Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuendesha vizuri mjadala huu wa bajeti kwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutambua michango iliyotolewa na Kamati ya bajeti chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Hawa Abdurahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini; na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Kandege, Mbunge wa Kalambo, lakini pia mchango uliotolewa na Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba na Kaimu msemaji Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango; lakini pia Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza au kwa maandishi hapa Bungeni. Ninawashukuru wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya Wabunge ambao wamechangia hoja niliyowasilisha, jumla yao 79 na kati ya hao 41 wamechangia kwa kuzungumza, waliobaki wamechangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, ninafarijika sana kwa michango mizuri iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wote. Nitapenda nieleze kwa muhtasari majibu ya hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge na ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kwa kunisaidia kujibu baadhi ya hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kabisa sitaweza kujibu hoja zote na wala kujibu kila kitu ambacho kimesemwa kwa sababu ya muda, lakini naomba niwahakikishie kwamba majibu ya hoja ambazo zimechangiwa na Waheshimiwa Wabunge tutazileta kwa maandishi kabla ya kuahirishwa kwa mkutano huu wa Bunge. Baadhi ya hoja nyingine kwa hakika zilikuwa na mwelekeo wa Bajeti Kuu ya Serikali, basi nazo tutajitahidi kuzitolea ufafanuzi kadiri inavyowezekana wakati wa mjadala wenyewe wa Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo hoja ambazo zimetolewa na Kamati ya bajeti; zipo zilizotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na zimerudiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ambao baadhi ya hoja hizo nitapenda nizitolee ufafanuzi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza kubwa sana ambayo nitapenda nitumie muda kuieleza ni hoja ya upelekaji hafifu wa fedha na hasa fedha za maendeleo kwamba zimeathiri utekelezaji wa bajeti, lakini hasa miradi ya maendeleo. Bajeti ni maoteo; na maoteo maana yake ni kwamba siyo halisi. Ni maoteo ya mapato na matumizi ya Serikali katika mwaka mmoja. Sasa pamoja na jitihada ambazo zinafanyika kuhakikisha kwamba maoteo yanakaribiana na hali halisi, ulimwenguni kote ni nadra sana mapato yakalingana na matumizi. Really, they seldom balance, ndiyo maana Serikali zote duniani zinakopa. Zinakopa ndani na nje na ndiyo maana kuna kubana matumizi na kupunguza matumizi na ndiyo maana tunaweka vipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa fedha kwa mafungu yote, unategemea hali halisi ya upatikanaji wa mapato. Hili limesisitizwa katika kifungu namba 45(b) cha Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015. Najua Waheshimiwa Wabunge wengi wanao weledi wa kuelewa mambo haya upatikanaji wa mapato unategemea mambo mengi. Niseme mawili tu la kwanza, ni ukubwa wa uchumi lakini pia muundo (structure) ya uchumi. Kwa hiyo, kwa mfano, uchumi ambao unategemea kilimo cha kujikimu au uchumi ambao unakuwa na sekta kubwa isiyo rasmi ulimwenguni kote, maana yake ni kwamba wigo wa kukusanya mapato unakuwa ni mdogo. Ukilinganisha nchi ambayo ina industrial base kubwa, nchi ambayo ina viwanda vingi, wao wanakuwa na wigo mkubwa zaidi wa kukusanya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, viko vingi; nchi ambayo ina Serikali dhaifu na Baba wa Taifa alitukumbusha kama mna-weak governance, kama mna rushwa iliyokithiri, daima hamtakusanya mapato. Ni vizuri pia Waheshimiwa Wabunge tukakumbuka na hili nafurahi sana