Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Joshua Samwel Nassari

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nawashukuru waliotangulia kuchangia Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Millya angalau wamegusa kidogo masuala yetu na hili suala la KIA na wananchi wa vijiji vinavyozunguka nashukuru leo limesemewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa hiyo nina uhakika limechukuliwa kwa uzito mkubwa zaidi kuliko ningelisema mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana niliongea sana hapa Bungeni, nililia sana, Mheshimiwa Lukuvi unakumbuka ombi langu kubwa kwako lilikuwa ni kama ikiwezekana uje Meru nikuambie nini cha kufanya kwenye mashamba yaliyoko Meru ambayo yaliachwa tangu enzi za walowezi waliokuwepo Meru kwa wale mnaojua historia, nilisema hapa mwaka 1952 watu wa Meru walimtuma Umoja wa Mataifa Ndugu Kiliro Japhet Ngura Ayo, miaka tisa kabla ya Uhuru alikuwa ni Mtanganyika wa kwanza aliyekwenda Umoja wa Mataifa kwa sababu ya kudai ardhi la Meru, Meru land case.

Sasa nishukuru tu kwa Waziri Mkuu kwanza, pili kwa Waziri wa Ardhi ambao wote mlikuja kwa pamoja na Waziri Mkuu alitoa yale maelekezo na Waziri ukaja na tukafanya kazi nzuri sana kwa pamoja, kwa kweli nikushukuru mno na niseme tu kwamba unapokuwa mpinzani siyo unapinga kila kitu kinapofanyika kitu kizuri huwa tunasema na leo mmeona kwa Waziri Lukuvi hapa amesifiwa mpaka na Kiongozi wa Upinzani, kwa wale Mawaziri wengine ambao mna-ego, huwa mnajisikia na huwa hamsikii, jifunzeni kwa Mheshimiwa Lukuvi, nafikiri mtaweza kutengeneza Serikali nzuri sana, na niliwakumbusha nikasema nikasema kuwa hii dunia inazunguka leo Mheshimiwa Profesa Muhongo naye anauliza maswali ya nyongeza humu ndani, juzi alikuwa huko.

Kwa hivyo ego siyo kitu kizuri sikilizeni Wabunge wanaleta vilio gani kwenu, halafu muende kusikiliza msaidie Watanzania, kwa sababu dunia inazunguka kwa kasi niliwahi kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, niseme tu baada ile baada ya ziara yako Mheshimiwa Waziri kule Meru, tulikubaliana kwamba Baraza la Madiwani na hususani Kamati, tufanye ziara kwenye mashamba yote na kujionea halafu tuandike mapendekezo ambayo yatakuwa na consensus ili yaweze kupita Mkoani kuja kwako ili uweze kufanyia kazi. It is very unfortunate na nilikuambia siku ile nikiwa jukwaani pale nikasema kunaweza kuwa na mashaka kwamba kusitokee consensus au siasa za kipuuzi ambazo zimekuwa zikiendelea kwenye Wilaya nyingi nchi hii, zikafanyika na pale Meru zimefanyika kwenye ziara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mapendekezo ambayo yamekuja kwako nashukuru Mungu yamerudishwa nyuma kuja kuanza upya hayakuwa na consensus hata kidogo na yatakayoletwa tena nakuomba ufanye verification utuulize wawakilishi wa wananchi, uwaulize Madiwani uwaulize Wenyeviti wa Vijiji, kwamba haya mapendekezo yamekuwa na consensus au yametoka kwenye ofisi moja pale Wilaya kuja moja kwa moja kwenye ofisi yako bila kuzingatia nini wawakilishi wa wananchi kwa maana ya Madiwani walichokipindekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyo ripoti ya kwanza iliyokuja kwako utaona ndani yake, vile vilio ambavyo nimekuwa nikiongea hapa ndani havijasikilizwa, havijaainishwa ndani yake kabisa, utaona kabisa inaandikwa ripoti ya kuja kumnyang’anya mtu shamba heka 10, heka 18, Meru hatulilii heka 10 na 18 tunalilia thousands of acres, hundred of acres. Mashamba ambayo yalikuwa yanamilikiwa na Walowezi ambayo yalipata kibali cha Rais pia miaka ya mwanzo ya tisini kufutwa, lakini usajili haukufanyika ambapo imerudi kwenye mikono ya baadhi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nilikukumbusha nafikiri unafahamu vizuri kwa mfano, shamba la Tanzania Plantation kwanza nikushukuru kwamba ulikubali kutoa hata fedha kutoka Wizarani kwako kwa ajili ya upimaji na yule mtu alikuwa ameshakubali, mkakubaliana kwamba anabaki na kiasi gani na kiasi gani kiende kwa wananchi, it is very unfortunate kwamba amekwenda Mahakamani kufunga mikono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya watumishi wa ardhi kwenye Mkoa wetu Arusha siyo watu wazuri kwako naomba nikuambie na ndiyo wanaokwenda kuwashawishi hawa Wazungu kwamba nendeni mkafungue kesi Mahakamani mfunge Wizara mikono, mfunge Halmashauri mikono, hakuna kinachoweza kufanyika. Ukweli ni kwamba huyu Mhindi wa Tanzania Plantation na sijui polisi wetu wa Interpol wanafanya kazi gani hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu huyu bwana ana passport mbili, ana passport ya Tanzania na ana passport ya Uingereza, na nchi hii haijaruhusu Dual Citizenship, tumefanya uchunguzi kabisa mara nyingi akiondoka nchini huwa anakwenda Nairobi anaruka na passport yake ya Uingereza, na huyu amekufunga mikono Mahakamani, naomba watu wa Mambo ya Ndani wakusaidie. It is very easy kum-capture huyu bwana, kwa sababu unaangalia rekodi zake za safari na unaangalia kwenye passport yake ziligongwa mihuri lini na lini na tarehe gani kwa sababu kuna tarehe ambazo ameondoka ambapo passport yake ya Tanzania haina hiyo mihuri kabisa, kwa hiyo huyu bwana anatuibia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Waziri anakumbuka kwenye ile list tuliweka hiyo list ambayo imekuja kwako ambayo nimesema haikuwa na consensus liliandikwa na shamba la Karamu, shamba la Karamu tumefanya mazungumzo na Halmashauri pamoja na mmiliki tumembana na amekubali kuingia kwenye terms ambazo Halmashauri kwa maana wananchi wa Meru wanafaidika, vijiji vinavyozunguka kwa maana vijiji vya Ndato na Mkwaranga wanapata share yao na Halmashauri inapanga ule Mji na ule ni Mji ambao ukiangalia master plan ambayo unakuja kuizundua mwezi wa Agosti Arusha, imependekeza lile eneo liwe ni eneo la residential, low density na hilo ndilo lengo letu tunakoelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tulete kwako ufute atakwenda Mahakamani atakufunga mikono tena tutafanya nini, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninaomba tu kwamba hilo liweke kwenye kumbukumbu zako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia kengele niseme tu mengine nitayaleta kwenye maandishi ikiwemo mgogoro wetu ikiwemo na wa Hifadhi ya Arusha na vijiji vinavyozunguka na Momela na mingine pia na issue ambayo ameiongea Mheshimiwa Mbowe lile shamba la Valeska tuende kwa staili aliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunisikiliza.