Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hon. Dr. Susan Alphonce Kolimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa ruhusa yako na kwa heshima kubwa niweze kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu, hoja ya kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika kuchangia hoja hii, nitachangia hoja ambazo zimetolewa na baadhi ya Wabunge kuhusu hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza ilitolewa na Mheshimiwa Kanali Mstaafu Masoud Ally Khamis ambaye alikuwa anaitaka Serikali iweke mkazo katika kusimamia alama za mipaka kwani tayari kumekuwa na tuhuma za kuondoa alama hizo katika mipaka ya Sirari na maeneo mengineyo. Naomba nitoe maelezo juu ya utekelezaji wa Serikali juu ya hoja ambayo imetolewa na Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la urekebishwaji wa mipaka ya nchi linafanyika kupitia mazungumzo baina ya nchi na nchi. Tayari Serikali imekwishaanza majadiliano na nchi ambazo zinapakana nazo na hivi karibuni nafikiri mmesikia, Tanzania ilifanya majadiliano na Serikali ya Uganda kuhusu mpaka katika Mkoa wa Kagera ambayo yameshakamilika na hatua inayofuata sasa ni kujenga na kuimarisha alama za mpaka ule. Aidha, Serikali inajiandaa kupitia upya mpaka wa nchi hizi mbili hasa kwenye upande ule wa ziwani kati ya Tanzania na Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa upande wa mpaka wetu wa nchi ya kwetu pamoja na Kenya, mazungumzo yalishakamilika na tayari Serikali imeshatoa mchango wake katika kugharamia, kujenga na kuziimarisha alama za mipakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, kwa upande wa nchi za Malawi, majadiliano bado yanaendelea. Kama mlivyosikia mara ya mwisho, Tanzania pamoja na Malawi waliitwa na lile jopo la Marais Wastaafu kule Kusini ili kujadili suala la mpaka wa Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa tofauti zozote zinazojitokeza kati ya nchi na nchi na hasa zinazohusu masuala ya mipaka, zitakuwa zinaendelea kusuluhishwa kwa njia ya mazungumzo na kwa amani kwa faida ya pande zote mbili kwa sababu hawa ni majirani zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya pili ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Kanali Mstaafu Masoud Ally Khamis. Hoja hii ilikuwa inahusu Ibara ile ya 12 (e) ya Itifaki inayozitaka nchi wanachama kushirikiana katika kukabiliana na wahamiaji haramu. Niseme tu kwamba nchi yetu imekuwa ikipokea wahamiaji haramu kutoka nchi za Eritrea na Ethiopia wanaokwenda Afrika Kusini, ambapo tatizo ambalo kwa Tanzania tumeshalisikia mara nyingi na limekuwa ni changamoto; Serikali ihakikishe kuwa nchi ya Kenya haiwaruhusu watu hao kupitia kuja kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kwa kusaini Itifaki hii, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watatumia mikakati ambayo iko ndani ya Itifaki na kuhakikisha kwamba hivi vyanzo na njia kuu na Vituo vya Wahamiaji haramu ambavyo vipo kwa sasa hivi, vitaondolewa kwa kupitia Itifaki hii ambayo sasa hivi tunairidhia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge nawaomba sana tuweze kuiunga mkono Itifaki hii ipite ili mikakati iliyowekwa na Serikali na kwa kupitia Itifaki hii, changamoto hii ambayo inapatikana kwenye nchi yetu na nchi za jirani itakuwa imekwisha kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja hii.