Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Saada Salum Mkuya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi nashukuru kupata nafasi hii kuchangia bajeti yetu ya Serikali mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, kwanza nami nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha. Naamini kufikia hapa kwa uzoefu haikuwa kazi rahisi, tumefanya kazi kubwa na tumeleta bajeti ambayo inatafsiri dhana nzima ya Tanzania ya Viwanda. Mengi sana yamo na yanatafsiri hilo, kwa hivyo, ni lazima tukupongezeni kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda niende katika maeneo specific, kwanza kuhusiana na ongezeko la Sh.40/= katika mafuta kwa ajili ya ku-compensate ile Road License fee


ambayo imefutwa iliyokuwa ikilipwa kila mwaka. Kiutawala nadhani hili limekaa vizuri zaidi na naamini kwamba Serikali itapata fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kutekeleza bajeti yake.

Mheshimiwa Spika, binafsi naomba badala ya kuwa Sh.40/= tungeongeza Sh.10/= ziwe Sh.50/= kwa sababu tutapata ongezeko la Sh.6,950,000,000/=, hizi Sh.10/= specific zikaingie katika Mfuko wa Maji kama vile ambavyo tulikuwa tumeshauri kabla. Kwa sababu hizi Sh.40/= zinakwenda kutekeleza bajeti kwa ujumla wake, naomba tuongeze Sh.10/= tu ili ziwe Sh.50/= ziende zikaingie katika Mfuko wa Maji kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji hususan katika maeneo ya vijijini ambapo ndipo kuna shida kubwa sana ya maji ukilinganisha na mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pengine wenzangu wanaweza wakauliza sasa tunaenda kuwapa shida sana wananchi ambapo hawatumii magari, lakini maendeleo ya nchi hayahitaji mtu yupo wapi, maendeleo ya nchi hii yanamhitaji mtu aliyeko kijijini na yule ambaye yuko mjini. Huko vijijini ambapo tunasema hawa watu tumewabebesha mzigo kutokana na kuongeza Sh.40/= ya mafuta ya taa lakini wao wana shida kubwa ya maji, wanahitaji sana barabara na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, hili ongezeko ambalo nashauri Mheshimiwa Waziri lifikirie liende specific kwa ajili ya kuondosha shida ya maji katika maeneo hasa ya vijijini. Nadhani siku ya bajeti ya maji karibu asilimia 60 ya Wabunge wote walisimama na wakapata nafasi ya kuongea kwa sababu ya dhiki ya maji ambayo ipo katika maeneo yao. Kwa hiyo, naomba hili tulifikirie ili twende tukatekeleze bajeti kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile na mimi nisiwe mkosefu wa fadhila sana, niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua za kiutendaji anazozichukua kuona kwamba resources za nchi zinafaidisha wananchi wenyewe. Ni kweli fedha nyingi zimepotea lakini it is high time now kuweza kusimamia zaidi hizi sekta za kiuchumi. Inawezekana sana kama tungekuwa tumesimamia vizuri basi tusingekuwa hapa tunadonoa Sh.10/=, Sh.20/= kwenda kupeleka katika Mifuko ya Maji.

