Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu hapa. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunipa afya njema ya kusimama hapa na kuchangia. Pili, niishukuru sana Serikali kwa kufanya kazi kwa jinsi hii ambayo angalau sasa kuna matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nianzie hapa alipoishia mzungumzaji aliyepita. Tunayo ahadi tumeitoa kule ya hizi milioni 50 (village empowerment), Ilani maana yake ni mkataba kati ya mtawala na mtawaliwa nasi tumeshaahidi kwamba wananchi tutawapatia mikopo ya milioni 50 na tumeandika. Kwa ushahidi zaidi naomba niitetee na kuiinua Ilani yetu ambayo tumeahidi katika uchaguzi. Ukiangalia ukurasa huu wa 112 tumeandika hapa na kwenye kifungu cha 57, kwamba tutapeleka milioni 50 kila kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Serikali ina changamoto nyingi, sikatai, lakini mwaka jana tumeahidi katika mpango ule wa bajeti kwamba tutapeleka bilioni 59, hatukuweza, mwaka umekwenda. Bilioni zile 59 tumeahidi tena nimeiona kwenye mpango wa bajeti ya sasa ya Serikali. Naomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, iko bilioni 60, ndugu yangu naamini anafanya kazi nzuri, nafurahi kwa sababu ametenga mwaka huu. Ukitenga basi peleka, nimesema kwa kifupi namna hii ili ajue kwamba wapiga kura wanatusubiri, baada ya kutoka Bungeni kwa vyovyote tunakwenda kwa wapiga kura, wanauliza swali la kwanza kwenye mkutano lini mnatuletea mkopo wa milioni 50 mlizotuahidi. Sasa Serikali naomba tufanye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri leo hii kwamba, katika kutekeleza ahadi ndiko unakomwona mwananchi wa kawaida anakubali mwelekeo mzuri wa Serikali yetu na tukitaka tuungwe mkono tutimize ahadi. Huu ni mwaka wa pili sasa tunaenda kumaliza na ni mwaka wa kazi, basi tuanze kwa kiwango fulani ili mwananchi aelewe kwamba, ni kweli Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeanza kutekeleza Ilani yake kwa kutoa milioni 50, angalau vijiji fulani vionekane, naamini wenzangu wamesema sana kuhusu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri kiuchumi. Uchumi wa nchi yoyote unahitaji maendeleo na maendeleo yanahitaji ushauri na ushauri unahitajika wa kitaalam. Ukiangalia, nimesoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, ukurasa wa 40, anaeleza jinsi Tume ya Mipango, nashauri kama inawezekana basi Tume hii iwe peke yake isiwe ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango ili inapopanga mipango yake iweze kushauri namna ya utekelezaji mzuri. Kwa sababu ikiwa pamoja inakuwa sio rahisi tena kushauri, naona kuna mkanganyiko hapo. Kama inawezekana iingie kwenye Ofisi ya Rais huko ili ikasaidie katika kutekeleza mpango wenyewe, maana wakati huu Tume ya Mipango inavyopanga na inapokuwa kwenye Wizara ya Mheshimiwa Dkt. Mpango, naona kuna mkanganyiko kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, katika uchumi wa nchi yoyote, sisi tuna benki, ni lazima Serikali iangalie benki zake. Kwa mfano, Benki tuliyonayo ya TIB Serikali isipowekeza kwenye benki yake yenyewe ambayo ina asilimia kubwa inayoendesha haiwezi kuendelea. Kwa nini nasema hivi; ukiangalia mitaji yoyote duniani Serikali ikiwekeza kwenye benki hii ni rahisi kwenda kwenye benki hii pia na kuona namna gani na hata ukienda kwenye soko la kimataifa huko ukiwa na asilimia 20 angalau umewekeza kwenye benki hiyo utaona pia mataifa mengine unaweza kufanya kazi nzuri katika biashara ya masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye research na wataalam wamsaidie Mheshimiwa Dkt. Mpango, najua ni mtaalam, nchi nyingi zilizoendelea zinalinda benki zao. Kama tatizo ni mtaji katika Benki ya TIB Serikali iwekeze pale. Kwa mfano, ukiangalia nchi ya China, China wana Exim na hawakubali pale mitaji yao ipotee, ukienda South Africa wana DBSA, hawakubali, ukienda Norway wana DNB, hawakubali, wana benki wanayoitegemea. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango aangalie hali hiyo, nimeona nishauri haraka kwa sababu dakika zangu sio nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwanza nimshukuru sana amenisaidia katika mambo mengi hasa kule Jimboni, lakini sasa tunao mkanganyiko wa sheria, Sheria ya Kodi au Zuio la Kodi (withholding tax). Sheria hii naamini katika Bunge lililopita walifanya zuio na kuondoa misamaha yote, huenda walikuwa na mapenzi mema lakini sasa mapenzi mema tumekuwa kama tumejinyonga wenyewe katika kuondoa misamaha yote na kuondoa uwezo wa Waziri kusamehe. Mheshimiwa Waziri alete ile sheria ili Bunge hili tubadilishe, tuone nafasi nzuri ya kufanya kazi kwa maslahi ya Taifa. Sitaki kutoa mwanya kwa mkwepa kodi yeyote lakini nimwombe alete sheria hiyo ili tuifanyie marekebisho kupitia Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao mfano hai, kama Mbunge yeyote tunaomba mara nyingi misaada na kama Serikali inavyoomba misaada, nilijaribu kuandika proposal katika Wilaya yangu kujengewa daraja na daraja hilo ni muhimu sana, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwanza ameliona, nashukuru amelishughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepewa na Serikali ya Norway na watu tu wanaosaidia wenye mapenzi mema milioni 125 ya mwanzo ya kujenga daraja sasa kutokana na sheria yetu, panatakiwa pawepo mtu atakayelipa zuio la kodi la asilimia 18. Sasa basi ukienda kwenye Halmashauri zetu ukitaka walipe pesa hizo hawana uwezo Halmashauri yenyewe tu haina uwezo wa kulipa hiyo pesa ya zuio la kodi kwa sababu haina chanzo kikubwa cha mapato….