limesemwa na baadhi ya wachangiaji, tunalo tatizo kwamba hata fedha hizi ambazo zinatolewa, zinatumika vibaya. Kwa hiyo, haitoshi tu kusema tumepeleka fedha, ni lazima kuangalia ile quality of expenditure. Pale Hazina tuna Kitengo cha Expenditure Tracking, kwa kweli ukiangalia taarifa zao ni madudu matupu kwenye Serikali Kuu na pia kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo taarifa mpaka unasikitika. Mtu anasema amenunua ubao wa mninga, lakini kanunua mpodo, bei tofauti. Ningeweza hata kutaja Halmashauri ambazo wanasema wametumia fedha kwenye mradi; mradi haupo, ni mradi hewa. Uko udanganyifu vilevile, fedha hizi hizi ambazo tunapeleka, kumbe iko haja ya kuangalia mambo mengi, iko haja pia hata ya kuangalia Serikali yetu ukubwa wake, imepanuka haraka sana japo kwa nia njema kabisa ya kufikisha huduma kwa wananchi wake. Ni lazima tujitathimini tuangalie kama inaendana na uwezo wa Taifa letu kumudu ukubwa wa Serikali ambayo imefikia hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge, mwaka 1996/1997 tulifanya maamuzi kutokana na nidhamu ndogo ya bajeti. Kabisa kulikuwa hakuna fiscal discipline tukafanya uamuzi kwamba tutatumia fedha kadiri tunavyokusanya, tukaanza utaratibu wa cash budget. Kwa hiyo, ni lazima pia kutumia vizuri kile kidogo ambacho tunakusanya kulingana na uchumi wetu. Kwa hiyo, ndiyo sababu kubwa kwa kweli kwa nini fedha ambazo zimekusanywa mpaka hivi sasa, kigezo kikubwa ni uwezo wetu wenyewe wa uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, napenda nitumie podium hii kuwataka Maafisa Masuuli wote, tena wa mihimili yote, Serikali, Bunge na Mahakama kutumia vizuri fedha hizi ambazo tunazikusanya kwa wananchi wetu masikini. Kila Wizara, kila Taasisi, Halmashauri, Mashirika, Mihimili yote ni lazima kujifunza kubana matumizi, kutumia fedha hizi ambazo tunakusanya kutoka kwa wananchi vizuri. Tusiangalie tu asilimia ya kiasi cha bajeti iliyokwenda, tuangalie hizo fedha zimefanya nini? Tuangalie uwezo wa taasisi mbalimbali kutumia hata hizi fedha ambazo ziko.

Waheshimiwa Wabunge, ziko taasisi ambazo hata hizo fedha ambazo zimebaki, wanazo kwenye akaunti mpaka leo hii. Kwa hiyo, ni muhimu sana viongozi wote tuhangaike kuhakikisha kuwa kila raia wa Tanzania anatimiza wajibu wake wa msingi wa kulipa kodi ili mapato yaongezeke, lakini ni lazima tuhakikishe kwamba na wale ambao wanakiuka huo wajibu wa msingi kwa kukwepa au kuvujisha mapato, lakini wanaendelea kufurahia huduma za Serikali, hao ni lazima tuwabane, hatuwezi kuwaacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ilikuwa kubwa sana ni imani ya wafanyabiashara kwa maana ya private sector confidence. Hoja ilikuwa kwamba baadhi ya matamshi ya viongozi yanakimbiza watu, lakini pia biashara zinafungwa na kadhalika. Nisisitize kwamba private sector confidence ni jambo muhimu sana na ni lazima lilelewe, it must be nurtured. Sekta binafsi tulishakubaliana ndiyo injini ya uchumi wetu, lakini katika maeneo tofauti huwa nasema, Serikali na sekta binafsi zinafanana na mapacha walioungana. Kama mapacha walioungana wasipofanya mambo yao kwa pamoja na kwa maelewano, basi hayo maisha hayawezekani na kadhalika hivyo hivyo kwa upande wa Serikali na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika hivyo hivyo kwa upande wa Serikali na sekta binafsi na maana yake ni kwamba lazima pawepo majadiliano (dialogue) kuhusu malengo ya Taifa letu, kuhusu vipaumbele, sera na mikakati. Hii ndiyo sababu kati ya mikutano ya kwanza ambayo Mheshimiwa Rais amefanya mara baada ya kuchukua kijiti cha uongozi wa Taifa letu, mikutano yake ya mwanzo kabisa amekutana na wafanyabiashara chini ya utaratibu wa TNBS na hivi karibuni amefanya nao tena mikutano na katika mkutano ule waliokuwepo ni mashuhuda siyo tu