Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Freeman Aikaeli Mbowe

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Na mimi nafikiri nisiwe mchawi, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Lukuvi na Naibu wake. Kwa kweli ni Wizara ambayo inafanya kazi bila itikadi za kisiasa, inasimamia wajibu wake vizuri. Mheshimiwa Waziri sifa unazopewa wewe na Naibu wako zinawastahili pamoja na Wizara yako yote, endeleeni kufanya kazi na tutawapa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo manne tu ya kuzungumza siku ya leo na yote naelekeza katika Jimbo langu la Hai. Kwanza, japo nafahamu ni suala linalohusu Wakala wa Barabara yaani TANROADS lakini kwa sababu linagusa ardhi nalizungumza ili Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, na nina hakika Mheshimiwa Profesa Mbarawa yuko hapa naye atanisikiliza, kwa pamoja mnaweza mkaona mnaweza kutupa vipi watu wa Hai ufumbuzi wa tatizo hili ambalo ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili linahusu barabara ya Kilimanjaro Machine Tools - Machame Girls’. Barabara yenye urefu wa kilometa 26, barabara ambayo ilijengwa wakati wa ukoloni na ni barabara kuu inayohudumia eneo lote la Machame lenye wakazi zaidi ya 200,000. TANROADS wame-declare kupanua wigo wa barabara hii na waka- declare kwamba eneo la mita 60 linahitajika liwe reserved kwa ajili ya barabara. Sasa sisi hatuna tatizo na ulazima wa kupanua na kuimarisha miundombinu yetu ya barabara. Ni kweli sheria hizi inawezekana kuna sheria ambazo zinasimamia mambo haya, lakini sheria hizi zinatungwa na Bunge na tukitunga sheria mara nyingi tunatunga sheria kwa kuangalia nchi nzima bila kuangalia mazingira mahsusi ya eneo moja baada ya jingine.

Mheshimiwa MWenyekiti, kwa eneo la Kilimanjaro ambako makazi yana watu wengi sana, mashamba hakuna. Watu wenye miaka 50 kushuka chini hawana ardhi, kuchukua eneo la barabara ya mita 60 ambayo inakwenda kwenye forest pamoja na Kilimanjaro Gate (Machame gate) kwenda kwenye National Park ni eneo kubwa sana. Tutambue kwamba kuna wakazi wamekaa kwenye maeneo haya kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita na kupanua barabara kwa upana huu maana yake ni kwamba tutabomoa misikiti, shule, makanisa, makaburi, tutapoteza kabisa flow ya Mto Weruweru, tutakata mashamba ya wananchi, hili ni jambo lenye ugomvi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upanuzi huu unazungumziwa kufanyika bila kulipa fidia. Ningependa kuishauri Serikali katika kutekeleza sheria lazima tuangalie mazingira ya maeneo na historia ya maeneo. Hii barabara ni muhimu ndiyo, lakini haijengwi reli, wala hatutegemei kwamba kweli mita zote 60 zitatumika katika kuipanua barabara hii, kwa sababu inakwenda ndani kwa kilometa 13 tu kuanzia maeneo ambayo wanakaa wakazi unaanza kukuta Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali, Waziri wa Barabara, Waziri anayeshughulika na mambo ya miundombinu pamoja na Waziri wa Ardhi tutafute ufumbuzi na ikiwezekana tafadhali m-visit Wilaya ya Hai, mkaangalie hali halisi ninayoizungumzia mahali hapa, muelewe namna ambavyo vijiji vya Nshara, kijiji cha Uduru, Warisinde, Warindoo na Foo katika Kata ya Machame Kaskazini mpaka kwenye Mronga na Mkuu wote hawa wanaathiriwa. Kwa hiyo ni jambo ambao kwa kweli linawakwaza sana wananchi. Bomoabomoa hii japo mnaona ni kilometa 13 kwa Hai, inagusa zaidi ya wananchi 6,000, zaidi ya kaya 800 zinaguswa katika jambo hili bila kuzungumzia hizo taasisi ambazo nimezizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo la kwanza ambalo ningependa kushauri Serikali na ningeomba sana Waziri katika majibu yako, na pengine niombe Waziri Mheshimiwa Mbarawa na timu yake nao vilevile pengine washirikiane katika kutupa ufumbuzi, tungependa tumalize hili tatizo bila kuleta mgogoro wa ziada na usumbufu usio wa lazima sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Mheshimiwa Waziri ni kuhusu hali nzima ya ardhi katika Mkoa wa Kilimanjaro. Tatizo kubwa la Mkoa wa Kilimanjaro ni ardhi. Tuna uhaba mkubwa sana wa ardhi, nitakiri kwamba ni Mkoa ambao idadi ya wakazi kwa kilometa za mraba ni kubwa kuliko kijiji chochote katika Afrika Mashariki na ya Kati.

