Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama tena mbele ya Bunge lako Tukufu kuhitimisha mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2017/2018. Utakumbuka tarehe 08, Juni, 2017 niliwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2016, Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/2018 na Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba zote mbili nilieleza shughuli mbalimbali zilizotekelezwa na Serikali katika kipindi cha mwaka 2016/2017 pamoja na mafanikio na changamoto zilizojitokeza. Aidha, nilieleza malengo na miradi ya kipaumbele ambayo Serikali inakusudia kutekeleza katika mwaka 2017/2018 na mapendekezo ya bajeti. Waheshimiwa Wabunge walipata nafasi ya kuzipitia hotuba hizo pamoja na viambatisho vyake na kutoa maoni na mapendekezo juu ya namna bora zaidi ya kufanikisha ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri mjadala huu ambao unatarajiwa kuhitimishwa hivi leo.

Mheshimiwa Spika, napenda kutambua michango iliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini pamoja na maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yaliyowasilishwa na Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba kwa niaba ya Msemaji wa Kambi hiyo kwa Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, ninathamini sana maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wote. Wabunge 193 walichangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali, kati ya hao wa kuzungumza walikuwa ni 165 na 28 kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi na Wizara yangu tunawashukuru kwa dhati kabisa kwa pongezi ambazo mlitupatia, nikianza na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alinipigia simu kutoa pongezi zake, lakini pia ninyi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wengi ambao wametupongeza kutoka ndani na nje ya nchi yetu, kwa kweli mmetupatia nguvu ya kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa hotuba nilizoziwasilisha, Serikali imepokea michango mingi sana na ushauri. Yapo maeneo yaliyoungwa mkono na mengine ambayo yalilenga kuboresha Bajeti ya Serikali au kuikosoa. Napenda kulihakikishia Bunge kwamba tumepokea michango yote yenye afya kwa maendeleo ya Taifa letu. Baadhi tutayazingatia katika bajeti hii na bajeti zitakazofuata; na leo nitadhihirisha tena kwamba bajeti hii haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya hatua ambazo ziliungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge wengi ni pamoja na zifuatazo:-

Kwanza, ni kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari, kutoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote ya ada ya leseni ya magari yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma, kuanzisha maeneo maalum (clearing houses) ya kukagua na kuthibitisha thamani ya madini kabla ya kusafirishwa, kuondoa VAT kwenye bidhaa za mtaji, kusamehe VAT kwenye vyakula vya mifugo, kutoa msamaha wa VAT na ushuru wa forodha kwenye vifaa maalum vya kutengeneza vifaa vya watu wenye ulemavu; pia miradi ya kielelezo itakayopewa msukumo maalum katika mwaka wa 2017/2018 ikiwemo miradi ya maji, zahanati, vituo vya afya, uendelezaji wa elimu katika ngazi zote, ununuzi wa vifaa tiba, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, uimarishaji wa Shirika la Ndege la Tanzania, miradi ya umeme, miradi ya makaa ya mawe na chuma, uendelezaji wa maeneo maalum ya uwekezaji, ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa na ule wa bomba la mafuta kutoka Hoima - Uganda hadi Bandari ya Tanga, lakini pia kuendeleza utulivu wa uchumi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba nami niungane pia na Waheshimiwa Wabunge wengi waliopongeza juhudi zilizochukuliwa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kulinda rasilimali za Taifa letu ili kuhakikisha kwamba Watanzania tunanufaika na rasilimali za nchi na hususan madini.

Mheshimiwa Spika, tunampongeza sana Jemadari wetu Mkuu kwa kuthubutu kufichua na kuweka hadharani udhalimu ambao tumekuwa tunafanyiwa kwa miaka mingi kupitia utoroshaji wa madini na upotevu wa mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamhakikishia Mheshimiwa Rais wetu kuwa tunamuunga mkono na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu amlinde, ampe afya njema na amtie nguvu katika kazi yake ngumu ya kuongoza mapambano dhidi ya uporaji wa rasilimali za nchi yetu. Ushindi ni lazima na hakuna kurudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niseme kidogo juu ya ushauri uliotolewa na Wabunge wengi. Kama nilivyosema mwanzo, yapo maoni yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wengi katika maeneo mbalimbali ili Serikali iangalie namna ya kuyazingatia katika bajeti hii na zijazo. Naomba kurejea ushauri muhimu sana uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:-

(i) Kuongeza kasi ya kutekeleza miradi ya maji nchini na hasa vijijini kwa kuongeza bajeti ya maji;

(ii) Kuboresha mfumo wa utozaji kodi ya majengo;

(iii) Kukamilisha haraka utaratibu mzuri na endelevu na kuanza kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji haraka iwezekanavyo;

(iv) Kuongeza kasi ya kulipa madeni ya ndani ya wakandarasi, watoa huduma na watumishi;

(v) Kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Taifa;

(vi) Kuendeleza utulivu wa uchumi ikiwa ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei;

(vii) Kuimarisha thamani ya shilingi na kuongeza wigo wa huduma za kibenki hadi vijijini; na

(viii) Kujenga mazingira rafiki kwa uwekezaji na kufanya biashara nchini kwa kudumisha mashauriano na ushirikiano wa dhati na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nianze kufafanua baadhi ya hoja.

Hoja ya kwanza, Serikali ilishauriwa iongeze tozo ya shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli kwa ajili ya Mfuko wa Maji ili kuwe na chanzo kinachotabirika (ring fence).

Mheshimiwa Spika, hii ilikuwa ni hoja mama ambayo ilitawala mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Baada ya Serikali kutafakari kuleta pendekezo la kufuta ada ya Motor Vehicle License ili kuondoa kero ya muda mrefu ya kutoza ada hiyo hata kama magari hayatembei na kufidia mapato hayo kwa kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya dizeli, petrol na mafuta ya taa kwa shilingi 40 kwa lita; Waheshimiwa Wabunge walishauri mapato yatakayotokana na hatua hiyo, ndiyo yaelekezwe kwenye Mfuko wa Maji kwa kutambua kwamba kuongeza zaidi ushuru wa bidhaa kwenye mafuta, kutaathiri wananchi wengi kwa kuwa kutasababisha bei za bidhaa karibu zote, chakula, usafiri, usafirishaji, gharama za uzalishaji na gharama za maisha kwa ujumla kupanda sana kutokana na kupandisha bei ya nishati hiyo muhimu tena katika kipindi ambacho bei za mafuta katika Soko la Dunia inatarajiwa kuongezeka kwa wastani wa dola 50 kwa pipa hadi dola 60 mpaka 65 katika mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuelekeza chanzo cha mapato mahususi kwenye matumizi maalum (revenue earmarking) unasaidia kuongeza fedha kwenye eneo linalolengwa na pia kuhakikisha upatikanaji wa fedha (funding stability). Ni kweli pia utaratibu huu umeleta matokeo chanya kwenye programu ya kusambaza umeme vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini. (Makofi)

Aidha, ahadi iliyopo katika katika ilani ya uchaguzi ya CCM 2015 hadi 2020, ni deni na Serikali ina nia thabiti ya kumtua mama ndoo kichwani katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali katika kipindi kifupi cha miezi 18 zinathibitishwa na kukamilika kwa miradi mikubwa ya maji ikiwemo Ruvu Chini ambayo inatoa lita milioni 270 kwa siku; Ruvu Juu lita milioni 196 kwa siku; Visima vya Mpera na Kimbiji lita milioni 260 kwa siku na Sumbawanga lita milioni 13 kwa siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya maji iliyokamilika ni Nansio, Ukerewe lita milioni 8.6 kwa siku, Bukoba Mjini lita milioni 18 kwa siku, Musoma Mjini lita milioni 30 kwa siku, Sengerema lita milioni 15 kwa siku, lakini pia mradi ule wa Msanga Mkuu kule Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, Serikali inapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge hili kwa ajili ya miradi ya maji kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambazo ni shilingi bilioni 249.5 na Mfuko wa Maji shilingi bilioni 158.5 zitatolewa kuendana na mpango kazi na kupitia Kamati ya Bajeti, Bunge litapewa taarifa rasmi ya utekelezaji wa hadi hii ya Serikali kila nusu mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, hatua nyingine zitakazochukuliwa na Serikali ni pamoja na zifuatazo:-

Kwanza, ni kuharakisha mchakato wa mikopo kwa ajili ya miradi ya maji kutoka taasisi mbalimbali na nchi rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba leo terehe 20 Juni, 2017 nimesaini mkopo wa dola za Kimarekani milioni 400 kutoka Benki ya Credit Swiss ili kugharamia miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna miradi mikubwa sita:- Kwanza kuna mradi wa upanuzi wa huduma za maji
Mijini ambao utagusa Mikoa ya Kagera, Rukwa, Dodoma,
Morogoro, Pwani, Simiyu, Iringa, Mara na Mwanza. (Makofi)

Mradi wa pili ni mradi wa uchimbaji wa visima na ujenzi wa Mabwawa katika Mikoa ya Rukwa, Mbeya, Shinyanga na Simiyu. (Makofi)

Mradi wa tatu ni mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji Mijini, itagusa Mikoa ya Rukwa, Dodoma, Morogoro, Kigoma, Kagera, Lindi, Manyara, Mtwara, Tabora, Ruvuma na Kilimanjaro. (Makofi)

