Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa Tume mbalimbali zilizotajwa muda mfupi uliopita, lakini ripoti zao si Msahafu wala Biblia ambazo haziwezi kubadilishwa. Kwa ujasiri alioonesha kwa kipindi kifupi Mheshimiwa Rais, kwanza cha angalau kutekeleza maamuzi ya kuhamia Dodoma, tangu mwaka 1973, lakini uamuzi wa kuanza ujenzi wa reli ya kisasa, uamuzi wa kuwaondoa watumishi wenye vyeti feki, uamuzi wa kuondoa watumishi hewa, uamuzi wa kuondoa wanafunzi hewa, naamini ripoti ya Profesa Osoro na Profesa Mruma zitafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ripoti hiyo tumefuatilia wengi, kwa kuwa Mheshimiwa Spika, ulihudhuria na kwa kuwa Mheshimiwa Spika ulitoa kauli ya kulitaka Bunge lako kuwa tayari kupokea maelekezo na sheria mpya zitakazoletwa, nina imani mwaka huu mwarobaini wa ripoti mbalimbali umepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ile ripoti ya jana ya Profesa Osoro na ripoti ya Profesa Mruma zilikuwa na mambo mengi. Ukiacha mambo ya kisera, ukiacha mambo ya kisheria lakini yapo mambo ya kiutendaji yaliyosababisha hasara kubwa lazima yashughulikiwe. Kwa mfano, katika ripoti ilisema kiwango cha mrahaba kilichooneshwa kwenye hesabu za makampuni ya Bulyankulu na Pangea zilionesha dola za kimarekani milioni 111, wakati zilizopelekwa Serikalini kama mrahaba kati ya mwaka 1998 mpaka 2017 ni dola za kimarekani milioni 42, tofauti ya bilioni 68. Hili la kiutendaji lazima lishughulikiwe, siyo la kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ripoti imeonesha namna ambavyo wasafirishaji kupitia Wakala wa Meli walivyofanya utapeli wa kutisha, takwimu zinatofautiana baina ya hati za kusafirisha meli na hati za Wakala wa Meli, hili ni jambo la kuachwa? Haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo naunga mkono bajeti hii na naunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais. Naunga mkono bajeti hii kwa sababu, kwanza bajeti ina nia ya kumwondoa Mtanzania kwenda kwenye kipato

cha kati. Pili, bajeti imewagusa Wanawake ninaowawakilisha kitendo cha kufuta VAT kwenye chakula cha mifugo inatosha kabisa mimi kuunga bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitendo cha bajeti hii kuondoa VAT kwenye vipuli vya viwanda ambako Mkoa wangu unaongoza kwa viwanda kwa sasa nina kila sababu ya kuunga bajeti hii. Pia kitendo cha bajeti hii kutoa motor vehicle licence ya mwaka mzima na kupendekeza tozo ya Sh.40/= nikiwaona wanawake wengi wananunua maji kwa elfu moja, kwa elfu mbili, kwa elfu tano dumu, naamini wana uwezo wa kuhimili tozo hii ya Sh.40/= endapo sehemu ya tozo hii itahamishwa kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napongeza namna gani Mheshimiwa Rais wetu anavyosimamia uboreshaji wa mapato. Amesimamia maboresho ya mtambo wa TTMS wa kurekodi dakika zote za simu, tunaona mapato ya simu yameongezeka. Amesimamia uanzishaji wa mfumo wa kukusanya mapato kielektroniki, amesimamia hata kutembelea data center na ameelekeza makampuni yote ya simu yaende kujisajali Dar es Salaam Stock Exchange.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, naomba nipendekeze, Waswahili wanasema ukiumwa na nyoka, ukiona nyasi unastuka. Kwa kuwa, tumeona makampuni mengi ya nje hata taarifa zilizotolewa zinaonesha makampuni mengi ya nje yanatutapeli kupitia transfer pricing, nishauri kwenye soko la Dar es Salaam Stock Exchange, makampuni ya simu, Serikali ilete mapendekezo ya kutafsiri upya maana listed shares ili Serikali yetu ipate fursa ya kuangalia miamala ya makampuni haya hata ile ambayo shares zake nyingi zinatawaliwa na wageni.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Kampuni ikiwa registered Dar es Salaam Stock Exchange ikiuza share zake kwa asilimia 25 ili zile share zote Serikali iwe na nguvu lazima tubadilishe maana halisi ya listed shares ili iende kwenye zile share za makampuni. (Makofi)

Mhehimiwa Spika, sambamba na hilo, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa ujenzi wa standard gauge kama nilivyosema. Hata hivyo, nashauri suala zima la kufuta VAT kwenye vipuri liende sio tu kwa viwanda vilivyotajwa vya mafuta peke yake, lakini viguse viwanda vya usindikaji wa korosho, Mkoa wa Pwani tunalima korosho, viguse pia viwanda vya kuzalisha mafuta ghafi hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, lakini nimalizie kama dakika zangu zipo kwenye suala zima la nia ya Serikali ya kufungua Escrow Account kwa ajili ya makampuni yanayotumia sukari ya viwanda. Niombe Serikali ilitazame upya suala hili, makampuni yale yenye viwanda vya kutengeneza vinywaji baridi kwa kweli wamezidiwa, pesa zao nyingi hazijarudishwa kiasi cha bilioni 20, imesababisha viwanda hivi kupunguza wafanyakazi, inasababisha viwanda hivi kupata tabu katika uendeshaji wa shughuli zao. Naomba Serikali itazame upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Serikali ione namna ambavyo itatusaidia wakazi wa Pwani viwanda hivi ambavyo vimeanzishwa vingi na namna ya kutusaidia jinsi ya kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda hivi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu bajeti hii Mheshimiwa Waziri amesema Mama Lishe watatambuliwa sasa hivi, wauza mboga ndogondogo watatambuliwa. Imani yangu utambulisho huu utakwenda sambamba na huduma za kifedha, utakwenda sambamba na uwezeshaji na naamini kupitia Baraza la Uwezeshaji la Taifa, wanawake wengi watafikiwa, bodaboda wengi watafikiwa kwa kuwa watakuwa na utambulisho rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa spika, mwisho, ni kuhusu Serikali zetu za Mitaa. Niombe sana kwa Mheshimiwa Waziri, nia ni njema ya kufanya mapato yote yakusanywe na Serikali Kuu, lakini niombe urejeshwaji wa mapato hayo uende kwa wakati. Halmashauri zetu nyingi zitashindwa kujiendesha endapo makusanyo yatakayokusanywa kupitia property tax, kupitia

vyanzo vingine vya mabango ambavyo vimekwenda Serikali Kuu kwa nia njema ya kuongeza hayo mapato yatakuwa hayarejeshwi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kushukuru kwamba kwa upunguzaji wa produce cess kwa wakulima wetu, kwa kweli ni suala ambalo ni la msingi. Kila siku tulikuwa tunalisemea lakini namna ambavyo Serikali mmelishughulikia. Mheshimiwa Waziri nakupongeza, bajeti hii imesikiliza maoni ya Kamati, bajeti hii inamgusa mwananchi wa kawaida, bajeti hii imemgusa mkulima na bajeti hii imemgusa mwanamama wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.