Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi niseme machache katika mada hii inayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia naomba niseme nakubaliana na pendekezo au hoja iliyoko mezani naiunga mkono, nina mambo machache tu ya kushauri lakini kabla ya hayo ya kushauri naomba nianze kwanza kutoa pongezi sana kwa hatua ambazo zinachukuliwa na Mheshimiwa Rais za kuongeza mapato ya Serikali na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze kipekee Mheshimiwa Rais kwa hatua ambazo amekuwa akizichukua kwenye suala zima la madini. Nadhani unafahamu na Bunge lako linafahamu kwamba mimi ndiye Mbunge wa Bulyanhulu. Mbunge ambae nimekuwa nikiishi na mgodi wa Bulyanhulu kwa miaka yote, nimekuwa nikizungumzia sana kuhusu Serikali kutokupata stahiki yake pamoja na wananchi, Wabunge wengi tumekuwa tukiungana kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishtuka sana juzi Jumatatu, pamoja na hatua nzuri sana iliyochukuliwa na Mheshimiwa Rais, zikatokea baadhi ya sauti hapa Bungeni zikitutisha kwamba eti tunaweza tukapata shida. Nawaomba sana Watanzania wenzangu, mimi kama Mbunge wa kule,
naomba muamini kwamba nchi inaibiwa. Tunaweza tukabishana kwenye kiwango cha wizi lakini suala la kwamba tunaibiwa halina ubishi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 2008 na 2009 niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge, wananchi wa kawaida kabisa vijijini walianza kuwa wanayavamia yale malori yanayosafirisha mchanga na kuiba ule mchanga, kwenye viroba vile vya mfuko wa saruji vya kilo 50 walikuwa wanaweza wakachenjua kwa kiteknolojia ya kienyeji na kupata dhahabu na mfuko mmoja walikuwa wanapata siyo chini ya shilingi milioni 50. Kufuatia hatua hiyo, wawekezaji walianza kusafirisha yale malori usiku kwa ulinzi mkali kuonesha kwamba kuna mali nyingi inayosafirishwa. Nilishtuka sana kusikia Watanzania wenzetu wakitia mashaka juhudi hizo za Rais, niwaombe sana na nikuombe Mwenyekiti na Bunge lako Tukufu watu wa namna hii inabidi pengine tuanze kujiuliza sana kuhusu Utanzania wao na uadilifu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani hata kidogo kwamba katika nchi ambayo ina uwekezaji mkubwa na rasilimali nyingi za namna hiyo ukifika leo Kakola, tena wao wenyewe wamekuwa wachochezi wa kwanza, wakifika pale wanasema hivi hapa kuna Mbunge? hakuna maji, hakuna hiki, hakuna hiki kwa sababu wanasema wanapata hasara. Wanapata hasara kwa sababu dhahabu iliyoko kwenye container la tani 20 wana-report kwamba kuna kilo nne wakati kuna kilo 28. Kwa hiyo kwa record za performance ya kilo nne lazima utasababisha hasara, lakini ukiweka kwa hesabu ya kilo 28 kwa container lile lazima una faida kubwa. Kwa kufanya hivyo maana yake wangeweza kuwa wanalipa corporate tax, wangeweza kufanya mambo mengi ambayo tunapaswa kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuungane kwenye hili jambo ni vita kama ambavyo Mheshimiwa Rais amesema na wananchi wa Msalala nilikuwa Kakola juzi nimeongea na wananchi wangu, wanamuunga mkono sana Rais na tunaomba Bunge lako limuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu kwamba katika mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Bomani yako mengi yaliyosemwa na machache yametekelezwa kwenye ripoti hiyo, nitaomba tu nikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba pengine ni vizuri report hiyo ikarejewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, moja ya vitu vilivyopendekezwa na Tume ya Bomani ni kwamba, katika dunia na nchi zote tulizozunguka mimi nikiwa Mjumbe, ilionekana kwamba hakuna sehemu ambayo wana utaratibu wa ku-share manufaa yanayotoka kwenye mgodi kama tunavyofanya Tanzania, kwenye nchi zingine wana revenue sharing plan, kwamba eneo ambalo kuna mgodi wanapata percent fulani kutokana na kodi na tozo mbalimbali ambazo zinatokea au zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba baadhi ya mapendekezo ambayo hayajatekelezwa na Serikali yarejewe na yatekelezwe, hata hili la kujenga smelter limo tulikwenda mpaka Sumitomo mimi mwenyewe nilikwenda na tukashauri kwamba Serikali ijenge smelter……

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru na naunga mkono hoja, nitazungumza tena kesho kwenye Wizara ya Nishati na Madini.