Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye hii hoja muhimu ya Wizara ya Fedha na Mipango. Niungane na wenzangu niwatakie wote waliofunga wawe na funga yenye heri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza hii Wizara, nimpongeze Waziri Mpango, Naibu wake, Watendaji wote na Taasisi nyingi ambazo ziko chini ya Wizara hii kwa mafaniko makubwa. Kwa sababu ukiangalia parameter za uchumi, utaona kwamba tunaenda vizuri, bila kuwa na coordination nzuri ya Wizara hii isingewezekana. Kwa hiyo nawapongeza sana wote. Niipongeze pia Mamlaka ya Mapato kwa makusanyo, napongeza pia usimamizi kwenye idara ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali. Kipindi hiki tumepokea ripoti nyingi sana, ukiangalia hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ripoti zaidi ya 600 kwenye majumuisho yake siyo kazi ndogo, kwa hiyo nitumie fursa hii kuwapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo moja kuhusu Wizara hii ya Fedha inayo mchango mkubwa sana kwenye maendeleo ya kilimo. Nataka nijikite kwenye eneo hilo. Nitapenda nizungumzie taasisi mbili kwa maana ya hii Benki ya Kilimo na kampuni ya mbolea. Kwa sababu kilimo kwa ujumla wake kina mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa uchumi, kwa hiyo nafikiri nizungumzie haya maeneo mawili ili nione kwa namna gani naweza kushauri Serikali kupitia Wizara hii muhimu itusaidie wakulima wa Tanzania, wakulima wa Ushetu na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kabisa katika kilimo kweli tutapata chakula, biashara zitashamiri lakini pia ni sehemu kubwa ya kutoa mchango wa mapato yasiyo ya kodi (non tax revenue) inatoka katika eneo hili la kilimo kama Wizara hii itasukuma vizuri na kilimo chetu kiwe chenye tija, ili tuweze kuondokana na kilimo hiki kwa ajili ya kujikimu, ili tuweze kwenda kwenye kilimo cha kibiashara na mapinduzi ya kilimo hasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona yako mambo mengi mazuri ambayo kama Serikali imeyaandaa yanahitaji sasa msukumo wa kipekee ili kuona mchango wake unakuwa mkubwa. Kilimo hiki kitachangia ajira, kilimo hiki pia kitachangia malighafi ya viwanda na katika hali ya ukuaji wa uchumi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kuangalia hata kwenye mfumuko wa bei tumekwenda vizuri sana tuko kwenye digiti moja kama Mheshimiwa Waziri alivyokuwa akizungumza, tuko kwenye karibu asilimia sita, lakini ukiiona hii kwenye upande wa chakula bado mfumuko wa bei siyo mzuri. Tungekuwa na indicator kwa ujumla wake ingeshuka sana kama eneo hili la kilimo litakwenda vizuri. Kwa mfano, sasa hivi kwenye chakula peke yake mfumuko wake wa bei uko kwenye asilimia 11 hivi, ukisoma kwenye tafiti mbalimbali. Kwa hiyo utaona kabisa kwamba tunavyokwenda kuiona inflation kwa ujumla wake kwenye asilimia sita lakini upande wa kilimo imejaribu kutupandisha juu, tungeweza kushuka chini zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko juhudi mbalimbali Serikali ikiwa inafanya ili kuhakikisha kwamba kiwango cha uzalishaji kinakuwa kina tija kwenye kilimo. Kwamba tuende kwenye ukulima ambao unatumia pembejeo za kutosha pia teknolojia ya kisasa, bado kuna matumizi madogo kwenye upande wa umwagiliaji. Sasa bila Wizara hii kuweka nguvu yake na kuwezesha vile vyombo ambavyo kimsingi vinasaidia sio moja kwa moja inaweza ikasaidia pia kwenda kupandisha uzalishaji kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji wakulima waende kulima kisasa, wawe na mashamba makubwa, wawe na mitaji ya kilimo, pamoja na kuwa kuna sekta zingine zinasimamiwa na Wizara zingine lakini bila Wizara hii ya Fedha utagundua kabisa kwamba hatuwezi kwenda kuwa na kilimo kikubwa ambacho kitachangia katika ukuaji wa haraka wa uchumi wetu. Kwa hiyo, nafikiri kwamba lazima Serikali kupitia Wizara hii ituangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia hata mikopo inayotoka ina riba kubwa na bado kuna uchache wa maghala ya kuhifadhia chakula, mara nyingi nimekuwa nikizungumza, naona iko haja ya kuwa na tafiti za kutosha ili kwanza tuwe na chakula cha kutosha ili tuende kwa usalama zaidi. Pia tunahitaji kuchakata mazao yetu ili yaweze kuongeza ubora wake hatimaye yatuingizie fedha za kutosha. Kuna madhara mengi pia katika uhifadhi wa mazingira, kwa hiyo uko umuhimu wa Serikali kupitia Wizara hii kutazama sana kwenye eneo hili la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Kilimo imeanzishwa mwaka 2014 lakini bado msukumo na mtaji ni mdogo sana. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aiongelee.

