Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima hadi kufikia wakati huu tukijadili bajeti ya pili toka niingie katika Bunge lako Tukufu. Katika mjadala wa bajeti wa mwaka huu wa fedha tunaomalizia, 2016/2017, nilisema humu katika Bunge lako Tukufu kwa namna wataalam na hivyo Wizara hii mahsusi inayohusika na suala hili wanavyofanya suala hili muhimu kimazoea tu. Hii maana yake ni kuwa Wizara hii inaonesha kushindwa kutekeleza majukumu yake muhimu kama Waziri alivyoorodhesha katika hotuba yake hasa yale ya ukurasa 75 mpaka ukurasa wa 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inahusika au ndiyo yenye jukumu la uandaaji na usimamizi wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali? Mheshimiwa Waziri atueleze ni vipi jukumu hili muhimu sana kwa uhai na mustakabali wa nchi yetu wamelitekeleza? Wizara zote zilizowasilisha bajeti zao zimeonesha hali ya kusikitisha kwa namna mipango, matarajio na utekelezaji wa malengo na majukumu yao ulivyokuwa chini sana. Eneo la bajeti za maendeleo kwa Wizara zote ndiyo limeathirika zaidi kwa kutopelekewa fedha ambazo Bunge lako Tukufu liliidhinisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali imekuwa mbaya katika maeneo yanayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi kama vile afya, maji na huduma za usafiri, lakini pia katika eneo ambalo linabeba hadhi ya nchi yetu katika Jumuiya ya Kimataifa kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Nje. Hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Taarifa ya Kamati husika ya Bunge ameeleza hali za Balozi zetu nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inaandaaje bajeti zisizotekelezeka? Bajeti ya Serikali maana yake ni hizi bajeti za Wizara moja moja. Wimbo umekuwa ni ule ule miaka nenda miaka rudi. Kutenga fedha, kutopeleka fedha kunakohusika, kushindwa kutekeleza yale yaliyopangwa. Hebu tufike mwisho kwenye hili. Serikali ipeleke fedha zinazoidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisoma bajeti iliyopita na Waheshimiwa Wabunge wengine na hasa Kambi Rasmi ya Upinzani wanasema kwamba tuwe na vipaumbele vichache vinavyotekelezeka badala ya wataalam kuachia Wizara kuwa mipango isiyotekelezeka. Hivi wataalam hawajui au ni nini hasa kinachoendelea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uwezekano kwa sehemu nyingine za hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri kwamba imerudia tu yale ambayo imekuwa ikiripoti miaka yote (i.e. cut and paste). Mheshimiwa Waziri anasema katika hotuba yake, ukurasa wa 75 aya 125, kuwa katika mwaka 2017/2018 itafanya uchambuzi na tathmini ya miradi ya kuondoa umasikini ngazi ya Wilaya na Vijiji. Hivi ni kweli muda wote huu uchambuzi na tathmini haijafanyika/haikufanyika? Utekelezaji utakuwa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi waliopata fursa ya kuchangia kwa kuzungumza kuhusu masuala halisi kama vile deni la Taifa kutovumilika, viporo visivyomalizwa kama Tume ya Pamoja ya Fedha, mfano ya wastaafu, riba za mabenki kwa mikopo kwa wananchi, ahadi ya milioni 50 kila kijiji na mengine yote yakionesha kushindwa kutekeleza yanayopangwa au yanayoahidiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalize kwa kuiomba Wizara hii ibadilike, ijipime kwa namna inavyotekeleza majukumu yake. Hivi ni kweli inaridhika na utendaji huu? Mbona Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri wake ni watu makini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.