ameelekeza kwamba viongozi wa Serikali ambao watakwamisha juhudi za sekta binafsi katika Taifa letu, hao wawajibishwe mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ameacha wigo wazi na kusema kwamba hata wafanyabiashara ambao wako tayari kuja kuweka viwanda yuko tayari kuwapa tax holiday. Sasa nafikiri ni vizuri kidogo tuwe tunayapima haya ambayo yanasemwa. Mbali na TNBC katika ngazi ya kitaalam kuna majadiliano yanayoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi chini ya TPSF (Tanzania Private Sector Foundation), lakini katika ngazi za Mawizara tumeendelea pia kuzungumza. Siyo zamani sana, mimi na mwenzangu Mheshimiwa Waziri wa Viwanda tuliitisha mkutano hapa Dodoma, tukakaa na wafanyabiashara tukawasikiliza na tumekubaliana tataendelea kukutana kila baada ya miezi minne Wizara ya Viwanda na Biashara imekuwa inakutana na wenzetu kutoka Sekta binafsi kwa kuendana na sekta.

Kwa hiyo, tunazungumza na mlango uko wazi kabisa maana Taifa ni letu wote. Tanzania isipoendelea, hakuna cha kusema huyu ni wa Sekta binafsi na huyu ni wa Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana sheria za mchezo zikawa wazi pande zote. Ni lazima sheria za mchezo zisibadilike badilike, siyo upande wa kodi peke yake, lakini pia na mambo mengine nitaeleza kidogo. Ni lazima gharama ya kufanya biashara kwa wafanyabiashara wetu, ziwe ndogo kadri inavyowezekana na ndiyo maana Serikali inahangaika kuwekeza kwenye umeme, kuboresha usafirishaji, kupambana kidete na rushwa, lakini pia kupambana na ukiritimba kama Mheshimiwa Rais wetu anavyoongoza njia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo katika mchezo wowote, mchezo lazima uwe na pande mbili, Serikali inao wajibu, lakini Sekta binafsi nayo inayo wajibu. Kwa mfano, ni muhimu sana sekta binafsi nayo izingatie business ethics. Ukwepaji kodi, madai ya marejesho ya kodi yasiyo na uhalisia lakini pia hata haya yaliyofichuka hivi karibuni kuhusu makasha ya mchanga ambayo yalikuwa yanapelekwa nje, ni kielelezo wazi kwamba hakuna uwazi na Watanzania tumekuwa tunaibiwa. Jamani hili liko wazi, hata watu ambao hawakwenda shule wanajua mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba viongozi wetu wana dhamana ya kulinda rasilimali za Watanzania kwa niaba yao. Kwa hiyo, pale ambapo kuna mushikeli wa wazi, ni lazima waseme na ukweli utabaki kuwa ukweli. Koleo haliwezi kuwa kijiko hata siku moja! Kama Mheshimiwa Rais mwenyewe anavyosema, msema kweli daima atabaki kuwa mpenzi wa Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee hapo kuhusu kufungua au kufunga biashara. Kufungua au kufunga biashara ni jambo ambalo limekuwepo tangu binadamu alipoanza kufanya biashara. Jambo la muhimu ambalo tunatakiwa kila mara kuzingatia ni kujua ni kwa nini biashara zimefungwa na kwa nini zimefunguliwa? Aina gani za biashara zimefungwa? Zipi zimefunguliwa? Sababu zake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape tu mfano Waheshimiwa Wabunge. Katika miaka ya 1980 ukiitazama China ilivyokuwa baadhi ya mambo haya tunayoyaona ya biashara kufungwa, siyo jambo geni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kitabu hapa kimechapishwa mwaka huu ambacho kinaeleza juu ya uongozi ndani ya Kampuni ya HUAWEI, mila ambazo wanazifuata na jinsi ambavyo walikuwa wanaungana na wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kitabu hiki unaona kabisa kwamba phenomena tunayoiona sasa hivi hapa nchini, inafanana kabisa na wenzetu ambacho walikuwa wana-experience China wakati wanafanya mageuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja ninukuu kidogo sehemu ya kitabu hiki. Inasema hivi, nanukuu kwa Kiingereza kama kilivyoandikwa. Inasema: “Over the decades of reform and opening up there have been many countless stories of rise, decline and heart-wrenching downfall of private companies, their many caucuses lining the street of transformation.