Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niendelee kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu lakini niendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunijalia afya njema ili niendelee kutoa michango yangu katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara ya Fedha ninaomba nianze kwa kuchangia suala la ukusanyaji wa mapato. Ni jambo ambalo nimekuwa nikilifikiria sana pamoja na kulifikiria hata Mheshimiwa Rais amewahi kuliongelea katika kampeni zake na hata wakati wa kufungua Bunge hili. Suala hilo ni suala la wafanyabiashara kuombwa kulipa kodi wakati hata biashara yenyewe hajaianza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo imani kubwa sana kwamba Wizara ya Fedha ndiyo Wizara ambayo inahusika kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu makusanyo haya ya mapato ya kodi yanakusanywa na TRA. Mfanyabiashara kama hajaanza biashara yake amechukua mtaji wake, anaanza biashara, maana yake ni kwamba anaanza kwanza kwa kulipia kama ni chumba cha kufanyia biashara, pili anaweka bidhaa anazotaka kuziuza. Sasa kama mfanyabiashara huyu unaanza kumwambia kwamba alipe kodi kwanza ndipo aendelee na biashara yake ina maana pesa hiyo anaitoa kutoka kwenye mfuko wake ambao ndio mtaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ninaona kabisa suala hili ni kuwadhulumu wafanyabiashara na sio tu kuwadhulumu bali ni kuwafanya wafanyabiashara wasiwe na moyo wa kulipa kodi. Ndio maana unakuta hapa Tanzania unaona watu hawana moyo wa kulipa kodi. Sio kwamba wafanyabiashara hawataki kulipa kodi, wanapenda sana kulipa kodi lakini kama mtu unataka kuanza biashara unaenda kuomba leseni kwenye Halmashauri, Halmashauri wanakwambia hatuwezi kukupa leseni pamoja na kwamba umejaza fomu mpaka utuletee tax clearance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linawaumiza sana Watanzania na mimi sitapenda kuona watanzania wakiendelea kuumia kwa sababu wanaoumia ni wafanyabiashara wale ambao ni wadogo wadogo ambao pesa zao wanazipata kwa taabu sana, halafu anapokuwa amepata mtaji wake ili aanzishe biashara Serikali na yenyewe inasogea inaanza kumwambia lipa kwanza kodi ndio uende kufanya biashara. Kwa akili tu za kawaida, hata hazihitaji uende darasani, hivi unawezaje mtu ukaanza kulipa kodi kabla hata biashara yenyewe hujaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kubwa sana kwamba nikifungua biashara yangu nikaanza kuifanya ndipo mtu aniijie aniambie lipa kodi, kwa sababu moja kwa moja nitakuwa nimejua baada ya zile administration cost na operation cost, sasa faida yangu ni kiasi gani. Kwa hiyo, hata ukija kuniuliza mapato yangu ninayajua kwa kichwa kwa sababu tayari nimeianza biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri sana Serikali iweze kuangalia na kutekeleza kwa sababu hili ni agizo la Mheshimiwa Rais. Wakati Mheshimiwa Rais anazunguka kwenye kampeni yake, alikuwa anaongea kwa uchungu sana na mimi namwamini sana Mheshimiwa Rais nikiamini yeye anayo nia ya kuwasaidia watanzania ambao ni wa hali ya chini, namwamini sana Mheshimiwa Rais. Sasa sisi watendaji ambao tunamsaidia Mheshimiwa Rais hatupo tayari kumsaidia kwa sababu yale anayoyasema hatuyaweki kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara hii, Mheshimiwa Waziri wa Fedha uweze kufanyia kazi masuala ya TRA kuanza kukusanya kodi wakati mfanyabiashara bado hajaanza kufanya biashara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nisemee kuhusu suala la shilingi milioni 50 katika kila Kijiji. Sitawahi kukaa ninyamaze hata siku moja kwa sababu mimi ni mwakilishi wa wanawake na kila siku nimekuwa nikisema mimi ni mwakilishi wa wanawake sio tu Mkoa wa Mwanza bali Tanzania nzima. Shilingi milioni 50 katika kila kijiji ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Waziri wa Fedha ameeleza kabisa mwanzo kabisa wa ukurasa wake kwamba anatengeneza bajeti hii kutokana na mambo mengi tu lakini Ilani ya Chama cha Mapinduzi ndio ambayo inamuelekeza ni namna gani aweze kutekeleza bajeti yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la shilingi milioni 50 kila kijiji sielewi nianzie wapi, nikiangalia katika kitabu hiki cha Waziri sijaona ni sehemu gani inaonekana shilingi milioni 50 kila kijiji itatoka. Mwaka jana nilisimama hapa hapa Bungeni kwa kutumia kitabu hiki cha Wizara ya Fedha cha mwaka 2016/2017 shilingi milioni 50 katika kila kijiji ilikuwepo, ilikuwa imetengwa. Nashukuru kwamba Kamati imeweza kutusaidia kutuonyesha kwamba katika mwaka wa fedha 2016/2017 shilingi milioni 50 kila kijiji ilikuwa imetengwa shilingi bilioni 59 na kwa mwaka huu wa fedha Kamati imetuambia kwamba katika ukurasa wake wa 20, Kamati inaeleza kabisa wazi pale kwamba shilingi bilioni 59, zilizotengwa 2016/2017 bado hazijatoka lakini kwa sasa Kamati imeeleza kwamba shilingi bilioni 60 sasa imetengwa kwa ajili ya kutekeleza suala la shilingi milioni 50 katika kila kijiji.