MWENYEKITI: Mheshimiwa siyo zuio la kodi ni VAT

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani ni VAT asilimia 18. Kwa hiyo basi sheria hii isipoletwa hapa tukafanya mabadiliko ndipo tunapojinyonga wenyewe.

Kwa mfano, mfadhili amenisaidia ametupa milioni 152 za kujenga daraja, Serikali ya Halmashauri au Serikali ya Mitaa haina uwezo unapata wapi? Ukija kwa Waziri hawezi kusamehe kwa sababu sheria haimruhusu na ukisema yule mfadhili akalipe hiyo VAT anakataa anasema mimi nakusaidia wewe kukujengea daraja halafu wewe unataka mimi nilipe kodi yako, haiji hata kwa utaalam wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuone zile sheria ambazo zinaweza kuletwa hapa Bungeni, niombe kabisa Serikali ilete tufanye kazi kwa niaba ya wananchi, tuzibadilishe Sheria hizi kwa manufaa ya nchi yenyewe kwa sababu vinginevyo tutajifungia nati mpaka msumari wa mwisho. Hii maana yake ni nini basi? Tumeweka sheria hizi lakini tusijifunge moja kwa moja tukashindwa kufanya kazi kwa ajili ya sheria na kwa sababu Wabunge ndiyo tunatunga sheria, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, naomba tena sana alete ile sheria tufanye marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea kwa uchungu kwa sababu Serikali kwa bahati mbaya au nzuri haina namna ya kuleta pesa ya kujenga madaraja. Kuna kitu kinachoitwa ceiling (ukomo wa bajeti), ukomo wa bajeti ukishafika madaraja yetu kule katika maeneo ya vijijini hakuna namna, tunapopata wafadhili kama hawa, basi ni vizuri akakubali ili akatoa msamaha wa kodi katika sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimesimama ili kusudi kulisemea hili. Hata hivyo, niipongeze na kuishukuru Kamati yangu kwenye ukurasa wa 23 imeandika, hili siyo la kwangu kama Flatei, Mbunge wa Mbulu Vijijini hapana! Hili ni jambo la Kamati lipo humu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwaombe sheria itakapoletwa tuisaidie Serikali pia kuweka mwanya huu ambao utasaidia Waziri, kama ikishindikana basi Waziri Mkuu apewe hiyo authority ya kusamehe kama inakuwa shida huku chini au tujue nani anatoa au Rais apewe basi, kuliko kuondoa kabisa ule wigo na kutoa mwanya huu wa sheria ambayo kimsingi ikiwekwa itatusaidia...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.