Mradi wa nne, ni mradi wa upanuzi wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira Dar es Salaam na hii itagusa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. (Makofi)

Mradi wa tano ni kuendeleza na kusimamia rasilimali za maji. Itagusa Mikoa ya Pwani, Rukwa, Ruvuma, Tanga, Kigoma, Dodoma, Manyara, Njombe, Singida, Shinyanga, Tabora, Songwe, Mwanza, Kagera, Geita, Mara na Morogoro(Makofi)

Mradi wa sita ni mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Kahama na Shinyanga na mikoa itakayohusika ni Shinyanga na Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha taratibu za mkopo kutoka Exim Bank of India dola milioni 500 ambazo ni takriban shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya miradi ya maji katika miji 17 nchini. Hivi sasa mkopo huo umeshakufanyiwa uchambuzi na Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Madeni na Waziri wa Fedha na Mipango amesharidhia kwa niaba ya Serikali, fedha hizi zikopwe. Taratibu zinazobaki sasa ni kukamilisha usanifu wa miradi hii na kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hatimaye kusaini mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Serikali inafuatilia upatikanaji wa fedha Euro milioni 102 kutoka Green Climate Change Fund kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji ya Simiyu. Pia nchi rafiki ikiwemo Morocco na Misri zimeonyesha utayari wa kugharamia utekelezaji wa miradi ya maji hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kwamba Serikali inatoza Kodi ya Leseni ya Magari kwa mwaka (Annual Motor Vehicle License Fee) kwa Watanzania maskini ambao hawamiliki gari kwa kutoza kodi hiyo katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uamuzi wa kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ikiwemo mafuta ya taa unalenga kuwalinda Watanzania dhidi ya madhara ya uchakachuaji wa mafuta (fuel adulteration).

Kwa sasa tofauti ya kodi zinazotozwa kwenye mafuta ya taa na Dizeli ni shilingi 53 kwa lita. Endapo ushuru huu wa shilingi 40 hautaongezwa kwenye mafuta ya taa, tofauti ya kodi itakuwa shilingi 93 kwa lita ambayo itachochea uchakachuaji wa mafuta utakaosababisha uharibifu wa magari na mitambo na kupoteza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ongezeko la tozo kwenye petroli, dizeli na mafuta ya taa limefikiwa ili kuondoa kero ya muda mrefu ya wamiliki wa magari kudaiwa ada ya Motor Vehicle License hata kama gari halitembei, lakini pia tumefanya hivyo kwa namna ambayo haitachochea uchakachuaji wa mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua hiyo pia itaiwezesha Serikali kupata mapato ambayo yatatumika kugharamia huduma muhimu za jamii kama barabara, afya, dawa na vifaa tiba ambavyo Watanzania masikini pia watafaidika nazo.
(Makofi)

Mheshimiwa Spika, palikuwepo na hoja kwamba msamaha (Tax Amnesty) ambayo nilitangaza ile tarehe 8 Juni, 2017 ambayo ulitolewa kwenye Ada ya Mwaka ya Leseni uhusishe na ada ya ukaguzi wa vifaa vya kuzima moto (Fire Inspection Fee).

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, hatua ya Serikali ya kutoa msahama (Tax Amnesty) kwa ada ya leseni ya magari itahusisha pia ada, riba na adhabu ya madeni yote ye fire inspection fee yaliyolimbikizwa miaka ya nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitarudia tena.

Mheshimiwa Spika, hatua ya Serikali ya kutoa msahama (Tax Amnesty) kwa ada ya leseni ya magari itahusisha pia ada, riba na adhabu ya madeni yote ye fire inspection fee yaliyolimbikizwa miaka ya nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba tozo ya shilingi 10,000 kwenye nyumba ambazo hazijathaminiwa hususan za vijijini ni kuwaongezea mzigo wananchi wa kijijini, lakini pia ile tozo ya shilingi 50,000 kwa ghorofa ambazo wanaishi wastaafu iondolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kodi ya majengo hutozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Miji (The Urban Authorities Rating) Sura ya 289. Kifungu cha pili cha Sheria ya Mamlaka ya Miji (The Urban Authorities Act) inabainisha kuwa kodi ya majengo inatozwa kwenye majengo yaliyojengwa kwenye Mamlaka za Majiji, Miji na Miji Midogo. Vijiji havitahusika katika kodi hii.

Mheshimiwa Spika, kodi ya majengo hutozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Miji (The Urban Authorities Rating) Sura ya 289 na kifungu cha pili cha Sheria ya Mamlaka ya Miji (The Urban Authorities Act) inabainisha kuwa kodi ya majengo inatozwa kwenye majengo yaliyojengwa kwenye Mamlaka za Majiji, Miji na Miji Midogo. Vijiji havihusiki katika kodi hii.

