Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Godbless Jonathan Lema

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa niipongeze kwa nguvu zote hotuba yetu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ni hotuba muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikipigia kelele sana habari ya viwanda lakini katika bajeti inayoishia kati ya shilingi bilioni 42.1, Serikali ilipeleka shilingi bilioni 7.6 asilimia 18 tu. Ndiyo maana Mheshimiwa Mwijage anavyosema cherehani nne ni viwanda halafu watu wakamshangaa mimi nawashangaa wanaomshangaa, ni ukweli viwanda vya Serikali ya awamu hii ni cherehani nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo agenda kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano, viwanda, viwanda, viwanda, kati ya shilingi billioni 42 mnapeleka bilioni saba, asilimia 18. Hamtaweza ku-transform nchi hii ili iende katika kuwa Taifa la viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maji, maji ni biashara, najiuliza kwa nini nchi hii haijawahi kuona maji ni biashara, tena maji ni biashara ambayo haihitaji matangazo, maji ni biashara ambapo kila mtu anahitaji maji. Mahitaji namba moja ya binadamu anayeishi ni maji. Maana yake mmeshindwa ku-connect pipe, mmeshindwa ku-connect vyanzo na kuweka mita Serikali ikusanye fedha kutoka kwenye maji. Kama mmeshindwa kuona maji ni biashara cherehani nne lazima iwe ni viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maji shilingi bilioni 33 ambayo walikuwa wapeleke wamepeleka shilingi bilioni 2.9 asilimia 8.4. Ukienda kwenye kilimo na mifugo ambayo ni uti wa mgongo unaajiri zaidi ya asilimia 80 ya Taifa hili fedha iliyokuwa inapaswa kupelekwa ni shilingi bilioni 101, wamepeleka shilingi bilioni 3.3 sawasawa na asilimia 3.31. Waheshimwa sio rahisi kukiri kwamba mmechoka, sio rahisi kabisa, lakini Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kazi yenu siyo kuitetea Serikali ni kuisaidia Serikali ifikie malengo muhimu ya Taifa letu. Leo kama kwenye kilimo kati ya shilingi bilioni 100 wanapeleka shilingi bilioni 3 hiyo tansformation ya agriculture itatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mazingira kwanza wamepanga hela ndogo kabisa, wamepanga shilingi bilioni
10.9. Leo ukiongelea tishio lingine la ulimwengu katika vizazi vinavyokuja ni mazingira. Mazingira ambayo yalipaswa kutengewa fedha nyingi kama ambavyo Jeshi la Ulinzi linatengewa. Leo Mheshimiwa January wamempa shilingi bilioni 10 halafu wakampelekea shilingi bilioni 1.2 sawa na asilimia 11.3, maana yake wao ambao wanasema wanajenga amani na imani ya kizazi kinachokuja kama hawawezi kuona mazingira ni jambo muhimu, kama hawawezi kuona mazingira ndiyo yata-sustain future za watoto wenu maana yake ni kwamba hawajui wanachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ni very seriously na Mheshimiwa Dkt. Mpango haya mambo lazima ayaelewe. Leo wanatoa makandarasi wa barabara, mimi niliongea na Mheshimiwa January nikamwambia habari ya mazingira ni habari sensitive na kwenye hotuba yangu ya Wizara ya Mambo ya Ndani niliiweka, nikasema tishio lingine la amani ya Taifa hili ni uharibifu wa mazingira kwa sababu yatakuja kusababisha njaa kali sana tunakoenda na Bob Marley alisema mtu mwenye njaa ni mtu mwenye hasira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zinajengwa, makandarasi wanaojenga barabara kuanzia sasa wapewe na contract ya kupanda miti. Wakati wanaendelea kujenga urefu wa barabara wapande miti na maji wanayojengea barabara hayo maji wajinyweshee miti. Mti ukiumwagia kwa mwaka mmoja huo mti hauhitaji tena kumwagiwa utakuwa umeota wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nirudi kwenye mambo ya msingi. Mheshimiwa Dkt. Mpango, kauli zao wanazoongea katika jamii zimefanya wafanyabiashara wamerudi nyuma. Leo hawatangazi tena mapato ya TRA kwa sababu wanajua nini kinaendelea. Ikiendelea hivi mwezi unaokuja Taifa hili litashindwa kulipa mishahara. Lugha za viongozi wa juu ni tishio kwa usalama wa uchumi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yetu imesema, leo wafanyabiashara hawana amani. Mheshimiwa Mpango amshauri Mheshimiwa Rais na hao watu wa TAKUKURU hii biashara wanapita Mbezi wanaona nyumba nzuri, wanachukua plot namba, wanakwenda kuanza kutishia watu, watu watahamisha pesa. Wakati Rais anasema fedha imehamishwa ilikuwa haijahamishwa lakini sasa ninavyokwambia watu wanahamisha fedha katika Taifa hili kwa sababu mazingira ya investment yamekuwa ni magumu, vitisho vimekuwa ni vingi, Wakuu wa Mikoa na ma-DC wanajiita ni Marais wa Mikoa, ni Marais wa Wilaya. Kila wakienda kutishia wafanyabiashara wanasema kuna maelekezo kutoka juu. Wafanyabishara wamevunjika moyo, wafanyabiashara wanaogopa kufanya investment kwa sababu ya kauli za viongozi, kauli za viongozi zinaua morale na Mheshimwa Mpango anafahamu uchumi ni confidence, kama huna confidence na Taifa, huna confidence na maisha yako mambo yatakuwa ni mabaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda magereza watu wote wenye fedha kwenye akaunti mbalimbali wanahojiwa na Polisi na TAKUKURU, wanatishiwa kupewa money laundering. Mfumo wenu ambapo nyie mlikuwa watawala uliruhusu hata mtu kununua round about. Nchi hii miaka iliyopita na hata sasa hata ungetaka kununua round about, hata ungetaka uuziwe Ikulu miaka iliyopita ungeuziwa. Ni Serikali hii ilishawahi kutaka kuuza Mahakama ya Rufaa iwe parking ya Kempinski. Kwa uchumi ulivyoyumba …


