Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote aliyenipa fursa ya kuweza kusimama na kuweza kutoa mchango wangu katika sekta hii muhimu sana ya ardhi ambayo baba wa Taifa aliasisi akasema ili nchi iendelee inahitaji mambo manne na suala la ardhi alilipa kipaumbele cha kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijakwenda kwenye hoja zangu naomba kwanza niseme naunga mkono hoja hii kwa sababu jana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya kazi nzuri sana ya kutukuka ambayo sisi Watanzania na hasa wanawake hatuna cha kumlipa zaidi ya kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu na kumsimamia aendelee kutekeleza kile alichokiahidi alipokuwa akiomba kura kwa Watanzania na Watanzania wakamwamini na kumpa kura za Urais mpaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba kwa kazi aliyofanya Mheshimiwa Rais, maana mimi hapa napokea simu mpaka simu imezima, kama kura zingepigwa leo ushindi wa Chama cha Mapinduzi ungekuwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono hoja hii kwa sababu nne zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwanza, kitabu hiki kimeandaliwa vizuri, ni ukweli usiopingika kitabu hiki hakina maneno, kimejeaa data, maneno ni ukurasa 1 – 70 lakini kuanzia ukurasa wa 1 mpaka 157 ni data. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Lukuvi na timu yake kwa kuandaa kitabu hiki vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa sababu Mheshimiwa Waziri, William Lukuvi, Mheshimiwa Naibu Waziri, Angelina Mabula; mimi huwa namwita Sanji, na Katibu Mkuu na timu yote wanafanya kazi nzuri sana na ndiyo maana leo naona kila Mbunge anayesimama muda unamtosha kwa sababu hana cha kuzungumza zaidi kwa sababu mambo mengi yamefanyika katika maeneo yake.

Naomba Mheshimiwa Lukuvi aendelee kufanya kazi, pamoja na timu yake na Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kweli watendaji wa Wizara Ardhi wamebadilika, ameeleza hapo Mheshimiwa Chikota, nimemsikiliza. Siku moja nimewahi kwenda kwenye Wizara fulani tukiwa naye, tulijionea maajabu ambayo yalikuwa hajawahi kutokea; hongereni sana, Mwenyezi Mungu awatie nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naunga mkono hoja hii kwa sababu Wizara ya Ardhi imetatua migogoro mingi sana iliyokuwa inawakabili wananchi kule Dar- es Salaam, Arusha, Mara, Morogoro na maeneo mbalimbali, nikianza kuyataja tutalala hapa kwa upimaji wa ardhi na maeneo mengine; kwa kweli Lukuvi hatuna cha kumlipa; naomba niungane na wenzangu kusema kwamba Mwenyenzi Mungu awatie nguvu na awasimamie katika kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada kuunga mkono hoja hii, sasa naomba nijielekeze katika mambo machache niliyojipanga kuyatilia mkazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nataka nizungumzie umiliki wa ardhi. Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali yetu ya CCM kwa kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume katika kumiliki ardhi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 1979 kifungu cha nne (4) mpaka cha tano (5) kimetoa fursa kwa wananchi wote bila kujali ni mwanamke ama mwanaume kwamba anayo haki ya kumiliki ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi bado yapo matatizo katika jamii ya watu wa Tanzania ambako baadhi ya wanawake hawamiliki ardhi. Kwenye ule utaratibu wa mila baadhi ya makabila mwanamke hamiliki ardhi. Hapa nitatoa mfano wa wajomba zangu kule Kagera ambako mwanamke hana chake, hawezi kumiliki ardhi yeye anamiliki mji tu. Kule Kilimanjaro na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika wakati kwamba sasa Mheshimiwa Lukuvi sisi tunakuamini hebu akaangalie taratibu za kimila ambazo ni kandamizi kwa wanawake ili zirekebishwe na wanawake waweze kumiliki ardhi sambamba na wanaume ili wanawake nao wafaidike na matunda ya nchi yao. Wanawake wana fursa, wanawake wana haki ni kwa nini inapofika wakati wa kutoa ardhi eti mila na desturi zinasema wanawake hawana haki? Kwa kweli Mheshimiwa Lukuvi nataka hapa kabla hajahitimisha hotuba atuambie sasa na namwaminia kwa uhodari wake, ana mkakati gani kuhakikisha hizi mila kandamizi zinaweza kuondolewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie migogoro ya wakulima na wafugaji na vile vile migogoro kati ya wananchi na hifadhi. Sitaki nirudie ya wenzangu waliyozungumza. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali lakini bado kuna migogoro mikubwa ya ardhi, bado wananchi wanaishi kwa mashaka, bado wafugaji hawana uhakika, bado mazao ya wakulima yanaliwa na mifugo ya wafugaji; bado hifadhi inawakandamiza wananchi; bado hata wananchi wanakwenda kwenye maeneo ya hifadhi ambako hawaruhusiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufike wakati sasa na hapa nataka nije na ushauri, umefika wakati Serikali ya Tanzania ipime ardhi yote ya Tanzania. Naomba nikatae kwamba haiwezekani suala la kupima ardhi kuwaachia Halmashauri, Halmashauri hazina fedha. Serikali itengeneze mkakati maalum wa kutafuta fedha hata kama ni kwa mkopo, hata kama ni kuanzisha mfuko na tuko tayari, zitafutwe hela za kutosha, ardhi ya Tanzania ipimwe yote, wakulima waambiwe ninyi eneo lenu ni hili, wafugaji hapa ni kwenu, wavuvi hapa ni kwenu na Hifadhi ya Taifa ni hapa, ili tuweze kuishi kwa amani na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza wenzangu kwamba sasa hivi population ya Watanzania imeongezeka, idadi ya mifugo imeongezeka lakini ardhi nayo inaendelea kutumika. Kama hatukujipanga na kuwa na matumizi bora ya ardhi huko baadaye kutakuwa na vita vya watu wanaopigania ardhi. Naomba tusifike huko, hebu Serikali ije na mkakati na mpango. Itengeneze mkakati wa kukopa fedha kwenye vyombo vya fedha ili tuweze kupima ardhi yote ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa kazi nzuri sana ya kuendelea kutoa hati kwa Watanzania. Napongeza sasa hivi sekta ya ardhi wameandaa utaratibu mzuri sana, sasa hivi wamefungua ofisi za kanda, ndani ya miezi mitatu mwananchi anapata hati. Zamani ilikuwa ni kero na shida, hongera sana Serikali ya CCM; na ndiyo maana wananchi wanasubiri uchaguzi ufike kwa sababu kazi inafanyika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri, kwamba pamoja na kazi nzuri, lakini zoezi linasuasua. Tumeona kazi nzuri ya Morogoro tumeona kazi nzuri kule Muleba na maeneo mengine ya kupima ardhi mpaka za vijijini. Sasa hivi naomba nishauri Serikali, hebu iongeze kasi ya kupima ardhi, hebu itafute fedha za kutosha, ipeleke kwenye hicho kifungu ili wananchi wote wapimiwe ardhi yao. Kama mwananchi akipimiwa ardhi yake akawa na hatimiliki hata mapato ya Serikali yataongezeka kwa sababu atalipa mapato kwa mujibu wa Sheria badala ambavyo sasa hivi wananchi zaidi ya asilimia 80 wanatumia ardhi lakini hawalipi chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ardhi itamkomboa wananchi na hasa mwanamke aliye kijijini atatumia hati yake kwenda kukopa fedha katika vyombo vya fedha. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Lukuvi na timu yake na Serikali yote kwa ujumla hebu waweke mkakati wa kuhakikisha tunakwenda kupima ardhi. Hapa nataka atakapo-wind up hotuba yake Mheshimiwa Lukuvi atuambie ana mkakati gani wa kuhakikisha kwamba anaharakisha kwenda kupima ardhi na wananchi wote wanapata hatimiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mipango miji. Ukiwa kwenye ndege ndio utaona hali halisi. Ukienda nchi nyingine utaona ardhi imepimwa vizuri. Afrika Kusini ni mfano na maeneo mengine, kwetu unaona viduku viduku vimekaa. Ufike wakati sasa tuwe na mipango miji, tuwe na master plan ya kila mji. Tumechoka kuona miji yetu inajengwa bila kuwa na master plan. Sasa hivi tunaanzisha Jiji la Dodoma, Makao Makuu ya Chama na Serikali, tunataka Mji wa Dodoma upimwe wote, tunataka mikoa mipya na mikoa mingine ipimwe yote na maeneo yote ya halmashauri na miji yetu ili tuwe na miji iliyopangwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile niipongeze National Housing kwa kazi sana wanayoifanya ya kujenga nyumba. Hongera Mr. Mchechu na timu yako, mmekuwa ni watu waaminifu na waadilifu, mmefanya kazi nzuri sana iliyotukuka ya kujenga nyumba za National Housing hapa Tanzania; lakini kama alivyosema Mheshimiwa Lupembe nyumba nyingine hazina watu, tatizo linalowapata nyumba ni ghali. Tunaomba mjaribu kufanya marekebisho. Tafuteni sasa, mkawasaidie na wanyonge hasa wanawake wanaoishi vijijini. Huyu mfanyakazi mdogo mwenye kima cha chini mshahara wake shilingi laki mbili ama laki tatu naye afaidike na mpango huu na inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mr. Mchechu namfahamu, huwa ana mipango; anaweza akatengeneza hata nyumba ya milioni kumi mtu akaishi, anaweza kutengeneza nyumba ya milioni ishirini mwananchi akaishi; ikiwezekana hata ya milioni tano, chumba na sebule ataishi mfanyakazi wa Tanzania na akafaidika kuliko ilivyo sasa milioni mia moja na nyumba ya kima cha chini milioni arobaini kwa kweli inashindikana. Siyo National Housing peke yenu hata na ile kampuni ya Watumishi Housing pia nao wamefanya nzuri lakini warekebishe hivi viwango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nipongeze sana mpango wa mashine za kufyatulia matofali kwa vijana, naomba sasa National Housing, Mr. Mchechu na wenzake waje sasa na mpango wa kusaidia wanawake. Wanawake nao wanao uwezo wa kufyatua matofali kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu, nao wakopesheni kupitia vikundi vyao ili nao wanufaike na mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, mchango wangu mwingine nitauwasilisha kwa maandishi, naunga mkono hoja, hongera sana Waziri wa Ardhi, hongera sana Mheshimiwa Dkt.Magufuli Mungu akubariki sana kura zikipigwa leo Rais ni wewe. Ahsante sana Kidumu cha Chama cha Mapinduzi.