Mheshimiwa Spika, ninasema, aidha kwa mujibu wa sheria, wananchi wenye umri zaidi ya miaka 60 hawapaswi kulipa kodi ya majengo wanayoyatumia kama makazi yao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, palikuwa na hoja kwamba Serikali isitoze kodi ya majengo kwenye nyumba za tope na tembe.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha (3); “Kodi ya majengo hutozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Miji, Sura ya 289 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Fedha ya mwaka 2015.” Kwa mujibu wa kifungu cha pili cha Sheria za Mamlaka za Miji (The Urban Authorities Act) kinabainisha kuwa kodi ya majengo inayotozwa kwenye majengo yaliyojengwa kwenye Mamlaka za Majiji, Manispaa, Miji Midogo na Halmashauri za Wilaya.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha tatu cha Sheria hii kimetafsiri nyumba zinazotakiwa kutozwa kodi ya majengo kuwa ni nyumba zote zilizoko ndani ya Mamlaka ya Majiji, Manispaa, Miji Midogo na Halmashauri za Wilaya ambazo zimeshajengwa na kuanza kutumika kwa makazi. Kwa maelezo hayo, kodi ya majengo inatozwa kwa nyumba zote zilizoko kwenye Mamlaka ya Majiji, Miji na Miji Midogo ambazo zimeshaanza kutumika kwa makazi kama ilivyobainishwa kwenye hotuba yangu ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018. Hata hivyo, tozo hizo hazitahusisha nyumba za tope na tembe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nilieleze Bunge lako na wananchi kwa ujumla kuwa kodi ya majengo kama nilivyosema itatozwa katika Miji, Majiji na Miji Midogo kwa mujibu wa Sheria za Kodi ya Majengo ya Mamlaka ya Miji Sura ya 289. Kodi hiyo itatozwa katika majengo ya kudumu yaani yale yaliyojengwa kwa tofali za saruji, tofali za kuchoma na kuezekwa kwa bati na siyo za udongo wala zilizoezekwa kwa nyasi au zile za tembe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu uwasilishaji wa mapato ya kodi ya majengo kwa Halmashauri. Mapato ya kodi ya majengo na mabango yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kuhifadhiwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, Serikali itaweka utaratibu wa kurejesha mapato hayo kwenye Halmashauri ambapo watatakiwa kuwasilisha mahitaji yao halisi. Aidha, Serikali itapitia mahitaji yao ili kujiridhisha kabla ya kuwarejeshea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kutokutoza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye magari ya kubeba wagonjwa. Kwa kutambua umuhimu wa huduma za afya kwa wananchi wetu na hasa katika maeneo ya vijijini, Serikali imeamua kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye magari yanayotumika katika kubeba wagonjwa (ambulance).

Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa magari yanayotumika katika kubeba wagonjwa (ambulance). Hatua hii itahusisha magari yanayoingizwa nchini yakiwa yametengenezwa mahsusi kwa ajili ya kubeba wagonjwa na kwamba yanaingizwa nchini kwa matumizi ya hospitali au vituo vya kutoa huduma za afya vilivyosajiliwa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali itatumia utaratibu wa Hati ya Malipo ya Hazina (Treasury Voucher System) katika kusimamia misamaha hii ambapo kodi inayosamehewa italipiwa na Serikali kupitia Hazina kama inavyofanyika kwa taasisi za dini na kadhalika ili kudhibiti matumizi mabaya ya misamaha hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye ada na vibali vya uwindaji vitolewavyo na Serikali. Serikali inaondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye ada, leseni na vibali vya uwindaji. Hatua hii ina lengo la kuhamasisha ukuaji wa shughuli za uwindaji na sekta ya utalii kwa ujumla. (Makofi)

Kulikuwa na hoja kuhusu ada ya tathmini ya mazingira. kutokana na kilio cha wawekezaji wengi na hasa katika Sekta ya Viwanda, napendekeza kufuta Ada ya Kufanya Tathmini ya Mazingira (Environmental Impact Assessment) kwa wawekezaji wote wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia.

Napendekeza kufuta Ada ya Kufanya Tathmini ya Mazingira (Environmental Impact Assessment) kwa wawekezaji wote wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba Serikali ifanye marekebisho kwenye Sheria ya EPOCA, Serikali imelisikia hili na baada ya kutafakari kwa kina, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya EPOCA ili:-

Moja, hisa za asilimia 25 zitakazouzwa na kampuni ya mawasiliano kwenye Soko la Hisa ziuzwe kwa umma ili kujumuisha Watanzania au Kampuni yoyote ya Kitanzania; Watanzania wanaoishi nje ya nchi, kampuni zinazomilikiwa kwa pamoja baina ya Watanzania na raia wa nje; raia na kampuni au taasisi za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; au raia wa kampuni kutoka nchi nyingine yoyote.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa sharti lililopo kwa mujibu wa sheria ni kwa hisa husika kuuzwa kwa raia wa Tanzania pekee.