T A A R I F A . . . .

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilindie dakika zangu, tuendelee na mambo ya msingi, nilisema toka mwanzo mnamjua huyu kijana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema siku za nyuma wote mnakubaliana na ndiyo sababu mnauona huu ukali wa Rais kwamba mfumo haukuwa rasmi sana kuzuia baadhi ya mambo. Hawa watu muwa-engage kwenye uchumi, msiwa-disengage. Kama mnafikiri kuna hela chafu zilitoka ndani ya mfumo wa nchi hii, ni muhimu mkafanya engagement na siyo disengagement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Putin wakati anaingia madarakani alikuta hali kama hii Russia, lakini wale wote ambao walikuwa wamepata hela katika mfumo usiokuwa rasmi hela ambazo zilikwepa kodi, wakiwaza kuwatisha, wakawapa kesi mbalimbali kama money laundering, watahamisha fedha katika njia isiyokuwa stahili na wataogopa kufanya investment katika Taifa hili, watapoteza fedha nyingi sana kupita kiasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Mpango hali inavyoendelea sasa, hali ni mbaya kupita kiasi. Namna pekee ya kusaidia uchumi wa Taifa hili namba moja ni lazima wafanyabiashara warudi kwenye confidence waliyokuwa nayo. Leo watu hawalipwi fedha, biashara za ndani hazilipwi fedha. Hapo Wizara ya Fedha, Katibu Mkuu amekuwa ndiyo Governor, tunajua! Haya mambo tunaambiwa kutoka huko huko kwenye corridor zenu, Katibu Mkuu ndiyo kila kitu. Fedha hazilipwi, mambo hayaendi na kama fedha hazilipwi, Mheshimiwa Mpango yeye ni mtaalam wa uchumi, ili uchumi uweze kupanda lazima watu wa- spend kama watu hawawezi ku-spend watapata wapi kodi? Leo nenda hata kwenye mahoteli hapa Dodoma, pamoja na kwamba Wizara nyingi zimehamishia makazi hapa watu hawana uwezo wa kufanya purchasing, watu hawawezi kununua, hoteli zinafungwa, biashara zinafungwa, watu wanahama kwa sababu wamekosa confidence ya kufanya investment. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Mheshimiwa Mpango namwomba sana aelewe confidence ni muhimu katika investment katika Taifa. Leo TRA wamekuwa kama polisi, ukimuona mtu wa TRA ni hatari. Leo TRA wanakwenda kukusanya kodi wakiwa na Usalama wa Taifa na TAKUKURU. Nawahakikishia, hawatajenga uchumi kwa ukali wanaou- pose katika society. Watajenga uchumi kwa wanasiasa ambaye ni pamoja na Rais, kujenga mahusiano mazuri na kuwapa confidence wafanyabiashara. Bakhresa alikuwa anaondoka nchi hii, wakaenda wakampa eneo la bure ili abaki, wanaoondoka ni wengi. Shares za DSE Mheshimiwa Mpango zinaporomoka mpaka kwa asilimia 90, Serikali imekaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Waziri afanye bidii ya namna yoyote ile arudishe confidence ya wafanyabiashara. Wakati tunawaambia bandarini meli haziji walisema bora zisije, wakaambiwa na TATOA kwamba truck zimepungua kwa asilimia 80, wakasema bora zipungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia, naomba dakika mbili za yule kijana aliyekuwa amenipotezea kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa hotuba ya Mheshimiwa Mpango mwenyewe, matumizi kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2016. Kati ya shilingi bilioni 791 zilizoidhinishwa kutumika katika Mafungu yote tisa jumla ya shilingi bilioni 323 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 68 ni fedha za nje. Hadi kufikia Machi, jumla ya shilingi bilioni 18 zimetumika. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni moja ni fedha za ndani, shilingi bilioni 17 ndiyo fedha za nje. Sasa hizi fedha za nje bado hata hao Wazungu wanaendelea kuwazingua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha muhimu ambacho ningependa nisisitize kwenye mchango wangu confidence ya wafanyabiashara imepotea, vitisho kwa wafanyabiashara zimekuwa nyingi, wataharibu na kuua uchumi kwa sababu ya sifa na kiki ambazo hazina msingi.