na kujua kwamba katika mkataba wa nchi kwa nchi ni give and take, huwezi kusema kwamba utachukua kila kitu uweze kuleta bomba Tanzania, au siyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, bomba hili lilikuwa na njia tatu na mnajua kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alikazana sana kulitoa Kenya kulileta huku, si kazi ndogo, naomba kabisa Bunge hili tumpigie makofi. Katika kulileta, katika mikataba, dhana ya treaty, dhana ya mikataba lazima uwe na concessions, sasa tuko katika kipindi ambacho tunaangalia mikataba yetu, hatutaki kuingia katika mikataba mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba mibovu inatokana na usiri, sasa tuko hapa tunajadili jambo na Kamati imeshaona mkataba unavyokwenda, sasa kuboresha, lakini watakapokuja wanaweza kuja wakasema tunapata nini. Mimi nilikuwepo Chongeleani, Tanga na Mheshimiwa Rais alisema faida tutakazozipata kwa hesabu ya haraka, mapipa 216,000 kwa siku na bei inaweza ikayumba lakini kwa bei ya chini tuliyoambiwa zilikuwa ni dola 12 kwa pipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kila siku tuna uwezo wa kupata dola 2,592,000, hapo utasema kwamba Dkt. Magufuli hakucheza jamani? Alicheza, kwa sababu mafuta haya sio ya kwetu, mafuta ni ya Waganda lakini na sisi tumeingia pale kwa sababu tumepata ushoroba, kwa hiyo tulinde amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuhimiza kwa wananchi wangu, tungependa amani. Sisi kazi yetu lazima tuwe na ulinzi shirikishi, ulinzi wa kitaalam lakini pia ulinzi shirikishi. Kulinda bomba hili litakuwa ni jukumu la Watanzania wote. Tumelipata kwa sababu ya utulivu ambao kwa kweli wahenga waliufanyia kazi na sisi tunaendeleza. Kwa hiyo, ulinzi ndicho kitu kikubwa ambacho nakiona hapa lakini pia na fursa na ajira ambazo Mheshimiwa Waziri ameshasema katika hotuba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi katika suala la ulinzi naomba sasa tusiibue migogoro ya ardhi. Naposimama hapa kule kwangu kuna watu wanapima ardhi katika hizi kata nilizozitaja ambapo bomba linapita na mimi kama Mbunge wa eneo wala sina taarifa yoyote. Kwa hiyo, naomba jamani hapa Serikali, Mheshimiwa Waziri, msituchanganye na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo naomba utusimamie. Suala hili, Waheshimiwa Mawaziri, mimi ntakuwa mkweli, nikiona mnasuasua mimi nakimbia naenda kwa Waziri Mkuu, naamini watatusaidia huko ngazi za juu kama ikibidi lakini tusifike huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabisa katika upimaji wa ranchi, watu wanaosema wanapima ranchi katika maeneo ambapo bomba linapita wanatuchanganya. Wananchi sasa hivi kuna taharuki kubwa sana, wananchi wanalia kabisa nbagila bati twafa twafa. Sasa kilio kule twafa, twafa, wakati tunasubiri bomba, sasa bomba likija upimaji wa bomba utakwendaje? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamezungumzia fidia, fidia ni muhimu na wanaochanganya mambo ya ardhi, ile ardhi itatwaliwa kwa fidia kwa mujibu wa sheria inakuwa sasa bomba litapita katika ardhi ushoroba itakuwa ni mali ya Serikali, haitakuwa tena mali ya watu binafsi. Huwezi kupitisha bomba la Serikali katika ardhi ya watu binafsi, itatwaliwa ile ardhi lakini mimi mwenyewe kama nilivyosema, tutasimamia haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa hili na wewe utuwekee nguvu, hao watu ambao wako kule Muleba wanawachanganya wananchi, naomba Serikali, Mheshimiwa Waziri ananisikia, naomba watusaidie.


Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipofika Biharamulo alisema kwamba suala la mifugo ni ufugaji wa kisasa sasa, mambo ya kurandaranda na mifugo hakuna tena. Kwa hiyo, tunakwenda kupima ardhi lakini kwa taratibu. Huwezi kupima ardhi za vijiji bila kuzihawilisha kwanza. Mimi ninavyojua mchakato wa kuhawilisha ardhi mpaka Rais anatoa notice ya miezi mitatu, sasa hiyo notice ya kwenda kuipima Muleba imetoka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili pia niliwasilishe, na suala lenyewe ni tete tena linavuruga bomba la mafuta, maana yake ni kwamba linakwenda kuvuruga amani tunayoizungumzia. Naomba barua hii ambayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, pia kwa Mheshimiwa Mwijage yeye mdomo wake hawezi akasema zaidi hapa labda lakini mimi nalitaja wazi wazi hapa. Wananchi wa Muleba hawawezi kutuelewa mimi na Mwijage hatutaeleweka na Wabunge wengine hapa kutoka Mkoa wa Kagera tusipozungumza suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili pia litavuruga amani, linapandikiza mgogoro wa ardhi, sisi hatukubali na tunaomba Serikali itusaidie, naamini watendaji wamekurupuka, wamekwenda kule bila kufuata utaratibu naomba mtusaidie na naomba barua hii niiwasilishe kwako na iwe sehemu ya Hansard. Kusema kwamba huwezi kwenda kupima kata sita, kata kumi. Hata na kule Kaskazini pia wameathirika hata sisi wawakilishi wa wananchi hatuna habari, wananchi wanatupigia simu katika taharuki kubwa sana. Wakati Mheshimiwa Rais alipokuwa Biharamulo alifafanua…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tibaijuka malizia maelezo yako dakika moja.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kimsingi ni siku ya furaha, ni wale wanaotaka kutuharibia hao ndio tujadiliane nao lakini nadhani hili ni jambo jema limekuja Tanzania, vijana changamkeni, jifunze mgambo, mkalinde bomba la mafuta. Ahsante sana.