Mheshimiwa Spika, ya pili ni kuziondoa kampuni ndogo za mawasiliano ambazo zina leseni ya application service kwenye sharti la kuuza hisa kwenye Soko la Hisa ili kubaki na kampuni kubwa za mawasiliano zenye leseni ya network facility au network service. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, Kampuni ya simu itakayoshindwa kufikia mauzo ya asilimia 25 kutokana na kutofaulu kwa toleo kwa umma (Unsuccessful Public Offer),Waziri mwenye dhamana atatoa maelekezo yaani directives ya namna kampuni husika itakavyoweza kutoa hisa kufikia asilimia 25 kwa kadri hali ya soko itakavyoruhusu, baada ya kupokea maombi ya kampuni ya simu iliyotolewa chini ya Sheria ya EPOCA na baada ya kupokea mapendekezo ya Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu watoa huduma na wauza bidhaa katika maeneo yasiyo rasmi kusajiliwa; ili kuhamasisha wafanyabiashara ndogo ndogo, kurasimisha shughuli zao na Serikali iweze kukusanya kodi, utaratibu nilioutangaza kupitia Bajeti Kuu ya Serikali kuhusu kuwatambua wafanyabiashara wa aina hii na kuwapa vitambulisho, itahusisha pia watoa huduma za chakula (caterers), washereheshaji (masters of ceremony) katika shughuli mbalimbali na wafanyabiasha wadogo wasio rasmi wanaofanya biashara katika maeneo rasmi.

Mheshimiwa Spika, naomba nirudie. Ili kuhamasisha wafanyabiashara wadogo kurasimisha shughuli zao na Serikali iweze kukusanya kodi, utaratibu nilioutangaza kupitia Bajeti Kuu ya Serikali kuwatambua wafanyabiashara wa aina hii na kuwapa vitambulisho; itahusisha pia watoa huduma za chakula (caterers), washereheshaji (masters of ceremony) katika shughuli mbalimbali na wafanyabiasha wadogo wasio rasmi wanaofanya biashara katika maeneo rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu utozaji wa tozo kwa kutumia fedha za kigeni kwenye vyombo vya uvuvi vilivyosajiliwa nchini; Serikali imesikia maoni ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na kero wanayopata wavuvi nchini ya kutozwa tozo mbalimbali kwa fedha za kigeni kwenye vyombo vya uvuvi vilivyosajiliwa nchini.

Mheshimiwa Spika, kuanzia sasa Serikali inaagiza taasisi zote zinazohusika na utozaji wa tozo hizo ziache utaratibu huo mara moja na zianze kutoza kwa kutumia shilingi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kukusanya kodi inayotokana na mapato kutoka kwenye sekta ya michezo ya kubahatisha.

Kwa kuzingatia ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, Serikali imeona kuna uwezekano wa kupata mapato mengi kutoka kwenye sekta ya michezo ya kubahatisha. Hivyo, kuanzia tarehe 1 Julai, 2017 mapato yote yatakayotokana na michezo ya kubahatisha yatakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mheshimiwa Spika, mapato hayo yatawasilishwa Mfuko Mkuu wa Serikali, Serikali itaweka utaratibu wa kuzirejesha fedha hizo kwenye Bodi ya Michezo ya kubahatisha baada ya kuhakiki mahitaji na matumizi ya Bodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba uchumi wa taifa siyo shirikishi, na bajeti iko kinyume na mahitaji ya ukuwaji shirikishi wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, niruhusu nitoe darasa kidogo.
(Makofi)

Mheshimiwa Spika, dhana ya uchumi shirikishi ni pana sana. Kwa lugha nyepesi ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi kama jamii inashiriki na kunufaika katika shughuli kuu zinazokuza uchumi wa nchi. Ndiyo kusema lazima uchumi kwa upana wake uwe unakua na kunemeesha wananchi walio wengi kwa namna ambayo ni endelevu (broad based growth that generate sustain progress in living standards).

Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi shirikishi unapimwa kwa viashiria vingi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa fursa za ajira (job creation), kupungua kwa umasikini, kuongezeka kwa tabaka la kati katika nchi (growth of the middle class), kupungua kwa tofauti za kipato (declined in income inequality), kupanuka kwa wigo wa fursa na huduma za kiuchumi na hususan masoko na huduma za kifedha (financial services) na usalama (security).

Mheshimiwa Spika, aidha, ukuaji wa uchumi shirikishi, unajengwa juu ya nguzo (pillars) takriban saba ambazo ni:-

(1) Elimu na ujuzi; (Makofi)

(2) Huduma za kijamii na miundombinu; (Makofi)

(3) Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; (Makofi)

(4) Huduma za kifedha na uwekezaji;

(5) Ujasiliamali na ukuzaji wa rasilimalia (accumulation of assets);

(6) Ajira na mafao ya wafanyakazi; na

(7) Uhawalishaji wa rasilimali fedha (fiscal transfers).

Mheshimiwa Spika, kwa Waheshimiwa Wabunge wanaopenda kupata elimu ya kina juu ya somo hili, kuna vitabu na machapisho mengi na wanaweza kujisomea ikiwa pamoja na taarifa ya hivi karibuni ya World Economic Forum ambayo inaitwa The Inclusive Growth and Development Report, 2017. Hivyo, siyo sahihi hata kidogo kuangalia kigezo kimoja tu na kutoa hukumu kwamba ukuaji wa uchumi siyo shirikishi au kwamba bajeti iko kinyume na mahitaji ya ukuaji shirikishi wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa 2016 ambacho kiligawiwa kwa Waheshimiwa Wabunge, tarehe 8 Juni, kinaonesha wazi kuwa Tanzania imepiga hatua nzuri katika viashiria vingi na ujenzi wa misingi ya uchumi shirikishi chini ya dhana ya kujenga uchumi wa viwanda. Bajeti ya mwaka 2017/2018 imejielekeza katika maeneo yote ya msingi kwa ujenzi wa uchumi shirikishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa kila kitu siyo waridi na haiwezekani kuwa na ukuaji wa uchumi shirikishi katika kipindi kifupi, maana maendeleo ni mchakato.

Mheshimiwa Spika, yapo maeneo ambayo bado yanahitaji msukumo zaidi ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo ambayo katika nchi yetu inaajiri takribani theluthi mbili ya Watanzania lakini imekuwa ikikua kwa kasi ndogo na ndiyo maana Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza tija kwenye kilimo kwa kutilia mkazo kilimo cha umwagiliaji kuhakikisha upatikanaji wa mikopo, pembejeo na masoko ya uhakika, kuhamasisha kilimo cha kibishara na kujenga mnyororo wa thamani.

Mheshimiwa Spika, aidha, Tanzania ni mfano bora duniani kwa upande wa huduma za kifedha jumuishi (financial inclusion), ambapo zaidi ya watu milioni 17 wanafanya miamala ya malipo kupitia simu za mkononi.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kodi na tozo nyingi, tozo 16 ambazo zinatoza wamiliki wa shule binafsi. Serikali imesikia maoni ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu kuondoa baadhi ya kodi na tozo kwenye shule binafsi. Serikali imezingatia maoni hayo na imeamua kuondoa tozo zifuatazo:-

Kwanza, ni tozo ya kuendeleza Mafunzo ya Ufundi (SDL); na pili, ni ada ya Zimamoto. Lengo la hatua hizi ni kupunguza gharama kwa wazazi na walezi katika kuwapatia watoto wetu elimu na kuziwezesha shule kutoa elimu kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni matumaini ya Serikali kuwa wamiliki wa shule wataipokea dhamira hii njema ya Serikali; na hivyo kupitia viwango na ada wanazozitoza ili kuzipunguza na hivyo kutoa fursa zaidi kwa watoto na vijana kutoka katika familia maskini ili ziweze kumudu ada za shule hizo binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya utegemezi wa kibajeti, kwamba pamoja na ukweli kuwa washirika wa maendeleo kutoka nje wanaendelea kupunguza kasi yao ya kutoa mikopo na misaada, bado bajeti ya Serikali imeendelea kuongeza kiasi cha utegemezi wa mikopo na misaada.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza kasi ya makusanyo ya mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi kutoka kwa washirika wa maendeleo. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2011/2012 kiwango cha utegemezi kimeendelea kupungua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012 fedha za nje zilikuwa shilingi trilioni 3.9 sawa na asilimia 29 ya bajeti; mwaka uliofuta 2012/2013, fedha za nje zilikuwa shilingi trilioni
3.1 sawa na asilimia 21 ya bajeti; mwaka wa 2013/2014 fedha za nje zilikuwa shilingi trilioni 3.8 sawa na asilimia 21 ya bajeti; mwaka 2014/2015 fedha za nje zilikuwa shilingi trilioni 2.9 sawa na asilimia 15 ya bajeti; mwaka 2015/2016 fedha za nje zilikuwa shilingi trilioni 2.3 sawa na asilimia 10 ya bajeti; na mwaka huu wa fedha 2016/2017 fedha za nje zilikuwa shilingi trilioni 3.6 sawa na asilimia 12 ya bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwenendo huu unaendana kabisa na fundisho la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere linalosema self-reliance is the means by which people develop. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba Serikali ichukue hatua ya kuyaelekeza mabenki ya kibiashara kupitia Benki Kuu ya Tanzania, kupunguza riba kama ambavyo wao wamepunguziwa ili wananchi waweze kukopa.