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani anaeleza mengi tu kuhusu biashara zilivyokuwa zinafungwa na zile ambazo zilikuwa zinahangaika na mpaka zikaendelea katika mazingira yao. Kwa hiyo ni kweli kabisa zipo biashara zimefungwa lakini zipo nyingi zaidi zilizofunguliwa. Niseme tu kwamba biashara ambazo zimefunguliwa ni zaidi ya zile zilizofungwa, lakini pia ni muujiza kutarajia kwamba hizi ambazo ni nyingi zilizofunguliwa jana, basi leo leo zitakapofunguliwa zitazaa kodi kuliko hizo ambazo zimekuwepo na zimefungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunafanya mabadiliko makubwa ya kimfumo. Kwa kweli hatuwezi kuendelea na uchumi ambao ulijengwa juu ya misingi ya utapeli na ujanja ujanja. Utaratibu uliokuwepo siyo endelevu na ulikuwa unawanufaisha watu wachache. Ni lazima tupige hii hatua na makampuni ambayo yanafuata taratibu hakuna mtu anayasumbua. Mfanyabiashara anayefanya biashara yake halali, anazingatia sheria huyo ni rafiki wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni kusema tutoe amnesty kwa wale ambao huko nyuma walizoea hivyo na tunawadai kodi; jamani mtakumbuka wakati baadhi ya makampuni yaliondoa makontena bandarini bila kulipa kodi, Mheshimiwa Rais aliwapatia wiki mbili za kulipa kodi. Sasa mnataka amnesty ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niseme kidogo juu ya Tume ya Mipango na hasa kwa sababu nina historia nayo; toka uhuru ukifuatilia historia ya Tume ya Mipango imekuwa inahama. Leo iko Wizara ya Fedha, kesho ni Wizara tofauti, kesho inakuwa Tume, kesho inakuwa kitu kingine. Nchi nyingine utaratibu huo unaonekana wazi na huu ni mjadala ambao haujawahi kukamilika popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo faida za Tume ya Mipango kukaa peke yake. Mimi nikiwa Tume ya Mipango, hoja ilikuwa kwamba nakosa hela za kutosha kuendeshea Tume kwa sababu Wizara ya Fedha iko mbali nami. sasa Tume ya Mipango imeunganishwa na Wizara ya Fedha, imekuja kinyume chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, pia naomba mkumbuke kwamba mwenye Mamlaka ya kutengeneza Muundo wa Serikali ni mwenye Serikali. Kwa hiyo, tumwachie maamuzi yake. Yeye anaona ni busara zaidi vyombo hivi viwili vikifanya kazi kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejitahidi katika Wizara ya Fedha kama ambavyo tunafanya kwa Taasisi nyingine yoyote. Tumeipatia Tume ya Mipango fedha kulingana na upatikanaji wa mapato. Hadi kufikia mwezi Machi, 2017 Tume ya Mipango ilikuwa imepokea shilingi bilioni 2.84 ambayo ni sawa na asilimia 70.38 ya bajeti yake ya matumizi ya kawaida. Kwa hiyo, haiwezi kushindwa ku-operate kwa sababu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuliambiwa pia kwamba tutoe fedha shilingi bilioni 1.9 zilizobaki kwa Tume ya Mipango ndani ya mwaka huu wa fedha. Kwa kweli hata kama fedha hizi zingekuwepo, Tume haiwezi kutumia fedha zote hizi kwa tija ndani ya mwezi mmoja uliobaki kabla ya mwisho wa mwaka. Let us just be realistic. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwepo hoja hapa kwamba na ushauri kwamba Serikali ihakikishe Wizara, Idara na Taasisi zake zinatumia mashine za kieletroniki katika kukusanya maduhuli. Huu ni ushauri mzuri tunaupokea kwa moyo mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niliarifu Bunge hili kwamba nimeshatoa maelekezo na tulianza na Wizara zile ambazo zinakusanya maduhuli makubwa kwamba wahakikishe wanatumia mashine za EFD katika kukusanya maduhuli ya Serikali. Niliahidi Bunge lako, tunapomaliza Bunge hili nitakwenda kuhakiki nikianza na Wizara Kuu ambazo zinakusanya maduhuli ya Serikali. Maafisa Masuuli