Nimeiona kwenye hotuba yake nzuri hii, katika ukurasa wa 47 ameizungumza lakini kidogo sana. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, tulipozungumza na benki hii tunaona yako mahitaji ya kuiongezea mtaji. Kwa hiyo, niombe sana Serikali itazame kwa sababu ilikuwa hairidhishi pale ambapo tunaona benki hii imejipanga kutoa mikopo yenye riba ambayo ni nafuu, sasa kama hawana mtaji wanahitaji nao waende kwenye Commercial Bank ili wakakope fedha halafu waje wakopeshe wakulima wetu, haitawezekana hizi rate ambazo wamezionesha kwenye sera yao. Kukopesha mikopo ya bei nafuu haitawezekana kama na wao wanaenda kwenye mabenki mengine yenye riba kubwa kwa sababu mtaji wao bado ni mdogo. Mtaji wao uko kwenye bilioni 60 lakini Serikali ilikuwa imeahidi kusaidia angalau bilioni 100 kila mwaka kwa miaka nane ili benki hii iende kwenye mtaji wa bilioni 800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona sasa muda umekuwa mwingi bado benki hii haina mtaji wa kutosha. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana aitazame benki hii ili mwisho wa safari tuweze kuona kwamba wakulima wetu wananufaika. Utaona kabisa kati ya majukumu mazuri ambayo benki hii tumeipa baada ya kuianzisha inatakiwa iweze kutoa mikopo yenye riba nafuu, itatakiwa ifanye tafiti za kifedha, tafiti za kiuchumi katika sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kabisa kwamba ukienda kwenye maeneo ya vijiji bado tuna shida hata hii mikopo inayotoka tunaiona ina sura nzuri ya riba ya asilimia 18 lakini effective rate yake kama hatufanyi tafiti za kutosha wakulima wale wanachajiwa kwa mwezi, ukifika mwisho wa safari utaona zile rate zina-attract cost kubwa ambayo ukirudisha ukafanya re-alculation utaona inakwenda mpaka zaidi ya asilimia 30. Kwa hiyo, wakulima wetu wanaumia hawawezi kufanya kilimo ambacho kitaweza kuwapa faida kama hii haitazamwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo benki hii ikiwezeshwa inaweza ikasaidia kuweza kufanya tafiti na kuona kama maeneo yanawapunja sana wananchi iweze kusaidia. Pia itakuwa zoezi zuri la kutoa elimu na kujenga uwezo kwa wakulima, kujenga uwezo kwa ushirika, kujenga uwezo kwenye taasisi zingine za kifedha kama hizi micro- finance hizi zinazokuwepo zinategemea sana chombo kuwe na ambacho itazisaidia ili mwisho wa safari wakulima wetu waweze kunufaika. Kwa hiyo, nafikiri iko haja ya kuiangalia benki hii iweze kupata mtaji ambao utaiwezesha kuweza kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu niliona kwamba kulikuwepo na utaratibu wa benki hii kupata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Sasa sijui Mheshimiwa Waziri tumefikia wapi? Kwa sababu ilikuwa inatia matumaini angalau wangepata hizi dola milioni 93.5 ambazo tulizungumza kwenye Kamati, kama bilioni 204 angalau ingekuwa nusu ya safari tunaanza kusonga mbele. Sasa tumefikia wapi na huu mchakato wa kuisaidia hii benki kupitia huu mkopo ambao Serikali kupitia Wizara hii ilikuwa imefanya arrangement, napenda tujue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado iko pledge nzuri sana kuelekea mwaka 2020/2021 kwamba tuwe tumefikisha hii benki kuwa na mtaji wa trilioni tatu, ingeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa sana katika hii sekta ya kilimo. Kwa hiyo, nafikiri tuitazame kwa nia ya kuiboresha lakini mwisho wa safari tunavyokwenda kwenye uchumi wa kati tutawasaidia sana wananchi wetu ambao wana utayari sana wa kuzalisha kwa tija ili iweze kuleta mchango mkubwa katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kampuni ya mbolea. Kampuni ya mbolea imeanzishwa miaka mingi, imeanzishwa mwaka 1968 lakini ilikuwa na shughuli moja tu ya kushughulikia uzalishaji wa pembejeo pamoja na mbolea kule Tanga. Hata hivyo, hapa mbele ya safari tumekuwa na mkwamo, matokeo yake sasa imekuwa ikiendelea kuwa na jukumu moja la kusambaza mbolea. Usimamizi wake haukuwa mzuri kwa sababu mbolea imekuwa ikitufikia huko vijijini ikiwa na gharama kubwa. Nashukuru Wizara ya Kilimo kuja na mpango wa kununua
mbolea kwa pamoja. Bado natazama na chombo hiki kitaingia wapi ili kiweze kusaidia? Kwa sababu chombo hiki kimekuwa na msukosuko mkubwa sana, kina changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali inadaiwa na kampuni hii, lakini pia utaona kwamba, imekuwa ikipata hasara kubwa sana. Mpaka kufikia mwaka 2015 ilikuwa na accumulated losses ya 30 billion, lakini hawa wanahitaji mtaji, walikuwa wanaomba wapewe kama bilioni 27. Sasa haipendezi kuona wanaomba shilingi bilioni 27 wakati wana madeni zaidi ya shilingi bilioni 30. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba aitazame hii taasisi ili iweze pia kutoa mchango wake katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.