Mheshimiwa Spika, uamuzi wa kutumia Mfumo wa Riba wa Soko Huru, ulichukuliwa na Serikali takribani miongo miwili iliyopita, baada ya mfumo ulikuwepo wa kudhibiti riba, kusababisha benki zetu kuwa na mikopo mikubwa chechefu na kupata hasara.

Mheshimiwa Spika, tangu mfumo wa soko huria umeanza kutumika, mikopo iliyokwenda kwenye sekta binafsi imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, uwiano kati ya mikopo kwa sekta binafsi na Pato la Taifa ilipanda kutoka 4% mwaka 2000 hadi 16% mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika, mfumo wa soko huria pia umesaidia kuelekeza mikopo kwenye shughuli za kiuchumi zenye tija zaidi na hivyo kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi. Kama wengi manavyojua, tumeshuhudia uchumi kukua kwa wastani wa 6.7% kila mwaka katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita. Hivyo, haitakuwa busara kurudi katika utaratibu wa kudhibiti riba ambapo hapo awali ulituletea shida. (Makofi)

Aidha, Benki Kuu, ikiwa msimamizi wa benki za biashara, ikitoa maagizo ya kupunguza riba itakinzana na jukumu lake la kuzisimamia benki ipasavyo, maana endapo benki zitapata hasara, itakuwa vigumu kuzichukulia hatua, kwani Benki Kuu itakuwa imehusika katika kuzipangia riba.

Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ili kuongeza ukwasi hivi karibuni yaani kupunguza discount rate na sehemu ya amana zinazowekwa Benki Kuu zinaonesha matokeo ya kushusha riba katika soko la jumla, ambapo riba ya mikopo ya siku moja baina ya benki za biashara imeshuka kutoka wastani wa 13% mwezi Disemba, 2016 hadi wastani wa 5% katika wiki mbili za kwanza za mwezi Juni, 2017.

Mheshimiwa Spika, wakati huo huo wastani wa riba ya dhamana za Serikali imeshuka kutoka 15.12% hadi asilimia
7.95. Matokeo haya yanaashiria kwamba riba za kukopesha nazo zitashuka kutokana na nguvu za soko.

Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo kwa sasa ni kuongezeka kwa mikopo chechefu ambayo inafanya benki zifanye tahadhari kubwa katika kutoa mikopo pamoja na kuendelea kutoza riba kubwa. Benki Kuu imezielekeza benki zenye uwiano mkubwa wa mikopo chochefu ziweke mikakati ya kurudisha uwiano huo kwenye kiwango kinachotakiwa cha 5% na kuzihimiza kutumia taarifa za Credit Reference Bureaus ili kupunguza mikopo chechefu na riba.

Mheshimiwa Spika, palikuwa na hoja ya malimbikizo ya VAT, na madai mbalimbali kwamba ni nini mkakati wa Serikali kulipa malimbikizo hayo?

Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kufungua akaunti ya Escrow kwa ajili ya kufanya marejesho ya madai yanayotokana na ununuzi wa sukari inayotumika viwandani na hivyo kuondoa changamoto zilizokuwepo kama nilivyotangaza siku niliposoma hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu madai mbalimbali (arrears), Serikali inaendelea kuyahakiki na kulipa. Kama nilivyoeleza katika hotuba ya bajeti, hadi mwezi Juni, 2016 madai yaliyokuwa yamewasilishwa na taasisi mbalimbali yalikuwa ya jumla ya shilingi bilioni 2934.4 ambapo jumla ya shilingi bilioni 1997.9 sawa na asilimia 68.1 zilithibitika kuwa madai halali baada ya uhakiki.