wanisikie waliyeko hapa; wale ambao watakuwa hawatumii EFD hao basi wajiandae kwa shughuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumeendelea na jitihada nyingine ikiwa ni pamoja na kutengeza revenue get way system ambayo itakuwa inatumiwa na Wizara na Idara mbalimbali katika kukusanya Maduhuli ili tuongeze tuboreshe usimamizi wa mapato. Kama nilivyoeleza kwenye hotuba yangu, tumeanza kufanya majaribio ya mfumo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwepo pia hoja kwamba katika mwaka 2015/2016 kuna Wakala 11 zililipa takriban shilingi bilioni 2.97 kwa Wazabuni bila kudai risiti za kieletroniki na hii ilisababisha walipa kodi kukosa kodi na kuisababishia Serikali mapato. Naomba tena kusisitiza kwa Wizara, Idara na Taasisi zote za Serikali, kutumia Wazabuni waliosajiliwa na wanaotumia mashine za kieletroniki ili kuhakikisha kwamba mapato ya Serikali hayapotei, asiyefanya hivyo nimeshamwagiza Mlipaji Mkuu wa Serikali awadhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikumbushwa hapa kwamba ni muhimu Serikali iendelee kuchukua hatua zaidi kupunguza misamaha ya kodi na hususan kwenye mafuta, lakini pia kwenye makampuni ya uchimbaji madini ili tuweze kufikia lengo la misamaha yote kuwa chini ya 1% ya pato la Taifa. tunakubaliana kabisa na ushauri huu na ndicho tumekuwa tunafanya. Shida kubwa iko kwenye vivutio ambavyo ni vya kimkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, zimesikika sauti mara nyingi kwamba ni muhimu sana pia Taifa letu likawa linatoa vivutio ili kuvutia uwekezaji mwingi zaidi. Bado tunabishana, mimi ni mmoja wa watu ambao wanaamini kwamba kodi sio kivutio peke yake. Kwa hiyo, tutaendelea kuichambua hii mikataba lakini pia hata kuhakiki yale maombi ya misamaha ili kuhakikisha kwamba hautumiki kama upenyo wa uvujaji wa mapato. Lengo letu bado ni lile lile; na tulikuwa tunakwenda vizuri mpaka mwaka 2015/2016 misamaha yote ilibakia kuwa 1.1% ya GDP. Kwa hiyo, tulikuwa tumekaribia lengo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina inafanya kazi kubwa sana kama msimamizi wa mali za Serikali. Tunakubaliana na tulichofanya mpaka sasa Wizara imeandaa Waraka wa Balaza la Mawaziri ambao una lengo la kurekebisha sheria iliyopo ili kuimarisha usimamizi unaofanywa na Msajili wa Hazina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka huo sasa uko kwenye ngazi za maamuzi na kwa kweli Serikali tunaona huo umuhimu wa kuimarisha Ofisi hii, na tutaendelea kuijengea uwezo na hususan iweze sasa kuhakikisha kwamba vile viwanda vyote vilivyobinafsishwa, basi waliokiuka mikataba kama nilivyoeleza kwenye hotuba yangu, tunavirejesha viwanda hivyo Serikalini kama hawawezi kuchukua hatua za dharura kuhakikisha kwamba vinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kwa nini Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa ndege, wakati Kampuni yetu ya ndege ina upungufu mkubwa? Kwanza naomba tu niwakumbushe kwamba suala la kununua ndege mahususi kwa ajili ya kuimarisha Sekta yetu ya Utalii, ni kipaumbele ambacho kiko katika mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ambao ulipitishwa na Bunge hili mwezi wa sita mwaka 2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani pia shirika hili ndiyo national pride na ndiyo maana Mheshimiwa Rais na Serikali yake, inahangaikia kupata ndege hizi. Nina hakika wamo Waheshimiwa Wabunge humu ambao wamenyanyasika sana na delays na cancellations za ndege za wenzetu kuja Dar es Salaam. Tutaendelea mpaka lini? Ziko hata nchi ndogo ambazo zina airline zake zinafanya kazi. Kwa nini watalii wapite nchi nyingine badala ya kupita hapa kwetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie kwamba tunatambua upungufu huu na ndiyo maana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amekamilisha