Mheshimiwa Spika, naamini kama tungekuwa tunasimamia vizuri, kwa utajiri ambao Tanzania upo tungeweza kutekeleza bajeti yetu kwa kutegemea kiasi kidogo sana cha misaada ama mikopo ya kibishara kutoka nje. Basi ndiyo hivyo imetokea, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amejitoa kuhakikisha kwamba tunasimamia vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili bajeti iwe bajeti ambayo inaleta ufanisi, ni lazima bajeti hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iweze vilevile kuona ina-support vipi bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwenye hili Mheshimiwa Waziri nina mambo mengi kidogo. Kwanza ni general budget support (misaada ya kibajeti). Nimeona katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri kwamba misaada ya kibajeti tunaotea kupata around bilioni 311. Vilevile kuna maoteo ambayo tunatarajia katika bajeti ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, wakati huo huo bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesomwa jana ambayo inaelekeza mwelekeo wa kimaendeleo katika mwaka 2017/2018 lakini bajeti hii ambayo inakamilika ina kasoro ya fedha za general budget support ambazo zimeandikwa kwamba tutazipata. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hizi fedha kwanza angalau tujue ni kiasi gani mpaka sasa hivi zimepatikana ili kuona kiasi gani kinakwenda Zanzibar kutekeleza miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haitakuwa busara sana kama bajeti yetu kwa upande wa Jamhuri ya Muungano inatekelezeka lakini kuna upungufu mkubwa katika kutekeleza bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tunaomba tujue ni kiasi gani zimepatikana na hicho kilichopatikana ifanyike haraka, kipelekwe Zanzibar kiweze kutekeleza miradi ya maendeleo. Hii vilevile ni pamoja na hizo fedha za mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, mwaka jana tulibadilisha Sheria yetu ya VAT, kuna bidhaa ambazo zilikuwa zimezalishwa hapa na zimekwenda kutumika Zanzibar. Kuna fedha za refunds zinakaribia shilingi bilioni 21, bado hazijapelekwa Zanzibar na hili ni tatizo kubwa sana. Refunds za VAT pamoja Excise Duty zinachelewa kupelekwa Zanzibar, sasa kule tunachelewesha kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri pamoja na usimamizi mzuri wa kibajeti tunaomba asimamie fedha za VAT na Excise Duty ambazo ni refund zipelekwe Zanzibar kwa wakati ili tuweze kutekeleza bajeti vilevile kwa upande ule ambao ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nataka kuchukua fursa hii kupongeza Shirika letu la Bima la Taifa, kwa mara ya kwanza limetoa gawio kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania shilingi bilioni 1.7. Ni kwa mara ya kwanza limetengeneza faida na limetoa gawio. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri katika eneo hili vilevile tulishauri kwamba taasisi za Serikali pamoja na vyombo vyake viwe vinaweka bima kupitia Shirika letu, hii itaongeza faida katika operation za Shirika letu la Taifa na kwa maana hiyo sasa hilo gawio litazidi zaidi. Kwa hiyo, tunaomba hilo lizingatiwe taasisi zetu za Serikali ziwe zinaweka Bima kupitia Shirika letu la Taifa ili tuweze kupata fedha zaidi kutekeleza bajeti yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili katika hilo hilo kuna ombi la kuanzisha Bima hii ya Kiislamu (Takaful) limekaa kwa Mheshimiwa Waziri muda mrefu sana bila ya kupatiwa majibu. Hizi ni products ambazo zinaendana na wakati tu. Kama tumeruhusu Benki zi- operate kwa principle za Kiislamu, kwa nini tunazuia bima zisi-operate katika principle za Kiislamu? Hili linawezekana lakini limekaa sana muda mrefu kwake bila kupatiwa majibu.

Mheshimiwa Spika, tunaomba sasa litekelezwe ili tuone kwamba wale ambao wana imani za Kiislamu na wao wanapata products ambazo zinaendana na imani zao. Ni biashara na ni products ambazo zinakuwa kutokana na mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusiana na Benki yetu ya FBME, Mheshimiwa Waziri amezungumza vizuri kwamba hii benki sasa hivi imeshanyang’anywa leseni hai- operate tena. Kuna mambo ya kadha wa kadha yametokea lakini wananchi wameweka fedha zao FBME na katika matoleo ya mwanzo tumeambiwa kwamba hii benki itafanyiwa auditing two weeks za mwanzo na baadaye wananchi wataambiwa benki gani watakwenda kuchukua fedha zao. Hivi tunavyokwenda nadhani tunaingia mwezi wa pili, hakuna taarifa yoyote kuhusiana na fedha au zile amana za wananchi ambazo wanataka wao wenyewe kuzitumia.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wetu wa Zanzibar Tawi la FBME linafanya vizuri zaidi kuliko matawi mingine ya FBME Tanzania. Wananchi wengi wa Zanzibar wameweka fedha zao kwa ajili ya kwenda kutekeleza Ibada ya Hijja baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kama leo hatujui wapi fedha zetu tutazipata mnakwaza watu ambao wanataka kwenda kutekeleza hiyo ibada.

Mheshimiwa Spika, tunaomba tufanyiwe utaratibu kujua kwamba fedha hizi zinapatikana wapi, wananchi waende kuchukua fedha zao ili waweze kufanya pamoja na mambo mengine utekelezaji wa ibada hii muhimu ya Kiislamu baada ya kumaliza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Namuamini sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, najua hili utalisimamia.

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nipate majibu…

MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naomba kupata majibu ya masuala hayo niliyozungumzia. Ahsante.