Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kusema hivi, CCM ni ileile, Mawaziri ni walewale, Wabunge ni walewale, Mheshimiwa Magufuli ni yuleyule na wananchi ni walewale. Sasa nasema hivi, wananchi wamejipanga vizuri kwa ajili ya kumuunga mkono Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Kwa maana hiyo, nimeimba kwa kusema, ningesema CCM ni ileile, kwa hiyo, tumejipanga kuhakikisha 2020 hakitoki kitu. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kuunga mkono bajeti hii na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Dokta Mpango na Naibu wake pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa bajeti yao nzuri. Naomba niunge mkono mapendekezo yote ya Kamati ya Bajeti ya tozo ya Sh.40/=. Mapendekezo yao ni mazuri, nayaunga mkono kwa asilimia 100 kwa sababu yatakwenda kumwondolea mwanamke adha ya ndoo kichwani. Kwa hiyo, bajeti hii ni nzuri na mapendekezo ya Kamati ni mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa tozo hiyo ya Sh.40 pesa zile ziweze kupelekwa kwa ajili ya maji vijijini. Wananchi wanapata shida sana ya maji kule vijijini, wanawake hawawezi kufanya shughuli za maendeleo kwa sababu ya shida ya maji, lakini pesa hizo zikigawanywa zikapelekwa kule kwenye maji kwa kweli…

TAARIFA....

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa vile analitambua hilo na mimi nilisema Mheshimiwa Magufuli ni yuleyule kwa sababu hata ule wimbo wa CCM unasema Magufuli ni yuleyule. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naendelea, wananifahamu kwa sababu niliwahi kuwaambia Wapinzani Kigoma hawatarudi na tuliwafuta wote wakabakia wawili. Kwa hiyo, wale waliosalia nafikiri wanajua kazi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kutenga asilimia 69 kwa ajili ya zahanati na vituo vya afya ili pesa hizo ziweze kwenda kumalizia miradi ile ya vile vituo vya afya na zahanati ambavyo wananchi kwa nguvu zao walianza kujenga. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali kwa kutenga pesa hizo shilingi bilioni 69 kwa ajili ya kwenda kusaidia miradi hiyo. Pesa hizo zikipelekwa kule wanawake watanufaika kwa sababu hawatapata shida sana kwenda kuvifuata vituo vya afya au zahanati maeneo ya mbali kwenda kutibiwa. Kwa maana hiyo, vifo vya wanawake na watoto vitapungua kwa sababu huduma zitakwenda kupatikana karibu. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali yangu inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka jana Mkoa wa Kigoma ulikuwa kati ya mikoa maskini na ilikuwa ni kwa sababu ya miundombinu ambayo haikuwa mizuri lakini naishukuru sana Serikali kwa sababu imeendelea kuutupia macho Mkoa wa Kigoma. Naomba pesa zilizotengwa kwa ajili ya barabara ya kutoka Nyakanazi kwenda Kanyonza, kutoka Kidahwe kwenda Kasulu, zipelekwe kwa ajili ya kwenda kumalizia barabara ile na ikibidi barabara ile yote iweze kumalizika kwa sababu ya kuunganishwa na Mikoa mingine ya Kagera na Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mkoa wa Kigoma ni wachapakazi sana, kwa hiyo miundombinu ikiwa mizuri kwa sababu ni wakulima wataweza kusafirisha vyakula vyao kwenda sokoni na tutawahamasisha wawekezaji waje kujenga viwanda ili wananchi wanapokuwa wanalima mazao yao waweze kupeleka kwenye viwanda ambavyo vitakuwa viko jirani na maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, sisi tumejaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji, tuna Mto Malagarasi, Mto Lwiche na Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iweze kumalizia miundombinu ile ili wawekezaji waweze kuja kufanya kilimo cha umwagiliaji tuweze kuwa na viwanda vya sukari na kukamua mawese. Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuutupia macho Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kuweka miundombinu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwa kuendelea kuuona Mkoa wa Kigoma, ndege zile za bombardier zinaenda Kigoma. Naomba sasa, reli ile inayojengwa ya standard gauge ianzie Dar es Salaam mpaka Kigoma, nyote mnajua reli ile ilikuwa inaanzia Kigoma kwenda Dar es Salaam, Dar es Salaam kwenda Kigoma, ndiyo maana inaitwa mwisho wa reli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba inapokuwa inafanywa mipango kuelekea Mwanza, chondechonde, tunaomba reli ile ije Kigoma. Kigoma mnaifahamu, tumepakana na DRC na Burundi, kwa hiyo, mkituwekea reli hiyo ya standard gauge hatutapata shida sana, tutaweza kuendelea kufanya biashara kwa kushirikiana na nchi hizo jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali na naipongeza kwa mipango ya umeme. Kwa hiyo, naomba pesa zipelekwe kwa ajili ya umeme wa REA awamu ya tatu ili pesa zikipatikana ziweze kuja Kigoma kwa ajili ya kuweka umeme katika vijiji vyetu vinavyozunguka miji yetu katika Miji ya Kibondo, Kakonko, Kasulu, Uvinza, Buhigwe na maeneo mengine yote. Kwa hiyo, naomba REA iongezewe pesa kwa sababu baadhi ya vijiji havijaweza kupata umeme, pesa zikipatikana umeme utaweza kupatikana katika vijiji vyote vinavyozunguka miji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo malalamiko ya mawakala ambao wamefanya kazi ya kusambaza mbolea kwa wananchi. Nafahamu wapo mawakala waliofanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, naomba Serikali ijipange, wale ambao ni waaminifu walipwe pesa yao. Ni muda mrefu sasa wamesubiri, nyumba zao zimeuzwa, wengine wamekufa kwa sababu walikopa kwenye mabenki lakini wameshindwa kurejesha kwa sababu hawajapata pesa. Kwa hiyo, naomba ufanyike utaratibu wa kuweza kuwalipa ili waweze kurejesha madeni yao benki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, SACCOs na SACAs, tumekuwa tukiwahamasisha wananchi kuanzisha SACCOs na SACAs lakini upo upungufu mkubwa wa watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Wafanyakazi hao wa ushirika hawatoshi na vile vikundi vilivyoanzishwa vijijini kwa maana ya SACCOs na SACAs wanahitaji elimu, hawajui jinsi ya kukopa, hawajui jinsi ya kurejesha na hawajui ili wakopesheke ni lazima wakaguliwe na vyombo vinavyofanya kazi ya ukaguzi wa pesa ili kubaini kama hawa watu tukiwapa pesa wataweza kuirejesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iliangalie eneo hili, watumishi wa ushirika hawapo kule vijijini na hata hao wachache waliopo hawana vitendea kazi. Kwa hiyo, tunaomba hawa watumishi wa ushirika, kwanza waajiriwe ili wawe wengi, lakini wapewe vitendea kazi ili waweze kwenda vijijini kuzifundisha SACCOs na SACAs zetu ziweze kuelewa vizuri, hatimaye tutakapopata pesa hata hizi asilimia 10 kwa maana ya wanawake na vijana zinapopelekwa kwenye vikundi wajue ni jinsi gani watatumia kwa sababu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.