Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sasa ni sauti kutoka Pemba ya kiyakhe inataka kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-wataalah kutujalia uzima na afya njema. Leo ni siku ya nane kwenye Kumi la Maghufira. Baada ya hapo, naunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani yaliyokuwa mazuri sana. Nawapongeza Viongozi wetu Wakuu wa UKAWA, Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mheshimiwa Riziki pamoja na Mheshimiwa Mbatia. Tunaenda kwenye bajeti hii ambayo ni kiini macho, kizungumkuti na bajeti ya kusadikika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni bajeti ambayo haitarajii kuondoa maumivu waliyonayo Watanzania kwa sababu zifuatazo: la kwanza, ikiwa tumefikia wakati tuna deni la Taifa shilingi trilioni 50.8 na tumejipangia sisi wenyewe kwenda kulipa kwa mwaka shilingi trilioni 9.6, ina maana kwamba tunaenda kulipa shilingi bilioni 788 kwa kila mwezi. Sambamba na hilo, kuna mishahara shilingi bilioni 600. Kwa hiyo, jumla itakuwa kwa kila mwezi tunatakiwa tulipe shilingi trilioni 1.3 na ushee, lakini makusanyo unaambiwa ni shilingi trilioni 1.4. Ina maana ni bajeti ya kusadikika, bajeti ya kufikirika, ni bajeti ya kwenda kulipa madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nashangaa na hilo. Watu wanapiga makofi, kumbe tunaenda kulipa madeni tu sisi. Ninachohisi ni kwamba wakati huu mzunguko wa fedha haupo, umaskini unaongezeka, mfumuko wa bei uko juu na juzi tarehe 8 saa 4.10 niliuliza swali hapa Bungeni kwamba katika hiyo APRM Serikali mnajitathmini kiasi gani katika hali hii ya uchumi?

Mheshimiwa Spika, majibu ya Serikali ninayo hapa. Walisema kwamba; changamoto waliyonayo ni ukuaji wa uchumi usiowiana na kupungua kwa umaskini. Uchumi unakua, umaskini haupungui. Leo Mheshimiwa Waziri wa Mipango anakuja anasema aah, umaskini unapungua. Siku hiyo hiyo moja, Serikali hiyo hiyo moja! Tofauti ni dakika tu. Tutakwenda kweli? Nashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapokwenda kuongeza shilingi 40/= za mafuta huko vijijini, wakati wanaotumia, wanaokoboa na kusaga mashine zao, wanaangalia kinachoongezeka kwa siku vijijini. Wanatumia generator, wananunua mafuta ya dizeli; ina maana umewaongezea mzigo wale watumiaji maskini ambao ni wakulima. Halafu unasema unapambana na umaskini. Kuna kitu hapo? Hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi 40/= iliyoongezwa huko vijijini ni taabu kweli. Wakoboaji na wanaosaga mashine zile pale huko basi ni shida. Sasa Mheshimiwa unaposema kwamba unataka kuwakomboa maskini, ni kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashangaa. Wala wananchi wa Tanzania hawahitaji maneno yenu ya kitaalam, sijui urari wa kibiashara, deni himilivu eeh, mnasema kwamba maoteo hayajakamilika, amana za benki hazijaiva bado mbichi, madeni chechefu. Hawahitaji hayo madeni chechefu! Maoteo ya fedha yameota mbawa; amana za benki hazijaiva. Zikiwa mbichi? Ndiyo nikasema kama Bunge hili lingekuwa live tukawaambia wananchi haya madeni chechefu, maoteo hajakamilika, amana za benki bado mbichi, hazijaiva vizuri, wananchi wakatusikia, twende kwenye uchaguzi mtazame kama hamtatumia nguvu ya dola nyie. Tuseme sisi na nyie mseme yenu mtazame. Hamtaki kuweka Bunge Live kuwaambia ukweli wananchi. Ni hilo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba niendelee. Kinachonisikitisha, alipotuachia Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, mwishoni tulikuwa tuna deni la Taifa shilingi trilioni 39.1. Ndani ya mwaka mmoja na nusu tumeongeza shilingi trilioni 11. Tuliondoka na shilingi trilioni 39 point, leo tuna shilingi trilioni 50.8. Mwendo kasi. Hapa kazi kweli mwaka huu za kulipa madeni. Nashangaa. Hii haihitaji kufikiri sana na utaalam, madeni chechefu kweli mwaka huu, tutafika kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi milioni 50 vijijini ni ndoto. Hamna uwezo wa kutekeleza, imekuwa ni hadithi za hapa na pale, paukwa pakawa. Mimi natoka, shauri yenu, mtajua wenyewe.

