Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Mazingira na Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba niwape pole wananchi wa Wilaya ya Itilima kwa kupatwa na msiba wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji uliotokea hivi karibuni kwa kuvamiwa nyumbani kwake na kupigwa hadi kuuawa. Nawapa pole sana na ni pole kwa Chama. Pia nichukue nafasi hii kukishukuru Chama changu ambacho kimeona umuhimu wa mimi kuwa Mwakilishi wa Mkoa wa Simiyu hasa kwa upande wa UKAWA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niende moja kwa moja kwenye Wizara ya Mazingira. Tunapozungumza suala la mazingira kwa uhalisia ni kwamba tunapaswa kuzungumza kwa mapana zaidi kwa sababu wananchi tulio wengi tumekuwa tukiamini kabisa kwamba mazingira ni kufagia tu. Naamini mazingira tunapaswa kuyatafakari kwa upana zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha taarifa yake, anasema anatarajia kuifanya nchi kuwa ya kijani. Sina hakika kama anaweza kuifanya nchi ya kijani ilihali hawaoneshi u-seriuos wa kubadilisha mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu, ukiangalia katika bajeti ambayo imetengwa kwa ajili ya kuboresha mazingira, haikidhi kile ambacho wanakizungumza. Tumejifunza pia kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, fedha iliyokuwa imetolewa pale ya mazingira ni kama shilingi 3.8 bilioni, lakini mpaka mwezi Machi, Wizara ilikuwa imepokea shilingi milioni 338 jambo ambalo linaonesha wazi kwamba hata ile fedha kidogo haitoki kwa wakati na kama ilitoka mwezi Machi tarehe 31, maana yake hata ile mipango iliyopangwa kwa mwaka wa fedha uliopita haijafanya kazi. Kwa hiyo, hata tukisema kwamba bajeti bado haikidhi, bado Serikali haitoi fedha kwa wakati. Nashauri kama kweli tunataka kufanya mabadiliko ya mazingira na Rais amefuta sherehe ya Muungano akimaanisha kwamba tuwe na nguvu ya mazingira Serikali itoe fedha hizo kwa wakati ili tuweze kuimarisha mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne, ilitoa kauli kwamba wafugaji wafuge ng‟ombe kisasa kwa maana ya kwamba ng‟ombe wanaleta uharibifu wa mazingira jambo ambalo siyo kweli. Nilidhani kwamba badala ya Serikali kutamka wazi kwamba wafugaji wapunguze ng‟ombe, ni vema basi ingeweza kutamka kwamba Mkoa wa Dar es salaam uanze kupunguza magari kwa sababu unaonesha wazi kabisa kwamba ni uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe kusema hivyo, badala ya kuwaambia wafugaji wapunguze ng‟ombe, Serikali ijipange kwenda kutoa elimu kwa hawa Wasukuma na wafugaji wengine wa mikoa mingine, badala ya kuwaambia wapunguze ng‟ombe, watoe elimu ya kuwafanya watengeneze biogas kama issue ni kwamba kinyesi cha ng‟ombe ndiyo kinacholeta uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha mazingira, bado minada yetu kwenye mikoa inafanya biashara, minada yote haina uzio, nashindwa kufahamu kwamba ni mazingira yapi ambayo tunayaboresha wakati minada tunayoiendesha tunathamini kukusanya ushuru badala ya kuimarisha minada ambayo haina uzio, haijulikani kinyesi cha ng‟ombe ni kipi na kinyesi cha mwanadamu ni kipi. Siyo hivyo tu bado minada hii haina vyoo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, tusizungumze mikakati ya kwenye makaratasi, hii mikakati ya kwenye makaratasi imepitwa na wakati. Waziri anasema anakwenda kuifanya nchi ya kijani, nataka anieleze kwamba nchi yetu inatumia usafiri wa meli, wasafiri wote wa meli naamini kabisa wanajisaidia kwenye bahari zetu, sasa nataka alieleze Bunge kwamba hivyo vinyesi vyote vinavyodondokea na mikojo yote kwenye bahari vinaenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujui hivyo vinyesi vinakwenda wapi na baadaye Wabunge tunakuja hapa tunasimama, tunasifia, tunasema namshukuru Waziri wa Maji ameniboreshea kwenye Jimbo langu maji safi na salama, wakati hujui yale maji kama kweli ni salama. Sasa tunataka kujua vile vinyesi vinakwenda wapi na ile mitambo inatumikaje? Naomba kufahamu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kidogo kwenye suala la Muungano. Nina imani kabisa kwa sasa inavyoonekana, kama Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauko hai. Nasema kwa sababu kwa sasa Zanzibar kwanza ina bendera yake, ina wimbo wake na mbaya zaidi bajeti ya Zanzibar haiji huku Bara. Naishauri Serikali kama inaamini kabisa kwamba Muungano ni salama, niiombe Serikali hii ipitishe maoni, tuone wangapi wanahitaji Mheshimiwa Mwenyekiti, sisomi nina akili. Mimi nilichojifunza humu Bungeni ukiona sindano inaingia utamsikia Mheshimiwa anatetea na hasa suala likitajwa jina la Rais, nashindwa kufahamu kwamba anatetea kwa misingi ipi, yeye ni Waziri hatakiwi kuonyesha itikadi yoyote. Lakini pia najua…….
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba Muungano siyo salama mpaka sasa hivi. Imeonesha wazi pia kwamba, Wazanzibari waliamua kuchagua Rais wao, lakini kwa sababu Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina mabomu, ina silaha, imeamua kupora ushindi waziwazi...
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu kwa leo. Ahsante sana