Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nachukua fursa hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunisaidia na kuweza kuchangia katika bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kwanza ambacho napenda kuanza nacho ni kitu ambacho kimeongelewa na Wabunge na Watanzania wengi, ni suala la makinikia pamoja na ripoti ambazo zimetokana na Tume ambazo ziliundwa na Mheshimiwa Rais. Siku zilizopita tumepata pia kusikia kwamba President wa Barrick amekuja kwa ajili ya kuweza kufanya mazungumzo, ingawa kauli tunazozipata, kauli iliyotoka mdomoni mwa Rais na kauli iliyotoka katika Kampuni yenyewe ya Barrick ni maneno ambayo kidogo yanakinzana ambapo tunashindwa kuelewa ni kitu gani hasa ambacho kimeongelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu ambacho napenda tujiulize, ni kwamba tunaenda kufanya negotiations kwa kitu gani, tunaenda kufanya mazungumzo kwa ajili ya nini, tunaenda kufanya mazungumzo kwa ajili ya makinikia ama tunakwenda kufanya mazungumzo ili kuweza kuangalia vitu vyote ambavyo tumepoteza kutokana na mikataba hii? Kama tunakwenda kufanya mazungumzo ili kuangalia ni jinsi gani ambavyo Tanzania tumeweza kupoteza kutokana na sisi wenyewe kama Serikali, sisi wenyewe kama nchi, sisi wenyewe kama viongozi ambao wamekuwepo kwa kuingia mikataba mibaya ambayo imetuletea wizi namna hii, migodi yote iweze kuhusishwa katika mazungumzo haya. Kama tunataka tuangalie suala zima la mikataba, kama tunataka kuangalia suala zima la sheria, ni lazima tuangalie kwa migodi yote, hatuwezi kwenda kwenye mazungumzo na mtu mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye hili suala zima la makinikia, napenda kutoa tahadhari kidogo, kumekuwa na taarifa ambazo zinakinzana, lakini ningetaka kuiamini Serikali kwa Tume na ripoti ambayo imeitoa. Naomba pia tuangalie na tuweze ku-verify information ambazo tumezitoa na Serikali iende kwenye hatua ya mbele zaidi kufanya uhakiki ili kama tunaenda kwenye negotiations, kama tunaenda kwenye mazungumzo twende kama watu wasomi, twende na timu imara, twende na watu ambao wanaweza kusimamia kitu ambacho kipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kutokana na muhtasari wa ripoti iliyotolewa inazungumzia kwamba makinikia haya yameanza kusafirishwa toka mwaka 1998 lakini ukisoma katika ripoti ya Lawrence Masha na ripoti ya Jaji Bomani inaonesha kwamba production ya mgodi huu imeanza mwaka 2001. Kwa hiyo, hebu tukaangalie mambo yetu vizuri, twende tusidharaulike, kama tunapeleka Maprofesa kweli ionekane tuna information ambazo ni sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala hili halijatuletea athari au kuibiwa tu kama tunavyosema au Serikali kupoteza mapato lakini suala hili la migodi na mikataba ambayo Serikali imeingia imeleta mpaka wananchi wetu kupoteza maisha. Wananchi wetu wamepoteza maisha huku migodi hii ikilindwa na askari polisi wetu. Vyombo vyetu vya usalama vimepiga risasi watoto wetu wa Kitanzania kulinda uwekezaji wa Wazungu. Ndiyo maana tumepata vifo vya wananchi wengi vilivyotokea kule Tarime lakini na athari kubwa sana ambazo ziko katika Mkoa wangu wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya bado hayajaisha, ni miaka imepita tangu wananchi wa Tarime wamekufa lakini bado athari na shida zinaendelea. Ukisoma katika ripoti ya Jaji Bomani inataja maeneo mawili ndani ya Geita, eneo la Nyakabale ambalo wananchi wanaishi ndani ya leseni ya mgodi. Wananchi ambao barabara yao ya mwanzo imefungwa, hawawezi kupita barabara yao ya mwanzo kwa sababu ya mgodi. Wananchi wanateseka, wanahatari ya kubakwa kutokana na hii njia ambayo imetengenezwa na mgodi. Wananchi hawana huduma hata ya umeme wala maji katika eneo lao kwa sababu ni eneo lenye leseni ya mgodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wananchi wa Katoma wametajwa kwenye ripoti ya Bomani kwamba wananchi wa Katoma na Kompaundi hawa ni watu wanaoathirika na mitetemo ya mgodi, nyumba zao zinapasuka. Waziri Kalemani alikuja Geita kuongea na hawa watu wa migodi ili kuhakikisha ya kwamba haya yote yanamalizika.

TAARIFA.......

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu akae chini, kwa sababu kama yangekuwa yamefanyika hayo, tusingekuwa na kikao na Kalemani juzi hapo Geita. Akae chini hajui kinachoendelea Geita, haishi Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kitu ambacho nasema ni kwamba ninaumia kwa sababu haki za watu zinaendelea kuvunjwa. Tunaongelea kodi kupotea lakini haki za binadamu zinavunjwa katika maeneo haya yanayozunguka maeneo ya migodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitoe suggestions, tuna kitu ambacho kinaitwa service levy, 0.3 percent ya gross revenue ya hii migodi, mimi natoa wazo kwa Serikali na kwa Waziri Mpango, Serikali ilete sheria humu ndani, tutengeneze Development Fund. Pesa hizi zote zinazokusanywa zitaingizwa kwenye hiyo Development Fund ili kuhakikisha zinaenda kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo husika ili wananchi hata baada ya shughuli za mgodi kuondoka waone kwamba kodi zilizopatikana zilijenga miundombinu kwa ajili ya watu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichangie katika suala la kuweka mfumo wa bajeti unaozingatia usawa wa kijinsia. Nilipokuwa mgeni kabisa ndani ya Bunge hili nilichangia kuhusu suala la sanitary pads, nikasema Serikali iweke pesa ili kuhakikisha watoto wetu mashuleni wanapata sanitary pads. Ni kitu ambacho hakijafanyiwa kazi na Wizara ya Afya wala hakijafanyiwa kazi na Wizara ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaona kwamba kama ni shughuli za maendeleo, watoto wa kike na wanawake wana haki sawa ya kushiriki katika uchumi wa Taifa lao. Kutokana na utofauti uliopo, wanawake na wasichana wanashindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli hizi. Kwa hiyo, niombe Serikali ipange pesa kwa kuzingatia kwamba kina mama wanaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwawekee hela za kutosha kwenye dawa na hapa nilipendekeza kwamba pesa ya dawa ihamishwe kutoka kwenye development budget zipelekwe kwenye recurrent expenditure. Hela za dawa peke yake, vifaa tiba vibaki kwenye development budget ili kuhakikisha kwamba hela za dawa na maji ya uchungu zinapatikana ili akina mama wetu waweze kupata tiba na kuepusha vifo wakati wanajifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye masuala ya kilimo, akina mama ambao wana uwezo wa kumiliki ardhi mpaka leo hii ni asilimia nane tu, wengine wanatumia ardhi ambazo ni za waume zao na ardhi za ukoo. Kama Serikali katika bajeti yake, inaweka mifumo gani ya kuhakikisha kwamba akina mama wanaweza kutengewa pesa kuwainua ili na wao waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo za maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho naomba nipendekeze kwenye suala la property tax ambalo limeshazungumziwa na wengi. Mimi natoka katika Halmashauri ya Mji wa Geita hapo ndipo ninapoishi na wananchi wale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.