Mheshimiwa Spika, deni chechefu ni deni baya lililokuwa huna; maana huwezi kulilipa kwa ufupi, ndiyo deni chechefu. Madeni yao chechefu, maana huna hakika ya kuyalipa. Madeni chechefu eeh, maoteo ya fedha, amana za benki hazijaiva bado mbichi, urari wa biashara. Wananchi wanataka nini bwana? Wapeni fedha wananchi sogezeni huko! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna bajeti ya kupandisha mishahara ya wafanyakazi, hakuna. Ndogo sana! Pension ya wazee, watu ambao wametulea, hakuna pension ya wazee wasiojiweza. Hawana bajeti hawa. Wanasema aah, tunapunguza umaskini, deni chechefu. Haya. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tumeambiwa ukanda ambao unataka uzalishe uvuvi katika Bahari Kuu, amesema Mheshimiwa Mbunge wa kule juu, mrefu mrefu kama mimi kidogo hivi; amesema kwamba uvuvi katika Bahari Kuu bado haujapewa nafasi yake. Ina maana ukiambiwa je, Serikali ina bajeti ya kununua meli za kisasa za uvuvi ambazo tutaweza kuvuna mazao yetu kwenye Bahari Kuu? Serikali hamna bajeti, hakuna kitu. Hawana! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi siku zote tule samaki kutoka China. Nunueni meli ya kisasa, meli kubwa za uvuvi ziende katika Bahari Kuu tuvue samaki. Samaki wanakufa tu huko! Eeh, hawana kitu! Hee, shida mwaka huu. Nashangaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukija kwenye afya, Watanzania ambao afya zao wanataka ziende vizuri, bajeti ya Afya kwa Azimio la Abuja 15% ya shilingi trilioni 32 waulize, wameweka? Hakuna. La kwanza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, ukiangalia katika magonjwa makubwa sasa ambayo yanasumbua Tanzania, ni suala la TB. TB hivi sasa kwa mujibu wa wataalam ambao wametupa semina juzi, wagonjwa wa TB kwa kila siku wanakufa 150. Ni mabasi maana yake yanapotea, lakini ukiwaambia je, ni kiasi gani mmeweka fedha za kupambana na TB, hakuna.

Mheshimiwa Spika, kuna mkakati gani kwenye mikutano ya hadhara, mna mkakati gani katika maeneo mengine ya migodi kukomesha mambo haya na kupunguza mambo ya TB? Hakuna. Aah, urari wa biashara huo! (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wastaafu. Aah, mwaka huu! Ukiwaambia wastaafu, wanakwambia aah, sisi tumetoka tangu mwaka 2016, kipindi gani, tumeweka wastaafu wa chini wale Sh.100,000/=. Hivi ni kweli inatosha? Itapunguza kweli umaskini!

Mheshimiwa Spika, hii Serikali, nikasema kwamba kwa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, Ripoti ya CAG, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alisema hapa kwamba kuna wizi wa fedha karibu shilingi bilioni 92. Hii ni mkataba baina ya Shirika la Ndege la ATCL ilipoingia mkataba na South African Airways wakati wamekodi ndege kutoka China, Air Bus. Ndege hizi kwa bahati mbaya sana zimetusababishia hasara ambayo ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, hapa imekuja wakati ndege hizi zililetwa hapa zikafanya kazi kwa muda wa miezi sita tena kwa kubahatisha. Ndege zikaondolewa zikapelekwa Ufaransa, mkazipaka rangi. Baada ya kupaka rangi, mkaziondoa mkazipeleka Guinea, mkazipaka rangi, baadaye hakuna aliyekamatwa. Deni chechefu hilo. Bado tu umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wapo, majibu ya Serikali yanasema kwamba TAKUKURU bado ipo kwenye mkakati wa kuchunguza, mnachunguza nini? Kumbe mnalindana? Wengine wakamatwe watumbuliwe, wengine wabinywe, wengine wapekuliwe. Hilo hamlijui Serikali au bado tu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashangaa! Sauti ya chombezo toka Pemba hiyo! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifikiria kwamba Serikali hii itakuwa makini kuangalia namna gani ya kuwakomboa Watanzania katika hali ya umaskini? Ni namna gani ambapo mtapambana na umaskini? Namna gani mtadhibiti mfumuko wa bei? Namna gani ambavyo mtaangalia kwamba umaskini uliopo hivi sasa unachangiwa na mambo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanasema katika ripoti yao Ukanda wa Pwani wana viwanda vidogo vidogo, sekta binafsi 82 ambavyo watajenga, lakini Serikali inasema itatoa vibali, watatoa leseni, sijui watatoa na ardhi. Ukiuliza huko Mkoa wa Pwani kwenyewe ni vichekesho.

Mheshimiwa Spika, sasa ninachoona ni kwamba, kwa hali tunayokwenda nayo hivi sasa ni kwamba, kuna tatizo kubwa sana, Serikali haijajipanga vizuri. Ukija kwenye mambo ya haya makinikia yanaitwa, haya sawa, kwani muda wote upungufu huu wa mabilioni ya fedha, matrilioni, Serikali iliyokuwepo; Serikali gani? Ya chama gani? Si Chama cha Mapinduzi! Serikali ipi? Mawaziri si ndio hao hao! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huo upotevu wa madini hayo yanayosemwa, kama kuna watu wamefanya ubadhirifu mkubwa, sawa nakubali, lakini tulipokuwa tukisema hapa Bungeni leteni mikataba, mlikuwa hamtaki kuleta mikataba. Ndiyo urari wa biashara huo. Haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja. Bajeti ni mbaya, inaenda kuumiza Watanzania. Nashukuru sana.