Nashangaa sana Mheshimiwa Mbunge sijui anataka kunipa taarifa gani, sijamuelewa, kwa sababu gani, suala ninaloliongea lipo katika kitabu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo mimi najitahidi kuhoji hapa ni kwamba kwa nini kamati imeeleza kwamba shilingi bilioni 60 imetengwa katika mwaka huu wa fedha 2017/2018, lakini katika kitabu chake cha Wizara shilingi bilioni 60 siioni. Kwa hiyo, naomba atakapokuja kusimama pale kuhitimisha hoja yake Mheshimiwa Waziri aweze kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba hii shilingi bilioni 60 ambayo Kamati ya Bajeti inaiongelea kwenye kitabu chake ipo ukurasa wa ngapi, aweze kutuelezea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla muda wangu haujaisha ninaomba niseme kwamba pamoja na kwamba hii shilingi milioni 50 kila kijiji imeelekezwa, lakini hizi fedha kama tutakuwa tunazitenga kila mwaka halafu haziendi, ninaiomba Serikali wakati wanakuja kuhitimisha watueleze ni lini itaanza kwenda. Tumekuwa tukijibiwa humu majibu, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiuliza maswali mara kwa mara na kujibiwa kwamba fedha hizi zitaanza kupelekwa pale ambapo utaratibu utakuwa umekamilika wa kupeleka fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi sasa hivi ukiniuliza tuanze na mradi gani, tupeleke katika vijiji gani, tupeleke katika Mikoa gani, ninaweza nikaisaidia Wizara ya Fedha. Hii ni kwa sababu mwaka jana wakati tunajadili hapa bajeti kuna mikoa ilitajwa kwamba ni Mikoa maskini, ikiwemo Kagera na Kigoma. Tunaomba Wizara hii ilipokuwa imeeleza mwaka jana kwamba wataanza na mikoa mitatu ambayo itakuwa ni mikoa ya pilot study, tunaomba basi hiyo mikoa mitatu watuambie ni Mikoa gani na kama wameshapeleka watueleze ni Wilaya zipi na kama wameshapeleka watueleze vijiji gani ambavyo vimepata pesa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaamini kwamba Watanzania watakuwa wamesikia ni kwa namna gani nimeweza kuwawakilisha katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tena niweze kuongelea suala la allocation ya bajeti, naamini Wizara hii ndiyo inahusika katika kuandaa bajeti, katika kuweka allocation ya resources. Suala la allocation ya bajeti naomba iwe inaangalia zile Wizara ambazo zinagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania. Naomba niishauri Serikali inapokuwa inaweka allocation ya bajeti, iangalie Wizara ya Maji.Wizara ya Maji iwekewe fedha za kutosha.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa Wizara ya Maji ikiwekewa fedha za kutosha wananchi wakipata maji wataweza kulima, baada ya kulima ndipo tutaweza kuanza kuongelea viwanda. Hatuwezi tukaanza kusema viwanda wakati hata kilimo hatukioni. Kilimo hakina dira kabisa, hatuwezi kulima kwenye ardhi ambayo ina ukame… (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini unapokuwa Mbunge, unapokuwa kiongozi katika nchi hii, lazima ujitofautishe. Ninamshangaa sana Mheshimiwa Keissy kwa sababu haelewi kitu anachokiongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeenda shule, hivi Hazina accountability yake iko wapi? Si ipo kwenye Wizara ya Fedha? Sasa unaponiambia kwamba hii shilingi bilioni 50 haihusiki katika Wizara hii, naomba niikatae taarifa yake na niendelee na mchango wangu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende moja kwa moja kuchangia suala la Benki ya Wanawake. Nimekwisha kujitambulisha mimi ni Mbunge na mwakilishi wa wanawake Mkoa wa Mwanza na Tanzania nzima. Suala la Benki ya Wanawake tumekuwa tukilipigia kelele sana humu ndani. Nitaendelea kusema nina amini Wizara ya Fedha ndio ambayo inahusika kupitia Hazina. Treasury ndiyo wanahusika kupeleka fedha, walioenda shule wote watakuwa wananielewa.(Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali itusaidie kupeleka fedha katika benki hii ili kuiongezea mtaji ili wanawake waweze kukopa kila sehemu. Matawi yawepo Tanzania nzima ili wanawake waweze kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie dakika zangu mbili kuhusu suala la malipo ya watu ambao walikuwa wanafanya kazi Afrika Mashariki. Ninaamini suala hili la watu ambao walikua wanafanya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki linamgusa kama sio mimi, litakugusa wewe na litamgusa Mbunge mwingine… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)