Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina heshima ya pekee naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi ili nami niweze kuwasilisha ushauri wangu juu ya ufanisi wa shughuli za Serikali chini ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nitapenda niguse masuala makuu matatu nayo ni kilimo, ufugaji pamoja na miradi mikubwa ya uwekezaji kwenye sekta ya miundombinu hususan miradi ya ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ugomvi wa wakulima na wafugaji na hata migogoro kati ya wafugaji na Serikali yamekuwa yanakithiri siku hadi siku na moja kati ya vyanzo vingi vinavyopelekea migogoro hii ni pamoja na conflict of interest. Kwa upande wa wafugaji, wakati Serikali inaweka juhudi za makusudi katika kuhifadhi eco -system kwa kusisitiza wafugaji wafuge kwa idadi ndogo ambayo ni manageable, wafugaji nao wamekuwa kwa muda mrefu wakiongeza idadi ya mifugo ili kuweza ku-maximize profit bila ya kuwa na mchango wowote kwa Serikali kupitia Halmashauri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ya kawaida huko vijijini unaweza kukuta mfugaji mmoja anamiliki ng’ombe 2000, mbuzi 500 na hata kondoo 300 lakini mfugaji huyu unakuta hachangii chochote kwenye miundombinu ya uhitaji wa wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kosa kubwa tena nafikiri lisilopaswa kufumbiwa macho kwa mfugaji mwenye umiliki wa idadi tajwa ya wanyama wenye thamani zaidi ya shilingi bilioni moja kufikia kudai Halmashauri imjengee bwawa la kunyweshea wanyama maji ama majosho ya kuogeshea wanyama. Ni Mawazo yangu na ushauri wangu kwa Serikali kuwa majosho, mabwawa, nyumba za Madaktari wa wanyama na gharama ndogo ndogo zinazofanana na hizi basi zisitoke tena Serikali Kuu kupitia Halmashauri na badala yake wafugaji washiriki kikamilifu kabisa kwenye ujenzi wa miundombinu tajwa kwani kwa kufanya hivi nao watakuwa responsible kwa miundombinu hiyo in case kutakuwa na uharibifu ama kuzuia uharibifu. Vile vile kwa wafugaji hawa wenye idadi kubwa ya wanyama itafika mahali watakubali kwa wepesi kauli na miongozo ya Serikali juu ya kufuga kwa tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niunge mkono hoja na maelekezo ya Serikali na kwa kupitia speech za Mheshimiwa Rais juu ya utayari wa Serikali, katika kutoa vyakula vya msaada naamini kabisa hakuna sababu yoyote ya Serikali kutoa chakula cha msaada na badala yake Serikali ihimize wananchi wawajibike katika kutafuta chakula, kuhifadhi na kutumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu iweze kusaidia wananchi wake katika kushiriki kikamilifu kwenye kilimo, tumtoe Mkulima wa Taifa hili kwenye kilimo cha msimu mmoja kwenda kwenye kilimo cha misimu miwili kwa kufikisha pembejeo kwa wakati pamoja na kuvuna maji ya mvua ama kwa kuchimba visima au mabwawa ili kuwezesha kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu Bure bado ni sera ya msingi na ina umuhimu mahsusi katika ustawi wa Taifa hili, lakini si jambo baya Serikali ikafikiria kuja kupongeza baadhi ya items kwenye package nzima ya elimu bure. Ikiwa tutafaulu kumnyanyua mkulima na tukatengeneza ajira nafikiri elimu bure inaweza kufanyiwa tathmini kikamilifu ili kuona kama kuna sababu za msingi katika kuendelea na sera za elimu bure ama laa. Siyo mbaya Serikali ikaenda na sera ya elimu bure kwa miaka 10 ikiwa uchumi na pato la mmoja mmoja utaimarika basi nafikiri elimu bure yawezekana ikaja kuwa ni mzigo mkubwa kwa Serikali yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji nalo linahitaji kuwa redefined, tunahitaji kuwa na tafsiri mpya juu ya umuhimu na impact tarajiwa kupitia gawio la milioni 50 kwa kila kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naona kuna sababu za msingi kabisa kuchelewa kuitoa hiyo milioni 50 kama hatutakuwa na tathmini kamilifu juu ya umuhimu na matarajio ya Serikali juu ya gawio la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Ni ushauri wangu kwa Serikali yangu kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi iweze kueleza kwa ukamilifu hiyo shilingi milioni 50 ni kwa ajili ya nini, sera iseme matarajio ama mlengo wa Serikali juu ya gawio la shilingi milioni 50 kwa ukamilifu wake. Leo kuna watu wanafikiri hii fedha ni zawadi ya Serikali ama ujira wa uchaguzi kwa wananchi waliotuchagua, wengine wanafikiri hii fedha ni VICOBA na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya ujenzi wa barabara, utamaduni tulionao kwa muda mrefu katika miradi hii ya barabara ni kwamba Serikali kupitia vyanzo vyake mbalimbali, imekuwa ndio ikifanikisha miradi ya ujenzi wa miradi mikubwa ya barabara kupitia makandarasi nje na ndani ya nchi. Nikiwa sipingani kabisa na utaratibu huu wa Serikali, lakini nafikiri ingekuwa jambo jema kabisa kama Serikali ingefanya tathmini (cost and benefit analysis) na kuona kama tuna sababu mahsusi kwa miradi kama hii itegemee fedha za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kuwa mifumo ya udhibiti juu ya ubadhirifu wa mali ya Serikali bado haijaimarika na ndiyo maana Mheshimiwa Rais bado amekuwa akikabiliana na zoezi la kuwawajibisha Watendaji Wakuu wa Taasisi za Serikali kila iitwapo leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo yangu ni kuwa Serikali iangalie upya juu ya umuhimu wa Serikali kushiriki moja kwa moja kwenye miradi ya reli, bandari, barabara, viwanja vya ndege, madaraja, meli na umeme, ni mtazamo wangu kuwa miradi hii mikubwa mikubwa iachiwe taasisi binafsi (private sector), Serikali ibaki kukusanya kodi na mapato mengineyo. Fedha ya Serikali ibaki kwenye mahitaji muhimu mfano elimu, afya, ajira na hata ulinzi wa wananchi na mali zao. Kwa kufanya hivi Serikali itabaki na majukumu machache ya kisera na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja ya Serikali. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Serikali yetu ya Awamu ya Tano, Mungu Mbariki Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.