Mheshimiwa Spika, kati ya madai yaliyohakikiwa, Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 796.5 hadi ilipofikia mwezi Machi, 2017 na hivyo kubakia na madai ya shilingi bilioni 1201.4 ambayo yataendelea kulipwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Madai yaliyolipwa; wakandarasi wamelipwa jumla ya shilingi bilioni 632.1, wazabuni shilingi bilioni 78.8, watumishi shilingi bilioni 67.5 na watoa huduma shilingi bilioni 17.8.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi bilioni 1,000 kwa ajili ya kuendelea kulipa madai hayo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu marejesho ya VAT Serikali imeboresha utaratibu wa uhakiki ili kudhibiti changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na udanganyifu.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba fedha za maendeleo zinaonekana kuwa nyingi kwa kuwa zimechanganywa pamoja na fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Mheshimiwa Spika, nitasema tu kwa kifupi kwamba uwekezaji katika elimu ndiyo uwekezaji bora (is the best investment), hivyo kuwezesha vijana wa Kitanzania kusoma elimu ya juu kwa kuwapatia mikopo, ni uwekezaji wa kimaendeleo kwa hakika na ndiyo maana ni lazima ziwekwe kwenye fedha za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba bajeti ya mwaka ujao wa fedha haina chochote kuhusu Benki ya Wakulima iliyoanzishwa mwaka 2015 kwa kusudio la mtaji wa shilingi trilioni moja na kukopesha wakulima 200,000 kwa mwaka, lakini sasa imeishia kukopesha wakulima 3,700 na mtaji wa shilingi bilioni 60 tu kwa miaka mitano. Mbali na shilingi bilioni 60 za awali, Serikali imeshaipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) fedha zaidi za kuongeza mtaji ambazo ni shilingi bilioni 209.5, baada ya Serikali na TADB kutia saini mkataba wa fedha hizo mnamo tarehe 5 Juni, 2017. Fedha hizo zinatokana na mkopo wa Serikali kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na ni sehemu ya utekelezaji kwa awamu azma ya Serikali ya kuipatia benki hiyo mtaji wa angalau shilingi bilioni 800. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea sasa ni taratibu za kibenki za kuhakikisha miamala stahiki inafanyika kati ya Benki ya Maendeleo ya Afrika na TADB, hii ikijumlisha pia Benki Kuu ya Tanzania kupokea fedha hizo kwa dola za Kimarekani ambazo ni milioni 93.5 na kuzibadilisha na kuziingiza kwenye akaunti ya TADB kwa shilingi za Kitanzania zilizotajwa.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi zinategemewa kuongeza kiasi cha mikopo itakayotolewa kwa wakulima na wafugaji na pia kuiwezesha benki kutekeleza mapango wake mpya wa kuwafikia wakulima nchi nzima kwa utaratibu maalum (clustery).

Aidha, Benki ya Maendeleo ya Kilimo tayari imefanya mawasiliano rasmi na Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchi na Wizara ya Kilimo, Utalii, Mifugo na Uvuvi na ile ya Viwanda na Biashara ya Zanzibar na kuwaomba waainishe na kuwasilisha katika benki hiyo miradi ya kilimo ya kipaumbele ambayo mikoa yao inapendekeza izingatiwe zaidi katika kupatiwa mikopo na benki.

Mheshimiwa Spika, kuiongezea mtaji benki yetu ya kilimo, ni sehemu ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano wenye lengo la kufungamanisha maboresho ya sekta ya kilimo na mpango mpana wa nchi kuelekea uchumi wa viwanda na hususan viwanda vile vinavyotegemea kiasi kikubwa malighafi zinazotokana na mazao ya kilimo ya ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa hii Benki ya Kilimo na benki nyingine za maendeleo zinawezeshwa ili kuchangia maendeleo ya kilimo na viwanda kama ilivyodhamiliwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha kuwa kama nilivyoeleza katika hotuba zangu, hatua zilizopendekezwa kwenye bajeti hii, zinalenga kujenga msingi madhubuti wa uchumi wa viwanda na kupanua fursa za ajira na biashara.

Mheshimiwa Spika, dhamira yetu sote ni kufikia kiwango cha uchumi wa kipato cha kati itakapofika mwaka 2025. Ili kushiriki katika mafanikio hayo, ni lazima kila mmoja wetu atakayeshiriki katika shughuli halali ya uzalishaji au kutoa huduma na afanye hivyo kwa juhudi na maarifa ili kuleta tija.

Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa bajeti hii kunahitaji nidhamu ya hali ya juu katika usimamizi wa mapato na matumizi. Ili kufikia azma hii, juhudi ya pamoja kati ya Serikali na wadau wote zinahitajika ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa kila Mtanzania kutimiza wajibu wake hususan kulipa kodi stahiki ili bajeti hii iweze kutekelezwa kama ilivyopangwa na kama Waheshimiwa Wabunge mlivyosisitiza.

Mheshimiwa Spika, napenda nirudie maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwamba kila mwananchi akinunua kitu au huduma, adai risiti na yule anayeuza kitu au huduma na yeye atoe risiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kuwashukuru sana watumishi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi zake zote kuanzia wahudumu wetu ambao walikesha na sisi usiku kucha ili kuandaa bajeti nzuri kwa Watanzania. Niseme kwa lugha ya kigeni I am proud of you and keep it up in service of our mother land. Maintain professionalism and integrity. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.