ukaguzi wa Shirika letu la Ndege ili kuweze kusafisha mizania ya hii kampuni, lakini pia tumeamua kwamba tutachukua madeni yote ya ATCL ili kuweza kusafisha hiyo mizania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameteua Bodi mpya ya Wakurugenzi ambayo ina weledi katika masuala ya usafirishaji wa anga na usimamizi wa fedha. Menejimenti mpya, lakini pia kuhakikisha kwamba shirika linakuwa na mpango wa biashara wa muda wa kipindi cha kuanzia mwezi Julai mpaka Juni, 2017. Pia wameandaa mpango wa biashara na hatua zote hizi zinalenga kuwa na Shirika la Ndege ambalo litachochea ukuaji wa Sekta ya Utalii, lakini pia kubakiza pride ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja juu ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kwamba kwa yeye kuomba fedha Wizara ya Fedha, basi anakuwa ombaomba, anapoteza uhuru. Kwanza naomba niseme tu kwamba ni good practice kwamba taasisi yoyote ya umma lazima iwe na mahali pa kuomba fedha. Hata mwenye mamlaka anapangiwa hata mshahara. Bajeti ya Ikulu, inajadiliwa humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu pia Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ikawa na mahali ambapo fedha zake zinapitia ili kuomba idhini ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili limeitendea haki bajeti ya CAG. Limekuwa linahoji pale ambapo tunakuwa kwa upungufu wa mapato tumeshindwa kumpatia fedha za kutosha, lakini kwa mwaka ujao wa fedha kama mtaipitisha bajeti ya Wizara yangu, tulikubaliana kwenye Kamati ya Bajeti kwamba Ofisi ya CAG kwa mwaka ujao basi ipewe fedha kama ilivyoomba na tutahakikisha kwamba fedha zinatoka kadri ukusanyaji wa mapato utakavyoruhusu. Uhuru wake uko pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna ofisi ambayo ina msaada kwa Wizara ya Fedha kama Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, huyu ndiye anayenifuchulia mchwa. Mheshimiwa Rais alinipa kazi ya kutafuta mapato na kuyagawa kwa mafungu mbalimbali ya Serikali, Ofisi hii ya CAG ndiyo inanionesha nani anatumia vibaya. Kwa hiyo, kwa kweli Wizara ya Fedha itakuwa ni taasisi ya mwisho kabisa kuibana Ofisi ya CAG kwa ya maana kumpatia fedha za yeye kufanya kazi yake ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kuhusu Mfuko wa Pamoja. Akaunti ya Pamoja ya Fedha kati ya Serikali mbili, hoja ilikuwa kwamba haijafunguliwa na hatua zilizochukuliwa kuhusu suala hilo ni nini? Kufunguliwa kwa Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa kifupi, kutafanyika baada ya uamuzi kuhusu mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha kufikiwa na pande mbili za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyelkiti, hata hivyo kila upande wa Muungano umeendelea kunufaika na mapato ya Muungano yatokanayo na kodi ya mapato, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi yanayopatikana katika kila upande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme moja tu nimalizie hili kwamba kwa mwenendo wa sasa wa mgawanyo wa mapato ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inapaswa kupokea 21%, ndiyo ilikuwa hoja kwamba ilitakiwa ipate 21% na SMT 79% ya mapato. Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Waziri anayesimamia masuala ya Muungano, mgao wa SMZ wa 21% na SMT 79% ni kuhusu ajira, siyo mapato. Ni kuhusu ajira katika Taasisi za Muungano na siyo mgawanyo wa mapato. Kuhusu mgawanyo wa mapato ya Muungano, mapendekezo yake bado yanafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, hoja ni nyingi na tutazijibu kwa maandishi. Naomba kwa heshima na taadhima niishie hapa nikiendelea kuomba kwamba Bunge lako Tukufu likubali maombi ambayo tumeweka mezani ili twende tukatekeleze kazi zilizoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.