Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa pili katika Wizara hii. Nami kama Msemaji aliyetangulia nianze kwanza kupongeza kwa jinsi ambavyo Mheshimiwa Lukuvi pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Angelina Mabula wanavyokwenda na kasi ya kuweza ku-solve migogoro mbalimbali ya ardhi katika nchi hii, kitu ambacho tulikuwa hatujazoea kukiona mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lukuvi amekwenda sehemu nyingi sana na pengine kama alivyosema Mheshimiwa Ndugulile, kwa kawaida alikuwa anapinga mambo mengi ya ardhi lakini leo anaunga mkono hoja, basi na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna changamoto chache ambazo nyingi tumeshazifikisha ambazo zinahusiana na Mkoa wetu wa Tabora na hasa Tabora Manispaa. Tabora Manispaa sijui niseme ina bahati mbaya au nzuri, lakini kwa ulinzi ni bahati nzuri kwamba tumezungukwa kwa kiwango kikubwa na Kambi za Jeshi. Sasa kumekuwa na mwingiliano mkubwa sana baina ya wanajeshi pamoja na wananchi na hili mara kwa mara nimekuwa nikilizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na migogoro mikubwa ambayo tayari imeripotiwa mara nyingi, ningemwomba Mheshimiwa Waziri watafute utaratibu wa Wizara ya Ardhi pamoja na Jeshi kwa maana ya Ulinzi ili kuweza kutatua migogoro ile kwa sababu inahatarisha amani. Maeneo mengi ambayo ni ya Jeshi kwa madai yao, wameweka zile beacon ambazo wanazitambua wao, lakini wananchi sehemu nyingi hasa maeneo ya Usule, Kata za Mbugani, Tambukareli, Cheyo, Mtendeni na Malolo wanazo beacon za muda mrefu ambazo walipimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Jeshi wanapokuja na wao wanasema wana alama zao, hili suala limekuwa na mgogoro wa muda mrefu, naomba Wizara iweze kulishughulikia suala hilo ili wananchi pamoja na Jeshi wasiwe na mgogoro na kwa kuzingatia kwamba Jeshi mara nyingi hawatumii maeneo yale, wananchi wamekuwa wakiyatumia kwa kilimo. Sasa wale wananchi waweze kupewe ruhusa, tunaongelea kilimo, sasa Jeshi eneo kubwa hawalimi kabisa na wananchi wamekuwa wakilima muda mrefu basi watatue hili suala ili wananchi waweze kuyatumia maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo lenyewe sitalizungumzia kwa undani ila kwa kuwa nimesikia hapa pia yupo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Dkt. Yamungu, tuna Chuo cha Ardhi pale Tabora Mheshimiwa Waziri cha Ardhi kina changamoto nyingi sana, kuna upungufu mwingi ikiwemo na vitendea kazi. Chuo hiki cha Ardhi ni cha miaka mingi na changamoto zile walimwakilishia Dkt. Yamungu akiwa ni mgeni rasmi kwenye mahafali ya Chuo cha Ardhi yaliyopita ambayo na mimi nilihudhuria, nina imani kama hajamfikishia Mheshimiwa Waziri changamoto zile basi amfikishie rasmi, kwa sababu yuko hapa waliorodhesha changamoto nyingi, basi nisiziorodheshe sasa hivi yeye atampatia ili aweze kuzifanyia kazi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu nije kwenye hivi viwango maalum wanavyolipa wamiliki wa nyumba na majengo. Tabora Manispaa ndiyo peke yake ambayo imekuwa inalipa Sh.25,000/= kwa mwaka ilikuwa ni flat rate. Tofauti kabisa na Manispaa na Halmashauri zingine ambazo nyingi zilikuwa zinalipa kwa mfano, Morogoro Sh.10,000/=, Temeke Sh.15,000/=; Mwanza Sh.10,000/=; Manispaa ya Songea Sh.12,500/=, lakini Tabora Mjini Sh.25,000/=. Sasa sijaelewa ni vigezo gani pamoja na kwamba kitu kinachotumika wanadai kwenye ile valuation wanatumia ile 0.25 thamani ya nyumba wana calculate kwa hiyo 0.25 kupata thamani au tozo ambayo anayotakiwa kutozwa huyu mmiliki wa nyumba au jengo. Hata hivyo, katika sehemu nyingi imekuwa ni Sh.10,000/=, haijafika Sh.20,000/= kwa nini Manispaa ya Tabora ni Sh.25,000/=? Naomba Mheshimiwa Waziri hilo aweze kuliangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne naomba nizungumzie nyumba zinazojengwa na National Housing. Nia ni njema kwamba waweze kuzikopesha nyumba hizi kwa watu mbalimbali na hasa wanyonge pia ikiwezekana, lakini kuna mchezo mchafu unafanyika kwenye hizi nyumba. Kuna wenzetu ambao wana uwezo mkubwa wa kifedha huwa wanazinunua hizi nyumba wao, wanazinunua kwa wingi na wakati mwingine kwa majina mbalimbali halafu wanakuja kuzipangisha. Sasa naomba wafanye uchunguzi watu wa namna hiyo waweze kudhibitiwa ili kweli lile lengo la kwamba watu wapate nyumba nafuu liweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee hili suala la Wathamini wa Ardhi (Valuers) wamekuwa hawawatendei haki wananchi wengi hasa wanyonge, siyo wote lakini baadhi yao. Wanapofanya valuation, hapa kwenye valuation huwa ndiyo kuna harufu hapa ya rushwa. Unaweza ukakuta kwa mfano kiwanja ambacho labda au nyumba ambayo ingekuwa na thamani ya Sh.50,000,000/= huyu Valuer kwa sababu hajaongea kwa matamshi ambayo angeyataka yeye ana-valuate ile labda kwa Sh.2,000,000/=. Sasa yule mnyonge anashindwa afanye nini kwa sababu huyu mtu wa valuation ndiye anayetambulika kisheria kwamba akifanya valuation basi hiyo ndiyo itafuatwa. Mheshimiwa Waziri naomba hawa Valuers siyo wote lakini baadhi yao siyo waaminifu na eneo hilo lina mambo mengi ya rushwa. Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kuongelea suala la Sheria ya Mabaraza ya Ardhi Namba mbili (Na.2) ya mwaka 2002. Ni kweli uanzishwaji wake ulikuwa ni wa muhimu kwa sababu kila Wilaya ikiwa na Baraza la Ardhi angalau migogoro mingi ya ardhi itapungua. Naiomba Wizara fedha ambayo inatakiwa kwa ajili ya kuanzisha Mabaraza ya Ardhi kila Wilaya ipelekwe kwa wakati unaotarajiwa ili sehemu nyingi kuwe na Mabaraza haya ya Ardhi kwa ajili ya kuweza kutatua migogoro mingi ya ardhi katika sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, narudia kuunga mkono hoja na nasema ahsante sana.