Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia hoja hii ambayo ni muhimu sana ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua ambayo ameichukua, hatua ambayo imedhihirisha madini yetu yalikuwa yanatoroshwa sana na yalikuwa yanaibiwa sana na ni hatua ambayo inadhihirisha kauli yake kwamba nchi hii ina mali nyingi sana. Kwa hiyo, ningependa kumpongeza sana kwa hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ningependa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Katibu Mkuu pamoja na Wakurugenzi wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Viongozi hao wamedhihirisha kwamba kweli wana nia ya kuondoa malalamiko mengi ya ardhi ambayo yalikuwa yamejaa kwenye nchi hii; wamezunguka takribani nchi mzima. Mheshimiwa Waziri amekuja Muheza takribani mara mbili, yote ni kwa ajili ya kutatua matatizo ya ardhi pale wilayani Muheza. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ardhi ni suala muhimu sana. Katika wiki iliyopita tulikuwa na hoja ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Katika hoja hiyo issue ya ardhi ndiyo ambayo wawekezaji wote wanataka wakija hapa nchini wakute ardhi iko sawasawa. Sasa vituo vyetu vya TIC na EPZA vina matatizo makubwa sana ya ardhi na sina uhakika kama Wizara hii imeweza kuwasaidia kwa kiwango gani ili waweze kuwa na ardhi pale waweze kuwa na land bank ili wawekezaji wanapofika wasipate matatizo yoyote. Kama hawajawa-approach ni vizuri wakati wanagawa ardhi kwa kweli kuangalia hivi vituo viwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIC na EPZA ni kitovu cha wawekezaji na ni kitovu cha maendeleo. Mwekezaji akija anahitaji hoteli, anahitaji kuweka viwanda lakini lazima awe ardhi. Hatutaki wawekezaji waje hapa na waanze kusumbuka kuanza kutafuta ardhi wao, wanatakiwa wakute ardhi ipo hapo. Kwa hiyo ni vizuri wakiwasiliana na Mawaziri wanaohusika ili kuhakikisha kwamba kwa kweli ardhi inakuwepo na wakati wanagawa ardhi Wizara hii kweli vituo hivyo visikose ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuja Muheza na alikuja mara mbili. Mara ya kwanza kukabidhi mashamba ambayo yamefutiwa hati, takribani mashamba saba na mara ya pili akaja tena kwa suala hilo hilo kwa sababu kulikuwa na shamba moja ambalo lilisahaulika la Kibaranga na akaja akatukabidhi hati, kwamba Mheshimiwa Rais amefuta hati ya hayo mashamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba yale, ukichukulia hili shamba la mwisho la Kibaranga, tulikuwa tumewawekea tunataka kuwahamisha wanakijiji takribani 1,128 ambao walikuwa kwenye hifadhi ya Amani kule Delema; ilitakiwa tuwahamishie pale na tumeshawaamisha pale sehemu kwenye hilo shamba la Kibaranga. Tatizo ambalo linajitokeza ni kwamba wananchi wa pale Kibaranga wanahoji kwamba utawapaje ardhi hawa kabla ya sisi wakazi wa hapa hamjatugawia?

Mhesheshimiwa Mwenyekiti, tulileta malalamiko hayo pamoja na mipango yote ya mashamba yote namna tutakavyogawa sehemu mbalimbali za wawekezaji, hospital, ofisi, shule na kila kitu, na barua hiyo nilimkabidhi Mheshimiwa Waziri. Ni muhimu sana barua hiyo iweze kujibiwa kwa sababu sasa hivi tumeanza kupata wawekezaji na tumeanza kuwaonesha maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunategemea kwamba baada ya kupata majibu ya barua hiyo tutaanza kupanga na kutekeleza namna tutakavyogawa mashamba hayo kwa wananchi, wawekezaji na namna tutakavyoweza kupanga mambo mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Muheza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri namwomba sana, kwamba tukipata majibu ya barua yetu hiyo itatusaidia sana sisi kuweza kupanga mipango yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba, sisi ardhi tunayo sasa hivi hatuna shida ya ardhi, tuna shida tu ya kutafuta wawekezaji Muheza. Hata hivyo, tatizo kubwa ni kwamba tuna upungufu sana la Wapima Ardhi; wapimaji hakuna; tuna mpimaji mmoja ambaye sasa hivi amekwenda kusoma. Sasa kila tukitaka kufanya mipangilio inabidi tuombe Mkoani Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwomba Mheshimiwa Waziri kwamba at least atusaidie wapimaji wawe pale ili tuweze kukamilisha hii kazi ya upimaji pale wilayani ambayo tunaamini kwamba kwa kiasi kikubwa sana itaweza kutusaidia kuweza kupima na kuweza kupanga (master plan) ya pale wilayani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho nataka kuongelea suala la National Housing. National Housing wamefanya kazi nzuri sana na wanaendelea kufanya kazi nzuri sana, wamejenga majengo mengi sana na sasa hivi wako kwenye mikakati ya kujenga nyumba za bei nafuu. Mheshimiwa Waziri naomba; National Housing tumewapa eneo pale Muheza la sehemu za Chatuu Kibanda pale, wameshalipia na wananchi wa Muheza walikuwa wanategemea kwamba ujenzi wa hizo nyumba nafuu ungeanza wakati wowote ule. Hata hivyo, mpaka wakati huu hatuoni dalili zozote, tunajiuliza hawa National Housing vipi, wamesahau kwamba tuliwapa eneo pale Muheza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba aweke msisitizo ili National Housing sasa hivi waje waanze ujenzi pale. Eneo lipo na wananchi wa Muheza wako tayari na wengine wako tayari wanaulizia namna ya ununuzi. Sasa tunamwomba sana aangalie uwezekano wa kuja kusaidia na kuwaamuru National Housing waanze kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, yangu leo yalikuwa machache na nakushukuru sana na naomba kuunga mkono hoja hii.