Tunapozungumzia Kilimanjaro, kilomita moja ya mraba sehemu za milimani zina watu kuanzia, ikipungua sana ni 650 mpaka 1,800 per square kilometer, hii density ni kubwa kuliko eneo lolote katika Afrika ya Mashariki na Kati. Watu wenye umri wa miaka 50 kushuka hawana ardhi kabisa sasa hivi na watu wameendelea kujenga, population imeendelea ku-increase kwa rate ya 1.9 people per annum ambayo siyo kubwa sana ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi, lakini kwamba kuna tatizo kubwa la ardhi ambayo inahitaji special management hili ni la lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namuomba Waziri wa Ardhi mfanye land auditing ya Mkoa wa Kilimanjaro, siyo Hai peke yake, Mkoa mzima wa Kilimanjaro. Kwa sababu katika maeneo mengine sasa watu wamejenga nyumba mpaka kumekuwa squatters, kuna squatter za vijijini. Sasa siyo kawaida sana kukuta squatter vijijini, kuna squatter za vijijini, kuna shida ya kupitisha huduma za barabara hizi feeder roads, kuna tatizo kubwa sana ambalo linahitaji kwa kweli kufanyiwa intervention. Ningeomba Serikali Kuu ifanye intervention na kama kawaida Mheshimiwa Waziri nakukaribisha ili uje na wengine kuangalia mnaweza kufanya jambo gani katika kutatua tatizo hili la wakazi wa Hai. (Makofi)

Jambo la tatu nizungumzie mashamba ya ushirika. Huko miaka ya nyuma wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere alitaifisha mashamba makubwa yaliyokuwa ya wawekezaji wa kizungu na akakabidhi kwa vijiji kadhaa vya Wilaya ya Hai na maeneo mengine ya Mkoa wa Kilimanjaro. Baadae yale mashamba yakahamishwa kupelekwa kwenye Vyama ya Msingi vya Ushirika, lakini baada ya Sheria ya Ushirika kubadilishwa yale mashamba hayakuwa tena miliki za vijiji yakawa ni washirika wale wanaushirika ambao ni kundi katika kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mashamba yame-hold uchumi mkubwa sana wa Wilaya ya Hai na katika Mkoa mzima wa Kilimanjaro. Ni ombi langu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Waziri wa Ardhi mje tuyafanyie tathmini mashamba haya. Hivi kweli kuna economic value tunayopata kwenye mashamba yale ama yanatumika tu bila kutengeneza kile ambacho kilikusudiwa. Kama ni lazima tubadilishe matumizi yake yaweze kurejeshwa kwa wananchi, yaweze kuwa na tija zaidi katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro hasa ukizingatia namna ambavyo ardhi imekuwa ni jambo adimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mashamba makubwa yamekodishiwa watu, hawalipi katika Vyama vya msingi vya Ushirika, wananchi hawafaidi chochote wakati wananchi wengine wa kawaida hawapati hata robo eka ya kulima. Kwa hiyo ni jambo ambalo linatakiwa kupatiwa ufumbuzi, ningeomba sana Waziri hili uliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia liko pale pale katika masuala ya ardhi ni kuhusu mgogoro wa KIA. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize vizuri kwa sababu Waziri Mkuu hili jambo amelisikiliza kwa muda mrefu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba Mkuu unisikilize sana katika hili unisaidie vilevile. Mheshimiwa Waziri Mkuu, unakumbuka bado mgogoro wa KIA tumeushughulikia, nakushukuru sana kwa effort yote uliyofanya, lakini bado hatujapata ufumbuzi, kwa sababu lile eneo la mgogoro wa KADCO uwanja wa Kilimanjaro wa KIA umegusa maeneo ya wananchi wa vijiji vitano vya upande wa Wilaya ya Hai na vijiji kadhaa katika Wilaya ya Arumeru kwa ndugu yangu hapa Mheshimiwa Nassari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Hai kama Mtakuja, Tindigani, Sanya Station, Rudugai, Chemka vimeathirika, kwa kipindi chote hiki chenye mgogoro wananchi wamenyimwa kufanya shughuli zozote za maendeleo katika maeneo yao mpaka mgogoro huu utakapotatuliwa.

Kwa hiyo, kuchelewa kutatua mgogoro huu na kuwapa wale wananchi haki ya kuendelea kuishi katika maeneo yao kunakwaza sana maendeleo na ujenzi wa huduma za kijamii kama shule, barabara, miundombinu nyingine, umeme, maji na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ningeomba sana tusaidiane tumalize tatizo hili, kwa sababu kuna suala la mgogoro wa ardhi na kuna suala la KIA. Suala la KIA hilo ni suala lingine na Waziri Mbarawa naye amekuwa anashughulika na Waziri Mkuu, nawashukuru sana, lakini ardhi kwa wale wananchi waliozunguka eneo hili inakuwa ni tatizo kubwa kweli kweli. Kwa miaka kadhaa sasa wananchi hawawezi kufanya chochote wamekaa kwenye vijiji vyao, hawaruhusiwi kujenga, kupanua mashamba, hawaruhusiwi kufanya chochote cha maendeleo ya kudumu. Sasa jambo hili ni gumu kidogo hasa inapogusa wananchi wengi sana katika Wilaya ya Arumeru na Wilaya ya Hai ambayo wote wanagusa eneo la KIA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe ile juhudi uliyokuwa umeianza uimalizie, Waziri Mbarawa atusaidie tumalizie jambo hili na Waziri Lukuvi nae vilevile aje tuwa-relieve hawa wananchi. Kama tutaendelea na mazungumzo kuhusu uwanja wa KIA tuendelee, kuhusu uwekezaji wa uwanja wa KIA na KADCO tuache wananchi katika maeneo yao waweze kufanya shughuli zao za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani Waziri Mkuu umelifanyia kazi vema jambo hili na nina hakika ukiamua wewe na Mheshimiwa Lukuvi na Mheshimiwa Mbarawa mlimalize tatizo hili, mnao uwezo wa kulimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuruni sana na nawatakia kheri.